ad

ad

JINI LA DARAJA LA SALENDA - 25 & 26 ZIPO HAPA




JINI LA DARAJA LA SALENDA - 25

ILIPOISHIA:
“Amefanya nini?” aliuliza kwa mshtuko.
“Hatujui malkia mtukufu,” walijibu kwa pamoja.
“Mmemkuta wapi?”
“Lango kuu malkia mtukufu.”

“Mpelekeni chumbani mara moja.”
Walimbeba na kumpeleka chumbani na kumlaza kitandani, baadaye walitoka. Malkia Huleiya alichanganyikiwa na kujiuliza mwanaye kafanywa nini na wanadamu. Alijua ile itakuwa vita na wanadamu ambao ni viumbe hatari aliokuwa akiwaogopa usiku kucha. SASA ENDELEA...

ALITAKA kwenda kumwita mumewe Mfalme Barami aliyekuwa kwenye kikao na baraza lake la mawaziri lakini alipata wazo la kumfuata mganga mkuu Bunusa ili akaangalie hali ya Balkis. Alimtuma mtwana kumfuata mganga mkuu Bunusa.
Bunusa alifika mara moja na kupelekwa chumba alichokuwa amelazwa Balkis ambaye muda wote alikuwa amepoteza fahamu.
“Bunusa naomba msaada wako hali ya mwanangu ni mbaya sana.”

“Hakuna tatizo,” Bunusa alisema huku akifungua mkoba wenye vitendea kazi.
Alimshika Balkis kichwani, kifuani, tumboni na miguuni kisha alimshika kwenye paji la uso na kutulia kwa muda akipata ripoti za uchunguzi wa mwili wake. Baada ya muda alipumua pumzi nyingi kuonesha kuna jambo. Malkia Huleiya akimfuatilia kutaka kujua vipimo vile vina majibu gani.

Baada ya kuvuta pumzi ndefu alimgeukia Malkia Huleiya na kumwambia:
“Balkis haumwi ugonjwa wa kutisha ni hali ya kawaida.”
“Bunusa, Balkis hajatokewa na hali hii toka nilipomzaa, leo atokewe na tukio la kutisha useme hana ugonjwa wa kutisha?”

“Nimesema hali aliyonayo si ugonjwa, ila tatizo kubwa ni uchovu, inaoneka kafanya kazi kwa mwezi mzima bila kupumzika. Kutokana na hali aliyokuwa nayo lazima hali hii imtokee.”
“Hali! Hali gani hiyo?”
“Ya ujauzito.”

“Unasema ana nini?”
“Ana ujauzito ambao hakujua kama anao na ndiyo uliomfanya kuchoka baada ya kufanya kazi nzito.”
“Mungu wangu ujauzito wa nani, wa jini au mwanadamu?” Malkia Huleiya aliuliza huku akiweka mkono wake kifuani kuzuia mshtuko.
“Wa mwanadamu.”

“Ooh! Mbona mwana huyu amenitafutia matatizo, baba yake nitamweleza nini anielewe.”
“Ni kweli hili ni tatizo inaonesha taarifa hizi za kupata ujauzito wa mwanadamu zitakuwa na mpasuko mkubwa ndani ya familia.”
“Sasa nitafanya nini? Tuutoe kabla baba yake hajajua?”

“Mmh! Katika kosa lingine kubwa mtakalofanya ni kuutoa ujauzito huu, nia kubwa ya mwanao ni kubeba ujauzito na kuzaa na mwanadamu kisha arudi kwa baba yake kwa kuamini hatakuwa na jinsi tena ya kuzuia matakwa yake.”
“Ooh! Sasa Bunusa utanisaidia kitu gani ili kutoleta mtafaruku mkubwa.”
“Dawa ni kumrudisha duniani ili aendelee na maisha yake na mumeo asijue chochote.”
“Tutafanyaje?”

