AHADI YA NDOTONI - 07
“Kutoka kwa Lakashi”
“Yupo wapi?” Lakasina alishtuka kumsikia Lakashi.
“Shemu ina maana hujui kama amesafiri?”
“Jamani mbona mnanichanganya?” SASA ENDELEA...
“Kivipi?”
“Mnasema jana kulikuwa na harusi yangu na Lakashi mbona mimi sijui?”
”Shemu hizi piko umechorwa kwa ajili ya nini?”
”Mmh! Tuachane na hayo, karibu.”
“Asante.”
Mgeni aliketi kwenye kochi na kutulia huku akipepesa macho kila kona ya nyumba ile.
“Mmh! Shemu karibu.”
“Asante.”
“Unatumia kinywaji gani?”
“Hapana mi si mkaaji niliagizwa nilete huu mzigo mara moja,” mgeni alisema huku akikabidhi mkoba wa ngozi uliokuwa wa saizi ya kati.
“Asante, na...na...,” Lakashina hakumalizia alichotaka kuuliza.
“Uliza tu shemeji.”
“Lakashi kaenda wapi?”
“Shemeji wewe mke wake usijue nitajua mimi?”
“Na atarudi lini?”
”Bado hilo ni swali gumu kwangu kwa vile siri ya mtu humpa mkewe.”
“Asante,” Lakashina hakutaka kuuliza kitu kutokana na kumuona mgeni hajui lolote zaidi ya kuleta mzigo alioelezwa na mumewe ambaye yeye anaamini ni wa ndotoni.
“Lakashi alinieleza nikueleze kuwa, tafadhali mkoba huo usiufungue, ukitaka pesa ingiza mkono na kuchukua kiasi chochote utakacho.”
“Kwani una shilingi ngapi?”
“Siwezi kujua ila kanieleza usiufungue huo mkoba wewe chukua kiasi chochote ukitakacho.”
“Hata milioni?”
“Si milioni tu hata zaidi ya milioni.”
“Kwa hiyo hata kununulia nyumba na gari.”
”Chochote kasoro pombe na nyama ya nguruwe.”a“Mmh!”
“Pia alinieleza kuwa usihame nyumba hii mpaka atakaporudi.”
“Sawa nimekuelewa.”
“Kingine amesema hivi haina haja ya kwenda kwa sonara kuijua thamani ya vito alivyokuvisha siku ya harusi yenu. Kwa vile vina thamani kubwa kuliko mtu utakaye mpelekea. Kibaya zaidi tamaa yao itakusababishia matatizo makubwa hata kukutoa uhai wako.”
“Ha! Shemu amejuaje?”
“Amesema muhimu ni kufuata maelekezo na si kujua amejuaje.”
“Sawa shemu, nimekuelewa.”
“La muhimu kuzingatia yote kama utakwenda kinyume utajiingiza kwenye matatizo ya kujitakia.”
“Nimekuelewa.”
“Nikuache, vipi unatoka?”
“Hapana.”
Mgeni aliaga na kuondoka huku Lakashina akibakia na maswali juu ya yale aliyoelezwa. Alijiona kama mtu aliyetembea uchi wakati kavaa nguo kutokana na Lakashi kumfahamu kila alilokuwa akiwaza. Alijikuta akijiuliza Lakashi ni nani. Aliubeba mkoba wake na kwenda kuuweka chumbani ndani ya kabati na safari ya kwa sonara ilikufa.
***
Maisha ya Lakashina yalibadilika ghafla ya kujikuta akiishi maisha mazuri na ya kifahari. Alinunua magari ya kifahari ya kutembelea, nyumba aliyokuwa akiishi mwenye nyumba alimuuzia na kuwa yake. Siku moja akiwa amejipumzisha sebuleni baada ya kutoka kuswali simu yake iliita alipoangalia ilikuwa namba ngeni alipokea.
“Haloo.”
“Haloo Jeska.”
“Mimi siitwi Jeska.”
“Mbona aliyetupa namba alituambia wewe ni mtoto wetu Jeska.”
“Wewe nani?”
“Mimi Zebedayo baba yake mdogo na Jeska.”
“Aah, kumbe ni ninyi, mnataka nini wakati mliyofanya sikutaka kuwapeleka kokote tafadhalini achaneni na mimi. Najua mmejua nina pesa mumeanza kunifuata tena ili mnidhurumu, lakini sasa hivi nitakufa kwa mali yangu.”
“Siyo hivyo Jeska.”
