JINI LA DARAJA LA SALENDA - 22

ILIPOISHIA;
Katika kutembeza macho aliwaona wajukuu wa mzee Njiwa wakicheza nje ya uzio, aliona kama atamuua mmoja basi mzee Njiwa Manga ataacha kazi ya kuwatibu ili ashughulikie msiba na kuwafanya Ashura na mwanaume wake kuondoka ili warudi siku nyingine. SASA ENDELEA...
Aliamini kama watatoka bila kupatiwa kinga yoyote angetumia nafasi ile kuwamaliza wote ili aweze kuishi na Muddy bila tatizo japo alijuwa kwa upande wa baba yake kulikuwa na vita nyingine.
Kila alivyotaka kuteremka roho ilimkataza kwa kuwaonea huruma viumbe wasio na hatia.
Kutokana na uwezo wake aliweza kuyasikia yote yaliyokuwa yakizungumzwa ndani na kupanga kama atakubaliana nao kabla ya kuwapa kinga naye, hatakuwa na budi kuua mtoto mmoja.
Ashura na mwanaume wake waliingia katika chumba cha mzee Njiwa Manga na kukaa kwenye mkeka.
“Karibuni,” mzee Njiwa Manga aliwakaribisha.
“Asante,” walijibu kwa pamoja.
“Mh! Niwasaidie nini?”
“Mzee tunahitaji msaada wako, tuna vita nzito na mwanamke mmoja jini.”
”Mmejuaje ni jini wakati majini hayaonekani?”
“Anatutokea katika umbile la kibinadamu na wakati mwingine katika maumbile tofauti, pia tunatokewa na mambo ya kutisha.”
“Tena jana kamuua mganga mmoja Mbagala kifo cha kutisha,” Ashura aliongezea.
“Mmh! Majina yenu?” Aliwauliza huku akichukua kibao cheusi na chaki.
“Naitwa Shuuna.”
“Shuuna...” mganga alilirudia jina lile kwa sauti ya chini huku akiliandika kwenye kibao.
“Mbona unaonekana una majina mengi?” Mganga Njiwa Manga alimuuliza Ashura.
“Lakini hili ndilo langu la kuzaliwa.”
“Sasa nikusaidie kwa jina gani kwani yote uliyatumia na watu tofauti wanakujua kwa majina hayo?”
“Kwa sasa natumia jina hili.”
“Kama ukifanikiwa kurudi kwa Muddy utatumia jina gani?”
Swali lile lilimfanya Ashura akae kimya na kukosa la kujibu kwa kuona kama siri yake inatoka nje.
“Lakini mzee suala la Muddy tulishaachana nalo, kama kutusaidia msaidie kwa jina la Shuuna,” Tonny aliingilia kati mazungumzo.
“Najua mmekuja pamoja lakini kila mmoja ana mawazo yake ambayo sitaki kuyaingilia kwa vile siyo kazi yangu,” mzee Njiwa Manga alijibu kwa fumbo lililomuacha gizani Tonny bila kujua dhamira ya Ashura kwa Muddy ilikuwa nini.
“Naomba niachane na mwenzako kwanza, hebu nawe nieleze jina lako?”
“Naitwa Antony.”
“Antoniii,” alilirudia jina lile kwa sauti ya chini huku akiliandika kwenye ubao.
Baada ya kuandika alitulia kwa muda akiandika vitu kwenye ubao na kukohoa kidogo kisha akauliza:
“Nimeona yote, sasa shida yenu nini hasa?”
“Mzee kama tulivyokueleza kuwa tuna tishio la mwanamke mmoja ambaye ni jini, anatishia maisha yetu.”
“Kwa hiyo mnataka nini?”
“Tunataka utukinge ili tuweze kupambana naye.”
“Mnamjua jina lake?”
“Balkis,” Ashura alijibu.
Mganga aliliandika jina lile, kama kawaida alilirudia kwa sauti ya chini.
“Balkis...Balkis.”
Baada ya kutulia kwa muda alisema:
“Lakini mbona mimi sioni madhara ya huyu mnayemuogopa?”
“Mzee huyu ni mtu mbaya sana, amenitokea mara nyingi kwenye gari katika sura tofauti na kutishia maisha yetu,” Ashura alisema huku macho yamemtoka pima kwa kusistiza.
“Mbona hapa panaonesha jini huyo ni mpole sana kuliko majini wengine?”
“Si kweli, ana roho mbaya sana, amemuua mzee Chujio kifo kibaya sana,” Ashura alisema.
“Unajua sababu ya kuuawa mzee Chujio?” mganga aliuliza.
“Kutokana na maelezo ya huyo mwanamke jini anasema aliingilia kazi yake na kuwa mbishi ndio akaamua kumfanya vile.”
