ad

ad

JINI LA DARAJA LA SALENDA - 08

 

ILIPOISHIA: Suzana aliposhtuka usingizini hakuamini macho yake alipojikuta yupo nyumbani kwake amelala kitandani. Alirudia kutazama tena ni kweli au alikuwa akiota, akili yake ilimjulisha kuwa jana alipigiwa simu na mpenzi wake Brighton kuwa amepata dawa ya matatizo ya nguvu za kiume na alipokwenda kweli alikuwa amepona.

Alikumbuka Brighton alimpa penzi tamu na kujikuta wote wakipitiwa na  usingizi, lakini ilikuwa ajabu kuamka asubuhi na kujikuta amelala kitandani kwake. Alijiuliza simu aliyopigiwa alikuwa anaota au kweli, kila alipolazimisha labda ni ndoto akili ilikataa na kuamini kabisa alikwenda kwa Brighton.

Alijiuliza labda baada ya kufanya mapenzi alirudishwa nyumbani, lakini kwa upande wake kitu kama kile hakikuwahi kutokea. Kingine kilichomshangaza hata kama alirudishwa ni kuwa alikuwa amepoteza fahamu. Alikaa kitandani kwa muda na kukumbuka anatakiwa kujiandaa kwenda kazini.

Aliamka na kwenda kujiandaa, alipofika kazini bado akili yake haikumpa jibu. Alimtafuta Sharifa amueleze kilichomtokea jana.
SASA ENDELEA ...

Alipofika alimkuta ndiyo kwanza anafuta vumbi kwenye kompyuta yake, Sharifa alipomuona Suzana aligundua ana matatizo.
“Karibu shoga.”

“Asante,” alijibu huku akisogeza kiti na kuketi.
“Mbona uko hivyo?”
“Mmh! Kuna kitu kimenitokea jana sikielewi hata kidogo!”
“Kitu gani hicho?”
“Unakumbuka jana nilikupigia simu?”
“Ndiyo.”

“Nikakueleza kuwa nimeahirisha kwenda kwa mganga?”
“Ndiyo.”
“Basi, Brighton si aliniita na kunieleza kuwa amepata dawa ya tatizo lake na kukosa nguvu za kiume.”
“Ehe?”

“Baada ya kunieleza vile nikaona hakuna sababu yoyote ya kwenda kwa mganga kwa vile dawa imepatikana.”
“Ehe!”
“Basi jana saa moja usiku nikaenda kwa mpenzi wangu.”
“Lete raha dada.”
“Tumekutana kama kawaida, baada ya kuoga tulipanda kitandani, si unajua usongo niliokuwa nao.”

“Najua sana.”
“Basi shoga, kama alivyonieleza ndivyo ilivyokuwa, mtoto wa kike nikajilia raha nilizozipoteza muda mrefu.”
“Alikuwa na nguvu kama kawaida?”
“Tena ziliongezeka mara mbili.”

“Mmh! Makubwa, kampata mganga gani huyo?”
“Anasema alikwenda hospitali.”
“Jamani ona sasa, kumbe tunakimbilia kwa waganga tiba ipo hospitali, nilikueleza toka awali waganga wengine wanatengeneza ugonjwa, ionekane kweli tuna matatizo makubwa ili tuwape fedha nyingi.”
“Shoga bado nakuja sijafika kwenye pointi yangu.”
“Ipi tena?”

“Sababu iliyonifanya nisiingie ofisini kwangu na kuja moja kwa moja kwako.”
“Una tatizo gani?”
“Tulipomaliza kufurahishana na mpenzi wangu huku nikifurahia mafanikio makubwa baada ya kupona tatizo lake, tulipitiwa na usingizi mzito. Lakini kwa maajabu makubwa nimeamka asubuhi na kujikuta nipo kwangu!”
“Kujikuta kwako kivipi?”

“Kitandani kwangu nimelala!”
“Sasa kipi cha  ajabu?”
“Ina maana hujanielewa?”
“Nimekuelewa! Yaani jana baada ya kukutana na mpenzi wako asubuhi ulipoamka ulijikuta umelala, sasa kipi cha ajabu kama ulilala usiku na asubuhi ukajikuta kitandani?”

“Hebu nielewe vizuri nisemayo, jana nilikwenda kwa Brighton kama ilivyo kawaida, ninapokwenda hulala huko huko, hata safari yangu ya kuja kazini huianzia kwake.”
“Hilo nalijua, sasa hapo tatizo nini?”
“Jamani huoni tatizo! Nilale kwa Brighton niamke kwenye kitanda nyumbani kwangu tena nikiwa peke yangu.”