“Siitwi Jeska naitwa Lakashina.”
“Hilo jina kama la Kihindi au umebadili dini?”
“Ndiyo.”
“Sasa ni hivi tunaomba utupe muda ili tuikusanye mali yako tukukabidhi.”
“Muikusanye ili iweje? Nimewafuata kuwaomba?”
“Hapana mama, ile ni mali ya wazazi wako lazima tukurudishie wewe mwenyewe.”
“Mliponinyang’anya si mliona ni haki yenu na kunitishia kuniua sasa mnanitaka nini tena?”
“Hapana mama tupo chini ya miguu yako, tunakuomba tukurudishie mali yako.”
“Sipo tayari kuipokea nimewaachieni, endeleeni na maisha yenu nami niacheni niendelee na maisha yangu.”
“Jeska, ooh, samahani Lakashina, tunaomba uipokee tupo chini ya miguu yako.”
“Jamani niwaeleze mara ngapi kuwa mali hizo sina shida nazo, ni miaka mingapi imepita, hamkujua nimeishi maisha gani, hamkunionea huruma mwana yatima baada ya uchungu wa kifo cha wazazi wangu ninyi ndiyo mliotakiwa kunitunza kwa vile tayari wazazi wangu waliacha mali. Lakini kwa tamaa zenu mlinitupa na kunitishia maisha yangu.
Sikwenda polisi wala mahakamani nilimshtakia Mungu, leo hii mmekumbuka nini? Naomba muachane na mimi, “ Lakashina alikumbuka mambo mengi ilikuwa sawa na kuchubua kovu lililokuwa limepona. Alijikuta akishindwa kuzungumza na kuangulia kilio.
Simu ile ilimtia hofu Lakashina kuona muda si mrefu mali zake zitachukuliwa na baba zake wadogo, aliizima simu ili wasiendelee kumsumbua. Wazo la haraka lilikuwa kutoiwasha mpaka atakapobadili namba ya simu. Alijiuliza ni nani aliyempa namba yake ya simu.
Akiwa bado anatafakari kuhusiana na simu za ndugu wa baba yake watu ambao kwake aliamini ni maadui na kuapa kutowasamehe mpaka anaingia kaburini, simu yake iliita tena, alishtuka na kuamini kabisa labda hakuizima, hakuipokea mpaka ilipokata. Aliichukua ili aizime lakini cha ajabu simu ilikuwa imezimwa, aliiangalia mara mbili na kuhakikisha ameizima.
Haukupita muda simu iliita tena, alishtuka na kuitazama kwa muda akijiuliza ni kweli au anaota. Iweje simu aizime itoe mlio wa kuita huku ikitetemeka kama haikuzimwa.
Japo miujiza aliianza kuizoea lakini ule kidogo ulimtisha, hakutaka kuipokea aliitazama iite mpaka inyamaze yenyewe. Lakini simu haikunyamaza iliendelea kulia kwa muda mrefu. Kila muda mlio uliongezeka na kufanya hahisi ngoma za masikio kutaka kupasuka. Aliamua kuipokea na kusema kwa sauti ya juu.
“Nimesema sitaki.”
“Sikiliza Lakashina,” sauti ya upande wa pili ilikuwa nzito iliyoufanya moyo wake kwenda mbio.
“Siwezi kukusikiliza nimewaambia sizitaki hizo mali nani kawaomba?”
“Wampelekee nani?”
“Watajua wenyewe.”
“Lakashina naomba ufuate maelekezo yangu,” sauti ile nzito iliyokuwa ikijirudia kama kwenye mwangwi ilimchanganya na kuamini lile ni jambazi lilitumwa kuchukua mali zake. Kutokana na kutetemeka kwa hofu iliyomjaa moyoni simu ilimponyoka, lakini sauti ile iliendelea kusema na kuonekana kutawala chumba kizima;
“Lakashina hofu ya nini?”
“We...we...eee nani?” Aliuliza kwa kitetemeshi.
“La muhimu sikiliza maelekezo yangu, washa simu na kubaliana nao kuhusu kurudishiwa mali zako, ni halali yako wala usimuonee huruma mtu yeyote. Kama wao hawakukuonea huruma basi nawe usiwaonee huruma hata kidogo.”
“La...la...kini...we...e...we...e nani?” Lakashina aliuliza kwa hofu.
“Lakashinaaa, nikueleze mara ngapi usipende kuuliza, fuata maelekezo yangu washa simu.”
