USIKU WA KIGODORO - 15
Endelea kulike: www.facebook.com/2jiachie
Tembelea: www.2jiachie.com
ILIPOISHIA:“Mh! Mwenzangu, naona anakata,” alisema Lina akianza kulia.
Mara meseji ikaingia…
“Kuna nini umesahau kwangu we binti?”
Ilitoka kwa James…
SONGA NAYO…
“Mh! Hebu soma meseji hii,” Lina alisema akimpa simu Eg.
“Kuna nini umesahau kwangu we binti,” Eg aliisoma meseji hiyo kwa sauti huku akitingisha kichwa. Alipomaliza, alimwangalia Lina kisha akasema…
“Unajua kama angeandika meseji hii huku hujui shemeji Semi atasemaje hapo sawa. Lakini sasa, Semi naye kaonesha kukwazika, ndiyo nahisi pana tatizo hapo.”
“Sasa Eg hebu nishauri, nifanyaje sasa?”
“Aisee sina cha kukushauri shoga yangu. We cha kufanya ni kumwachia Mungu tu, yeye ndiye anaweza kulitatua tatizo lako lakini kwa akili zetu hakuna kitu. Unajua nini Lina?”
“Niambie…”
“Kama angetokea mmoja wao ndiye akawa amegundua kuwa upo kwenye ndoa nyingine, yaani awe Semi au James isingekuwa tatizo lakini sasa wamejua wote halafu kwa siku moja,” alisema Eg na kuzidi kumpa maumivu mwenzake.
Lina alilia sana, alifika mahali sauti ya kilio chake ilionekana kama amefiwa na mzazi wake.
“Lina shoga yangu, maisha yako hivyo, nilishakwambia mbona. Leo unalia, kesho utafurahi. Cha msingi we mwombe Mungu tu,” alisema Eg naye akisikitika. Lakini moyoni alijua alichokifanya Lina, yeye asingediriki kukifanya hata iweje!
“Unajua Eg maisha yangu yamebomoka?”
“Ni kweli Lina. Maana hali yenyewe ndiyo hivyo tena.”
“Da! Sijui nitafanya nini mimi Lina? Hivi, ni kwa nini nilikubali kuingia kwenye ujinga kama ule?”
“Ni shetani tu shoga yangu.”
***
James alikuwa ameweka laptop kwenye mapaja yake akiandika. Alionesha hana amani kivile, mfanyakazi wake mmoja wa ndani akamfuata na kusimama pembeni yake, akamuuliza…
“Bosi, shemeji vipi, jana uliondoka naye lakini hukurudi naye, kuna tatizo?”
“Hebu waite wenzako wote niwaambie kwa pamoja,” James aliagiza.
Wafanyakazi wake wote, hadi wa getini walifika na kukaa kwa adabu…
“Jamani nataka kutoa tamko. Lina si mke wangu tena?”
“Umemfumania bosi?” waliuliza kwa pamoja.
“Hapana, ila imekuja kubainika kumbe ana mume wa ndoa kama mimi.”
“Eee?” waling’aka wote wakamtumbulia macho.
“Jana nilipoondoka naye tulikwenda kukaa Mlimani City ili tupate chakula cha pamoja, akaja bwana mmoja akasema amenifumania mimi na mkewe. Nilimwambia ni mke wangu akasema ni wake, tena wamefunga ndoa kanisani…”
“Ye Lina alisemaje?” mmoja wa wafanyakazi aliuliza.
“Hakusema kitu, alibaki analia. Kwanza alizimia, alipozinduka akaondoka mbio.”
“Aaa! Itakuwa kweli.”
“Siyo itakuwa, ni kweli. Nilikwenda hadi nyumbani kwa yule bwana, nilikuta picha yao ya harusi ukutani.”
“Mh! Hiyo kali. Sasa aliwezaje kuwa na wewe halafu ana mume nyumbani? Au waliachana?”
“Hawajaachana.
Kuna mchezo alikuwa akinifanyia Lina, anaaga anakwenda kulala hospitali kuna mgonjwa kumbe anakwenda kwa mume wake, kule nako anaongopa anakwenda kulala hospitali kumbe anakuja kwangu. Yaani sijui ni kituko gani hiki! Kuna mambo makubwa mengi tu. Alisema anasafiri kwenda kwao, hakwenda alirudi kwa mume wake…
“Sasa mbona amerudi na vitu?”
