ad

ad

JINI LA DARAJA LA SALENDA - 17



Like: www.facebook.com/2jiachie
Web: www.2jiachie.com
#SOMA SEHEMU ZILIZOPITA ZA SIMULIZI HII HAPA ==>http://bit.ly/

ILIPOISHIA;
Muddy alitembea taratibu huku akipepesa macho huenda akaliona jumba lile la kifahari, lakini mpaka anavuka Daraja la Salenda bado hakuona jumba lile.
SASA ENDELEA...

Hakukata tamaa alitembea hadi Agha Khan, pia nyumba zilikuwa zile zile za siku zote alizozizoea. Baada ya kutembea kwa muda mrefu alijikuta akichoka sana na kuamua kurudi taratibu kulifuata gari lake ili arudi nyumbani. Alitembea kwa mwendo wa kivivu huku kiu na njaa ikiwa kali.

Alimwita muuza maji ambaye alimletea maji, alikunywa kidogo na mengine alijimwagia kichwani kupunguza uchovu. Lakini ilikuwa tofauti na alivyofikiria, alihisi usingizi wa ajabu na mwili kuchoka maradufu. Alitafuta mti wa kivuli uliokuwa pembeni ya bahari na kujilaza chini yake.

Usingizi mzito ulimpitia uliomfanya alale kwa muda mrefu, alishtuka saa moja usiku, giza lilianza kuimeza nuru ya mchana. Alijikuta amelala pembeni ya maji yaliyokuwa yakirudi baada kupwa kuanzia asubuhi. Alishangazwa na sehemu aliyojikuta kuwa eneo la ndani ya bahari wakati yeye alilala nje ya bahari  kwenye miti ya pembezoni. Alinyanyuka na kujikung’uta kisha taratibu alielekea sehemu lilipokuwa gari lake. Wasiwasi wake mkubwa gari linaweza kuibwa au kuchukuliwa baadhi ya vitu.

Alijiuliza kama gari litaibwa ataieleza nini mahakama, lakini ilikuwa ajabu gari lilikuwa lipo katika usalama pia hakuna kitu chochote kilichopotea. Alimshukuru Mungu na kuingia kwenye gari ili arudi nyumbani, lakini kabla hajawasha gari ili aondoke alishtuka kumuona Balkis.
Balkis alitokea mbele yake na kulisogelea gari huku akichanua tabasamu pana, alipomfikia alimsemesha:
“Muddy vipi?”

“Safi.”
“Za toka jana?”
“Nzuri.”
“Mbona upo huku?”
“Mbona hukuonekana mahakamani kama ulivyoniahidi?”

“Kwa hilo naomba samahani mpenzi wangu, nilitumwa na baba asubuhi nilijua nitawahi lakini amini usiamini ndiyo narudi. Na hivi nilikuwa nimetumwa tena nashangaa kukuona hapa.”
“Balkis huwezi kuamini toka nizaliwe leo nimesulubika vibaya.”
“Kwa nini tena mpenzi wangu?”

“Baada ya kutoka mahakamani...”
“Kabla ya kuendelea hebu nielezee imekuwaje huko?”
“Kesi imehahirishwa mpaka wiki ijayo.”
“Hakuna kitakachobadilika, kila kitu wamekwishakamilisha hata hakimu wa kesi yako ameshachukua chake mapema, kinachosubiriwa ni kukumaliza tu. Lakini nakuhakikishia fedha watakazochukua zitawatokea puani.”
“Utawapeleka polisi?”

“Wakafanye nini, ila utasikia tu nini kitawatokea.”
“Alafu...”
“Nimekuelewa Muddy, kwanza samahani kwa kutotokea mahakamani, umesema umesulubika kivipi?”
“Hivi kwenu wapi?”
“Muddy, si hapo mbele.”
“Wapi?”

“Unataka kupajua au kufika, twende maana sasa hivi nipo peke yangu.”
“Sehemu gani?”
“Si hapo mbele? Unaona nyumba ile kwa nyuma.”
“Mbona jana tulikwenda huku?”
“Si ndipo tunapopitia, kwani tatizo nini?”