“Sasa hamuoni na mimi nikiingilia kazi si yangu anaweza kunifanya kama mzee Chujio?”
“Hawezi.”
“Kwa nini asiweze?”
“Tunasikia wewe ndio kiboko ya majini.”
“Ni kweli kazi yangu ni kutibu na si kushindana na majini.”
“Lakini mzee kazi yako si kutusikiliza wateja shida yetu na kukupa kiasi ukitakacho,” Tonny alimueleza mganga..
“Sikiliza kijana, mimi si mchawi ni mganga wa kuwasaidia wenye matatizo, ndiyo maana nipo mpaka leo.Waganga wengi wamepoteza sifa zao kutokana na kuingilia kazi ya wachawi.
“Tumekuwa tukifanya makosa ya kuingia kwenye kazi ya kutesa, kuua au kuingia kwenye vita na viumbe kama majini ambayo wakati mwingine huwa hayana matatizo na watu.”
“Sasa mzee utatusaidiaje?”
“Mpaka sasa sijajua shida yenu nini?”
“Tunataka kinga ili tusiweze kudhuriwa na jini.”
“Jini gani wa kuwadhuru ninyi?”
“Balkis,” Ashura alijibu.
“Balkis atawadhuru vipi bila ninyi kumchokoza?”
“Yule hana cha kumchokoza bali huamua kuua bila sababu,” Ashura alitengeneza uongo.
“Sitawapa dawa yoyote zaidi ya kauli ya Balkis mwenyewe.”
“Mbona hatukuelewi, kauli gani?”
“Mtaisikia muda si mrefu kutoka kwake Balkis.”
Mzee Njiwa alitoka nje na kurudi na kitezo chenye moto, akakiweka mbele yake, akatoa mavumba kwenye chupa kisha akasema:
“Hii dawa kazi yake kuyavuta majini mazuri, kama Balkis ni jini mbaya hatakuja nikimwita.”
Baada ya kusema vile alianza kuweka mavumba kwenye moto huku akisema:
“Balkis binti mfalme wa bahari, naamini wewe ni jini mwema nakuomba uje mbele yangu, lakini kama si jini mwema ukiingia himaya yangu ndiyo mauti yako...Balkis njoo mbele ya wanadamu hawa wana mashtaka juu yako.”
Je, Balkis ni jini mzuri au mbaya?
Moshi ulikuwa mwingi kiasi cha kujaa chumbani, baada ya muda upepo mkali ulianza kuvuma na kusababisha baadhi ya vitu kutaka kupeperuka lakini mzee Njiwa Manga aliutuliza kwa kusema:
“Najua una hasira lakini naomba uwe mpole kama ulivyo, wewe ni mpole tena mwenye upendo kwa wanadamu.”
Upepo ulitulia taratibu wakati huo Balkis akiwa katika umbile la njiwa alijikuta akizidiwa na nguvu na kudondoka toka juu ya mnazi na kujikuta akijitahidi asianguke na kuingia kwenye dirisha la chumba cha uganga cha mzee Njiwa Manga.
Alitua pembeni ya mzee Njiwa Manga, Ashura na mwanaume wake walishtuka kumuona njiwa mzuri sana mwenye rangi nyeupe aliyepakwa wanja mwekundu uliozunguka katika macho yake.
Manyoya yake yalikuwa kama ya plasitiki iliyokuwa ikimelemeta.
“Karibu Balkis kwa mzee Njiwa Manga.”
Balkis katika umbile la njiwa hakujibu kitu alitulia akiwatizama Ashura na mwanaume wake. Mzee Njiwa Manga alisema: ”Najua hukupenda muda huu kuwa hapa, lakini nimekuita kwa nia njema kwa vile wewe ni jini mwema mwenye upendo kwa wanadamu. Nakuomba uwe kwenye umbile tunaloweza kuzungumza kibinaadamu.”
Baada ya kusema vile kilipita kiza cha ajabu na baada ya muda ilirudi hali ya kawaida. Sehemu aliyokuwa njiwa alikuwepo Balkis katika umbile la kibinaadamu.
Ashura na mwanaume wake kidogo wakimbie kwa hofu. ”Msihofu, kama nilivyowaeleza kwa dawa niliyoichoma ni jini mwema tu anayeweza kuingia katika himaya yangu. Balkis asalam aleykumu.”
“Waaleiykum msalaam,” alijibu kwa sauti tamu.
“Karibu.”
“Asante.”
Balkis aligeuza uso wake na macho yake yaligeuka rangi na kutoa machozi ya damu, kitu kilichozidi kuwatisha Ashura na mwanaume wake.