“Nitampa dawa ya kumrudisha katika hali yake kisha arudi duniani kuendelea na maisha yake.”
“Lakini watwana na vijakazi wanajua alikuja, si watamwambia?”
“Hao ni wa kuwaita na kuwaeleza wasizungumze chochote kuhusiana na Balkis na kutoa vitisho vikali.”
“Sawa nitafanya hivyo.”
Mganga mkuu Bunusa alianza kumshughulikia Balkis kwa kumnusisha dawa iliyomfanya apige chafya na kuzinduka. Balkis alijishangaa kuwa mbele ya mama yake na mganga mkuu Bunusa.

“Mama,” alimwita kwa sauti ya chini.
“Abee mwanangu, unaendeleaje?”
“Sijambo kidogo, baba yupo wapi?”
“Yupo kwenye baraza na mawaziri wake.”

“Mmh! Siamini kama nipo salama, asante Bunusa nilijua ndiyo basi.”
“Ndiyo basi kwa vipi?” Malkia Huleiya alimuuliza mwanaye.
“Nilijua mganga niliyemuulia mke wake kaamua kunimaliza.”
“Ni kweli alikuwa na wazo la kukumaliza lakini kiburi chako ndicho kilichokusaidia,” mganga Bunusa alisema.
“Ni kweli alinitumia kombora?”

“Walaa.”
“Sasa nini kile?”
“Ni kizunguzungu kikali, inaonesha umefanya kazi ngumu bila kupumzika na kusababisha uchoke sana.”
“Mmh! Mbona kazi hiyo ni ndogo, nimekwishafanya nyingi zaidi ya hizo bila matatizo.”
“Ni kweli, lakini sasa hali yako haikuruhusu kuusumbua mwili kwa muda mrefu.”
“Hali! Hali gani?”

“Ya ujauzito.”
“Ujauzito?” Balkis alishtuka huku akishika mikono kifuani kwake.
“Eeh, vipi hukuutegemea?” Bunusa alimuuliza.
Swali lile ambalo lilikuwa zito kulijibu mbele ya mama yake, Malkia Huleiya alimgeukia mwanaye aliyekuwa bado amekaa kitandani.

“Balkis.”
“Abee mama.”
“Kwa nini umefanya hivi?”
“Mama sina jibu lakini ndivyo nilivyoamua.”
“Na vizazi vya wanawake unavyoleta vitakuwa na kazi gani?”
“Kama kweli nina ujauzito kazi hiyo itakuwa imeishia hapa, siwezi kupata dhambi kila kukicha kisa niolewe na jini mwenzangu.
Majini wangapi wanaishi na wanadamu maisha ya furaha, itakuwa mimi!”
“Lakini kumbuka baba yako akijua una ujauzito wa mwanadamu utafia chumba cha giza.”
“Na wewe mama utakubali?”
“Japo siwezi kukubali lakini kumbuka kauli ya mwisho ni ya baba yako, vile vile anaweza kutufungia wote kwenye chumba cha giza.”
“Kwani anajua nina ujauzito?”
“Hajajua lolote, hata ujio wako hatutaki ajue. Si unajua bado una kesi ya kuachana na mwanadamu.”
“Ni kweli, lakini nikitoka hapa nitarudi na mtoto.”
“Ila nakuomba acha kuingia katika vita na wanadamu ili upate muda wa kupumzika ulee mimba yako, bila hivyo itatoka na kukufanya usizae tena hata ukitumia dawa za kijini,” Bunusa alimshauri Balkis.

“Kabla ya kupumzika lazima niwape adhabu ambayo itakuwa fundisho kwao.”
“Kweli mwanangu wamekuudhi, pamoja na huruma yako umeshindwa kuwasamehe? Kweli wamekuudhi,” mama yake naye alichangia.

“Niwasamehe watu waliopanga leo kunibakiza jina, wale watu wabaya sana,  lazima niwatie adabu.”
“Basi ondoka ili uwahi kabla baba yako hajamaliza kikao, naona huu ndiyo muda wao wa kumaliza.”
Balkis alimuaga mama yake na mganga mkuu Bunusa kisha akarudi zake duniani.

