JINI LA DARAJA LA SALENDA - 24

ILIPOISHIA;
Mara alisikia sauti za vilio vya mashoga wa mkewe ambao walikuwa wakizungumza nao. Vilio vile vilizidi kumtisha na kumchanganya.
“Jamani kuna nini?” aliuliza tena macho yakiwa yamemtoka pima.
SASA ENDELEA...
“Sauda,” walisema mashoga zake waliokuwa wakilia huku mikono ikiwa kichwani, wengine hata nguo ziliwaanguka bila kujua.
“Sauda kafanya nini?”
“Ame...”
“Amefanya nini mbona mnanichanganya, mke wangu kafanya nini jamani?” mganga alijikuta kwenye mtihani mzito wa kujua mkewe amefanya nini kwani muda mfupi uliopita alimtuma dukani.
Mara aliingia mwanamke mwingine aliyekuwa akilia huku akisema:
“Haiwezekani Sauda atutoke kirahisi namna hii.”
“Huu lazima uchawi haiwezekani njiwa amgonge afe,” mwingine alisema huku akijitupa chini kwa uchungu.
“Jamani mke wangu kafanya nini?” pamoja na kuwasikia wakisema lakini hakuwaelewa.
Mara watu waliingia na mwili wa mkewe ambaye alikuwa amekwishapoteza uhai.
\“Ha! Amefanya nini?” Kakakuona alitaharuki.
Alimvamia mkewe ambaye alikuwa amefunikwa kanga, akamfunua na kumwinamia! Hakuamini alichokiona mbele yake.
“Sauda mke wangu umepatwa na nini? Kwa nini nilikutuma kwenda kuchukua dawa? Kwa nini nilikuwa na wazo baya? Maskini mke wangu nimekuponza, ulikuwa ukizungumza na wanawake wenzako, ona sasa umebadilika jina na kuitwa marehemu! Nini faida ya kazi yangu?” Mganga alilia kama mtoto mdogo huku akimgeuza mkewe ambaye alikuwa ameanza kupoa.
Ashura na mwanaume wake nao walikuwa wametoka na kushuhudia tukio lile. Balkis naye hakuwa mbali, moyo ulimuuma kwa kitendo chake cha kuyachukua maisha ya kiumbe kisicho na hatia.
Machozi ya damu yalimtoka.
Kila mganga alipokuwa anamlilia mkewe kwa maneno ya uchungu na yeye ndivyo alivyokuwa akiumia na kulia zaidi.
Ashura alipoangalia pembeni alishtuka baada ya kumuona Balkis akiwa katika kundi la watu huku naye machozi yakimtoka. Baada ya kumuona alipatwa na mshtuko mkubwa, akaanguka na kupoteza fahamu. Hali ile iliwatisha watu wote waliokuwa pale.
Mganga alimwacha mkewe na kukimbilia ndani kuchukua dawa ya unga kwa ajili ya kuzuia nguvu zozote mbaya.
Aliimwaga hewani lakini Balkis aliwahi kuondoka eneo lile na kwenda kukaa njiani kuwasubiri Ashura na mwanaume wake. Mganga baada ya kufanya vile bado hakuamini, aliuchukua mwili wa mkewe na kuuingiza ndani kujaribu tiba zote anazozijua akiamini atafanikiwa kumrudisha mkewe.
Alikuwa amesahau kuwa hakuna mtu wala kiumbe chochote dunia chenye uwezo wa kurudisha roho ya mtu au kiumbe zaidi ya Muumba peke yake.
Licha ya kuhangaika zaidi ya saa nzima kurudisha roho ya mkewe iliyopotea, bado hakufanikiwa.
Hatimaye alikubaliana na ukweli kwamba mkewe amefariki.
Ilibidi atoe taarifa za kifo cha mkewe kwa ndugu na jamaa, mipango ya mazishi ikaanza. Kutokana na kuchanganyikiwa na kifo cha mkewe alisahau hata kama kuna wateja aliokuwa akiwashughulikia.
Ashura baada ya kupata nafuu alijikuta akichanganyikiwa kwa kuamini kabisa kifo cha mke wa mganga kimefanywa na Balkis. Wasiwasi ulizidi kumpanda na kujiuliza kama ni yeye basi hata maisha yao yalikuwa hatarini.
“Tonny nimemuona Balkis?”
“Wapi?”
“Alikuwa kwenye kundi la watu.”
“Mwongo!”
