ad

ad

USIKU WA KIGODORO - 14


ILIPOISHIA:
Semi akiwa hana amani, alizitaja namba zake za simu kisha naye James akamtajia za kwake. Wakaagana na kuondoka.
Semi alisema moyoni kwamba hatampigia simu Lina mpaka atakaposema mwenyewe lolote na pia kama ni kweli alifunga ndoa na James, yeye basi!
JIACHIE SASA…
Lina alikwenda kupiga kambi nyumbani kwa shoga yake, Eg ambapo alipofika tu na jinsi alivyokuwa akihema, Eg alijua kuna ishu nzito sana imetokea. Walipokutana macho, Lina akaanza kuporomosha machozi palepale…
“Lina, nini kimetokea?” aliulia kwa mshtuko Eg…
“Nimenaswa leo Eg, sijui itakuaje?” alisema Lina huku akilia.
“Umenaswaje? Hebu nisimulie.”
“Nilikwena Mlimani City na James, Semi alisafiri kwenda Zanzibar jana na alisema angerudi leo. Sasa nashangaa kumbe kaamua kurudi leo, akaja Mlimani City akanikuta nimekaa na James.”
“Mmmh!” alishtuka sana Eg. Aliliona tatizo kweli ni zito.
“Ikawaje sasa?” aliuliza Eg.
“Yaani Eg, amenikamata hivi nimekaa na James,” kabla hajamaliza kusema, Lina alilia tena. Ilibidi Eg atumie nguvu kubwa sana kumtuliza.
“Naomba utulie kisha uendelee kunisimulia,” alisema Eg akimkumbatia Lina.
Lina alitulia kwa muda kisha akasema…
“Yaani Eg iko hivi. Nilikaa na James Mlimani City, tena kwa kujiachia nikijua Semi si yupo Zanzibar anarudi kesho, kumbe karudi leo. Akaja Mlimani City, alinipigia simu nikamwambia nipo saluni, alipokuja pale kanikuta. Akanishika geba na kusema Lina.
“Yaani huwezi amini shoga nilianguka nikazimia palepale. Nilipokuja kupata fahamu nikakimbia. Aibu iliyoje?”
“Da! Pole sana shoga…sasa?”
“Sijui lolote. We unadhani naweza kwenda kwa nani kati yao?” aliuliza Lina.
“Mh! Uchaguzi ni wako.”
“Hamna Eg. Nikienda kwa Semi atanishangaa sana, kwa James pia. Hapa sijui wao wameachanaje! Kama walizungumza kila mmoja akajieleza kwa mwenzake mwisho wa siku si mimi nitaonekana wa ajabu sana?”
“Sana. Mi nadhani tumtafute mtu mzima mmoja ili asaidie busara zake,” alisema Eg…
“Eg, nilishaongea na watu wazima wote walishtuka na kuonesha dalili kwamba, mzigo ni wangu mwenyewe.”
“Mh!”
***
James baada ya kufika nyumbani kwake aliingia chumbani, akampigia simu Semi. Semi naye alikuwa chumbani kwake amelala ubavuubavu akishangaa kilichotokea…
“Haloo,” Semi alipokea simu…
“James hapa bwana.”
“Ndiyo kaka, tunaweza kukutana muda huu?” aliuliza James…
“Mi nadhani itakuwa muhimu. Wapi sasa?”
“Tukutane popote pale.”
“Wewe njoo nyumbani kwangu, nitakuelekeza ukifika.”
James alitoka, aliendesha gari akiwa amempigia simu Semi akampa maelekezo mpaka nyumbani kwake. Aliposhuka, alichukua bastola na kuisunda sehemu fulani ya nyuma, akampigia simu  Semi kwamba ameshafika.
Alitoka, akampokea na kumkaribisha ndani. Ile anakaa tu James, macho ya kwanza yakatua kwenye ukuta na kukutana na picha kubwa ya siku ya ndoa ya Lina na Semi…
“Kumbe kweli,” alisema moyoni.
Baada ya salamu ya muda huo, James alianza kwa kuelezea alivyokutana na Lina na alivyomuuliza kama ameolewa, akamjibu hana mume na alivyojitosa yeye kufunga naye ndoa…
“Ina maana umefunga ndoa kweli na Lina?”