***
Baada ya Balkis kuondoka, ghafla Ashura na mwanaume wake walishindwa kuelewa nini kinaendelea. Walibaki wamepiga magoti wakisubiri hukumu yao.
Muda nao ulikwenda bila kuonekana Balkis. Kutokana na woga wa kumuudhi Balkis waliendelea kupiga magoti mpaka giza lilipoingia.

“Tonny sasa itakuwaje?” Ashura alimuuliza mwanaume wake baada ya kuhisi miguu imekufa ganzi kwa kupiga magoti kwa muda mrefu.

“Hata sijui atakuwa amekwenda wapi.”
“Sasa tutateseka hivi mpaka saa ngapi?”
“Lakini sisi ndiyo tuliolazimisha kupiga magoti!” Tonny alikumbuka.
“Kwa hiyo tunyanyuke?”
“Mmh! Hata sijui tufanye nini.”
“Tutaendelea kukaa hivi mpaka saa ngapi? Bora tunyanyuke tukae ili tusubiri atakachotufanya kwani hatuna jinsi,” walijikatia tamaa ya maisha kwa kuamini adhabu watakayopewa ni kubwa sana.

Ashura na mwanaume wake walinyanyuka walipokuwa wamepiga magoti na kukaa kwenye kochi kusubiri hukumu ya Balkis.
Walikaa huku wakiendelea kumuomba Mungu awaepushe na kikombe kile cha adhabu ya Balkis. Usiku uliwachwea wakiwa wamekaa kwa kuogopa kuwa wakinyanyuka wanaweza kuongeza hasira za Balkis.

Siku ya pili iliingia wakiwa wamekaa kwenye kochi bila kumuona wala kusikia sauti yake. Tonny kwa kujitoa muhanga alimwambia  Ashura:
“Shuuna sasa tutakaa hivi mpaka lini? Kwa nini tusinyanyuke tuendelee na mambo yetu? Litakalotokea hatuna jinsi.”
“Mmh! Kwa nini tusisubiri, huenda ametutega ili aone tutafanya nini,” Ashura alikuwa na hofu ya kuzidi kumuudhi Balkis.

“Sasa tutakaa mpaka lini hebu angalia toka jana hatujala wala kunywa chochote, kama kosa tumetenda na hayupo tayari kutusamehe tutafanya nini?”
Walikubaliana kuendelea na kazi huku wakisubiri chochote watakachofanyiwa na Balkis ambaye muda wote hakuonekana.
Kutokana na uchovu wa usiku na mchana, baada ya kuoga hawakuwa hata na hamu ya chakula, walipanda kitandani na usingizi mzito uliwashika.

Waliamka jioni wakiwa wamechoka, baada ya chakula cha usiku walirudi kulala huku wakisubiri adhabu ya Balkis bila mafanikio.
Siku ile pia ilikatika bila Balkis kuonekana, waliamua kufanya mambo yao kama kawaida huku wakiapa kutomfuatilia tena Balkis na kuamua kuishi maisha yao ya kawaida.
  ***
Balkis baada kurudi kutoka chini ya maji alikuwa na furaha isiyo na kifani baada ya kugundua dhamira yake ya kubeba ujauzito wa mwanadamu imetimia.
Alimkuta Muddy akiwa amejilaza kitandani, alipofika alimkumbatia na kumbusu kama ilivyokuwa  kawaida yake kila alipoondoka na kurudi baada ya siku moja bila kuonana.
LAKINI siku ile furaha iliongezeka mara mbili kitu kilichomshtua Muddy.
“Vipi mpenzi kulikoni mbona una furaha sana?”
“Muddy niambie zawadi yoyote unayoitaka kwangu nikupe.”
“Ya upendo.”

“Muddy ya kitu kingine kwani hakuna kiumbe nitakayempenda chini ya jua kama wewe.”
“Sihitaji zawadi zaidi ya hiyo.”
“Basi mimi nakuchagulia zawadi ya kuyafanya maisha yako yawe kama ya peponi hata kama sipo.”
“Ina maana unataka kuniacha?’

“Hapana mpenzi ni tahadhari tu, mimi ni kiumbe siwezi kuishi milele.”
“Nashukuru kwa hilo.”
“Nikwambie kitu?”
“Niambie.”

