JINI LA DARAJA LA SALENDA - 27 NA 28 ZIPO HAPA

JINI LA DARAJA LA SALENDA - 27
ILIPOISHIA:
Alitembea ndani ya maji katika mvua kubwa ya radi, kuna kipindi alizama ndani ya maji na kujitahidi kuogelea na kuendelea na safari yake.
Hata alipopata sehemu ya kujibanza bado hakuona umuhimu wa kujibanza kutokana na kusikia baridi kali kutokana na kulowa mwili wote na maji.
Aliendelea na safari yake yenye mateso ya shetani motoni huku akiomba Mungu amkute Tonny nyumbani pia amtambue na kukubali kuishi naye kwenye umbile la mbwa. SASA ENDELEA...
Alishangaa kutembea umbali mrefu bila kufika, alijikuta akichoka huku njaa kali na kiu ikiwa imemshika na kushindwa kujua atakula wapi.
Alipofika eneo ambalo alijua ndipo kwao alishangaa kuona hakuna nyumba yao, alizunguka mpaka kuna kucha huku akiteseka na baridi kali bila mafanikio.
Ashura alitamani kifo lakini kilikuwa mbali naye, alijiuliza mateso yale mpaka lini au ndiyo ya kudumu lakini hakupata jibu.
Alitamani amuone Balkis mbele yake ili amueleze ya moyoni kuwa amekoma na hatarudia tena katika maisha yake.
Katika hali ya kawaida aliamini kabisa Balkis hakuwa na kosa lolote, japo walitaka kumuua mateso yale yalikuwa makubwa heri angemuua akajua moja lakini si mateso ya kutengwa na jamii kwa kumchukia kila atakapokwenda kwa kujulikana mbwa kumbe mwanadamu yalikuwa makubwa sana.
Wakati akiteseka vile, Tonny naye alikuwa kwenye mateso mazito pembeni ya jalala kwenye tawi la mti uliokuwa na afadhali kutokana na mvua kuwa kubwa sana.
Baada ya mvua kukatika aliendelea kukaa kwenye tawi lile ambalo mvua haikufika sehemu ile kama ingefika aliamini angekufa.
Lakini chini yake kulikuwa na mzoga wa mbwa aliyekufa siku mbili zilizopita na kutoa harufu kali ambayo iliongezeka baada ya kunyeshewa na mvua.
Harufu ilikuwa mbaya sana lakini hakuwa na jinsi, aliendelea kuvumilia kwa kuhofia kupoteza maisha yake kutokana na eneo lote kuwa na maji ya mvua iliyokuwa inanyesha kwa nguvu.
Yalikuwa mateso makubwa kutokana na adhabu ya kuvuta harufu kali ya uchafu na mizoga.
Njaa na kiu ilikuwa kali pamoja, licha ya umbile la kugeuzwa nzi bado alikuwa na akili za binadamu asingeweza kula mizoga wala kinyesi.
Aliamini asingefikisha siku nyingi lazima angekufa kwa njaa.
Aliwaza kama Balkis angetokea mbele yake angemuomba amuue kuliko kumtesa vile,
kama siku moja hali ilikuwa vile kwa mwezi mzima ingekuwaje.
Majira ya saa tisa za usiku akiwa amejikunyata kwa baridi kali la usiku kucha aliamshwa usingizini.
Alipofumbua macho hakuamini kumuona Balkis mbele yake, alitaka kufunua mdomo wake kumuomba msamaha, lakini angewezaje kuzungumza katika umbile kama lile la nzi.
Balkis alimchukua na kwenda naye sehemu na kumtemea mate, palepale Tonny alirudi katika umbile lake la kawaida.
Alikuwa amemletea chakula kitamu, alimkaribisha.
“Karibu chakula, najua huwezi kula chakula cha nzi ambacho ni kinyesi na uchafu kwa vile wewe bado mwanadamu.”
“Ba..ba..ba..lkis naomba u..uni..samehe,” Tonny alipiga magoti huku akitetemeka.
“Tonny sikuja kusikiliza msamaha wako, ulishaomba sana siku za nyuma, nimekuletea chakula kula niondoke.”
