ad

ad

AHADI YA NDOTONI - 10


ILIPOISHIA;
“Sister sisi tupo hapa muda mrefu umekuja mmetukuta, sasa nani kaondoka?”
“Mbona sasa siyo wenyewe.”
”Kina nani?”
“Sadat tuondoke hapa hapatufai.”

“Samahani brother,” jamaa aliyekuwa amekaa meza ya pili alisema.
“Bila samahani.”
“Huyu ni mpenzi wako?”
“Ni dada yangu.”

“Hajawahi kupatwa na ugonjwa wa akili?”
“Bado.”
“Muwahishe hospitali huenda malaria imeanza kumpanda.”
SASA ENDELEA...

Kauli ile ilimuumiza moyo Lakashina, hakutaka kusema kitu, alijikuta akidondokwa na machozi.
“Sadat unasubiri nini? Kama hutaki kuondoka nakuacha,” Lakashina alitoka eneo la hoteli na kwenda kwenye gari la Sadat, alifungua mlango wa gari na kuingia ndani. Wakati huo Sadat alikuwa bado anazungumza na jamaa ambao walikuwa wakimshangaa Lakashina.

Lakashina alimuona Sadat anachelewa aliteremka kwenye gari na kwenda kukodi gari lililokuwa likishusha mtu njiani. Alipoingia ndani ya gari hakuwa na hamu ya kurudi dukani, alimwambia dereva ampeleke moja kwa moja kwake.

“Nipeleke Mbezi.”
“Ipi?”
“Beach.”

“Elfu thelathini.”
“Nani kakwambia siwezi kukulipa?” Lakashina alijibu kwa hasira.
“Siyo hivyo dada, wapo ambao ukiwaambia mwisho wa safari wanalalamika.”
“Nimekueleza sitaki maelezo zaidi niwahishe nyumbani.”

Dereva aliondoa gari kuelekea Mbezi akiwa na mawazo mengi juu ya hali ya yule dada aliyeonesha kuchanganyikiwa.
Alipofika kwake alilipa fedha na kwenda moja kwa moja chumbani kwake, alijilaza kitandani akiwa mwingi wa mawazo juu ya yote yaliyomtokea muda mfupi baada ya kumuona mwanaume aliyefanana na mumewe Lakashi zaidi ya mara mbili.
Alijiuliza ni wasiwasi wa kuonesha anatoka nje ya ndoa yake na Lakashi kufikia hatua ya kumuona kila sehemu aliyokwenda. Aliamua kujilaza ili Lakashi aje ndotoni na kuzungumza naye lakini alilala mpaka jioni hakukuwa na sura wala kivuli cha Lakashi.
Baada ya kuamka alikwenda kwenye kabati kuangalia mafusho ya kumwita Lakashi lakini cha ajabu hayakuwemo. Alijiuliza yamekwenda wapi au aliyamaliza, alijikuta akipandwa na hasira na kusema kwa sauti.

“Nasema siogopi chochote kama na wewe umeamua kuondoka sawa, njoo uchukue kila kilicho chako na uniache peke yangu. Nahitaji maisha ya kujitawala.”

Lakini hapakuwa na jibu lolote zaidi ya kimya cha ajabu kutokea ndani, hali ile ilimtisha na kujiuliza ilitokana na kitu gani au Lakashi amekasirika na kuja kumtia adabu? Wasiwasi ulimjaa na kutoka nje, kama kuna tatizo basi apate msaada.

Alitoka nje lakini alikuta hali ya kawaida, alizidi kushangaa mauzauza yakimuandama. Aliamua kurudi ndani, akiwa ndani alipigiwa simu kuwa anatakiwa dukani. Aliingia kwenye gari na kwenda mjini, alipofika dukani alishangaa kukuta duka limepungua sana, kitu kilichomshtua.
“Vipi kuna usalama?” Aliuliza huku akitweta.

“Kwema tu vipi ulikwenda wapi, kuna mteja mmoja alikuwa akitaka mali nyingi hivyo tulikupigia ili mzungumze naye lakini alionesha ana haraka ameacha karatasi na kuondoka.”
“Na vitu vya dukani vimekwenda wapi?”
“Amenunua yeye.”

“He! Alikuja na gari kubwa?”
“Eeh dada.”
“Ningempata mtu kama huyo ningefanya naye biashara nzuri.”