“Nina ujauzito wako.”
“Utani huo!” Muddy alishtuka kusikia vile.
“Ndiyo maana nimejawa na furaha isiyo na kifani na nikifanikiwa kujifungua salama nitakupa zawadi kubwa sana isiyo na mfano.”

Balkis alimkumbatia Muddy kwa furaha huku akiomba ajifungue haraka kabla baba yake mfalme Barami hajatimiza dhamira yake ya kuvunja mpango wa uhusiano wake na Muddy ili aolewe na jini mwenzake.
   ****
Balkis baada ya kupata habari njema za kupata ujauzito wa Muddy, alikuwa mwenye furaha kupita kiasi. Lakini aliamini furaha yake ingekamilika baada kuwakomesha wabaya wake. Adhabu aliyoipanga ingemfanya aishi kwa furaha mpaka muda wa kujifungua lakini hakutaka kuwaua.

Wakati akipanga adhabu ya kuwapa Ashura na mwanaume wake, upande wa pili ulishangaa kuona siku zikikatika bila kusikia chochote kutoka kwa Balkis. Waliamua kufanya kazi zao kama kawaida huku wakiachana kabisa na Balkis.
Ashura akiwa katikati ya mji akiendelea na mambo yake ya ununuzi wa vitu muhimu kwa ajili ya matumizi ya nyumbani. Balkis naye alikuwa karibu yake bila mtu yeyote kumuona. Alipomkaribia aliokota udongo kidogo kisha alimpulizia mwilini.

Ashura akiwa amebeba mfuko mkubwa akielekea kwenye gari alihisi kama kuna vitu vinamuwasha mwilini. Ilibidi aweke mzigo chini ili ajikune kwanza, kila muda ulivyozidi kwenda ndivyo alivyohisi  nguo zake zikimuwasha kama vile zimemwagiwa upupu.

Alianza kuvua nguo huku akipiga kelele  za kuwashwa, kila mtu alishtuka na kumshangaa kumuona mwanamke akivua nguo zote na kubakia mtupu. Wasamaria wema walimsogelea na kumvisha lakini alizikataa nguo zake na kusema zinamuwasha.

Ilikuwa ni kihoja Ashura aliadhirika mbele ya watu, kila alipopewa nguo na kinamama  waliokuwa wameshikwa na mshangao kumuona mrembo kama yule akionekana amepandwa na mapepo. Ashura aliondoka pale na kuanza kutembea bila ya kuwa na kitu mwilini, alielekea baharini.

Ilikuwa ni adhabu aliyokubaliana na Balkis kama atamfuata Muddy aliyekuwa mumewe wa zamani. Baada ya kuridhika na adhabu yake alimtokea kwa mbele akiwa na upande wa kanga. Ashura alipomuona alipiga magoti kumuomba msamaha.
“Balkis najua jinsi gani tulivyokukosea lakini sasa hivi tumeachana na wewe, naomba utusamehe.”
“Adhabu ya kutembea uchi nani aliichagua?”

“Mimi.”
“Sasa mbona hukutaka kutembea uchi baada ya kujua kabisa dhamira yako ilikuwa nini juu ya Muddy?”
“Nisamehe Balkis.”
“Balkis unayemuomba akusamehe angefariki ungemuomba nani msamaha?”

“Najua tulikuwa na dhamira mbaya kwako lakini tumegundua makosa yetu tunakuahidi hatutakufuata tena.”
“Nilikuonyeni mara ngapi, kama ningekuwa na roho mbaya hata mali ya Muddy usingechukua. Lakini nilifanya vile ili muachane na mpenzi wangu, bado hamkusikia mliendelea kunichokonoa, kuonesha sitaki kuwafanya lolote nilimuua mganga wenu lakini bado mliendelea kunitafuta.

“Mzee Njiwa Manga alitukutanisha mbele yake na kukuonyeni lakini bado mliona labda utani na kufikia hatua ya kumdharau kuwa hana uwezo wa kukabiliana na mimi. Mkaamua kwenda kwa mganga mwingine kwa lengo la kuchukua mali yangu na kunimalizia. Hebu nieleze ni kiumbe gani mwenye moyo wa uvumilivu wa kiasi hicho?”
“Hakuna.”