“Basi niue kabisa chakula hiki sili,” Tonny alionesha jeuri kwa Balkis.
“Tonny hunijui hata kuwaletea chakula kizuri ni huruma yangu, lakini mlitakiwa mle kinyesi na uchafu.”
“Nimesema sili niue kabisa,” Tonny alionesha jeuri kwa Balkis kuonesha yupo tayari kwa lolote.
“Tonny usinione nakuchekea ukaniona ni bwege mwenzio, sasa hivi nitakugeuza funza maisha yako yawe ndani ya kinyesi usiniletee upumbavu unijue eeh! Alaa,” Balkis alibadilika na kusema kwa hasira huku macho yake yakiwaka kama taa na usiku ule yalikuwa kama tochi yenye mwanga mkali.
“Ba..ba..si ni..ni..”
“Nyamaza mpumbavu mkubwa wewe, ni kiumbe gani anayeweza kuwaletea chakula na maji baada ya kutaka kumuua zaidi ya mara mbili?” Balkis alimuuliza huku amemshikia kiuno na kitumbo chake kilionekana kwa mbali.
“Na..na..te..seka Balkis harufu ni mbaya sana naomba unitafutie adhabu nyingine.”
“Huwezi kunichagulia adhabu kwa vile muda wa kubembelezana ulikwisha, hebu maliza kula nataka nimpelekee na mwenzako, muda unakwenda kukipambazuka ujue hali mpaka kesho kama saa hizi.”
Tonny hakuwa na jinsi, alikula chakula kile kilichokuwa kitamu ajabu, hakuwahi kula chakula kitamu kama kile, alikuwa akijiuliza Balkis ni kiumbe gani pamoja na ubaya waliomfanyia bado kawaletea chakula kitamu na maji. Moyoni aliamini huenda atamsamehe.
Lakini ilikuwa tofauti na alivyodhania baada ya chakula ambacho alishiba vizuri na kunywa maji matamu, alimpulizia vitu kama unga, vilipomgusa usoni palepale aligeuka hali yake ya mwanzo ya nzi.
Alitamani kuomba msamaha lakini alichelewa, alichukuliwa na kurudishwa kwenye tawi la mti na kukumbana tena na harufu kali ya uchafu wa mzoga wa mbwa aliyekuwa akinuka.
Kwa harufu ile kama angekuwa katika umbile la kibinaadamu basi angetapika mpaka utumbo. Lakini bahati nzuri alikuwa kwenye umbile la nzi, aliendelea kuteseka na harufu na baridi kali.
Balkis baada ya kutoka kwa Tonny alikwenda moja kwa moja kwa Ashura aliyekuwa amelala pembeni ya nyumba mbovu.
Karibu yake kulikuwa na mtaro wa maji machafu lakini yeye aliichagua sehemu iliyokuwa kavu. Lakini ukali wa ubaridi ulikuwa ukimpata kisawasawa.
Alijuta kwa mambo yote aliyoyafanya kwa kuwatepeli wanaume kwa ajili ya Tonny ambaye ndiye aliyemuingiza kwenye kazi ile ya kuolewa na wanaume na mwishowe kuwadhulumu kwa kuvunja uhusiano.
Kitu kilichowafanya wanaume zaidi ya wawili kujiua baada ya kufilisika na wengine kupatwa na ukichaa.
Aliamini hali ile ingemtokea na Muddy lakini kwa bahati ya ajabu Balkis aliyaokoa maisha yake. Alitamani Balkis atokee mbele yake amuombe msamaha lakini hakuonekana.
Usingizi ulimpitia pale alipokuwa amejilaza huku akichonyotwa na njaa pamoja na kiu.
Alishtuliwa kutoka usingizini na kujiona akiwa mbele ya Balkis, kama Tonny alivyotaka kuomba msamaha, naye alikuwa kama anataka kumuuma Balkis aliyemchukua na kumpeleka sehemu iliyokuwa nzuri, alimtemea mate na muda uleule alibadilika kurudia katika umbile lake la kibinadamu.