“Suzana! Unayosema ni kweli au ulikuwa unaota?”
“Sharifa, yaani niote mchana na usiku? Sikukupigia simu?”
“Ulinipigia?”
“Saa ngapi?”

“Mchana”
“Sasa huko kuota gani?”
“Mmh! Basi kama ni kweli usemayo kuna namna lazima tuliangalie kwa macho mawili.”
“Yaani toka nimeamka sijielewi kabisa.”
“Umempigia simu Brighton kumuuliza?”

“Huwezi amini kila nikipiga simu yake inaonekana anazungumza.”
“Basi kuna umuhimu wa wewe kwenda kwake ili ukapate ukweli, japo mimi bado naamini baada ya kunipigia simu inawezekana kabisa ulipitiwa na usingizi na kuota ulikuwa na Brighton na asubuhi ulipoamka ukajishangaa upo kitandani kwako. Lazima utaamini kabisa umetokewa na kitu kisicho cha kawaida.”

“Sharifa hiki ninachokueleza ni kweli kabisa si cha kuota, haya ni maajabu.”
“Au ndiyo Jini Balkis?”
“Jini Balkis! Kama ni Balkis, Brighton asingeweza kufanya kazi.”
“Nimekueleza yule jini ana mambo mengi ya kukuchanganya pale unapokaribia kuujua ukweli.”
Suzana anaanza kuingia kwenye mtihani mzito wa Jini Balkis, nini hatima ya yote?
“Kwa hiyo kuna umuhimu wa kwenda kwa  mganga?”
“Ikiwezekana, lakini kwanza nenda kwa mwenzako ili umuulize kama kweli jana mlilala pamoja.”
“Mmh! Itabidi nifanye hivyo.”
“Asubuhi hii?”

“Sharifa siwezi kufanya kazi vizuri, akili yangu bado ipo njia panda ukweli wa kitu hiki nitaupata kwa Brighton.”
“Kazi?”
“Lazima niombe ruhusa, nimechanganyikiwa, sijui itakuwaje kama huyo jini atakuwa kanivaa na mimi?”

“Kama kukuvaa kakuvaa muda mrefu, sasa inawezekana ndiyo anajionesha kwamba na wewe upo kwenye mtandao wake.”
“Mungu wangu! Kama ni hivyo nitakuwa nimekwisha,” Suzana aliingiwa na hofu.
“Suzana acha kujikatia tamaa, hebu tafuta ukweli ili tujue tufanye nini, ikiwezekana twende leo leo, nitaomba ruhusa nikusindikize.”

“Basi wacha nikaombe ruhusa niende kwa Brighton nikapate ukweli, bila hivyo nitachanganyikiwa.”
“Haya shoga utanijulisha,” Suzana aliagana na Sharifa na kwenda kuomba ruhusa kisha alielekea nyumbani kwa Brighton.
                                                            ***
Balkis akiwa amejilaza kitandani na Brighton, alimuona Suzana akielekea pale, kama kawaida yake alimueleza mpenzi wake:
“Suzana anakuja.”
“Umejuaje?”

“Nijue vipi, la muhimu jiandae kumpokea mpenzi wako.”
“Sasa nimpeleke chumba gani?”
“Mlete humu humu.”
“Wewe unatoka?”
“Niende wapi?”

“Si chumba wa wageni.”
“Mi sitoki, Suzana anakuja kukuuliza kama jana alikuja kulala hapa.”
“Umejuaje?”
“Nisikilize kwanza ndipo uliniulize maswali.”
“Mh!”

“Naomba unisikilize, ukijichanganya shauri yako.”
“Mbona unaniambia hivyo?”
“Ndiyo maana nakueleza, nisikilize kwa makini.”
“Sawa.”
“Suzana anakuja kuulizia kama kweli jana alikuja hapa, mjibu kuwa hakuja. Tumeelewana?”
“Lakini mbona mimi nafahamu jana alikuja?”

“Kama alikuja mbona asubuhi hukumuona?”
“Hata mimi nashangaa.”
“Wewe na Suzana mliota ndoto ya aina moja kuwa jana mlikuwa pamoja lakini kila mmoja alipoamka hakumuona mwenzake.”

“Balkis! Mbona unanitisha, wewe ni nani?”
“Kwani wewe unanionaje?”
“Nakuona mtu wa kawaida, lakini unayozungumza yananishangaza sana.”
“Mbona ya kawaida, ni kipawa ambacho mwanadamu hupewa na Mungu kujua yajayo.”
“Mmh! Nilikufikiria vibaya.”