“Kabisa.”
“Kanisani?”
“Ndani ya kanisa kabisa na honeymoon tulikwenda.”
Semi alianza kuunganisha matukio, akaanza kukubali moyoni mwake kwamba, Lina alifunga ndoa na kijana huyo.
“Inawezekana kweli, maana naanza kukumbuka kwamba kuna wakati amekuwa na safari nyingi za hospitali na wakati mwingine kulala hukohuko,” alisema Semi kwa sauti iliyojaa majonzi…
“Hata kwangu, kuna wakati alikuwa na safari nyingi na kusema anakwenda kulala kwa mgonjwa wa rafiki yake mmoja anaitwa…”
Kabla James hajamaliza kumtaja jina, Semi akamtaja…
“Eg?”
“Ee Eg. Huyohuyo.”
Semi alizidi kuvuta picha na kukumbuka siku moja Lina alipomwambia anakwenda kwenye sherehe ya Eg. Akakumbuka siku hiyo alikuwa  na safari ya gafla ikabidi amfuate Lina kwa Eg ambapo alimkuta amependeza sana.
Kifupi aliunganisha matukio na kukumbuka mambo mengi sana yaliyoonesha uhalisia.
“Hivi mimi leo ninavyojua ametoka safarini kwao, Korogwe, Tanga ambapo alisena anakwenda mama yake ni mgonjwa,” alisema James.
“Wewe jana si ulikuja pale Mlimani City?” aliuliza Semi.
“Nilikwenda kumpokea Ubungo maana alisema anarudi. Kufika napiga simu haipokelewi, ndiyo nikaamua kuja hapa.
“Kufika hapa, nakaa kidogo tu, akanitumia meseji kwamba ameingia Ubungo alikuwa amelala, lakini simu yake inaisha chaji, ndiyo maana nilitoka mbio.
“Kufika kule sikumpata tena hewani, nikaenda nyumbani naingia na yeye anaingia na bodaboda na ana mizigo.”
“Ana mizigo kabisa?” aliuliza kwa kuhamaki Semi…
“Kabisa.”
“Da! Huenda alinunua vitu sokoni ili ujue alisafiri kweli. Mimi nilikaa naye Mlimani City, wakati umekuja alikuwa chooni. Nahisi alikuona ndiyo maana akakutumia meseji ya kukwambia umefika ili uondoke. Maana ulipoondoka tu, akaja tukaondoka,” alisema kwa kirefu Semi.
Semi alionesha dalili za kujisikia vibaya kwa kitendo alichokifanya mkewe, Lina…
“Mimi bwana mzee sidhani kama nina la kuongeza tena, kwani kama nilivyokwisha kwambia, nilifunga naye ndoa na picha unaziona hizo hapo ukutani, hakuna cha kuficha,” alisema Semi huku akihisi kuporomosha machozi.
James pia alijisikia vibaya sana, naye alijilaumu ni kwa nini hakufanya utafiti wa kina kabla ya kufunga ndoa na Lina. Aliamini kama angechukua jukumu la kwena hadi kwa wazazi wake, yasingetokea hayo.
“Mimi mwenyewe mkubwa kama ningejua ana mume, sidhani kama ningekubali kugharamia harusi kubwa kama ile,” alisema James.
“Najua…najua.”
James aliaga na kuondoka kwa ahadi kwamba, hawezi kumpigia simu Lina. Semi naye akamwambia vivyo hivyo…
“Mimi nadhani tufanye hivi. Usipokee simu yake akikupigia kwani hata mimi sitapokea akinipigia,” alisema Semi.
***
Lina alilala kwa Eg usiku huo, lakini alishindwa kupata usingizi. Muda mwingi alikuwa akimwambia Eg kwamba anataka kujiua kwa sumu…
“Hapana, usifanye hivyo. Maisha yako hivyo siku zote. Kuna kupanda na kushuka, kuna raha na tabu. Kwa sasa upo katika kipindi cha tabu, lakini naamini kuna kipindi cha raha uliwahi kukipitia na kitakuja tena,” alisema Eg kwa sauti iliyojaa busara kuliko siku zote.