“Kweli! Tena alikuwa analia machozi ya damu.”
“Mungu wangu! Unataka kuniambia aliyefanya haya ni yeye?”
“Inawezekana kabisa, si unakumbuka kauli aliyotoa kwa mzee Njiwa Manga kuwa kama angetusaidia angemuua mjukuu wake.”
“Sasa unafikiria anaweza kutufanyia kitu kibaya?”
“Hata mimi nimechanganyikiwa.”
“Sasa mganga atatusaidia nini?” Tonny aliuliza huku mapigo ya moyo yakimwenda kwa kasi.
“Wee! Tena nyamaza, inavyonekana sisi ndiyo chanzo cha kifo cha mkewe.”
“Kwa hiyo unaniambia nini?”
“Tuondoke, ikiwezekana tusirudi tena na Balkis tuachane naye,” Ashura alisema huku akitetemeka.
Wakati huo watu walizidi kusogea eneo la tukio, kila mtu alikuwa akisema lake juu ya kifo cha ghafla cha mke wa Kakakuona.
Wapo walioelezea jinsi walivyomuona njiwa yule akimpiga kichwani mke wa mganga na kutoweka kisha kuanguka chini na kupoteza uhai.
“Kweli kabisa Balkis ndiye aliyemuua mke wa Kakakuona,” Tonny alipata uhakika.
“Sasa unaona tumechokoza nyuki wakati hatuna mbio.”
“Sijui tufanye nini ili Balkis atuelewe?”
“Nimekueleza tuachane naye.”
“Atatuelewa?”
“Mmh! Kazi ipo, kama amejua tunataka kumuua unafikiri atatufanya nini?” Ashura alisema kwa sauti ya kukata tamaa.
“Hapo ndipo ninapochanganyikiwa, kwa nini tusiendelee kuwa hapa ili mganga atupe hata kinga ili asitudhuru?”
“Tonny hebu kuwa na akili, umesikia aliyefanya vile ni Balkis mganga atatufanya nini, hiyo milioni mbili yako itarudisha roho ya mkewe?”
“Mmh! Na kweli, kwa hiyo unasemaje?”
“Tonny hebu ondoa gari kama huwezi nipishe miye niendeshe.”
“Ashura njoo uendeshe nina imani Balkis anajua mimi ndiye mbaya wake namba moja, hata sijui itakuwaje?”
“Tonny we twende nyumbani lolote litakalotokea tuwe tayari kukabiliana nalo.”
“Mmh! Haya sina jinsi yaani najuta kumfahamu Balkis.”
“Lakini si tumeambiwa ni kiumbe mwenye huruma?”
“Si umesema umeona akitokwa na machozi ya damu kuonesha hasira unafikiri mtu tuliyetaka kumuua atakuwa na huruma na sisi?”
“Bwana wee hebu tuondoke mengine tutayajua huko huko.”
Tonny alijikaza na kuwasha gari kisha waliondoka eneo la Kiwalani, Balkis aliwaona kwa mbali wakija, akiwa amejawa na hasira kutokana na kiburi walichokionesha alikosa adhabu inayowafaa kutokana na roho zao mbaya ili wasirudie tena kumfuatafuata. Adhabu aliyoipanga ilikuwa kuhakikisha kwanza anamtia aibu Ashura na mumewe kwa kumgeuza kiumbe wa ajabu asiyependwa na wanadamu au wanyama.
Hakutaka kuwasumbua aliwaacha warudi mpaka nyumbani kwao ili aweze kufanya alichokikusudia. Ashura na mwanaume wake walishangaa kwenda mpaka nyumbani kwao bila kukutana na tatizo lolote, walipofika walishukuru Mungu.
Baada ya kuingia ndani hata kabla hawajakaa vizuri mlango uligongwa, Tonny alikwenda kuufungua na Ashura alikwenda chumbani. Alipofungua alipatwa na mshtuko uliomfanya aanguke chini na kupoteza fahamu.
Ashura aliyekuwa chumbani alishitushwa na kishindo cha mtu kuanguka chini, alimwita mwanaume wake huku akitetemeka ili ajue kimetokea nini.
“Toooni,” aliita kwa sauti ya juu bila kupata jibu, woga ulimwingia.
Alirudia tena kumwita Tonny bila jibu lolote, alitoka chumbani huku akiwa na wasiwasi, kabla ya kufika sebuleni alisikia harufu ya manukato aliyoyazoea kuyasikia wakati Balkis akiwa karibu yake. Harufu ile ilimjulisha tayari walikuwa wamevamiwa ndani ya nyumba yao.