“Kweli dada hatujawahi kuuza mali nyingi toka tufungue duka, mali ya kuuza miezi mitatu tumeuza kwa siku moja. Ukipata wanne kama yule kaka ungekuwa milionea.”
Habari zile zilirudisha furaha moyoni mwake na kusahau yaliyomsibu muda mfupi. Akiwa na furaha alizungumza na wafanyakazi wake:
“Jamani leo mmefanya kazi nzuri naombeni mfanye usafi kisha niwape mapumziko ya wiki,  kesho kutwa lazima nisafiri kufuata biashara nyingine. Pia mtapata ahsante ya mshahara wa mwezi mmoja.”
“Asante dada, inaonesha yule kaka alikuwa na fedha nyingi, roho iliniuma pale alipotuonesha fedha na kutueleza alitaka zote ziishie dukani, alisikitika na kusema fedha alizokuja nazo hata robo haikufika.”
“Jamani, hakusema atarudi lini?”

“Hakusema zaidi ya kuacha mawasiliano kwenye karatasi.”
“Haya endeleeni kufanya usafi mimi nipo hapa nje.”
Lakashina alikaa kwenye kiti chake na kufungua kile kikaratasi ili apate mawasiliano na mteja ambaye alionesha kutaka kuyabadili maisha yake. Alifungua na kukutana na neno lililomfanya arudie kusoma zaidi ya mara tano lilikuwa lile lile, hakuyaamini macho yake ilibidi amwite mfanyakazi wake mmoja amsomee aliamini kabisa alichokisoma sicho kilichoandikwa, kingine kilichomshtua na manukato ya karatasi ambayo hayakuwa mageni puani mwake.
“Zubeda njoo unisaidie kusoma kikaratasi hiki.”

Alipofika alimpa na kukisoma kisha alimgeukia Lakashina na kumuuliza:
“Kwani dada kuna nini?”
“Hilo karatasi limeandikwa nini?”
“Sijui ni jina au nini?”
“Zubeda kumeandikwa nini? Sitaki maswali,” Lakashina alisema kwa sauti ya ukali kidogo.

“Limeandikwa Lakashi.”
“Eeh!” Alishtuka.
“Lakashi.”
“Mmh! Upo sahihi?”

“Sahihi kabisa kwani vipi?”
“Huyo kaka unamfahamu?”
“Ndiyo leo tumemuona.”
“Hakuniulizia?”

“Mmh, sidhani kwani alipofika mimi ndiye wa kwanza kuonana naye kisha aliniuliza tunauza vitu gani. Nilimueleza tunavyouza, akafungua begi lake na kutoa pesa kununua vitu alivyotaka. Nilishangaa duka lilipungua kabisa kutokana na vitu vingi alivyonunua na baada ya manunuzi aliondoka. Kwani vipi?”

“Mtu huyo yuko vipi?”
“Kama Mpemba hivi.”
“Amenyoa o?”
“Ndiyo.”

“Ana kionja mchuzi?”(ndevu za chini ya mdomo).
“Ndiyo.”
“Hana nywele nyingi kichwani?”
“Ndiyo.”

“Si mtu wa kukasirika, ni mtu wa kutabasamu muda wote?”
“Tena lazima niseme ukweli, nimeshaona wanaume wazuri lakini yule kaka ni mzuri sana. Pamoja na uzuri wake ni mwenye huruma na mpole sana.”

“Siyo mume wangu huyo?”
“Mumeo! Dada umeolewa?”
“Ooh, samahani achaneni na hayo, alivaa nguo gani?”

“Alivaa  kama Wahindi, suruali na shati kama kanzu lakini vilikuwa vimedariziwa kwa nyuzi kama za hariri, pia chini alivaa makubazi ya bei mbaya.”
“Jamaniii.”
“Kwani vipi?”

Wakati huo Sadat alikuwa akiingia dukani na kumshangaa Lakashina.
“Mbona umeniacha?”
“Sadat naomba leo uwe mbali nami nina mambo mengi sana yanahitaji niwe peke yangu.”

“Kwa nini nisikupe msaada wa kimawazo?”
“Sadat kuwa mwelewa, sitaki chochote kwako nakuomba uondoke mbele yangu mara moja.”

Lakashina alikuwa mkali kitu kilichowashangaza hata wafanyakazi wa dukani kwake. Waliamini kabisa Lakashina na Sadat ni wapenzi. Sadat aliondoka bila kuongeza neno, akizidi kuamini maneno ya jamaa waliowaacha hotelini kuwa Lakashina lazima atakuwa amechanganyikiwa.