“Hapana Balkis huna sifa hiyo wewe ni mpole nimekuita hapa kwa makusudi ya kuwaeleza hawa wanadamu ubaya wao mbele yako.” Mganga Njiwa Manga alisema huku akimshika kichwani na kumpigapiga taratibu kumpunguza hasira. Balkis alitikisa kichwa kuonesha amekubali.
“Balkis.” ”Abee.”
“Nataka uniambie unataka nini wafanye hawa wanadamu wajue wewe si adui yao?” ”Wanajua wenyewe, nilizungumza nao nini,” Balkis alijibu kwa sauti tamu kama kinanda.
“Naomba unieleze mbele yao.”
“Nikisema mimi nitaonekana muongo, napenda waseme kwa vinywa vyao.”
“Eti mlizungumza nini na Balkis?” mzee Njiwa Manga aliwageukia na kuwauliza.
“A...ali...nikataza nisimfuate mume wake ambaye ni mtalaka wangu,” Ashura alijibu katika hofu kubwa.
“Na kingine?”
“Tusimfuatilie maisha yake.”
“Mmefanya yote aliyowaeleza?”
Wote walibakia kimya wakitazama chini, mganga alimgeukia Balkis na kumuuliza.
“Wewe umeona nini?”
“Hawa walio mbele yako ni viumbe wabaya kuliko hata nyoka, wamepoteza maisha ya wanaume zaidi ya wanne na Muddy kama nisingemuwahi alikuwa wa tano. Wamekuwa na tabia za kuwatafuta wanaume na huyu mwanamke kujifanya anawapenda sana, kisha anajitambulisha kwa majina tofauti.
“Kila mwanaume anamfahamu kwa jina tofauti kama waliokufa kwa ajili yao wakisimamishwa mbele yake watamtaja kwa majina tofauti, Muddy anamtambua kwa jina la Ashura lakini wengine walimtambua kwa majini ya Fatuma, Hilki, Masha.
“Lakini jina lake halisi ni Shuuna, kwa utaalamu wako nina imani majina hayo yote umeyaona alipojitambulisha kwako na kujua sababu ya majina hayo?”
“Ndiyo,” Mzee Njiwa Manga alijibu kwa sauti ya chini.
“Hawa si viumbe wa kuonewa huruma hata mara moja, hebu angalia kila kukicha wamekuwa wakipanga mipango ya kudhulumu mali za watu na kuwatoa roho zao bila hatia kwa kigezo cha uzuri wa Shuuna. Hivi mimi na yeye nani mzuri?”
Balkis alinyanyuka na kujigeuza pande zote kuonesha ufundi wa Maulana kumuumba katika umbile la uzani.
“Ni wewe Balkis mwana wa mfalme wa chini ya bahari.”
“Mbona siui watu kama ninyi? Mtauliza kwa nini nilimuua mganga Chujio, kiburi chake kilimponza. Nilijua mtakwenda kule na kutaka kinga ya kupambana na mimi kama alivyowasaidia kudhulumu na kutoa roho za watu wasio na hatia. Lakini kwa busara zangu nilimuonya na kuonesha kiburi kwake ndicho kilichomponza.
“Nimewaonesha ishara nyingi za vitisho ili wajue mimi si kiumbe wa kawaida ili wachane na mimi, lakini wamekuwa wabishi, kabla ya kuja huku niliwapa onyo zito lakini wamekuwa kama kenge, hawasikii mpaka watoke damu masikioni.
“Tena wana bahati kubwa leo ningepata dhambi nyingine, wakati natoka nyumbani niliwaona wamekaribia kwako lakini kasi yangu ilichelewa kidogo na kuwakuta wameshaingia kwenye ngome yako.
“La sivyo kama ningefanikiwa kuwatia mikononi ningewaulia mlangoni kwako na kama ungewasikiliza na kuwapatia tiba kabla tiba yao haijatimia ningemuua mjukuu wako mmoja ili uhalalishe kazi hii na wangetoka ningewamalizia mbali,
” Balkis alisema kwa sauti isiyotaka mzaha, huku kauli yake ikizidi kuwatisha moyoni walioomba msaada wa mzee Njiwa Manga.
“Nimekuelewa sana Balkis binti wa mfalme Barami, sasa ulikuwa unataka nini?”
“Kama nilivyowaeleza waachane na mimi, waendelee na maisha yao.”
“Wakifanya hivyo utakuwa na vita nao?”
“Niwe nao ili iwe nini ikiwa kila mmoja na maisha yake, ila tofauti ya hapo nitakachokifanya Mungu anajua.”
“Nina imani mmesikia yote aliyosema Balkis, niliwaeleza ni mpole mwenye huruma na upendo kwa viumbe wenzake.