“Basi adhabu yangu ya awali ya kukutembeza uchi baada ya wewe mwenyewe kutamka kwa mdomo wako imetimia kama utamfuata Muddy. Ya pili nitakugeuza mbwa atakayeishi kwa mateso mpaka hapo nitakapojifungua salama. Kama mwanangu akifariki na wewe na mumeo mtakufa.”

“Ni...ni...ni..sa...sa...,” hakumaliza kusema alitemewa mate usoni na Balkis huku akisema:
“Kuwa mbwa mweusi.”
Ashura aligeuka mbwa mweusi, Balkis aliendelea kusema:
Kazi imeanza Ashura ameshageuzwa mbwa.
 Je, mpenzi wake atapata adhabu gani? Kuyajua yote tukutane

JINI LA DARAJA LA SALENDA -  26

ILIPOISHIA;
Ya pili nitakugeuza mbwa atakayeishi kwa mateso mpaka hapo nitakapojifungua salama.
Kama mwanangu akifariki na wewe na mumeo mtakufa.”

“Ni..ni..ni..sa..sa..,” hakumaliza kusema alitemewa mate usoni na Balkis huku akisema:
“Kuwa mbwa mweusi.”

Ashura aligeuka mbwa mweusi, Balkis aliendelea kusema:
SASA ENDELEA...

“Hii ni adhabu itakayokufanya uhangaike, hutapendwa na wanadamu mpaka hapo utakapotoka kifungoni na sasa namfuata mwanaume wako, naye ana adhabu kubwa kuliko hii.”

Balkis baada ya kusema vile aliondoka na kumuacha Ashura kwenye umbile la mbwa asijue aende wapi. Wazo lilikuwa kuendelea kuwa pale ufukweni mpaka jioni ndiyo aende kwake.  

Nyumbani, Tonny alikuwa akijiandaa kwenda kwenye mihangaiko yake akiamini kabisa Balkis aliamua kuwasamehe.
Alikuwa anakwenda kwenye kabati kuchukua glasi ili anywe juisi kabla ya kuondoka.
Hakujua kama Balkis tayari yumo mle ndani na alikuwa na hasira za ajabu baada ya kujua Tonny ndiye aliyekuwa na kimbelembele wa kumuua.

Wakati anakwenda kwenye kabati alimpulizia vitu kama matone ya maji, Tonny alishtuka lakini hakujali sana. Alipokaribia kwenye kabati alishtuka kujiona amegeuka kiumbe wa ajabu.
Kilichomshangaza ilikuwa ni kujiona kwenye kioo mwili wake ukiwa umeota mizizi na kutoka damu.
Tonny alishtuka na kujiangalia, akawa anashangaa kuuona mwili wake ukiota mizizi iliyoingia ardhini huku ukitoa damu.
Alianza kusikia maumivu makali zaidi ya mtu aliyeng’olewa jino bila ganzi.
Alijiuliza yale mateso makali yanatokana na nini na kwa nini aote mizizi mwilini kama mti lakini hakupata jibu.

Balkis alimwacha apate mateso makali kwa kuongeza kumpulizia maji maji mwilini na kuufanya mwili wa Tonny utoe ufa, kila sehemu ya mwili ilipasuka, damu zilimtoka na maumivu yake yalikuwa makali sana.
Kila alipopiga kelele kuomba msaada sauti yake haikutoka.

Alitamani ardhi ipasuke ili immeze lakini haikuwezekana.
Alishangaa kuona damu yake iliyokuwa ikitoka mwilini, kila ilipondondoka chini ilipotea, akajiuliza inakwenda wapi lakini hakupata majibu.
Maumivu aliyoyasikia hakukuwa na mfano wake. Alilia mpaka machozi yalimkauka kutokana na maumivu kuongezeka ukali kila dakika kutokana na mwili wake kupasuka kila kona.