Ashura baada ya kurudi katika hali yake ya kawaida alipiga magoti mbele ya Balkis na kuanza kuomba msamaha.
“Balkis nisamehe sana nimekosa, adhabu ya leo inatosha hali yangu ni mbaya,” alisema huku akibubujikwa na machozi.
“Hii si adhabu ya siku moja ni ya muda mrefu kama nilivyokueleza muombeni Mungu nijifungue salama, kama mwanangu akifa au mimba ikitoka mjue na nyinyi maisha haya yatakuwa ya milele kwenu.”
“Naomba unisamehe, sitarudia tena, niliyokutananayo leo yanatosha, ukiongeza zaidi nitakufa.”
“Ashura sikufuata kuombwa msamaha, nimekuletea chakula, kula haraka kabla hapajakucha, ukichelewa utalala na njaa, kuonana na mimi tena ni mpaka kesho muda kama huu, tapeli mwenzako kanichelewesha na wewe unataka kufanya hivyo.”
“Nani, Tonny?”
“Eeh.”
“Yupo wapi?”
“Yupo jalalani.”
“Anafanya nini?”
“Kwani nzi makazi yake wapi?”
“Mungu wangu umemgeuza kuwa nzi?”
“Tena ana bahati angeendelea kuniletea ujeuri ningemgeuza kuwa funza na makazi yake yangekuwa kwenye kinyesi milele.”
“Sa...sa...”
“Ee...eeh! Hebu kula niondoke.”
Ashura hakuwa na jinsi alikula chakula kitamu na kuamini kama Balkis ameamua kumletea chakula ambacho hakuwahi kula katika maisha yake ya kibinaadamu, lazima atakuwa amerudiwa na roho ya huruma na kumsamehe.
Lakini dhana yake ilikuwa ni tofauti, baada ya kumaliza kula alirudishwa katika umbile lake la mbwa na kurudishwa alipotolewa na Balkis akatoweka.
****
Siku zilikatika huku adhabu ya Ashura na mwanaume wake zikiendelea, walikuwa wakiteseka kwenye maumbile yao ya mbwa na nzi. Maisha ya Tonny yalikuwa ya jalalani na chooni japo hakuweza kula uchafu.
Ashura maisha yake yote yalikuwa ni kuzurura jiji zima kutafuta sehemu iliyokuwa salama kutokana na kukimbizwa kila kukicha na watoto watukutu.
Mimba ya Balkis iliendelea vizuri na baadaye alijifungua salama salmini watoto mapacha wa kike na kiume, kila mmoja alifanana na mzazi wake mmoja.
Wa kike alifanana sana na mama yake na wa kiume alifanana na baba yake. Balkis alifurahi sana na kuamini dhamira yake ilitimia.
Aliamua kwenda chini ya bahari na wanawe kuwatambulisha kwa wazazi wake, wakati akiwa njiani kuelekea chini ya bahari.
Baba yake Mfalme Barami alikuwa na mazungumzo mazito na mkewe juu ya kukosa taarifa za Balkis.
“Mke wangu hivi huyu mtoto anataka kupimana nguvu na mimi?”
“Kwani tatizo ni nini?”
“Hulioni? Tangu nilipomueleza aachane na yule mwanaume amepotea, haleti tena vizazi vya wanawake mwaka unakatika.”
“Mume wangu jambo hili linatakiwa busara siyo kutumia nguvu.”
“Kama anaona ni utani, nitamtuma Pweku mtwana mkuu akamuulie mbali huyo mwanaume wake.”
“Mume wangu unatafuta vita mpya.”
“Na nani?”
“Siamini kama Balkis atakubali kirahisi mwanaume wake auliwe, atawamaliza watwana wako wote kwa kuwaua.”
“Inamaana sasa hivi mwanao anataka kunipanda kichwani?”
Walinyamaza kuzungumza baada ya kusikia kelele za chereko chereko nje, zilikuwa ni shamrashamra zilizowashangaza wote.
Msafara ulikuwa ukiingia ndani, ukiongozwa na vijakazi na watwana akiwemo mtwana mkuu Pweku, sherehe kama ile hutumika kukaribisha mgeni aliyezaliwa.