Napenda kuwaeleza kuwa maelezo yake ndiyo tiba yenu na mkitoka hapa mkienda kinyume na haya aliyosema, nisione mtu hapa, mtamalizana wenyewe, mmenisikia?”
Alijibu kwa kunyanyua vichwa kwani hata midomo ilikuwa mizito, baada ya majibu yao ya kibubu mzee Njiwa Manga alimgeukia Balkis.
“Nina imani wamekuelewa ila wakienda kinyume mimi simo.”
“Wewe unasema hivyo lakini mioyo yao imejaa tamaa ya mali na uhai wa watu, narudia tena sitawaua ila nitawaadhiri mbele za watu, hilo litakuwa pigo kubwa na mkizidi nitawageuza mbwa.”
“Nimekuelewa sana Balkis unaweza kwenda,” mzee Njiwa Manga alisema.
Baada ya kuruhusiwa kutoka alinyanyuka na kutoka chumbani katika umbile la kibinadamu, wote walimsindikiza kwa macho hadi nje.
Waliokuwa wamekaa nje kusubiri huduma macho yao yalishuhudia mwanamke mzuri akipita mbele yao huku wakijiuliza amepita saa ngapi kutokana na watu wengine kuwepo kwa muda mrefu. Balkis baada ya kutoka katika uzio wenye nguvu wa mzee Njiwa Manga alitoweka.
Baada ya kuondoka Balkis, mzee Njiwa Manga aliwageukia wateja wake na kusema:
“Nina imani tatizo lenu limekwisha?”
“Mzee litakwisha vipi wakati umemsikia mwenyewe amesema nini,” Tonny alihoji.
“Kasema nini?”
“Si amesema tukifuatilia mambo yake atatugeuza mbwa,” Ashura alijibu.
“Sasa mnataka kufuatilia mambo yake?”
“Hapana.”
“Sasa tatizo nini?”
“Tulikuwa tunaomba kinga.” Tonny alisema.
“Ya nini?”
“Ili tujikinge na matatizo ya wanadamu na majini.”
“Ili?”
“Mzee kama hujui kazi yako, kwani wanadamu wanakuja kwako kutafuta nini?”
“Tiba ya matatizo yao.”
“Sasa mbona hutaki kutusaidia?”
“Kwani shida yenu iliyowaleta hapa ni nini?”
“Kuzuia nguvu za jini Balkis.”
“Sasa niwape kinga ya nini?”
“Anaweza kutugeuka na kutufanyia kitu kibaya.”
“Hawezi na sina tiba yoyote labda muwe na tatizo lingine.”
“Hatuna, ni hili hili la huyu mwanamke ndilo linalotutisha, unamuona kwa macho tu lakini ni kiumbe kibaya sana.”
“Yule hana ubaya kama nilivyowaeleza, lakini mioyoni mwenu mna dhamira mbaya naye, kwa hilo mimi halinihusu kama mnataka ushindani dawa hiyo sina.”
“Kwa hiyo huna msaada wowote kwetu?” Tonny aliuliza.
“Msaada niliowapa ni mkubwa kuliko kukuchanjeni au niwape dawa ya kufukiza.”
“Mzee msaada gani uliotupa zaidi ya kutuacha njia panda?” Tonny alizidi kuhoji.
“Msaada niliowapa hamuujui lakini ni mkubwa sana, najua mmezunguka kwa waganga wengi kwa kazi zenu za dhuluma. Hamkuwahi kukutana na tatizo kisha mkatibiwa bila kunywa, kujifusha au kuchanjwa dawa? Mliyekuwa mnamuona adui ameeleza hataki kitu gani, sasa mnataka nifanye nini?”
”Basi inatosha inawezekana na wewe umemuogopa,” Tonny alisema kuonesha alitaka zaidi ya yale aliyoelezwa.
“Kweli nimemuogopa nipo kwa ajili ya kutibu si kujiingiza kwenye matatizo ya kujitakia, kutokana na maelezo yake nilikuwa nampoteza mjukuu wangu kwa ajili yetu. Nawaeleza mkikosea kwenda kwa mganga mwingine kitakachowakuta hamtakisahau mpaka mnakufa.”
“Tumeelewa.” Tonny alijibu kwa shingo upande.
“Basi mnaweza kwenda ili niendelee na wenzenu.”
“Sasa mzee tukupe kiasi gani?”
“Nina imani hamkuona nilichokifanya, nendeni msitoe kitu chochote.”
“Hapana mzee hata ya kuangalizia, sijui elfu moja?”
“Hapana nimewasamehe kila kitu.”
Walitoka huku wakiamini mzee Njiwa Manga uwezo wa kutibu umepungua ndiyo sababu ya kushindwa kuwasaidia kupambana na Balkis.
Itaendelea SIKU YA KEHO
Post a Comment