MFALME MPYA SIMBA
Mshambuliaji Danny Sserunkuma raia wa Uganda.
UONGOZI wa Simba, sasa umeamua iwe isiwe ni kuhakikisha inamnasa mshambuliaji Danny Sserunkuma raia wa Uganda ambaye ni mfalme wa mabao.Sserunkuma amekuwa mfungaji bora wa Ligi Kuu Kenya mara mbili ndani ya misimu mitatu aliyoichezea Gor Mahia.
Pia ameiwezesha timu hiyo kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Kenya baada ya kuikosa kwa miaka 18, Nairobi anatambulika kama Mfalme wa Gor, sasa atakuwa Mfalme wa Simba.Habari za uhakika kutoka ndani ya Simba zimesema uongozi umemaliza mchujo na Sserunkuma ndiye chaguo la mwisho-mwisho.
“Mazungumzo yameanza na wahusika, inaonekana tunakwenda vizuri, lengo ni kuhakikisha anatua nchini kufanya kazi Msimbazi.“Ukiangalia msimu huu amekuwa mfungaji bora, miaka miwili alitwaa taji hilo tena kwa kufunga mabao 18. Utaona kuwa anastahili,” kilieleza chanzo.
Nani ataachwa?
Mchezaji wa kigeni atakayetemwa, nafasi ya kwanza ipo kwa Paul Kiongera kwa kuwa kwa ugonjwa wake wa goti, inaonekana hakuna nafasi ya kurejea ndani ya miezi miwili, Simba inataka ‘jembe’ la kazi sasa.
Gor Mahia:
Hata hivyo, taarifa zinaeleza uongozi wa Gor Mahia nao umekuwa katika harakati za kuhakikisha mkali huyo kwa misimu mitatu mfululizo anabaki Nairobi.
Phiri:
Kocha Mkuu wa Simba, Patrick Phiri, amethibitisha kwamba naye anaona ni vema kumpata Sserunkuma.
“Ni mshambuliaji mzuri, kama atapatikana atatusaidia sana na uongozi najua unalishughulikia,” alisema Phiri.
Okwi & Sserumkuma:
Simba inaamini, mshambuliaji huyo mwenye umbo dogo atashirikiana vizuri na Mganda mwenzake Emmanuel Okwi kuhakikisha wanatengeneza safu kali ya ushambuliaji.
Okwi na Sserrunkuma, wote wamesoma shule moja ya St Mary iliyo katika eneo la Kitende jijini Kampala. Shule hiyo imekuwa maarufu kuzalisha wachezaji kama David Obua, Eric Obua na Ibrahim Juma.
Mataji:
Sserunkuma yuko katika kikosi cha Uganda ‘The Cranes’ chini ya Sredojevic Milutin ‘Micho’.
Mwaka 2012, Sserunkuma alikuwa Mchezaji Bora wa Kenya baada ya kuisaidia Gor kutwaa ubingwa.
Mwaka 2013, Sserunkuma alitwaa tuzo ya mchezaji bora inayotolewa na wanahabari wa Uganda ya USPA, akimshinda Tonny Mawejje anayekipiga nchini Norway.
Zola:
Sserunkuma amekuwa akifananishwa na kiungo wa zamani wa Chelsea, Gianfranco Zola kwa kuwa ana umbo dogo, lakini ana nguvu, kasi, mashuti, fundi wa kufunga na pia anatoa pasi za uhakika za mwisho.
CREDIT: CHAMPIONI
Post a Comment