“Wewe ni nani, Lakashi?”
“Huwezi kunijua kutokana na hofu iliyokujaa moyoni, la muhimu chukua mali yako. Lakashina washa simu...washa simu.”
Sauti ile ilipotea taratibu huku ikijirudiarudia ikitoka katika uzito na kuwa nyepesi iliyokuwa kama ikimbembeleza Lakashina aliyepitiwa na usingizi, mfanyakazi aliyekuwa amemtuma aliporudi alimkuta amesinzia.
“Dada...dada.”
“Mmh.”
“Vipi?“
“Aah, kwani vipi?”
“Naona umelala huku ukitabasamu na kutikisa mguu unaota upo kwenye muziki nini?”
Lakashina aliposhtuka, alimuangalia mfanyakazi aliyekuwa amerudi toka dukani alipomtuma.
“Dada vipi mbona kama unanishangaa?”
Kabla ya kumjibu aliitazama simu yake aliikuta imezimwa, alimtazama Sara aliyekuwa amesimama mbele yake akimtazama. Alijinyoosha na kupiga miayo kisha alimuuliza.
“Eti Sara umekuja saa ngapi?”
“Mmh, muda ila mlango ulikuwa umefungwa kwa ndani ikanibidi nisubiri labda una kazi zako, baada ya muda mlango nilisikia ukifunguliwa na kujua umemaliza shughuli zako. Nilipousukuma niliukuta upo wazi, lakini cha ajabu nimekukuta umelala mkono kifuani ukitabasamu na mguu ukiuchezesha.”
“Sara unasema kweli?”
“Kweli, kwani vipi?”
“Mmh, tuachane na hayo, ulipokuwa nje hukusikia sauti yoyote?”
“Mmh, palikuwa kimya kama nyumba haina watu, kama usingenituma au mtu angekuja siku ya kwanza angeamini nyumba haina mtu. Kilichonifanya niamini kuna mtu, muziki wa kiarabu unaopenda kuupiga.”
Lakashina alitulia kwa muda akitafakari ya nyuma kabla hajatokewa na sauti ya ajabu ndani ya simu aliyoizima baada ya kukerwa na kauli za baba zake wadogo kutaka kumrudishia mali zake walizomdhurumu muda mrefu na kumtishia kumuua. Lakini sauti ya ajabu ilimsisitiza awashe simu.
“Dada upo sawa?” Sara alimuuliza.
“Nipo sawa, ila kuna watu wanataka kunichanganya...,” alinyamaza ghafla baada ya simu kuita tena, si yeye hata Sara aliiona, lakini ilikatika. Hakusema kitu aliichukua simu ile na kuiwasha. Baada ya kuiwasha hazikupita hata sekunde kumi iliita kwa mlio aliouzoea. Aliipokea kwa unyenyekevu.
“Haloo,” alisema huku akimuonesha kwa ishara Sara atoke nje, Sara alitekeleza bila kuhoji.
“Haloo Lakashina tupo chini ya miguu yako tunaomba tukurudishie mali zako, tunakuomba utuombee msamaha vitu vingine hatuna.”
“Jamani mbona siwaeleweni niwaombee msamaha kwa nani?”
“Kwa mumeo.”
“Mume wangu? Nitawaombea vipi naye kasafiri?”
“Atarudi lini tunateseka tuonee huruma, mateso tunayopata ni makubwa.”
“Mateso gani?”
“Tumekuwa watu wa kipigo kila kukicha ili turudishe mali zako.”
“Kipigo! Toka kwa nani?”
“Mumeo, tena amekuwa akitufuata ndotoni na kutusumbua turudishe mali zako zote bila kuacha kitu chochote.”
“Ina maana bila kupata kipigo msingenirudishia mali yangu?”
“Hapana Jeska...ooh samahani Lakashina tulikutafuta muda mrefu bila mafanikio, lakini sasa hivi mali zote zimekatika, sasa hivi maisha yetu yamekuwa ya kubahatisha.”
“Sasa mimi niwafanyeje?”
“Muombe mumeo atusamehe au atupe muda tuitafute.”
“Mmh, mimi sina neno labda mwenyewe.”
“Basi mwambie umetusamehe ili atuache.”
“Nitamwambia akirudi.”
“Amekwenda wapi?”
“Sijui.”
“Atarudi lini?”
“Sijui.”
“Lakashina mtumie ujumbe hata kwa njia ya simu kumueleza umetusamehe ili kutupunguzia mateso.”