Mlangoni alikuwepo Tonny aliyekuwa amelala chini, alianza kutetemeka. Akiwa bado katika hali hiyo, mlango uligongwa tena, alitamani kurudi chumbani kwake lakini alijikaza na kusogea hadi mlangoni na kuufungua. Alipofungua alikutana uso kwa uso na Balkis, kwa woga alioupata haja ndogo ilimtoka bila kutarajia.
“Samahani Balkis,” aliomba msamaha huku akipiga magoti kwa kujua kiama kimefika.
“Ya nini?”
“Najua nimekukosea.”
“Kosa gani?”
“Unajua, naomba usituue.”
“Kuua ni kazi ya Mungu peke yake si ya kiumbe chochote.”
“Mbona ume..,” Ashura alisita kusema Balkis kamuua mke wa mganga Kakakuona kwa kuhofia kumzulia jambo ambalo huenda hakulitenda na kumuongezea hasira.
“Nimefanya nini?”
“Hujafanya kitu.”
“Najua ulitaka kusema nini.”
“Ha...ha...pana,” Ashura alitetemeka kwa hofu.
“Kwanza mmwagie maji mwenzako azinduke, nashangaa anakuwa mwoga wakati yeye ni bingwa wa kutoa roho za watu.”
“Naomba unisamehe Balkis najua kiasi gani tumekuudhi.”
“Hebu fanya kwanza niliyokuagiza,” Balkis alisema kwa sauti kali kidogo.
Ashura alikwenda jikoni na kurudi na maji kwenye bakuli.
“Mmwagie kidogo kichwani.”
Ashura alifanya kama alivyoelekezwa, baada ya kumwagia maji mwanaume wake alirudiwa na fahamu. Tonny alipozinduka alishtuka kujikuta yupo mbele ya Balkis. Alinyanyuka na kupiga magoti mbele ya Balkis kuomba msamaha.
“Samahani Balkis najua umekuja kutudhuru, lakini tunakuhakikishia hatutarudia tena kukufuata,” Tonny alisema huku akitokwa na machozi.
“Kabla ya kuzungumza lolote naomba Ashura aende akajisafishe, siwezi kuzungumza na mtu aliyejipaka najisi.”
Ashura alikwenda bafuni kujisafisha kisha kubadili nguo na kurudi mbele ya Balkis bila kujua nini hatima yao baada ya kumchokonoa kwa muda mrefu. Baada ya kurudi alisogea kwa mwanaume wake na kuungana naye kupiga magoti.
“Naomba mkae chini, magoti yenu yataniongeza hasira niwageuze kuwa manyani”
Baada ya kukaa alimuuliza Ashura swali lake la awali.”
“Ashura, uliuliza mbona nimemuua mke wa mganga?”
“Ha...ha...pana sikumaanisha hivyo.”
“Naona unataka kunichefua nikugeuze kuwa nyoka sasa hivi muuaji mkubwa, hivi mimi nikifa ninyi mtafaidika nini?”
Hakuna aliyejibu kitu, wote walibakia kimya nyuso zao wamezielekezea chini kwa aibu.
“Kwa kweli wanadamu ni viumbe wenye kiburi kuliko kiumbe chochote kilichoumbwa na Mungu. Matendo yenu mabaya kuliko hata ya shetani. Shetani siku zote humvuta mtu kwenye dhambi lakini si kuua. Ninyi kila kukicha mnatoa roho za watu kwa ajili ya mali.
Mmesababisha nimuue mke wa mganga bila sababu kutokana na nia yenu ya kuhakikisha nakufa. Jamani kosa langu nini, kama Hemed mliachana baada ya kumfilisi, sasa hivi umemuona mzuri?”
Ashura hakujibu kitu, aliendelea kuinama na kumfanya Balkis aendelee kuzungumza kwa hasira huku machozi ya damu yakizidi kuichafua nguo aliyokuwa amevaa.
“Kwa vile mmekuwa kenge msiosikia mpaka mtoke damu masikioni, sasa chagueni adhabu yoyote ila iwe mbaya kuliko zote zilizowahi kutolewa chini ya jua.”
“Tunaomba utusamehe,” walisema kwa pamoja huku wakitamani kunyanyuka kwenda kumlamba miguu.