“Kanunua sokoni ili niamini ametoka safari. Nimejua kila kitu chake.”
***
Semi siku hiyo alishinda ndani tu, alikuwa akiwasiliana na ndugu zake mbalimbali na kuwapa taarifa ya alichokifanya Lina. Wengi walishtuka sana, wengine walisema hawajawahi kusikia achilia mbali kuona…
“Labda ungeniambia aliomba talaka kwako ili akaolewe na mwanaume mwingine, lakini kufunga ndoa nyingine na ya kwanza ipo na tena anaishi na wanaume wote kwa nyakati mbalimbali, sijawahi kusikia,” alisema kaka yake Semi, anaitwa Trela!
“Ndiyo hivyo kaka. Hivi hapa ninachotaka ni kufanya utaratibu wa talaka mahakamani,” alisema Semi…
“Hata mimi naunga mkono mdogo wangu. Kwani kuna kila dalili kwamba huyo mwanamke angeweza kukuua wewe ili abaki na mume mmoja.”
“Ni kweli kaka.”
***
Lina alikuwa ameduwaa, simu yake ikaita. Aliichukua haraka akiamini inaweza kuwa imetoka kwa mmoja wa waume zake. Kuangalia skrini lilijitokeza jina Boss!
“Mh! Eg bosi wangu anapiga simu.”
“Pokea.”
Lina akapokea…
“Haloo bosi…”
“Wewe uko wapi?”
“Nipo mahali bosi.”
“Upo mahali? Kivipi?”
“Bosi nina matatizo makubwa sana, siko nyumbani niko kwa rafiki yangu. Zile ndoa zote zimevunjika bosi wangu. Maisha yangu yameharibika bosi wangu, Lina si Lina tena,” alisema mrembo huyo huku akianza kulia tena.
“Ilikuwaje tena Lina?”
“Nilikuwa na James tumekaa Mlimani City tunakula, akatokea Semi…”
“Duu! Hiyo kali. Kwani hukujua kama Semi ataweza kuja?”
“Alikuwa Zanzibar kumbe akarudi bila kuniambia, ndiyo na yeye akaamua kuja Mlimani City…uuuuwi! Eeee! Najiua bosi,” alisema Lina huku akilia…
“Lina,” aliita bosi wake…
Abee bosi…”
“Kujiua si sababu wala dawa kwani wako waliokufa bila kukumbwa na mkasa kama wako. Mwombe Mungu akusaidie kwa namna yoyote ile,” alisema bosi huyo na kukata simu baada ya kubaini kwamba, Lina alikuwa akiendelea kulia.
“Mjinga sana huyu mtoto...ala! Yeye alitarajia nini sasa. Wenzake wakirubuniwa sana wanachepuka tu, sasa yeye mpaka kuamua kuolewa kabisa, hata kama ningekuwa mimi ndiyo mume wake nisingemwacha,” alisema bosi huyo huku akifikiria namna ya kumsimamisha kazi Lina.
***
Semi alikuwa safarini kwenda Korogwe, nyumbani kwa akina Lina kuweka wazi mambo ya mtoto wao. Safari yake hiyo hakumwambia Lina wala mtu mwingine yeyote yule.
Alifika saa kumi na mbili jioni na kukaribishwa kwa mshangao mkubwa maana mara zote anazoendaga, Lina huwajulisha kwanza…
“Karibu baba, za mjini? Mbona ghafla sana,” alisalimia mama Lina huku baba Lina akimwekea kiti.
Walichoona kimepungua au kuna jambo ni baada ya kumwona hajashusha zawadi yoyote kama walivyozoea kumwona akienda.
Baada ya salamu na mazungumzo mengine ya hapa na pale, Semi akaanza…
“Wazee kama mnavyojua, mshenga wangu alishafariki dunia hivyo kuna mambo yamenifanya nije mwenyewe hapa nyumbani…”
“Ndiyo ndiyo,” alisherehesha baba Lina huku mama akikaa vizuri…
“Nataka kuweka wazi kwamba Lina si mke wangu tena…”
“Eee!!” alishtuka mama mtu akamtumbulia macho Semi…
“Lina si mke wangu tena, iwe kwa talaka mahakamani au bila talaka. Nasema hivyo kwa sababu amefanya jambo moja la ajabu sana ambalo sijawahi kulisikia likifanywa sehemu nyingine hapa duniani.”