“Mume wangu sijawahi kumuona na simu hata siku moja, na muda huu hayupo.”
“Basi akija nitamueleza kuwa umetusamehe.”
“Mmh! Sawa.”
Baada ya simu kukatwa Lakashina alijikuta akijawa na mawazo juu ya kauli za baba zake wadogo waliomdhulumu mali yake. Moyoni alikuwa radhi kuwasamehe, aliamini mali ile isingewafikisha popote. Lakini alikumbuka kauli ambayo hakujua ni ya nani iliyomuelekeza awashe simu na kuikubali mali yake yote na asiwaonee huruma hata kidogo.
Lakashina aliamini kama ni mali yake, alikuwa na uwezo wa kusamehe hata kuigawa kwa mtu aliyempenda. Hakuona umuhimu wa kung’ang’ania kulipwa mali asiyokuwepo. Akiwa katika lindi la mawazo simu yake iliita, aliipokea.
“Asalamu aleykum,” Lakashina alisalimia.
“Waleyku musalam,” sauti nzito ilijibu upande wa pili na kumfanya Lakashina ashtuke na simu kumponyoka, lakini sauti ilisikika kama ameweka ‘loud speaker’.
“A..a..abee.”
“Lakashina nani kakuita, acha kujitia hofu usipokuwa na kosa.”
“Sa...sa...wa,” alijibu kwa kutetemeka.
“Lakashina.”
“Abee.”
“Tuliza moyo wako kabla hatujazungumza lolote.”
“Nimetuliza,” Lakashina alisema huku akijiweka vizuri kwenye kochi na kufuta mikono usoni kujipa ujasiri.
“Lakashina,” Sauti ile nzito ilimwita tena.
“Abee.”
“Umetulia?”
“Ndiyo.”
“Vizuri, umewasikia baba zako wadogo?”
“Ndiyo.”
“Wamesema wataleta lini mali yako yote?”
“Mmh, wameomba niwaombee msamaha kwa vile mali yote hawana kwa sasa.”
“Lakashina hakuna kitakachobadilika mali yako inatakiwa mara moja.”
“Wamesema tuwape muda.”
“Ha...ha...ha...he...he...he...ee,” sauti ilicheka sana mpaka ikamkera Lakashina.
“Lakashina,” sauti ilimwita baada ya kicheko.
“Abee.”
“Unataka tugombane?”
“Hapana.”
“Sasa nisikilize, nakuomba hiyo mali iletwe mara moja, mbona wao hawakukusubiri mpaka upate akili ndipo wakudhurumu...Lakashina,” sauti ilijirudia kama mwangwi.
“Hii ni amri na siyo ombi, nataka uwakaripie wakuletee mali yako mara moja, kila kitu walichochukua warudishe. Hawakukuonea huruma wakati unamatatizo kwa nini unawasamehe. Kilio chako ndicho kilichofanya niitafute mali yako na kukupa maisha mazuri. Kama hutafanya hivyo adhabu yao itakurudia wewe.”
Sauti ile ilinyamaza ghafla na kumfanya Lakashina azidi kuchanganyikiwa, sauti ya adhana ndiyo iliyoufanya moyo wake utulie. Alinyanyuka na kwenda kutia udhu kwa ajili ya swala ya adhuhuri. Alipomaliza kuswali alirudi sebuleni kujipumzisha simu iliita tena moyo ulimpasuka, aliichukua na kuzungumza.
“Asalamu aleykum.”
“Lakashina, mama wewe pekee wa kuiokoa familia yako, bila huruma yako tunateketea wote,” sauti ya upande wa pili iliyoambatana na kilio pili ilikuwa ya baba yake mdogo.
Lakashina alishindwa awajibu nini, huruma ilimjaa moyoni lakini onyo alilopewa muda mfupi lilimtisha kwa kuhofia maisha yake. Alijikuta akiporomokwa na machozi na kukosa la kuwaeleza baba zake wadogo.
Like: www.facebook.com/2jiachie
Web: www.2jiachie.com
Ni simulizi mpya na tumekuja na mambo mapya KAMA UNAPENDA SIMULIZI HII ITOKE KWA Urefu zaidi ndani ya page hii kwa siku hakikisha kila unapomaliza kusoma UNA SHARE HATA ZAIDI YA MARA MOJA tutawapa Uhondo wa aina yake tunazo Simulizi nyingi sana KAZI NI KWENU. SHARE TUNAZOITAJI KWA SIKU n kuanzia 150.

Post a Comment