Baada ya Sadat kuondoka, Lakashina alichukua karatasi na kuisoma upya, jina lilikuwa lile lile Lakashi, manukato yaliyokuwa yakinukia ni yale yale ya Lakashi mume wake ambayo hakuwahi kuyasikia sehemu yoyote duniani.

“Eti baada ya kununua alisema nini?”
“Dada alisema shida yake akuone wewe, kwa vile hatukujua upo wapi nawe ulitueleza unapokuwa umepumzika hutaki simu hatukuwa na jinsi.”
“Mkononi hana pete ya rangi ya zambarau?”
“Mmh! Dada kwa kweli hatukumchunguza.”

“Sasa fanyeni hivi, kila mmoja atachukua kiasi chake cha pesa, zitakazobaki mtaziacha kisha fungeni duka, funguo mtaniletea nyumbani.”
Kauli ya Lakashina iliwachanganya sana wafanyakazi wake kuonesha taarifa walizompa zimemchanganya sana. Walijiuliza mteja na tajiri yao wana uhusiano gani kiasi cha kumchanganya kiasi kile?

Kabla hawajapata jibu, Lakashina alikuwa tayari kwenye gari lake na kuondoka bila kuongeza neno. Lakashina alionekana kama kuchanganyikiwa na habari zile. Alijiuliza kile kinachomtokea ni nini? Muda mfupi amemwona mtu kama mumewe akipita lakini hakuwa yeye, wakati amekaa amemwona mtu mwingine kama yeye lakini hakuwa yeye. Anakwenda dukani anakutana na taarifa za mtu anayeitwa Lakashi, jina ambalo alijua ni mumewe, hata manukato ya karatasi iliyoachwa ujumbe yalinukia harufu ile ile.

Alijiuliza maswali yasiyo na majibu kuhusu mtu anayejiita Lakashi, bado akili yake haikukubali kwa kuamini Lakashi anayemfahamu yeye asingefika kununua vitu kwenye duka lake akijua kabisa yeye ndiye mmiliki mkuu wa duka lile.

Alipofika nyumbani alikwenda kuchukua udhu japo alikuwa ameshaasi kuswali, baada ya kuchukua udhu alilala usingizi. Pamoja na kuchukua udhu bado Lakashi hakuonekana usingizini. Alishtuka alfajiri ya siku ya pili bila kumwona Lakashi alijikuta akizidi kuchanganyikiwa.

Wazo lingine lilikuwa huenda ni wasiwasi wake Lakashi ameamua kuachana naye, alijikuta akijilaumu kwa kumkaripia Sadat, alichukua simu yake na kumpigia Sadat ili kumuomba msamaha.

Alipopiga simu ilipokelewa upande wa pili na sauti ya kilio ya Sadat akiomba msamaha.

“Basi nimekoma... sirudii tena... simfuati tena... mama nakufa.”
Kelele za Sadat kuonesha anapata kipigo kizito zilimshtua Lakashina.

Aliyenunua vitu dukani ni Lakashi gani? Na Sadat anapigwa na nani?
LakasHina alijiuliza kauli ya Sadat ilikuwa inamaanisha nini, amekoma, amekoma nini? Harudii tena, harudii tena nini? Hamfuati tena, hamfuati tena nani?
Lakashina alipiga tena simu kwa Sadat kupata uhakika wa kile alichokisikia.

Simu upande wa pili iliita na kupokelewa.
“Haloo Lakashina.”
“Haloo Sadat, upo sawa?”
“Nipo sawa kwani vipi?”
“Hapana.”

“Mbona simu usiku?”
“Sadat kabla ya yote hebu nieleze ukweli upo sawa?”
“Lakashina mbona tangu tulipoachana mi nipo sawa, nilijua kuna kitu kimekuchanganya ndiyo maana niliondoka bila kukusumbua,” Sadat alimjibu Lakashina bila kulielewa swali lake lilikuwa likimaanisha kelele za muda mfupi alizosikia kwenye simu na si mambo yaliyotokea mchana.

“Sadat si mambo ya mchana, ya usiku huu.”
“Mi nipo sawa.”
“Kama upo sawa vizuri.”
“Vipi ulikuwa unasemaje?”

“Kuhusiana na mambo ya mchana, najua nimekukosea naomba unisamehe.”
“Lakashina mbona nilikusamehe tokea hiyo jana, na pia suala hili hata ungenipigia asubuhi tungezungumza bila tatizo.”
“Sadat basi nilikuwa naomba kesho nije kwako usitoke.”
“Hakuna tatizo.”