“Amefanyaje tena baba?” aliuliza baba mtu huku akianza kuhisi maisha magumu kwani msaada wa Semi kwao ni mkubwa sana tangu amemuoa binti yao…
“Lina amefunga ndoa na mwanaume mwingine, anaitwa James. Suala hilo halina ubishi kwake wala kificho, hajasingiziwa wala kuonewa…”
“Ngoja kwanza mkwe,” alidakia baba Lina…
“Eee…”
“Ina maana Lina amefunga ndoa na mwanaume mwingine wakati ndoa yake na wewe haijavunjika au imevunjika kwanza?”
“Amekwenda kanisani akiondokea kwangu, aliniambia anakwenda kwenye sherehe ya rafiki yake akaniomba alale hukohuko kumbe ndiyo wamekwenda kupumzika na huyo mumewe mwingine.”
Semi alihisi wazazi hao wa Lina hawataweza kumwelewa hivyo aliamua kuanika mkasa mzima mwanzo hadi mwisho na jinsi yeye alivyojua na alivyokaa na James na kumweleza ilivyokuwa.
Mama Lina aliangua kilio kikubwa sana kama amefiwa na huyo Lina, baba akachukua simu palepale na kumpigia Lina, ikawa hivi…
“Shikamoo baba,” Lina alisalimia baada ya kupokea simu…
“Lina,” aliita mzee huyo.
“Abe baba…”
“Una baba yako mwingine zaidi ya mimi?”
“Sina baba mwingine zaidi ya wewe baba, kuna nini?”
“Mumeo yuko hapa nyumbani. Sasa tambua mwenyewe kaleta habari gani kwetu?”
Lina alikata simu, akaizima kabisa…
“Vipi tena shoga?” Eg alimuuliza…
“Nimekwisha Eg…”
“Kivipi?”
“Semi yuko nyumbani Korogwe.”
“Mungu wangu! Kimenuka Lina, kila kitu sasa wazi hadi kwa wazazi, maskini shoga yangu wewe, utafanyaje sasa?”
“Eg mimi nakwambia sina namna, ni kujiua tu,” alisema Lina akasimama…
“Unakwenda wapi sasa Lina?”
“Nakwenda kujiua Eg, baki salama.
Niliipenda dunia na mambo yake lakini kifo nacho kimenipenda zaidi. Sina jinsi, simchukii Semi kwa kitendo chake cha kwenda kusema nyumbani wala simchukii James kwa kunitumia ile meseji bali najichukia mwenyewe kwa uamuzi wangu ulioshindwa kuangalia mbele ya safari.
“Nilidhani binadamu kuheshimika ni neema ya Mungu kumbe ni jinsi unavyoweza kutengeneza maisha yako mwenyewe. Mimi si wa kuheshimiwa tena. Kwanza niheshimiwe kwa ajili ya kitu gani nilichokifanya. Nikifa Eg nakuagiza wewe nizikwe kokote kule na vyovyote vile.
Lakini pia kukwambia kwamba uwaambie ndugu zangu wamuombe mume wangu wa ndoa halali, Semi asimamie mazishi yangu,” Lina aliondoka kwa kasi Eg alimfuata nyuma akimzuia kuondoka.
Kwa vile Eg alikuwa ndani ya kanga moja tu, alishindwa kutoka hadi nje, akarudi kuvaa gauni na kutoka mbio lakini alikuta Lina ameshapanda Bajaj…
“Nipeleke Kijitonyama,” alisema Lina akimwambia dereva wa Bajaj.
Lina alirudi nyumbani kwake, akakuta mlango umefungwa kwa nje. Alilijua hilo baada ya kuambiwa Semi yupo kwako, Korogwe.
Alikwenda mtaa wa pili akamwita fundi na kumwomba auvunje mlango ili aingie ndani. Fundi hakuwa na maswali kwa vile anamfahamu Lina kuwa ni mke wa Semi, akauvunja, akapokea malipo yake, Lina akazama ndani.
Alichukua chupa tupu ya bia akaipasua na kusaga vipandevipande ili avinywe. Aliona ni vema akanywea maji, akafuata maji kwenye glasi.
***
Akili ilimruka Eg, kwamba Lina atakuwa ameshika uelekeo gani, akahisi nyumbani kwake, yeye akakodi bodaboda…“Please anko nikimbize Kijitonyama haraka sana,” Eg alimwambia suka.
ITAENDELEA KESHOOOOOOOOOO

Post a Comment