“Sitawasamehe, lazima niwape adhabu kubwa sana ambayo hata mimi mtekelezaji itaniuma moyoni mwangu kwa jinsi mtakavyoteseka,” Balkis alisema kwa hasira.
Wote walibakia kimya wakishindwa kujua wachague adhabu ipi, kila adhabu waliyoifikiria ilikuwa nzito kwao. Baada ya kukaa kimya, Balkis alisema huku akitembea taratibu ndani ya nyumba na kuifanya nyumba inukie vizuri:
“Ashura, adhabu yako ya kwanza ni kutembea uchi mbele za watu kama tulivyokubaliana, baada hiyo itafuata nyingine ambayo nitaijua mwenyewe.”
“Na wewe,” alimgeukia Tonny aliyekuwa amejikunyata kwa hofu ya maisha yake.
“Tena wewe ndiye nitakayekufanya kitu kibaya, kwanza nitakugeuza nzi wa kijani maisha yako yawe chooni na jalalani, adhabu nyingine nitajua hapo baadaye.”
“Ni semehe Ba..ba..lki....”
“Shatap mashetani nyie,” alimkata kauli kwa sauti kali.
“Nina imani mzee Njiwa Manga aliwaeleza vizuri japo mwanzo hata mimi niliwaeleza lakini mlijitia viburi, sasa kiburi chenu kitawatokea puani.”
“Tusamehe hatutarudia tena.”
“Hebu niambieni kosa langu nini?” aliwauliza huku akiwa amewakazia macho.
“Hu..hu..na kosa.”
“Sasa kwa nini mnataka kuniua?”
“Tu..tu..sa..sa..mehe.”
“Nina imani uwezo wangu mlikuwa hamuufahamu lakini leo ndiyo mtaujua.”
“Balkis haki ya nani tunakuahidi hatutarudia tena,” walirudia kupiga magoti mbele yake.
“Hivi mngefanikiwa kuniua haya magoti mngempigia nani? Kumbukeni nimepata dhambi kwa ajili ya mtu mwingine hivyo lazima nitimize nilichopanga kuwafanyia.”
Wakati wakizungumza yale, Balkis alihisi mabadiliko mwilini mwake yaliyomfanya ahisi kizunguzungu kikali.
Kwa haraka alishika kwenye paji la uso na kutoweka mle ndani. Ile hali ilimtisha na kuamua kwenda moja kwa moja chini ya bahari kuwahi kujisalimisha kwa wazazi wake. Wasiwasi wake ulikuwa huenda mganga ameamua kulipa kisasi baada ya mkewe kuuliwa.
Akiwa amechoka alijivuta huku kizunguzungu kikizidi, akatembea kwa kujivuta huku akipepesuka lakini alipofika lango kuu la kuingilia kwenye jumba la mfalme alianguka chini na kupoteza fahamu. Vijakazi na watwana walifika na kumuokota hadi ndani ya jumba kuu akiwa hajitambui kabisa.
Malkia Huleiya alishtuka kupata taarifa za kuletwa Balkis akiwa hajitambui, akiwa na kanga mkononi alikimbilia sebuleni na kumkuta Balkis akiwa amelazwa chini akiwa hajitambui.
“Amefanya nini?” aliuliza kwa mshtuko.
“Hatujui Malkia Mtukufu,” walijibu kwa pamoja.
“Mmemkuta wapi?”
“Lango kuu Malkia Mtukufu.”
“Mpelekeni chumbani mara moja.”
Walimbeba na kumpeleka chumbani na kumlaza kitandani, baada ya kumlaza walitoka.
Malkia Huleiya alichanganyikiwa na kujiuliza mwanaye kafanywa nini na wanadamu. Alijua ile itakuwa vita na wanadamu ambao ni viumbe hatari aliokuwa akiwaogopa usiku na mchana.
TUKUTANE SIKU YA KESHO

2JIACHIE.COM Tunawatakia heri ya Krismasi na Mwaka Mpya wasomaji wetu.
2jiachie wanapenda kuwataarifu wasomaji wake anayetaka kuweka picha yake kwenye tovuti yetu akionyesha akiwa amejiachia kwa mwaka mzima na habari ya 2jiachie atume picha.
Tutatuma picha kuanzia leo Desemba, 25 - January 5, 2015 kama sehemu ya kuwa pamoja na wasomaji wetu.
Picha zitumwe kwenye emailhii 2jiachie@gmail.com au WhatsApp +255 654 50 42 66
Post a Comment