ad

ad

NILIISHI DUNIA YA PEKE YANGU - 10






ILIPOISHIA:
Niliposogea karibu yake alinitazama, nilijikuta nikikwepesha macho yangu, hakuendelea kunitazama bali aliendelea kusoma Biblia yake. Hakusoma sana, aliiweka pembeni na kunigeukia.
“Ester,” aliniita.
“Abee mama.”
“Una tatizo gani mwanangu?” aliniuliza huku akinitazama usoni.
“Mimi?” swali lile lilinishtua kwa vile sikulitegemea.
“Ester, kwani swali hili nimemuuliza nani?”
“Mimi.”
“Hebu nieleze una tatizo gani?”
“Sina tatizo,” nilikataa kwa kuamini hajui lolote juu ya ujauzito wangu, labda kitu kingine.
SASA ENDELEA...

“Ester mwanangu una tatizo, mimi ndiye mama yako, japo sijakuzaa lakini sasa hivi ni zaidi ya mama yako, naomba unieleze usinifiche kitu, una tatizo gani linalokusumbua?”
“Mama mbona mimi nipo sawa,” nilijitetea.
“Hapana, mi’ mtu mzima nina uzoefu wa kumjua vizuri mtu, si wewe Ester niliyekuwa nakujua mwanzo, kuna mabadiliko makubwa sana hasa toka siku ile uliyoweweseka usiku.”
“Mama nipo sawa ni wasiwasi wako tu.”
“Si kweli, unaonesha kila siku unailazimisha furaha usoni kwako lakini kuna kitu kizito moyoni mwako. Hata ndugu zako wameshaniuliza kama una tatizo gani, lakini sikutaka kukuuliza haraka. Nilijitahidi kuona labda utabadilika lakini tokea jana kuna kitu kingine kimetokea, hata ule uchangamfu wa kulazimisha umepotea.
“Umekuwa mtu mwenye mawazo, kila unapokuwa peke yako unakuwa unahama kabisa kimawazo na kubakia mwili pekee lakini wewe haupo kabisa. Nakuomba mwanangu nieleze tatizo linalokusumbua au hata umueleze baba yako kama unaona huwezi kuniambia mimi.”
 Mama aliniuliza kwa sauti iliyoonesha jinsi gani anaumia na matatizo yangu asiyoyajua. Maneno ya mama yalikuwa mazito moyoni mwangu kama kisu butu kilichoupasua moyo wangu bila ganzi. Nilihisi uchungu wa ajabu na kuanza kulia kilio ambacho niliamini kabisa kitazidi kumweka njia panda mama.
Sikuweza kuvumilia, nilijikuta nikijitupia kifuani kwa mama na kuangua kilio cha sauti, nikiamini bado sitakiwi katika dunia ya watu bali najilazimisha tu kuishi. Nilijiuliza kwa nini kila siku niwe mimi tu, mama aliendelea kunibembeleza.
“Ester mwanangu kuna kitu kizito kilitokea humu ndani, maono yangu ya kwenye njozi yananionesha lakini kwa nini hutaki kusema?”
“Kitu gani mama?” nilishtuka kusikia vile na kujiuliza ni maono gani aliyoyaona ndotoni kwa kujitoa kifuani mwake.
“Kuna kitu kinanionesha kuna tukio umefanyiwa na baba yako japo unaficha.”
“Hapana mama sijafanyiwa kitu chochote na baba,” nilikataa kwa nguvu zote.
“Lakini maono yangu yananionesha kuna aibu kubwa itaikumba nyumba hii bado sijajua ni kwa ajili ya ukimya wako au nini.”
“Mama, baba hajanifanyia kitu chochote, kama angekuwa kanifanyia jambo kwa nini nisikwambie? Pia hata baba nisingekuwa naye karibu.”
“Mmh! Sawa, lakini ndoto zangu huwa hazisemi uongo lazima itanipa jibu ndani ya miezi mitatu.”
“Lakini mama labda ni ndoto za kumkumbuka mama yangu ndizo zilizonichanganya.”
“Umeota mara ngapi?”
“Ni siku ileile tu mama.”
“Si kweli, ndoto ile ingetoka kama ungekuwa unanyanyaswa, lakini hapa unaishi kama wewe na kina Martha mmezaliwa tumbo moja. Kuna kitu unakificha lakini kumbuka mwanangu moto hata siku moja haufunikwi kwa shuka, lazima moshi utaonekana.
“Kumbuka toka siku ile ulipoweweseka usiku umekuwa ukipungua kila siku, naishika Biblia hii ambayo naiamini, una jambo zito ambalo linahitaji msaada wa haraka kulitatua bila hivyo linaweza kupasuka kama bomu.”
Niliamini mama alikuwa akihisi kitu ambacho alitaka nikitamke kwa mdomo wangu na si kingine, nikiri nimebakwa na baba ili auwashe moto. Lakini niliapa mpaka naondoka duniani nitaondoka na siri yangu moyoni. Niliamua kusema uongo ili aniache akitegemea kuna kitu nitamwambia. Lakini akishtuka atakuta sipo hivyo bado atabakia na swali lisilo na jibu.
“Mama kuna kitu kinanisumbua wala hakihusiani na humu ndani, nimepata shida sana kusema lakini kwa vile umenitambua nakuahidi mama yangu kukueleza kila kitu, lakini si leo.”
“Unataka kunieleza lini?”
“Baada ya siku mbili.”
“Kwa nini usinieleze leo?”
“Hapana mama mazungumzo yanahitaji nijiandae.”
“Estaaa! Ujiandae vipi mwanangu?”
“Najua utashangaa lakini kwa vile nimekueleza nitakwambia, nakuomba nipo chini ya miguu yako nikubalie.”
“Sawa nimekukubalia, lakini nakuomba mtangulize Bwana Yesu kwa kila tatizo linalokuja mbele yako, hakika utaibuka mshindi.”
“Sawa mama.”
Baada ya kusema vile mama alinishika mkono kichwani na kunifanyia maombi mazito ili niondokewe na matatizo. Baada ya maombi ya zaidi ya dakika ishirini mama aliniacha.
“Ester mwanangu kila unachokiona ni hila za shetani ambaye yupo kwa ajili ya kutuharibia wanadamu. Lakini siku zote mfanye Bwana ndiye kimbilio lako na siku zote shetani hushindwa.”
“Amina, mama, siku zote nimekuwa nikifanya hivyo lakini bado matatizo yananifuata likitoka hili linakuja hili.”
“Usichoke kuomba kwani si wote wanaoomba hupata kwa muda ule, wengine huchelewa kupata kama roho mtakatifu hayumo mioyoni mwao lazima watakata tamaa.”
“Nitafanya hivyo mama, wacha nikaandae chakula cha usiku.”
“Na Bwana akutie nguvu.”
“Amina.”

