ad

ad

NDEGE YA AIRASIA QZ8501 YAPOTEA IKIWA NA WATU 162

Shughuli ya kutafuta ndege ya AirAsia ambayo ilipotea jana Jumapili imeendelea leo tena baada ya zoezi hilo kusitishwa kwa muda.


Ndege za kijeshi kutoka indonesia na singapore zilikuwa zikiisaka ndege hiyo kusini magharibi mwa pwani ya Borneo ambapo ndege hiyo ilitoweka.

Ndege ya AirAsia ya Indonesia imepotea usiku wa kuamkia jana ikiwa na abiria 162 ikitokea Surabaya nchini humo kwenda Singapore.

Habari za kupotea ndege hiyo QZ8501 zilianza kutolewa katika akaunti mbalimbali za Twitter za vyombo vya habari vya kimataifa saa 12.30 asubuhi kwa saa za Afrika Mashariki na kufuatiwa na taarifa ya Kampuni ya AirAsia Indonesia iliyotolewa kupitia akaunti yake ya Facebook.

Tukio la kupotea kwa ndege ni la pili mwaka huu baada ya ndege ya Shirika la Ndege la Malaysia, MH370 iliyokuwa ikitokea Kuala Lumpur, Malaysia kwenda Beijing – China, kupotea Machi ikiwa na abiria 239 na hadi sasa haijapatikana.

Ndege nyingine ya Malaysia, MH17, ilitunguliwa kwa kombora huko Ukraine Julai 17 na kusababisha vifo vya abiria wote 298 waliokuwamo.

Taarifa ya AirAsia Indonesia

Taarifa zilizopatikana kutoka vyanzo mbalimbali vya kimataifa zilisema marubani waliomba kuichepusha njia kadri ya maelekezo ya waongozaji wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga ya Indonesia (CAA) kutokana na hali mbaya ya hewa lakini baadaye ikapoteza mawasiliano.

Uongozi wa kampuni hiyo ulibainisha kuwa ndege hiyo aina ya Airbus 320-200 yenye namba za usajili PK-AXC, iliondoka kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Juanda, Surabaya saa 11.35 (Tanzania saa 7.35 usiku) na kupoteza mawasiliano na waongozaji wake saa 1.24 asubuhi (9.24 usiku).

“Ndani ya ndege kulikuwa na abiria 155 ambao kati yao watu wazima ni 138, watoto 16 na mto mchanga mmoja. Pia, walikuwamo marubani wawili, wahudumu wanne na mhandisi wa ndege mmoja,” ilieleza sehemu ya taarifa hiyo na kuongeza kuwa kati yao, 156 ni Waindonesia, Wakorea Kusini watatu na raia mmoja mmoja kutoka Ufaransa, Malaysia na Singapore.

Kwa mujibu wa AirAsia, mara ya mwisho ndege hiyo ilifanyiwa matengenezo ya kawaida Novemba 16. Hata hivyo, habari zaidi kutoka tovuti ya airfleets.net zilionyesha kuwa ndege hiyo ilikuwa matengenezoni kwa kipindi cha zaidi ya miaka sita.

Shirika la habari la Uingereza (Reuters), lilimkariri Mkurugenzi wa Uchukuzi wa Wizara ya Uchukuzi wa Anga wa Indonesia, Joko Muryo Atmodjo akisema hadi jana mchana hakukuwa na mawasiliano yoyote tena na ndege hiyo.
Alisema ndege hiyo ilipoteza mawasiliano ikiwa kati ya Bandari ya Tanjung Pandan, Indonesia na Mji wa Pontianak, Magharibi mwa Jimbo la Kalimantan katika Kisiwa cha Borneo, Kusini Mashariki mwa Asia.

Atmodjo alisema ndege hiyo ilikuwa ikisafiri katika umbali wa futi 32,000 kutoka usawa wa bahari na baada ya kutokea hali mbaya ya hewa marubani waliomba waongeze umbali hadi futi 38,000 kukwepa mawingu.

AirAsia Indonesia inamilikiwa na Kampuni ya AirAsia yenye makao yake makuu Malaysia kwa asilimia 49 na zilizosalia zipo chini ya wawekezaji wazawa wa Indonesia.

“Hadi sasa jitihada za utafutaji na uokoaji zinaendelea zikisimamiwa na CAA. AirAsia Indonesia inashirikiana kwa dhati na kusaidia uchunguzi kwa hali na mali,” ilisomeka sehemu ya taarifa hiyo.

Habari zaidi zilieleza kuwa Jeshi la Indonesia lilikuwa limeanza kuitafuta ndege hiyo huku nchi jirani za Malaysia na Singapore pia zikijitolea.

Ofisa Mtendaji Mkuu wa AirAsia, Tony Fernandes aliwashukuru watu wote kupitia akaunti yake ya Twitter kwa mawazo na sala katika kipindi hiki na kuongeza: “Tuendelee kuwa imara.”

Taarifa ya AirBus

Kampuni ya kutengeneza ndege ya AirBus ya Ufaransa ilisema ndege hiyo ilikabidhiwa kwa Kampuni ya AirAsia ikiwa miongoni mwa ndege zilizozalishwa mwaka 2008 na hadi jana ilikuwa imesafiri kwa saa 23,000 katika safari 13,000.

Kwa nini ndege zinapotea?

Swali hili lilijibiwa na Mkaguzi Mkuu wa Ajali za Ndege kutoka Wizara ya Uchukuzi, John Nyamwihura akisema sababu kubwa ya matukio hayo ni mabadiliko ya hali ya hewa na kuharibika kwa miundombinu, mambo ambayo husababisha kukatika kwa mawasiliano kati ya waongoza ndege na marubani.

“Matukio mengi kama haya ni kuwa ndege hugonga milima na kuanguka. Zikianguka sehemu za milima ni vigumu kupatikana kwa sababu wakati mwingine huganda katika barafu au kuzama kwenye makorongo,” alisema.

Alisema hata ndege zinazoanguka kwenye maji, pia ni vigumu kuonekana kutokana na kina kirefu au barafu.
Mtaalamu huyo alisema kuna baadhi ya ndege ambazo hupotea kutokana na rubani kukata mawasiliano kwa makusudi kwa sababu ama za kigaidi au magendo.

No comments

Powered by Blogger.