ad

ad

AHADI YA NDOTONI - 08



ILIPOISHIA;
Lakashina alishindwa awajibu nini, huruma ilimjaa moyoni lakini onyo alilopewa muda mfupi lilimtisha kwa kuhofia maisha yake.

Alijikuta akiporomokwa na machozi na kukosa la kuwaeleza baba zake wadogo.
SASA ENDELEA...
Lakashina huruma ilimjaa moyoni jinsi baba zake wadogo walivyokuwa wakilalamika mateso waliokuwa wakipata kutoka kwa mumewe. Pamoja na kulazimishwa kuchukua mali zake bado aliona kuna umuhimu wa kusimama yeye kama yeye kuwatetea baba zake wadogo.

Alikumbuka siku moja ndotoni aliyaona maisha ya tabu ya baba zake wadogo baada ya kumdhulumu mali yake. Alijikuta akiwahurumia wao badala ya kuwachukia na asubuhi alipoamka alikosa raha kabisa.

Alijifikiria  kama ni kweli baba zake wadogo ndivyo walivyo, kwa muda ule hakukuwa na haja ya kuwalazimisha warudishe mali zaidi ya kuwasamehe.

Akiwa bado anabubujikwa na machozi huku upande wa pili wa simu ukiendelea kuomba msaada wake kuwaokoa na mateso. Aliwasikia wakisema;

“Mama siku hizi hatulali ni mateso mtindo mmoja ili turudishe mali yako, japo tunajua tuna kazi ya kurudisha vitu vyote.

Basi mtupe muda, nasema laana yako kwetu ilikuwa kubwa kwani baada ya kukufukuza haikupita muda tukaanza kugombana wenyewe kwa wenyewe na kufikia uamuzi wa kuuza sehemu kubwa ya mali, hata pesa tulizogawana iliyeyuka bila kufanya jambo lolote la maana.

“Lakashina tunakuomba utusamehe tunajua tulikutenda, lakini hakuna tulichopata toka kwenye mali ya wazazi wako zaidi ya dhambi na mateso.”

Maneno yale yalizidisha kuumiza moyo wa Lakashina kuona jinsi gani dhuluma ilivyo na malipo mabaya. Machozi yalimtoka bila kizuizi kila alipotaka kuzungumza alikosa maneno zaidi ya kuendelea kulia.

Ghafla sauti ya upande wa pili ilibadilika na kuwa nzito, haikuwa ngeni tena masikioni kwake wala hakuishangaa, aliisikiza ina ujumbe gani tena.
“Lakashina...Lakashina,”  sauti ilijirudia kama mwangwi zaidi ya mara tatu.

“Moyo wako unaonekana kabisa unataka kuniudhi, sitaki ubadili uamuzi wangu.”
“Siwezi...siwezi.”
“Lakashina huwezi nini?”
“Nasema siwezi.”

“Sikia Lakashina najua kabisa unataka kuwahurumia baba zako wadogo viumbe wasio na huruma, kama huwezi niachie hiyo kazi mimi watarudisha tu.”

“Watatoa wapi?” Lakashina alijikaza na kujibu.
“Hiyo hainihusu, watapata mateso mpaka wanaingia kaburini.”
“Hapana...hapana.”

“Hapana nini?”
“Nasema tena hapana.”
“Huwezi kuzuia hasira zangu huenda zikakurudia wewe.”
“Sawa...sawa na zinirudie, lakini nakuomba uwaache kama mateso uliyowapa yanatosha na mali hawajarudisha.”

“Hapana Lakashina hata siku moja mwanamke hana kauli kwa mumewe.”
“Ha! Kumbe ni wewe mume wangu Lakashi?”
“Si muhumu kujua.”
“Kama si muhimu kujua nakuomba uachane nao mara moja.”

“Unanishurutisha?”
“Ndiyo, kama mali zako chukua niache na maisha yangu ya mateso,” Lakashina alijibu kwa ujasiri mkubwa.
“Lakashina ujasiri huo umeutoa wapi?”
“Si muhimu kujua.”

“Lakashina,” sauti nzito ilimuita, lakini  hakuitikia aliendelea kulia kuonesha hasira zake zipo kwa yule mtesaji asiye na chembe ya huruma.
“Lakashina umekasirika?”