Balkis alitoa adhabu ile kwa zaidi ya saa mbili kisha alijitokeza mbele yake, Tonny alipomuona alishtuka na kutamani kumlamba miguu lakini hakuweza kutembea baada ya sehemu ya mwili wake kuzama chini ya ardhi.
Kila alipofumbua mdomo kuomba msamaha sauti haikutoka akawa anarusha mikono kama anaimbisha kwaya bila ujumbe wake kumfikia mlengwa.

Balkis alisimama na kumtazama kwa hasira, mara machozi ya damu yalimtoka akifikiria ampe adhabu gani kubwa kuliko zote alizowahi kumpatia kiumbe aliyemchukiza.
Alitamani kumchuna ngozi na kumwacha atembee na maumivu bila kufa lakini alikumbuka adhabu ya kupasua pasua mwili ilikuwa inatosha kwani maumivu yake yalitofautiana kidogo na mtu aliyechunwa ngozi bila ganzi.
Tonny aliendelea kurusha mikono kuomba msaada kama mtu aliyekuwa anataka kukata roho.

Aliusikia mwili wake ukiwa umekauka kama kipande cha kuni kilichopigwa na jua kwa muda mrefu.
Ulimi nao ulikauka kama mti na kushindwa hata kuunyanyua.
Yalikuwa mateso makali kuliko hata shetani motoni, moyoni Tonny alijiapia kama atatoka salama kwenye mateso yale mazito asingerudia tena kufanya makosa.
Aliona kuokoka kwake ni sawa na ngamia kupita katika tundu la sindano.

Balkis alijikuta akiingiwa na huruma, alisogea karibu na kumshika kichwani.
Dakika ileile Tonny alirudi katika hali ya kawaida lakini bado mwili wake ulimuuma kama kidonda.
Tonny alipiga magoti mbele ya Balkis kuomba msamaha.

“Najua tumekukosea, lakini nakuahidi hatutafanya upumbavu mwingine, tupo chini ya miguu yako, tunaomba utusamehe.”

“Sawa mmekosa, hebu nielezeni kosa langu kwenu ni nini?”
“Huna kosa lolote.”

“Kwa nini mlidhamiria kuniua?”

“Tusamehe Balkis ni shetani mbaya tu alitupitia.”

“Leo unaniomba msamaha, ningekufa ungemuomba nani?”

“Najua tumekukosea kwa kiasi kikubwa.”

“Labda mlikuwa mnaona natania, mwenzako nimempa adhabu ya kutembea uchi mbele za watu muda si mrefu.”
“Ha!” Tonny alishtuka kusikia vile.
“Unashtuka nini, si alisema mbele yako akimrudia Muddy atafanya nini?”
“Atatembea uchi.”
“Mbona kamfuata mume wangu kupitia waganga.”
“Nilikuwa sijui.”
“Utajuaje na roho yako imejaa tamaa na harufu ya damu za viumbe wasio na hatia?”
“Ni kweli nilikuwa na roho mbaya lakini nimeujua ubaya wangu, nitajirekebisha.”
“Kama nilivyokueleza Ashura amevua nguo mbele za watu na kupata aibu ya mwaka.”
“Mungu wangu yupo wapi?”
“Atakuja usiku kwa njia ya kujifichaficha.”
“Kwa hiyo nguo kavua kwa hiyari yake?”
“Kwani wewe adhabu uliyoipata umeipenda?”
“Hata.”
“Au nikuongeze?”
“U...u...usifanye hivyo ni...ni...”
“Baada ya tapeli mwenzako kuvua nguo mbele za watu, na kumpa adhabu ndogo aliyoichagua mwenyewe pia nimempa adhabu yangu atakayotesekanayo kwa muda mrefu.”
“Ungemsamehe nina imani hawezi kurudia tena,” Tonny alimuonea huruma Ashura na kujisahau yeye.
“Kwa sasa sitawasamehe lazima nitimize kile nilichokipanga kuwafanyia.”
“Usituue Balkis.”
“Niliapa kamwe sitawaua ili kizazi chenu kijue madhara ya ubaya ni nini?”
“Sasa utatufanya nini?”
“Mpenzio tayari nimeshamgeuza kuwa mbwa.”
“Mungu wangu!”
“Na wewe kama nilivyokueleza nitakugeuza kuwa nzi wa kijana, maisha yako yatakuwa jalalani na chooni hakuna mwanadamu atakayekupenda.”
“Jamani si nitakufa?”
“Hutakufa, hayo ndiyo maisha niliyowachagulia baada ya kuwabembeleza kwa muda mrefu, Lakini mmekuwa na viburi pamoja na kuwatisheni bado mkawa na masikio magumu kama kenge, nina imani adhabu ya leo itakuonesha mimi ni kiumbe wa aina gani.