“Hakuna tatizo twende nikapumzike nimechoka hapa nilipo pia nina kiu na njaa kali.”
Kama kawaida Balkis aliingia kwenye gari na kuliendesha, pamoja na Muddy kukaza macho ili ajue nyumba ile ipo wapi. Gari lilienda kidogo na kukata kidogo, Muddy hakuamini kuona jumba la kifahari lile lile alilolala jana yake. Baada ya kupaki gari  sehemu yake aliteremka na kumfungulia mlango Muddy kisha alimshika mkono na kumuongoza mpaka ndani.

“Karibu mpenzi wangu,” alimwambia kwa sauti ya mahaba huku akimlegezea macho na kumfanya Muddy asahau tabu zote alizokutana nazo.
 Kama kawaida alipelekwa kuoga kisha alifungwa vazi refu na kupelekwa kwenye meza iliyokuwa na vyakula tayari. Wakati akiendelea kula chakula kitamu ambacho kwake ilikuwa siku ya kwanza kukila, Balkis alimuaga kwenda kuoga. Aliondoka kwa mwendo wa madaha na kumfanya Muddy aache kula na kumsindikiza kwa macho huku akiusifia utundu wa Rabuka kumuumba binti mrembo kama yule.

Kwake aliona kama ndoto kumpata msichana mzuri kama Balkis pamoja na uzuri wake lakini umemuonesha mapenzi ya kweli kiasi cha kumsahau mkewe Ashura. Akiwa katikati ya chakula, alimuona Balkis akisogea mezani akiwa amejifunga upande wa khanga.

Kila dakika Balkis alizidi kujijaza moyoni kwa Muddy ambaye kwake aliona ngekewa kuokota dhahabu katikati ya soko la Kariakoo. Baada ya chakula kama kawaida alipelekwa kwenye chumba alicholala jana yake. Kwa raha za muda mfupi hakutamani kufa na kujilaumu kwa uamuzi wa kijinga aliotaka kuchukua.

Kama kawaida alfajiri alirudishwa kwake huku akijiuliza kwa nini baba yake arudi alfajiri tu anatoka wapi. Kitu kingine kilichomchanganya kilikuwa jumba zuri analoishi Balkis lipo sehemu gani mbona hajawahi kuliona. Wazo lake lilikuwa mchana arudi tena kulitafuta.

Lakini aliporudi alipitiwa na usingizi na kuamka jioni ya siku ile na wakati huo Balkis alikuwa amekwishafika na kumfanya siku ile aimalize nyumbani, lakini bado alitaka kutoka usiku ule kama Balkis akiondoka ambaye alikuwa halali pale na kwenda kufanya uchunguzi wake.
Baada ya Balkis kuondoka majira ya saa nne usiku, Muddy aliamua kurudi tena maeneo ya Daraja la Salenda kufanya uchunguzi wa jumba lile la ajabu. Aliingia kwenye gari lake na kwenda hadi sehemu aliyokutwa na Balkis. Alisimamisha gari lake na kufunga kila sehemu kwa usalama wa gari lake kisha aliteremka na kutembea taratibu kuifuata njia aliyopita na Balkis.

Kila alivyolitafuta lile jumba la kina Balkis hakuliona, alijikuta akitoka sehemu moja kwenda nyingine bila mafanikio. Saa zilimkatikia kwa kuzurula kulitafuta lile jumba ambalo aliamini kwa muono wake akiwa ndani yake kama akiwa kwa mbali angeliona kutokana na kuwa na taa kila kona ya jumba lile zilizokuwa na mwanga mkali.

Lakini kila alipotupa macho labda ataziona taa angani, kulikuwa na kiza tu kilichotawala angani. Bado hakuamini alirudi sehemu aliyoanzia zaidi ya mara kumi ili aanze upya kulitafuta jumba la kifahari la kina Balkis. Muda ulizidi kukatika, kutokana na kutembea sana kulitafuta jumba hilo alijikuta akichoka sana na kukaa chini ya mti mmoja apumzike kidogo ili arudi kwenye gari lake na kurudi nyumbani kulala kwani usiku ulikuwa mkubwa.

Alipokaa chini ya mti usingizi haukuchelewa ulimchukua, ulikuwa usingizi mtamu ajabu uliomfanya alale kama yupo kitandani. Kibaridi cha alfajiri kilimshtua kwenye usingizi mzito na kujikuta amelala pembeni ya ufukwe chini ya mnazi, sehemu ambayo ilimchanganya kidogo.