Balkis alionekana akiwa juu kwenye farasi mwenye matandiko ya dhahabu.
Mama yake Balkis Malkia Huleiya alipowaona watoto wa Balkis, alikimbia kwenda kumpokea mwanaye na wajukuu zake kwa furaha ya ajabu.
Mfalme Barami alikuwa amebaki njia panda, asielewe kilichokuwa kikiendelea mpaka wageni wale walipokuwa wakiingia ndani, hakujua watoto wale aliokuwanao Balkis walikuwa ni wa nani.
BAADA ya kuingia ndani, Balkis alijua amefanya makosa. Alipiga magoti mbele ya baba yake na kusema:
“Mtukufu mfalme wa bahari, najua nitakuwa nimefanya kosa kubwa la kuzaa na binadamu, lakini sikuwa na jinsi. Nimefanya hivi kutokana na moyo wangu kuwa na hofu kuu kwa Muumba wetu.
Niliamua kukaidi amri yako na kufunga ndoa na binadamu ambaye niliamini atanisaidia kupata watoto ambao ndiyo ilikuwa kiu yangu kubwa.
Pia nilijua nitaepukana na dhambi ya kuvunja ndoa za watu pia kuwanyima watu haki zao za kupata watoto. Najua nimekukosea lakini uamuzi huu niliona unafaa kwa kuamini siku ya mwisho mbele ya Muumba nitahukumiwa mwenyewe kwa vile tayari najua zuri na baya.
Hawa mbele yako ni wanangu wapendwa Zaaanuna na Labeiiki, kwa vile nimefanya kosa una haki ya kunifanya lolote, nipo radhi kwa adhabu yoyote ila nakuomba usiwaue wanangu.”
Kauli ile ilikuwa kama mshale mkali moyoni kwa Mfalme Barami.
Aligeuka bubu ghafla na kushindwa amfanye nini Balkis, mwanaye kipenzi aliyefanya kosa kubwa la kuzaa na binadamu. Lakini mke wake naye aliwahi mbele ya mume wake na kupiga magoti kumuombea msamaha mwanaye.
“Mume wangu, Balkis ndiye mtoto wetu wa pekee, kama kosa amekwishafanya. Najua amekuudhi sana lakini nakuomba umsamehe mwanao. Kama adhabu naomba unipe mimi mama yake, nipo radhi kwa adhabu yoyote lakini wajukuu zangu usiwaguse.”
“Kwa kweli hata sijui nifanye nini, basi tu kwa vile ni mwanangu lakini bila hivyo ningekuchemsha supu na kukunywa kwa jinsi nilivyochukia.”
“Najua nimekuudhi sana baba yangu lakini niliamini kuna aliye zaidi yako ambaye si mwingine bali Muumba wetu ambaye ana uwezo wa kufanya lolote bila kuingiliwa na mtu. Ni yeye ndiye mwenye adhabu kali yenye kuumiza.”
“Nimekuelewa mwanangu sina jinsi, karibu nyumbani wewe na wajukuu zangu ambao siwezi kuwafanya lolote kwa vile hawana hatia.”
“Baada ya kunisamehe naomba nimlete na mkweo mbele yenu mumtambue.”
“Kwa vile tayari una watoto wake hatuna la kufanya zaidi ya kukubali kumtambua.”
“Na hawa watoto watakuwa wa nani?” Malkia Huleiya alimuuliza Balkis.
“Ni wa kwetu wote.”
“Wataishi wapi?”
“Huku, duniani watakuja siku moja moja.”
“Kwa hiyo hata mimi nitafurahi kucheza na wajukuu zangu,” Malkia Huleiya alionesha furaha kubwa.
Ilikuwa ni furaha kubwa kusamehewa na kutambuliwa rasmi watoto wa Balkis kwa mfalme Barami.
***
Balkis baada ya kupata ruhusa ya kumpeleka mume wake kwao, alijikuta akijawa na mawazo juu ya kumweleza Muddy kuwa yeye ni jini, tena anayeishi chini ya bahari. Siku zote Muddy alijua Balkis ni binadamu wa kawaida.