Kwa vile sitaki dhambi ya kuua na kisasi ni haki ya kila kiumbe, nilichokuchagulia ndicho saizi yako.”
“Balkis naomba uni...sa...sa... “ 
Bwana wa Ashura hakumalizia kuomba msamaha alipuliziwa kitu kama unga huku Balkis akisema:
“Kuanzia leo utakuwa nzi wa chooni.”

Muda uleule Tonny aligeuka kuwa nzi wa kijani, ghafla mazingira ya pale nayo yakabadilika na kumfanya Tonny kuruka na kwenda moja kwa moja jalalani.
Alijikuta akiishi maisha mapya ambayo yalimlazimisha kuishi chooni na kwenye majalala.

 Tonny pamoja na kuishi kwenye harufu kali ya mizoga na kinyesi hakuwa na jinsi kwa kuamini kuwa maeneo yale ndiyo yaliyokuwa salama kwake kwa kuogopa kuuawa na mwanadamu pale atakapokwenda ndani mwake kwa kuamini kuwa yeye ni binaadamu.

Balkis baada ya kutoa adhabu ile alirudi kuilea mimba yake kwa kuamini kuwa hakukuwa tena na mwanadamu atakayemfuatilia maisha yake.
Balkis alikuwa akiyafurahia maisha yake na  Muddy kwa kuamini muda si mrefu wataitwa baba na mama.

Baada ya kiza kuingia, Ashura aliondoka ufukweni na kurudi nyumbani akiwa katika umbile lake la mbwa.

Alitembea huku akiomba Mungu afike salama nyumbani kwake, moyoni akijiuliza Tonny atamuelewa kutokana na umbile lake jipya alilokuwa nalo, alifikiria hivyo bila ya kujua kwamba mpenzi wake naye maisha yake yalikwishabadilika na kuwa kiumbe cha jalalani na chooni baada ya kugeuzwa kuwa nzi.

Hakutembea umbali mrefu mvua kubwa ilianza kunyesha, alikimbilia kwenye nyumba moja iliyokuwa njiani na kujibanza upenuni.

Mwenye nyumba alitoka na kumfukuza akiamini ni mbwa.
Kutokana na mvua kuwa kubwa na barabara kujaa maji, Ashura alijitahidi kumwambia yule mwanadamu kuwa yeye si mbwa bali ni mwanadamu.

Sauti yake ilikuwa ni ya mbwa kwa kuwa aliitoa kwa kubweka, tu hicho kilizidi kumuuzi mwenye nyumba ambaye aliingia ndani na kutoka na bakora na kumtoa mbio.
Ashura hakuwa na jinsi ilibidi aingie kwenye mvua iliyokuwa ikiendelea kunyesha huku akiogelea kwenye maji machafu yaliyokuwa yakitoka kwenye mitaro.

Aliendelea kunyeshewa na mvua kubwa iliyoambatana na radi, kuna kipindi alizama ndani ya maji na kujitahidi kuogelea ili kuendelea na safari yake.

Hata alipopata sehemu ya kujibanza bado hakuona umuhimu wa kufanya hivyo kutokana na kusikia baridi kali mwilini mwake iliyotokana na kulowana kwa mvua.

Aliendelea na safari yake yenye mateso  huku akitaka amkute Tonny nyumbani na kuomba amtambue na kukubali kuishi naye kwenye umbile lile la mbwa.



No comments

Powered by Blogger.