Niliachana na mama na kwenda jikoni kuandaa chakula cha usiku kutokana na muda kuwa umekwenda sana. Jioni ile ilitakiwa upikwe wali kutokana na mchana kupikwa mboga ya moja kwa moja.
Nikiwa jikoni nilijawa na maswali mengi yaliyoambatana na huruma kwa mama Mather ambaye nilijua kuwa atakuwa katika wakati mgumu baada mimi kuondoka bila kumuaga.

Huenda akachuma hata dhambi kwa kufikiria kuwa labda nimeona walikuwa wakininyanyasa, wakati kwa upande wake anajiona yupo sawa na kujikuta akimtafuta mchawi bila mafanikio.
 Japo nilijua nitamuweka katika wakati mgumu hata kumuongezea mawazo lakini niliamini nitakachokifanya kitakuwa ni jambo la busara hasa baada ya kuamini kuwa ana maono ambayo yatamwonesha kila kitu, hivyo sikutakiwa kuendelea kuwepo pale, niliona bora nikafie mbele kuliko kuvunja ndoa ya watu.
   *****
Usiku ulipoingia nilibadili mawazo yangu kutokana na maneno ya mitego ya mama Mather kwa kuamini ana wasiwasi na mumewe juu yangu japo aliuficha.
Mwanzo nilikuwa na wazo la kuzungumza na baba baada ya kurudi kazini ili nijue nguo zangu nitazitoa vipi. Niliamini kama nitasimama naye kwa siri halafu kesho yake nitoroke lazima ningeacha matatizo mazito, hivyo niliamua kuiacha siku ile ipite ili kesho nikitoka wasijue nimekwenda wapi na chanzo ni nini.
Usiku wakati wa kulala Mather alinifuata chumbani kwangu, baada ya kukaa aliniuliza:
“Ester mdogo wangu, una matatizo gani?” Lilikuwa swali kama aliloniuliza mama jioni.