Alirudi hadi duniani na kumkuta Muddy amejipumzisha sebuleni akisikiliza nyimbo laini kutokana na kuambukizwa na Balkis kupenda kusikiliza nyimbo za Bara Asia.
“Vipi mbona umerudi peke yako, watoto wapo wapi?” Muddy alimuuliza Balkis baada ya kumuona yupo peke yake.
“Nimewaacha nyumbani.”
“Mke wangu, watoto wadogo kama wale umewaacha nyumbani?”
“Nimekufuata wewe twende kwa wazazi wangu.”
“Mmh! Itakuwaje si ulisema baba yako mkali sana?”
“Ni kweli lakini kwa sasa hakuna tatizo, watoto wamemaliza kila kitu.”
“Sawa tunaweza kwenda.”
Siku zote Muddy alijua Balkis hakai nje ya Dar es Salaam, kabla ya kuondoka Balkis alijikuta akipata wakati mgumu kumueleza Muddy kuwa yeye ni jini, lakini mwenzake aliitambua hali ile mapema. Alimsogelea na kuzungumza naye kwa sauti iliyomtoa machozi Balkis.
“Nini tena malkia na kipenzi changu?”
“Muddy nina wakati mgumu wa kujieleza kwako.”
“Kujieleza nini tena mpenzi wangu?”
“Najua hunifahamu vizuri, nina imani ukinielewa unaweza kuniacha.”
“Siwezi kukuacha, hata ungekuwa jini siwezi kukuacha nakupenda sana Balkis.”
Kauli ya kusema hata kama angekuwa jini ilimshtua sana Balkis na kujiuliza anayosema ni kweli au ni kusherehesha maneno. Lakini kwa njia nyingine yalimpa nguvu ya kusema bila wasi.
“Muddy unanipenda?” alimuuliza huku akimtazama kwa jicho la mahaba.
“Zaidi ya kukupenda.”
“Nikikueleza kitu huwezi kuniacha?”
“Hata ukisema unahitaji uhai wangu, kwa mapenzi yangu mazito kwako nipo tayari na nitakufa nakupenda.”
“Kweli Muddy?”
“Kweli kabisa kwani bila wewe sasa hivi mimi ningekuwa nani?”
“Muddy mimi si binadamu.”
“Kama si mwanadamu wewe ni nani?”
“Mimi ni jini.”
“Nani?” Muddy alishtuka na kusogea nyuma toka alipokuwa amekaa, kitendo kile kilimfanya Balkis apige magoti mbele ya Muddy kuomba asimuache.
JINI LA DARAJA LA SALENDA - 28 SEHEMU YA MWISHO
ILIPOISHIA
“Muddy unanipenda?” Alimuuliza huku akimtazama kwa jicho la mahaba.
“Zaidi ya kukupenda.”
“Nikikueleza kitu huwezi kuniacha?”
“Hata ukisema unahitaji uhai wangu, kwa mapenzi yangu mazito kwako nipo tayari na nitakufa nikikupenda.”
“Kweli Muddy?”
“Kweli kabisa, kwani bila ya wewe sasa hivi mimi ningekuwa nani?”
“Muddy mimi si mwanadamu.”
“Kama si mwanadamu ni nani?”
“Mimi ni jini.”
“Nani?” Muddy alishtuka na kusogea nyuma kutoka alipokuwa amekaa, kitendo kile kilimfanya Balkis apige magoti mbele ya Muddy na kumuomba asimuache. SASA ENDELEA...
“Muddy usiniache
nakupenda sana.”
“Balkis unayosema ni kweli?”
“Kweli mpenzi wangu mimi ni jini la chini ya bahari na baba yangu ni mfalme wa majini katika bahari hiyo. Kukubali kuwa na mimi umeokoa vizazi vya wanawake mia ambavyo nilitakiwa nivitoe ili nipate dawa ya uzazi na kuniwezesha kuolewa na jini mwenzangu.”
“Balkis unayosema ni kweli?”
“Ni kweli kabisa.”