Lakashina aliagana na Sadat na kujilaza kitandani akiwa bado hajapata jibu la lile alilolisikia kwenye simu. Alijiuliza sauti aliyoisikia kwenye simu kama ya Sadat akiomba msamaha ni ya nani? Lakini akili yake iliamini ni ya Sadat, kilichomshangaza baada ya kumpigia simu Sadat amemkuta kwenye hali ya kawaida.

Hakutaka kujisumbua sana kuwaza, alivuta shuka na kujilaza.
Siku ya pili Lakashina aliamka na kwenda moja kwa moja kwa Sadat, alipofika alimkuta ndiyo anaamka. Sadat alipomuona Lakashina ambaye siku ile hakuvaa mavazi ya kuuficha mwili, alichanganyikiwa. Alivaa nguo za kidunia za kuiacha sehemu kubwa ya mwili wake wazi.

“Karibu mpenz....,” Sadat hakumalizia neno lake.
“Sadat hofu yako, niite tu mpenzi.”
“Haya mpenzi karibu.”
“Asante, ndiyo unaamka?”

“Ndiyo, huwezi kuamini leo mwili umekuwa mchovu kuliko kawaida, yaani jana baada ya kuzungumza na wewe kuna njozi moja niliota na nilipoamka asubuhi bado mwili ulikuwa umechoka kama nimepigwa.”
“Sadat hiyo njozi umeota kabla ya kukupigia au baada ya kukupigia?”
“Baada ya kunipigia.”

“Uliota nini?”
“Ni mmh, we acha, ngoja nitoke kuoga nitakueleza.”
“Mmh! Sawa.”

Sadat alimuacha Lakashina sebuleni na yeye kuelekea bafuni kuoga, kwa upande wa Lakashina ile ndiyo ilikuwa siku yake ya kwanza kuingia ndani kwa Sadat. Aliliangalia jumba zuri la Sadat ambalo halikuwa na mwanamke ambaye angeongeza uzuri wake.

Moyoni alilisifia huku akitamani siku moja awe mama wa jumba lile. Akiwa katikati ya dimbwi la mawazo, sauti ya kilio cha kuomba msaada ya Sadat ilisikika kutoka bafuni.

“Samahani... utaniua bure, sijamwita... kaja mwenyewe, nisamehe...nisamehe nimekoma...nakuapia sitarudia tena, kama ukiniona hata namsalimia nifanye lolote, nipo chini ya miguu yako tafadhali usiniue.”

Sauti ile ilimshtua,  haikuwa na tofauti na aliyoisikia usiku wakati alipompigia simu Sadat kwa mara ya kwanza. Alijiuliza sauti ile ni ya Sadat lakini mhusika alikuwa amekwenda kuoga, alijiuliza ni nani mwenye sauti kama ya Sadat anayemchezea akili.

Sauti ya kulalamika maumivu iliendelea huku sauti ya mtu kupigizwa ukutani ikizidi ndani ya nyumba ile. Mwanzo aliidharau, baada ya sauti ile kuzidi kulalamika huku ikionesha wazi malalamiko yale yanamhusu yeye, alishtuka. Wasiwasi ulimjaa lakini kwa ujasiri mkubwa alielekea bafuni akaone kuna kitu gani kimempata Sadat au ni hali ile ile sauti ya ndotoni.

Mlango wa bafu ulikuwa umerudishwa kidogo, Lakashina alisimama mlangoni na kumwita Sadat, wakati huo hakukuwa na sauti ya mtu kulalamika.
“Sadat... Sadat,” hakukuwa na jibu zaidi ya ukimya wa ajabu kutawala sehemu ile.

Akiwa anajifikiria kufungua mlango alishtushwa na michirizi ya damu, alitaka kukimbia lakini alijipa moyo ili ajue mwisho wa damu ile. Alipaza sauti yake tena kumwita Sadat kwa sauti ya kitetemeshi.
“Sadat upo sawa?”

Vile vile hakupata jibu lolote, kitu kilichozidisha wasiwasi. Wakati huo damu zilizokuwa zikitoka bafuni zilianza kuongezeka. Kabla ya kuusukuma  mlango alijiuliza damu ile ni ya nani na Sadat alikuwa wapi?

Je, damu ile ni ya nani? Sadat yupo salama kweli na zile sauti ya kutisha ni za nani? Kuyajua yote tukutane wiki ijayo. 
Like: www.facebook.com/2jiachie
Web: www.2jiachie.com

No comments

Powered by Blogger.