“Kwa vipi dada?”
“Unajua sasa hivi mdogo wangu haupo sawa hasa baada ya siku ile nilipokukuta unalia. Hata haiba yako imepotea japo kuna kitu unakificha, nilimwambia mama ambaye naye alisema ameliona ila alikuwa anakutafutia siku akuulize.
Lakini kila nikirudi na kumulizia kama ameshaongea na wewe alikuwa akisema bado. Basi naomba mdogo wangu kipenzi kipi kilichokusibu kufikia hatua ya kuonekana kama mgonjwa?”

“Mmh!” Nilishusha pumzi kidogo na kuamini bado hajazungumza lolote na mama na kuelezwa tulichozungumza mchana.
“Niambie mdogo wangu, japo hatuzidiani sana umri lakini naweza kukusaidia.”
“Ni kweli nina tatizo hata mama leo aliniuliza lakini kwa vile na ninyi mmeliona niliomba hili nilizungumze kesho kutwa, Jumamosi siku ambayo wote tutakuwepo nyumbani.”
“Kwa nini usinidokeze kidogo mdogo wangu?”

“Hapana dada kama mama nilimwambia hivyo, basi naomba na wewe uvute subira, kwani Jumamosi siyo mbali kishindo cha kesho na muda huu ni usiku, kesho haipo mbali.”
“Mmh! Sawa,”
Dada Mather aliondoka na kuniacha nilale, baada ya kuondoka nilibaki na uamuzi mgumu, japokuwa kuondoka ilikuwa lazima. Niliamini kabisa kuondoka kwangu kungeacha simanzi nzito, kwani ucheshi wangu na heshima iliitangaza nyumba yetu lakini sikuwa na jinsi kwani kisu kilikuwa kimegusa mfupa.

Usiku ulikuwa mrefu kuliko kawaida, moyo uliniuma kila nilivyofikiria kutengana na familia ya mama Mather, nililia sana.
Familia mbayo ilinifanya nisahau matatizo yangu na kujiona nilitakiwa kuzaliwa katika familia ile lakini kitendo cha mzee Sifael kunibaka na kuamua kukaa kimya kilinitesa sana. Kama alivyosema mama Mather siku zote moto haufunikwi na shuka niliamini. Nilikumbuka maneno ya bibi kuwa kinywa cha mkubwa kinanuka lakini maneno yake hayanuki na aliyetangulia anayajua mengi.

Niliamini ujauzito ni moshi na kukaa kimya ni sawa na kuufunika moto kwa shuka, nilimuomba Mungu kama mzee Sifael amenibaka na kunipa ujauzito lakini aniepushe mbali asiwe ameathirika na kuniongezea zigo lingine.
Lakini nilikuwa na moyo wa ujasiri na kuuapia moyo wangu kukabiliana na lolote litakalojitokeza mbele yangu kwa vile nilikuwa naishi katika dunia isiyonihitaji.

Japokuwa sikupenda niupate lakini niliamini kama atakuwa ameniambukiza ukimwi, basi hiyo ni zawadi yangu ya kuishi dunia ya peke yangu, dunia isiyohitaji furaha zaidi ya huzuni na kilio kila wakati lakini kifo nacho kikikukimbia ili uendelee kuteseka.
Usingizi mzito ulinipitia na niliposhtuka ilikuwa ni alfajiri wakati wa maombi, niliamka lakini sikuwa katika hali ya kawaida.
Mwili wangu ulikuwa katika hali ya unyonge kama mgonjwa macho yalikuwa yamevimba kidogo na kuwa mekundu kutokana na kulia sana kila nilipokumbuka kutengana na familia niliyo izoea  kwenda kuishi sehemu nisiyoijua.
Lakini bado niliamini sikutakiwa kuogopa chochote zaidi ya kuondoka na kuwa tayari kukabiliana na lolote nitakalo kutananalo. Waliponiona waliitana na kuzungumza kwa muda kisha walikuja kwa ajili ya maombi na kunieleza jioni ya siku ile kutakuwa na kikao cha kuzungumzia matatizo yangu kwa kina.

Sikutaka kuwabishia niliwakubaliana, waliondoka na kuniacha na mama ambaye aliendelea kunitia moyo na kuamini nitayashinda yote yanayonikatisha tamaa. Nilikubaliana naye na kufanya kazi zote za muhimu za asubuhi ikiwa pamoja na kuandaa chakula cha mchana. Baada ya kuoga na kujiandaa kutoka  niliomba kwa mama nitoke mara moja.
“Ester mwanangu kwa nini usipumzike tu leo maana nakuona haupo sawa.”
“Hapana mama baada ya maombi ya asubuhi sasa hivi nipo sawa wala usihofu.”
“Umesema unakwenda wapi?”