“Kwa nini hukunieleza mapema?”
“Ujini wangu ndiyo uliokoa maisha yako na hata kuendelea kukulinda na akina Ashura waliokuwa wakiendelea kuyafuatilia maisha yetu.”
“Balkis japo moyo wangu umeshtuka kusikia wewe ni jini lakini bado nitaendelea kukupenda maisha yangu yote. Sikuwahi kuamini kama jini ana roho nzuri kuliko mwanadamu, niliamini majini ni wabaya na kama ungenieleza mwanzo ningeachana na wewe.
Nakuahidi kwenda mbele ya wazazi wako kujitambulisha na kuwa tayari kuishi na wewe.”
Kauli hiyo ilimfanya Balkis alie machozi ya furaha na kumkumbatia Muddy.
“Asante Muddy kwa kuonesha mapenzi ya kweli, nitakupenda milele.”
“Nikushukuru wewe kuonesha mapenzi ya kweli kwangu pia, kulinda maisha yangu kwa nguvu zote.”
“Muddy niwafanye nini akina Ashura waliopanga kukuua na kuniua mimi?”
“Kwani bado wanatufuatilia?”
“Walikuwa wanataka kuniua nikawawahi na kuwageuza mbwa na nzi ili niweze kujifungua salama.”
“Kwa hiyo mpaka sasa bado wapo katika hali hiyo?” Muddy alishtuka.
“Ndiyo.”
“Wewe ulitaka kuwafanya nini?”
“Lolote utakaloliamua wewe nipo tayari kulifanya kwa vile umeusikia ubaya wao.”
“Naomba uwasamehe.”
“Kwa kuwa umesema wewe nitawasamehe.”
Naomba kabla ya kwenda kuwaona wazazi wako wawe wamerudi katika hali yao ya zamani.”
Baada ya makubaliano, Balkis alitoka na kurudi na mbwa na nzi aliyekuwa juu ya mgongo wa mbwa na kusema:
“Hawa ndiyo maadui zetu.”
Muddy hakuamini kuwaona mbwa na nzi na kuelezwa kuwa ni Ashura na mwanaume wake. Balkis aliwatemea mate wote wakarudi katika hali yao ya kawaida ya kibinaadamu.
“Mna bahati kubwa kwa kuwa mpenzi wangu amewasamehe, japo hata mimi nilikuwa na wazo la kuwasamehe, nashukuru Mungu nimejifungua salama. Kuanzia leo nina imani kwa adhabu ndogo ambayo hailingani na dhamira yenu ya kuniua kwa kipindi cha mateso imetosha kuwafanyeni viumbe wapya. Naomba mkaendelee na maisha yenu.”
“Asante Balkis, asante Muddy, tunaapa kwa mbigu na ardhi kuwa hatutathubutu hata kuua nzi, mateso tuliyoyapata yametosha. hatukufa lakini cha moto tumekiona.”
“Nakutakieni maisha mapya nina imani mtakuwa viongozi wema na kuwaeleza watu kuwa ubaya haulipi na jini si mbaya ila roho mbaya ya kiumbe chochote ndiyo mbaya.”
Ashura na mwanaume wake walirudi kwao na kukuta kila kitu chao kikiwa katika hali ya usalama. Balkis naye alikwenda mpaka chini ya bahari kumtambulisha mumewe Muddy. Ilikuwa sherehe kubwa ambayo haikuwahi kutokea chini ya bahari iliyobadilisha amri ya jini kuolewa na mwanadamu.
Pia, Balkis alichukua nafasi ile kuwarudishia vizazi vyao wanawake wote ambao baada ya kusumbuka sana kutafuta watoto, wote walifanikiwa kupata watoto bila kujua kuwa kitendo cha Muddy kumkubali Balkis ndiyo ilikuwa tiba yao.
Baada ya hapo maisha ya Muddy na Balkis yaliendelea bila watu kujua kama Balkis ni jini zaidi ya Ashura na mwanaume wake. Muddy na Balkis kila mmoja alimpenda mwenzake mapenzi ya dhati.
MWISHO
Post a Comment