“Ulinifikiria vipi?”
“Labda jini!”
“Brighton tokea lini jini akazungumza na mwanadamu?”
“Huwa nasikia majini huweza kujigeuza na kuwa wanadamu na kuishi nao.”
“Kama ningekuwa jini ungefanyaje?”
“Ningekufa kwa mshtuko.”

Mara kilipita kimya cha ghafla, kitu kilichomshangaza Brighton. Haukupita muda mlango wa chumbani uligongwa.
“Mkaribishe Suzana,” Balkis alimwambia Brighton aliyepatwa na mshtuko.
“Wapi?” Ilikuwa ajabu Balkis alizungumza kwa sauti ya juu, lakini Brighton aliuliza kwa sauti ya kunong’ona.

“Kuwa muelewa, nimekueleza mkaribishe humu ndani.”
“Ili atufumanie?”
“Ndiyo.”
“Ili iweje?”
“Utajua akiishaingia ndani.”

Sauti ya kugonga mlango iliendelea nje huku ikionekana kabisa kitendo cha kuchelewa kufunguliwa mlango kilimuudhi sana Suzana.
“Brighton kama hutaki nije kwako si uniambie kuliko kunifanyia visa?”
“Mkaribishe,” Balkis alimueleza Brighton kwa kumkaripia.
“Ingia,” alimkaribisha akiwa na wasiwasi mkubwa.

Suzana aliingia na kwenda kukaa kitandani, pembeni kabisa ya Balkis. Brighton alikuwa kama mtu aliyeshikwa na ganzi na kushindwa kuelewa kama mpenzi wake ameingia ndani. Suzana baada ya kuingia alimshangaa kwa mara nyingine.
“Brighton upo sawa?”

“Eeh.... aah.. Unasema?” Brighton alijikuta akibabaika kujibu.
“Makubwa ina maana hujaniona naingia?”
“Nimekuona.”
“Hata kunikaribisha? Kweli mapenzi yamekwisha,” Suzana alizungumza kwa sauti ya kilio.
“Suzana...,” Brighton alipotaka kusema alimtupia jicho Balkis aliyekuwa amejilaza pembeni ya Suzana huku akitabasamu.

“Brighton, una nini mpenzi wangu?”
“Si..si..sina,” majibu ya Brighton yalizidi kumshangaza Suzana.
“Kuna nini humu ndani, mbona sikuelewi? Jana nilikuja ukawa katika hali hii hii na leo tena, kuna kitu gani mpenzi wangu! Kwa nini hutaki kuniambia?”
“Brighton mkatalie kwamba jana hakuja hapa,” Balkis alimwambia kwa sauti aliyosikia Brighton peke yake.

“Brighton mbona kama haupo na mimi! Una nini mpenzi wangu?” Suzana aliporomokwa na machozi na kumfuata Brighton alipokuwa amesimama kama kapigwa na shoti ya umeme. Alianza kumpapasa huku akiendelea kumuuliza jinsi alivyoonekana mtu aliyehama kimawazo.

Brighton alikuwa kama yupo ndotoni akijiuliza yanayotokea mbele ya macho yake ni kweli au ni kiini macho. Chumbani kulikuwa na watu watatu, Balkis hakujificha zaidi ya kulala kitandani, tena peupe. Hata Suzana alipoingia, pamoja na kukaa pembeni yake hakuonesha kuona kitu cha tofauti mle ndani.

Alizidi kuingiwa na wasiwasi kuwa huenda Balkis si kiumbe cha kawaida, hata sauti yake aliyompa maelezo bado ilionesha kuisikia peke yake. Kuhama kimawazo kulizidi kumnyima raha mpenzi wake ambaye naye alikuwa na yake yaliyotakiwa kupata majibu kutoka kwa Brighton.

“Brighton jana nimekuja hapa na kulala na wewe, lakini ajabu nilipoamka asubuhi nimejikuta nipo kitandani kwangu. Ni kweli jana nilikuja au nilikuwa naota?”
“Brighton, kataa! Sema hakuja?” Balkis alipaza sauti ya juu.
Lakini Brighton alijikuta mdomo ukiwa mzito kumjibu mpenzi wake huku jasho la hofu likimtoka.

“Brighton una nini mpenzi wangu, nijibu basi, si ni wewe ndiyo ulinipigia simu jana na kuniambia nije?”
“Brighton kataaa,” Balkis alizidisha sauti iliyoumiza ngoma za sikio.
“Brighton kuna nini hapo kitandani mbona unapaangalia sana, au kuna mwanamke?”
“Ha..ha..kuna..ki..”