Hakumjibu aliendelea kulia kilio cha kwikwi, kifua kikiwa kimefura kwa hasira,  alijiegemeza kwenye kochi. Mkono laini  uliokuwa ukimpapasa shingoni ukifuatiwa na manukato aliyoyazoea yalimfanya anyanyue uso.  Alishtuka kumuona mumewe Lakashi katika uso wa tabasamu.

“Laazizi unalilia nini?”
“Unajua, unajua Lakashi,” Lakashina alilia kilio cha kwikwi.
“Kuhusu nini?”
“Mimi nani yako?”
“Mke wangu.”

“Kwa nini hutaki kunisikiliza?”
“Kuhusu nini?”
“Baba zangu wadogo.”

“Ni hilo tu mpenzi?”
“Ni hilo, pia ni maisha gani ya kutishana.”
“Nani kakutisha?”

“Sijui nani kanipigia simu amesema kama nikiwasamehe basi nitamtambua.”
“Asikutishe, mwenye mamlaka juu yako ni mimi mumeo na si mwingine.”

“Na aliyekuwa akizungumza ni nani?”
“Achana naye ila nakuahidi baba zako hawataguswa tena na ikiwezekana nitawabadilishia maisha yao.”
“Asante mpenzi,” Lakashina alitabasamu na kumkumbatia mumewe kwa furaha.

Aliposhtuka alijikuta amelala kitandani peke yake na kujiuliza yaliyotokea ilikuwa ndoto au kama kweli mume wake kipenzi yupo wapi ila harufu ya manukato ilitawala chumba kizima.
Lakashina alitoka hadi sebuleni, lakini hakumuona mtu. Milango ilikuwa imefungwa kama alivyoifunga ila manukato ya Lakashina yalitawala kila kona. Hakutaka kumuuliza mtu kwani alijua mumewe alirudi kwa ajili ya kutuliza akili lakini hakurudi rasmi.
Baada ya mwezi mmoja, siku moja akiwa anatoka kuswali swala ya alasiri, alipigiwa simu kutoka kwa baba zake wadogo.

“Haloo ba’ mdogo.”
“Haloo mama.”
“Shikamoo.”
“Marahaba.”
“Ndiyo baba.”

“Tunashukuru sana mama.”
“Kwa kipi?”
“Kweli wewe ni kiumbe cha ajabu.”
“Kivipi?”

“Pamoja na kukufanyia mambo mabaya bado umeonesha moyo wa kibinadamu, mumeo ametusamehe na wewe kutuwezesha tuishi maisha ya raha.”

Lakashina alishtuka na kutulia kwa muda kujiuliza amewezaje kuwawezesha kuishi maisha ya raha, lakini alikumbuka kauli ya mumewe kwenye njozi kuwa ataisaidia familia yake.
“Ndiyo hivyo baba, siku zote ubaya ukilipwa wema, hukosa nafasi.”

“Ni kweli mwanangu, kwa ulichotutendea tumejifunza kuwa ubaya haufai.”
“Ni kweli wazazi wangu, mimi niliwasamehe japo niliapa sitawasamehe.”

“Asante mama, sasa tumekaa kikao cha familia zote tumepanga kuja kukutembelea tujue unapoishi na kuja kukushukuru kwa kuyanyanyua tena maisha yetu.”

Lakashina kabla ya kuzungumza alihisi simu ya moto iliyomuunguza sikioni, kitu kilichomfanya aitoe haraka. Alipoiangalia alikuta imezima, alishtuka na kujiuliza kuna kitu gani kilichofanya simu iwe ya moto kiasi kile. Alipotaka kuiwasha iligoma kuwaka, alizidi kushangaa. Kama kuichaji muda si mrefu alikuwa ameitoa kwenye chaji na ilionesha imejaa.

Haikuwahi kutokea hata siku moja simu izimike muda mfupi toka alipoitoa kwenye chaji. Wakati akijaribu kuiwasha ilimuunguza  tena mikononi kitu kilichofanya aitupe chini. Ilipogusa chini ilijiwasha yenyewe na kuanza kutoa mlio wa simu kuingia.