 Alitembeza macho yake na kuwaona watu waliokuwa wakiteremsha samaki kwenye boti. Sehemu ile ilimchanganya sana na kujiuliza pale ni wapi? Pamoja na kuwa amejilaza chini ya mnazi bado hakuna mtu aliyekuwa na habari naye kwani kila mmoja alikuwa na hamsini zake.

Wengi walipita pembeni yake wakiwahi kununua samaki walioletwa na majahazi asubuhi ile. Akiwa bado amekaa chini akitafakari yupo wapi, kijua nacho kilianza kuchomoza kwa mbali lakini bado baridi iliendelea kumchonyota mwilini.

Alijinyanyua taratibu alipokuwa amekaa na kuanza kutembea taratibu pembeni ya bahari huku akijitahidi kuyakumbuka maeneo yale ambayo yalikuwa mageni kichwani mwake. Aliona akikaa kimya atazidi kupotea, ilibidi amuulize kijana mmoja aliyekuwa na kapu lililoonekana limejaa samaki wabichi, alionekana ni mchuuzi aliyelangua na kwenda kuwauza mitaani.

“Samahani ndugu,” Muddy alimuuliza baada ya kumkaribia.
“Bila samahani kaka yangu.”
“Kwanza ni vizuri kutanguliza salamu kuonesha uungwana, habari za asubuhi?”
“Nzuri tu.”
“Eti hapa ni wapi?”
“Kigamboni.”

“Mungu wangu, kuja huku si lazima utumie pantoni?”
“Kutoka wapi?”
“Mjini.”
“Ndiyo.”
“Sasa mimi nimefikaje bila kutumia Pantoni?”
“Kutoka wapi?”
“Mjini.”
“Kwani wewe umefikaje huku?”
“Hata najua, hii kali ya mwaka.”

“Samahani kaka, mbona kama unajishangaa kwani wewe mara ya mwisho ulikuwa wapi?”
“Njia panda ya  barabara ya Ali Hasani Mwinyi na Masaki.”
“Ulikuwa ukifanya nini?”
“Mmh! Tuachane na hayo, hebu nioneshe njia ya kuelekea kivuko cha Pantoni?”
“Twende pamoja na mimi naelekea huko huko.”

Muddy aliongozana na yule kijana kuelekea kwenye kivuko cha Pantoni, njiani alijawa na mawazo jinsi alivyojikuta Kigamboni wakati yeye alikuwa maeneo ya Daraja la Salenda. Alijiuliza kuhusu gari lake atalikuta kwenye hali gani, alipofika kivukoni bahati nzuri alikuta kivuko ndiyo kinapakia abiria na magari.

Alipanda na kutulia kwenye siti huku kichwa chake kikiwa hakikubaliana na kilichotokea.
Bado alijawa na mawazo juu ya kujikuta Kigamboni bila kujielewa, kivuko kilivyofika mwisho aliteremka na kuelekea kwenye daladala za kuelekea Mwenge iliyomrudisha mpaka njia panda ya kuelekea Masaki. Alipofika alilikuta gari lake lipo katika hali ya usalama.

Aliingia ndani ya gari lake na kurudi hadi kwake, alishangaa alipofika kwake kumkuta Balkis amekaa mlangoni akilia. Alijikuta akishtuka, akateremka kwenye gari bila kufunga mlango na kumfuata alipokuwa amekaa.
“Mpenzi unalia nini?”
“Muddy hunipendi.”
“Mimi?” Muddy alishtuka kusikia vile.

“Muddy nazungumza na nani?”
“Na mimi.”
“Ulikuwa wapi?”
“Nilitoka kidogo alfajiri kuna sehemu nilikwenda mara moja.”
“Muddy unanipenda?”
“Tena sana.”
“Niambie ukweli ulikuwa wapi?”
“Kama nilivyo kueleza mpenzi,” Muddy alijua Balkis alikuja asubuhi ile.
“Nikuambie nini mpenzi zaidi ya hayo.”

“Mbona kichwani una majani na mwili na nguo zimechafuka?”
Kauli ile ilimshtua Muddy na kujikuta akijikagua upya na kujikuta kweli alikuwa amechafuka kwa mchanga wa bahari pia kichwani alikuwa na majani. Alijikuta akipatwa na kigugumizi, alijifikiria amjibu nini Balkis aliyekuwa akimtazama usoni huku machozi yakimtoka.

Nini kitaendelea? SIKU YA KESHOOOOOOOOO




No comments

Powered by Blogger.