“Brighton unafanya nini?” Balkis alipiga kelele iliyokuwa na mlio mkubwa kama radi iliyofanya ngoma za sikio za Brighton zisikie maumivu makali.
“Brighton mpenzi wangu una nini au umeshavamiwa na jini Balkis?”
“Nani?” Jina la Balkis lilimshtua.

Kauli ile ilimuudhi jini Balkis, akapuliza upepo uliompata usoni Suzana ambaye aliishiwa nguvu na kupitiwa na usingizi mzito. Brighton alimuwahi kabla hajaanguka chini na kumlaza kitandani pembeni ya Balkis.
“Suzana... Suzana,” alimwita kwa kumtikisa.

Suzana hakujibu kitu, alionekana mwenye usingizi mzito. Brighton alimuona Balkis jinsi alivyompuliza hadi kupitiwa na usingizi mzito.
“Balkis umemfanya nini Suzana?”
“Acha upumbavu,” Balkis alimjibu kwa hasira.

“Balkis mbona sikuelewi?”
“Hunielewi kivipi?”
“Itakuwaje umpulize mtu apoteze fahamu?”
“Nilikwambia nini?”
“Nilikwambia utoke, kwa nini hukutoka?”

“Mimi ni nani yako?”
“Kwa tabia yako ya miujiza siwezi kukuoa, unaonekana si mtu wa kawaida.”
“Unasemaje?” Kauli ile ilimchefua Balkis.
“Siwezi kukuoa.”
“Kweli?”

“Kweli,” Brighton alijibu kwa kujiamini.
“Asante.”
Baada ya kusema vile Brighton alishangaa kuona sura ya Balkis ikijikunja na kuwa kama mzee, uzuri wote ulipotea. Wasiwasi ilizidi kumjaa kwa kuamini huenda kweli Balkis si mwanadamu wa kawaida bali ni jini.

Baada ya kugundua kuwa Balkis si kiumbe wa kawaida, aligeuka ili awahi kuchukua Biblia ili amkemee, hakupiga hata hatua moja, mkono wa Balkis alinyooka na kuwa mrefu, ukamrudisha alipokuwa, kisha alimshika sehemu za siri na kuzivuta kwa nguvu kama anatoa kitu.

Brighton alihisi kama amepigwa shoti ya umeme sehemu za siri kisha alizisikia zikiwa za baridi kama zimetoka kwenye jokofu. Kwa sauti kali ya hasira Balkis alisema:
“Hutasimamisha milele, na mkeo hatazaa milele.”

Baada ya kusema vile aliingiza mkono sehemu za siri za Suzana ili amtoe kizazi, kabla hajamtoa Brighton alipiga kelele:
“Hapana, Balkis usifanye hivyo.”
“Lazima niwatie adabu, binadamu gani asiye na shukrani.”
“Nisamehe Balkis nipo tayari kukuoa.”

“Mpaka kwa shinikizo?”
“Siyo hivyo, mambo yako yananichanganya nashindwa kukuelewa wewe ni mtu wa aina gani?”
“Mimi ni jini?”
“Eeh!” Brighton alishtuka.
“Unashtuka nini, mimi ni jini la chini ya bahari.”

“Mungu wangu nimekwisha miye.”
”Uishe kivipi, katika muda tuliokuwa wote uligundua tofauti gani kwangu?”
“Sijagundua.”
“Penzi langu na wanadamu wenzio lipi lilikuwa tamu?”
“La kwako.”

“Mimi na mchumba wako nani mzuri?”
“Wewe.”
“Nani aliyesema kwamba Suzana hafai kuolewa?”
“Mimi.”

“Nilijitoa kwako ili kurudisha furaha iliyopotea, pamoja na kukubali kunioa bado nilimheshimu mpenzi wako, kosa langu nini?”
“Nisamehe.”
“Nitakusamehe, lakini nakurudishia ugonjwa wako ambao hautapona milele.”
“Nisamehe Balkis nilikuwa sijajua.”

“Hujajua nini?”
“Hata sijui nilimaanisha nini nimechanganyikiwa Balkis, nisamehe sana.”
“Mimi nakusamehe, lakini nakuacha na matatizo yako na mpenzi wako.”
“Hapana usinifanye hivyo.”
Balkis atamsamehe Brighton? Kuyajua yote tukutane KESHO.
Like: www.facebook.com/2jiachie

No comments

Powered by Blogger.