“Lakini Eg, wewe kama shoga yangu ulitakiwa uwe mkweli, ungenikatalia tangu mwanzo kwamba dili ninalolifanya lina matatizo mbele ya safari nisingelifanya,” Lina alitupa lawama…
“Lina! Wewe ndiyo ulikuwa unajua mazingira ya watu wako. Semi unamjua wewe, James unamjua wewe, nilijua unaelewa jinsi gani ungeishi nao maisha wasijuane. Lakini niliwahi kukwambia
kwamba huoni ni hatari, ukasema nikuachie wewe.”
“Basi yaishe bwana, nitamwomba Mungu mwenyewe hadi yataisha tu,” alisema Lina akimwaga machozi.
Usiku huo ulikuwa wa mang’amng’amu kwake, alishangaa kuona mpaka inagota saa saba, si Semi si James aliyempigia simu…
“Eg…Eg,” aliita Lina. Eg wakati huo alikuwa akikoroma usingizini…
“Mmmh! Vipi Lina?”
“Unajua mpaka muda huu sijapigiwa simu na yeyote yule?”
“Lina, hii ishu ni nzito sana. Ili upigiwe simu ni lazima mtu awe amekaa na kufikiria kwanza. Kama James angekuwa jamaa tu ndiyo umefumaniwa naye, angekupigia yeye lakini naye anajihesabia kama mume. Ni kazi sana,” alisema Eg huku akichombezea na kufikicha macho kwa usingizi.
***
Mpaka kunakucha, Lina alipata usingizi kwenye saa kumi na moja alfajiri lakini alipoamka na kuangalia simu hakukuwa na hata meseji ya Semi au James…
“Da! Yamenikuta Lina mimi! Hiki chote ni kiherehere changu,” alisema moyoni, akamuita Eg…
“Vipi Lina, umeamkaje?”
“Ah! Nimelala basi. Mimi Eg nafikiria jambo moja…”
“Lipi hilo? Lilelile la kujiua?”
“Hapana, naacha kazi pale.”
“Mh! Unadhani ni busara?”
“Kuendelea ndiyo siyo busara.”
“Kwa nini?”
“James anakuja sana pale, we unajua. Unadhani nitafanyaje kazi?”
“Ni kweli, lakini nadhani ni bora kupeleka akili kwenye ndoa kwanza kabla ya huko kazini. Unadhani mwisho ni nini kama hakuna aliyepiga simu?”
“Nataka kwenda nyumbani.”
“Wapi?”
“Kwa Semi.”
“Ukifika?”
“Nitaangalia mazingira kwanza. Kama yamekaa sawa nitamwomba msamaha kama siyo nitaondoka kurudi.”
“Lakini Lina jana usiku ulikosea sana, ulitakiwa urudi kwa Semi. Ukienda asubuhi hii anaweza akajua ulipowakimbia ulikwenda kulala kwa James…
“Ilikuwa mistake, sina jinsi, ngoja niende tu.”
Lina alijiandaa, akachukua Bajaj hadi nyumbani. Alimkuta Semi ameshaamka, yuko sebuleni anakunywa maji ya moto kwenye glasi…
Alikaa kwenye sofa, akamsalimia…
“Umeamkaje?”
Semi alimwangalia kwa macho makali sana bila kuitikia salamu yake. Alitamani kumrukia.
Baada ya kuona hajaitikiwa na sura ya Semi haijakaa vizuri, Lina alisimama, akatoka bila kuingia chumbani wala kwenda popote.
Alipanda tena Bajaj hadi kwa Eg…
“Vipi? Umemkutaje shemeji?”
“Mh! Mwenzangu, we acha tu. Nimeamua kuondoka mwenyewe maana nilipomsalimia tu, akaniangalia kwa macho hayo, sijawahi kumwona hata siku moja.”
“Aliitika?”
“Hapana, aliniangalia tu.”
“Mh! Sasa itakuaje Lina? Hebu mpigie simu James,” alishauri Eg.
Lina alikuwa kama amechanganyikiwa sasa, kila hoja aliikubali, akampigia simu James ambapo iliita mpaka ikakatika. Akapiga tena, pia iliita mpaka ikakatika. Mwishowe, simu ilipoita ikakatwa upande wa pili!
“Mh! Mwenzangu, naona anakata,” alisema Lina akianza kulia.
Mara meseji ikaingia…
“Kuna nini umesahau kwangu we binti?”
Ilitoka kwa James…

No comments

Powered by Blogger.