Aliitazama kwa muda akiiogopa kuipokea, mlio uliongezeka kila dakika na mwisho wake kuwa kero, aliinama aichukue.
Kwa kuhofia kuungua aliigusa kwa mbali ili kuona kama moto wake unashikika, lakini ajabu simu ilikuwa ya kawaida haikuwa na moto wowote.

Aliiokota na kushangaa kutoonekana namba ya mpigaji. Simu iliita ikiwa kama imezimika, akaipeleka sikioni na kuzungumza.
“Ha..a..loo.”

“Haloo,” sauti ya upande wa pili iliitika, ilikuwa nzito kama ya awali iliyokuwa ikimtisha, mapigo ya moyo yalimwenda kwa kasi lakini iliyadhibiti.
“Ndiyo unasemaje?”

“Nakuomba usiwaruhusu ndugu zako wakusogelee, ulichowafanyia kinatosha.”
“Kwa nini wasinisogelee?”
“Ni viumbe wabaya.”

”Lakini wameshagundua kosa lao, hivyo wanakuja kunishukuru pia kurudisha uhusiano uliopotea.”
“Lakashina nisikilize mimi tusibishane,” sauti ya upande wa pili iliongeza ukali.

“Sibishani na wewe, siku zote kiumbe anayegundua makosa yake na kuyakubali kisha kuomba msamaha anatakiwa kusamehewa.”
“Nakuomba uniamini nikwambiayo, familia yako ni viumbe wabaya kuliko kifo, nakuomba achana nao kabisa.

Ni kweli kwa sasa hawana nia mbaya, lakini nakuhakikishia maisha unayoishi wakiyaona, lazima watabadilika na kupanga mipango ya kukudhuru.”

“Wee umejuaje?”
“Sitaki malumbano, wee wakaribishe litakalotokea utalimaliza mwenyewe. Wewe si mwepesi wa kujiua sasa hivi kifo kitakukimbia ili ufaidi jeuri ya kiburi chako.”

“Sasa niwajibu nini?”
“Wajibu kwamba haupo nchini.”
“Nikikutana nao je?”
“Hautakutana nao milele.”

“Sawa nimekuelewa.”
“Umenifurahisha Lakashina, unaonekana muelewa.”
Baada ya kusema vile, sauti ile iliendelea kushukuru kwa kusema maneno ya kujirudia:
Asante Lakashina...Asante Lakashina sauti ile ikizidi kufifia na kutoweka kabisa.

Baada ya sauti ile kutoweka, Lakashina alibakia akiwaza juu ya ujumbe ule na tabia za baba zake wadogo.

Aliamini kabisa kama baba zake kweli watayaona maisha anayoishi ni mazuri kiasi kile, lazima roho zitawauma na kuanzisha mpango mwingine wa kumuangamiza ili wazipate zile mali.
Alijiuliza hali ile inatokana na nini? Na kwa nini sauti zile kuna moja ilitaka atiwe adabu na nyingine ilikataa. Alikumbuka dua aliyofundishwa na ustaadh mmoja aliyekuwa akimfundisha mafunzo ya dini ya Kiislamu ya kufukuza vitu vibaya.

Aliisoma komoyomoyo huku mbavu zikimbana, alipoimaliza ile dua viungo vya mwili aliviona vinafanya kazi. Lakini hali ya hewa bado ilikuwa nzito na harufu mbaya iliendelea kutawala chumba kizima. Alipapasa mkono kuitafuta swichi ya taa. Alipoipata aliwasha, baada ya taa kuwaka alishangaa kujikuta yupo kitandani mwake na ndani ya chumba kulikuwa kama siku zote.

Kingine hali ya hewa ilikuwa ya kawaida ya harufu nzuri ya manukato, wala hakukuwa na sauti tena za watu kubishana. Aliketi kitandani jasho likimvuja na kifua kikiwa kizito, alikohoa mfululizo mpaka machozi yakamtoka.

Alijiuliza mbona chumbani kuna hali ya kawaida lakini kifua chake bado kizito? Kilichotokea ilikuwa ni ndoto au nini? Alinyanyuka kwenda kutawadha kwa vile alfajiri ilikuwa inaingia. Alikwenda kuswali, alipomaliza kuswali hakunyanyuka haraka kwenye msala wake. Aliyafikiria yaliyomtokea muda mfupi kabla ya kuamka yalikuwa na maana gani.