“Kwa Suzana kuna kitabu cha maombi  alisema atanipa.”
“Basi usichelewe.”
“Sawa mama.”niliagana na mama na kuelekea ofisini kwa baba.
Nilikwenda hadi ofisini kwa baba, aliponiona alinichangamkia na kunikaribisha kwa bashasha.
“Karibu Ester.”

“Asante baba.”
“Karibu mama yangu, karibu kwenye kiti,” alisema huku akinyanyuka toka nyuma ya meza yake kwa kunikaribisha kama mgeni maalumu, ilikuwa ina tofauti na siku za nyuma nilipokwenda ofini kwa baba nilipotumwa na mama, alinikaribisha kwa heshima lakini si kwa kunyanyuka kitini na kuzunguka meza.

Alikikaribisha akionesha moyo wa upendo ambao nilijifikia jinsi ya kuachana nao, nilikumbuka mapenzi ya awali ambayo alinifanyia kiasi cha kusahau matatizo yote ya nyuma. Kosa alilofanya ni kunibaka ambalo nalo nilimsamehe lakini Mungu naye akatoa ushahidi wake wa mimi kushika mimba.

Lakini hakuwahi kunitendea kitu chochote kibaya zaidi ya kunilea kama mtoto wake wa kunizaa ndiyo maana niliamua kumsamehe aliponiomba msamaha japo historia yake ya nyuma ilionesha ana huruma ya mamba kukulia ukiwa nje ya maji ukiingia unakugeuza kitoweo.
“Za nyumbani mama?” aliniuliza kwa unyenyekevu.
“Nzuri tu baba.”
“Mmh! Sasa kwa hiyo bado una msimamo wako?”

“Baba nina imani tumeisha zungumza kinachotakiwa ni utekelezaji,” sikutaka kulegeza msimamo wangu.
“Sawa, mzigo huu hapa hesabu mwenyewe,” baba alisema huku akiweka bahasha ya fedha juu ya meza.
“Kama zipo sawa sina umuhimu wa kuzihesabu nakuamini,” nilisema huku nikichukua bahasha.
“Lakini kwa nini hukutaka tufanye zoezi dogo tu.”

“Zoezi gani?,” sikumuelewa alikuwa na maana gani.
“La kutoa hiyo mimba kwanza ni changa isingesumbua.”
“Naomba kauli hiyo uachane nayo,  labda unaona hasara fedha zako, nitaondoka hata kwa miguu bila senti tano yako na kwenda kufia mbele ya safari.”

“Hapana Ester, ni mawazo yangu tu wala si lazima.”
“Sasa baba nilikuwa na wazo jingine,” baada ya kuona msimamo wangu nilimueleza ninachowaza.
“Wazo gani?”
“Nataka nikitoka hapa nisirudi nyumbani.”
“Unakwenda wapi?”

“Ndiyo safari yangu imeanza, jioni nitapanda malori mpaka Iringa na kesho asubuhi nipande basi mpaka Dar.”
“Ulipoondoka nyumbani na mizigo yako ulimuaga vipi mama yako?”
“Sikuondoka na kitu chochote zaidi ya nilivyo hapa.”
“Amemwambiaje mama yako?”
“Nimekwambie nimefuata kitabu cha maombi kwa shoga yangu.”

“Kwa hiyo utaondoka vipi bila nguo zako?”
“Inabidi iwe hivyo kwa vile siwezi kutoka nyumbani na mzigo bila kuulizwa mswali. Kingine sasa hivi hali nyumbani imechafuka.”
“Imechafuka! Una maana gani?”
“Nimekuwa nikiulizwa maswali ya mitego na mama ambayo huenda majibu yake anayo anasubiri kauli yangu kukamilisha.”
“Una maana gani?”

“Toka siku ya kwanza mama alikuwa na wasiwasi huenda umenibaka, nilimkatalia bado alikuwa na wasiwasi na majibu yangu. Jana alinibana na maswali mazito huku akitaka niseme umenibaka nilikataa lakini bado alikuwa na mimi mpaka nilipomdanganya nitampa jibu kesho. Huoni nikirudi leo nyumbani sitakuwa na majibu ya maswali ya mama? ”
Nini kitaendelea? Tukutane siku ya kesho

No comments

Powered by Blogger.