Alinyayuka na kwenda kulala kutokana na kusumbuliwa na kifua, akiwa amejilaza kitandani simu yake iliita. Aliipokea na kuanza kuzungumza.
“Haloo.”

“Lakashina kwa nini umepinga amri yangu?” Sauti nzito ya upande wa pili iliuliza, kwa vile alikuwa ameizoea hakushtuka.
“Ndiyo maana unataka kuniua?” Aliiuliza ile sauti ambayo hakujua ni ya nani.

“Hujanijibu kwa nini unapinga amri yangu?”
“Nipinge! Wewe nani?”
“Siyo lazima kunijua.”
“Kama hutaki nikujue basi achana na mimi.”
“Mbona unaonekana una kiburi?”

“Kiburi gani, jitokeze ili nijue nazungumza na nani na unieleze kwa nini unanikataza.”
“Lakashina kumbuka hukuwa mtu mbele ya watu, leo unajisahau?”
“Sijajisahau, kosa langu nini?”

“Sasa kwa nini unapinga kila ninachokueleza, umevunja amri kwa kuwaleta wazazi wako, bado hukuona kuwa hiyo imetosha, umeamua kukaa na adui ndani.”
“Adui?”
“Eeh, adui.”

“Adui nani?”
“Kwani unakaa na nani?”
“Na wafanyakazi wangu wawili na mdogo wangu.”
“Basi huyo mdogo wako ndiye atakayekumaliza.”
“Mbona sikuelewi, animalize vipi mtoto mdogo?”

“Lakashina unasahau matatizo haraka sana lakini utanitafuta na hautanipata.”
“Lakini wewe ni nani?”
“Kama hutaki kunisikiliza kwa lile la ukweli hata ukinijua haitasaidia kitu.”

“Basi kama hutaki nikujue, niache na maisha yangu.”
“Eeh, leo unasema hivyo wakati ulikuwa ukitembea barabarani ukizungumza peke yako?”
“Hata nikizungumza, wewe inakuhusu nini?”
“Asante mama yangu, yameishia hapa ila utanitafuta na hautaniona kamwe.”

“Nikutafute vipi mtu sikujui?”
Baada ya mabishano yale simu ilikata. Ilikuwa ni jambo la kushangaza kwa Lakashina, hasira alizokuwa nazo zilisababisha kifua chake kujaa. Zilipopoa maumivu yote kifuani yalipotea na sauti yake ilirudi katika hali ya kawaida.

Alishangaa kujiona hajambo kabisa, kila dakika matukio yalizidi kumchanganya, alijikuta akitamani mumewe Lakashi awepo ili amsaidie matukio yale ya kutisha ambayo aliamini yeye ndiye mhusika mkuu. Akiwa katika mawazo mazito ya kumuwaza mumewe, usingizi ulimpitia na kuota yupo na mumewe kitandani.

“Vipi mke wangu mbona unalia?” Lakashi alimuuliza mkewe aliyekuwa akitokwa na machozi baada ya kumuona mumewe.
“Hali hii mpaka lini?”
“Kwani tatizo nini?”
“Kwa nini niishi maisha ya mashaka?”

“Mashaka unayataka wewe mke wangu.”
“Kivipi?”
“Umesahau ulipotoka na upo wapi na kwa nini umetoka huko.”
“Lakini mume wangu kosa langu nini, kuna kosa kuwasamehe ndugu zangu?”

“Hakuna kosa lakini kumbuka umeshaumwa na nyoka, kwa nini huogopi unapoguswa na nyasi?”
“Mume wangu kama wewe umeweza kuwasamehe na kukubali kuyabadili maisha yao kuna ubaya gani wa kuwa karibu nao?”
“Unayakumbuka maswali ya baba zako wadogo?”
“Ndiyo.”

“Kwa nini ulikasirika?”
“Maswali yao yalikuwa hayana msingi.”
“Sasa mpaka iwe vipi ndiyo ujue kuwa hao siyo watu wema?”
“Mmh!” Lakashina alikosa jibu na kuguna tu.
Itaendelea siku ya kesho.
Like: www.facebook.com/2jiachie
Web: www.2jiachie.com

No comments

Powered by Blogger.