USIKU WA KIGODORO - 06
Endelea kulike: www.facebook.com/2jiachie
Tembelea: www.2jiachie.com
ILIPOISHIA: Lina alichukua Bajaj ambayo ilimfikisha nyumbani kwake akiwa amechoka sana. Ile anaweka simu mezani tu, mumewe Semi akaichukua.
JIACHIE SASA…
“Kuna mtu nataka kumpigia nijue alipo halafu simu yangu haina hela,” alisema akiminya vitufe.
Moyo wa Lina ulilipuka kwani alikumbuka kuwa ndani ya simu hiyo kulikuwa na meseji za James ambazo hakuzifuta na zilisomeka vibaya kama zingeonwa.
Alitaka kupeleka mkono kumpokonya mume wake lakini alijua akifanya hivyo pia angempa picha mbaya kama nia yake haikuwa kupekua meseji.
Semi alipiga simu na kuongea na mtu ambapo alisikika akisema…
“Wee kama nilivyokwambia, hakikisha unatumia kila njia ili tuujue ukweli wa mambo. Unajua hakuna kitu kibaya kama mke awe wako halafu kumbe kuna mwingine anamwona ni mke wake, hiyo ndiyo maana yangu kuu.
“Sawa kaka, sawasawa, fanya uchunguzi wako halafu utanipa majibu.”
Lina aliishiwa nguvu, miguu ilimtetemeka, akataka kukaa lakini akajisikia kuumbuka. Alitamani kuuliza kinachoendelea, pia akashindwa.
Semi hakuwa na nongwa, alimrudishia simu yake huku akimwangalia usoni ambapo Lina aliamua kuukimbiza uso wake pembeni.
“Pole na starehe,” alisalimia Semi, Lina akashindwa acheke au ajibuje…
“Nzuri.”
“Mambo yaliisha salama?”
“Ndiyo.”
“Una uhakika?”
“Ndiyo, kwani umesikia nini?”
“Nimesikia umenisaliti.”
Lina moyo ukamfanya paa! Mpaka akajishika kifua kwa hofu…
“Mungu wangu,” alisema ndani kwa ndani…
“Pole lakini, maana kulala nje ya nyumbani nako...” Semi alisema huku akicheka, kidogo Lina akajua mumewe anafanya utani kwani kwa anavyomfahamu asingeweza kucheka kama angekuwa analo jambo moyoni.
Lakini bado yale maneno aliyoongea mumewe na mtu kupitia simu yake kwamba achunguze mtu anaweza kusema ni mke wake kumbe kuna mwanaume mwingine naye anasema ni mke wake yalimtesa akilini.
Alienda chumbani huku akifungua simu kuangalia namba iliyopigwa, akabaini ni ya mtandao ambao anao na yeye hivyo aliisachi…
“Issac Majurila ni nani, mbona sijawahi kumsikia,” aliwaza moyoni. Aliamua kumsaka ili kujua mumewe alimwambia amchunguze nani ambaye anaweza kuwa mke wa mtu kumbe kuna mwingine anasema ni mke wake!
***
“He! Kumbe leo ni Jumapili, nilisahau kabisa, nikajua utachelewa kazini,” alisema Semi akiwa ameingia chumbani ambapo hata Lina mwenyewe alishtuka, akakumbuka kwamba, alifunga ndoa jana yake Jumamosi, amelala na James usiku wa Jumamosi kuamkia Jumapili.
“Mh! Mi mwenyewe kusema za ukweli nilijua leo ni siku ya kazi,” alisema Lina akiendelea kushangaa. Mara simu yake iliingia meseji, akaisoma chapchap...
“Baby leo ni Jumapili, sasa umeondoka bila kusema utakuja muda gani?”
Lina aliijibu palepale…
“Mchana nitakuwa hapo baby, hata mimi nilisahau kabisa kwamba leo ni Jumapili, sijui ni kwa nini wote tulisahau.”
“Oke, ilitokea tu, uje basi kwa muda huo.”
Bahati nzuri pale nyumbani napo, Semi aliaga anakwenda kwenye shughuli zake hivyo Lina akabaki yeye na msichana wa kazi tu. Ikawa ni nafasi yake ya kurudi hotelini aliko James.
Alikwenda sebuleni, akazima tivii maana alimkuta mumewe Semi ameiwasha akitazama mambo mbalimbali. Lina aliizima kwa sababu alihisi inamchanganya, kwa wakati huo alihitaji kutafakari zaidi kwa kitendo alichokifanya.
Kwanza alijua amemfanyia kitendo kibaya sana James, kufunga naye ndoa ambayo ni batili. Alihisi huruma anatakapogundua wakati mwenzake mapenzi yote aliyaelekeza kwake kama mke.
Pili, alimini kuwa James anajua amejikomboa kwa kupata mke na yeye anapitia sera za kike maana yake ametoa mkosi, sasa kumbe badala ya kuondoa mkosi amejiongezea…
“Hivi huu mtego nitawezaje kujinasua nao? Ni kwa nini nimeuingia? Ni tamaa ya hela au mapenzi ya dhati?” aliwaza Lina. Lakini kwa harakaharaka alipata jibu kwamba, zile laki mojamoja kila kukicha zilimchanganya akili licha ya kwamba ni kweli James ni kijana mtanashati sana.
Lina aliamua kumpigia simu shoga yake, Eg na kumwambia anavyojisikia…
“Halo Lina…”
“Eg…”
“Bee.”
“Naweza kujiua mwenzio.”
“He! Kwa nini Lina, kuna nini kimetokea? Shemeji kajua?”
“Hapana! Ila…”
“Ila nini tena Lina?”
“Unajua nimefanya jambo la kipuuzi sana? James anajua mimi ni mke wake wa ndoa. Halafu sasa, mbaya zaidi ndoa yenyewe ya Kikristo, ni kama loki. Siku akijua nina mume tena wa ndoa nini kitatokea?
“Mtu mwenyewe ana hela, nahisi atanifunga na hakuna wa kunitetea. Najuta Eg, najuta kabisa. Sijui ni kwa nini na wewe rafiki yangu kipenzi hukinikataza?”
“Lina, nisingekukataza mtazamo wako na wangu ni mmoja tu. Kama ni kujuta sasa tujute wote, kwani kwa maneno yako ya saa hizi hata mimi nimegundua hilo…”
“Eg subiri nipokee simu ya James…halooo.”
“Mke wangu Lina…”
“Abee baba.”
“Mwambie dada ukija mchana hakuna kurudi tena huko. Utakuwa unatokea hapa kwenda kazini na kurudi mpaka siku tano tunahamia nyumbani, hivyo ukija beba nguo zako kwenye sanduku chukua teksi.”
“Mh! Sawa baby.”
“Mbona umeguna kwanza?”
“Basi tu, nafikiria jinsi ya kumwambia huyo dada.”
“Unafikiria jinsi ya kumwambia dada? Kwa nini ufikirie? Mimi si mume wako kwa sasa? Tena wa ndoa.”
“Ni kweli my love.”
“Sasa?”
“Oke, nimekuelewa.”
James alikata simu na kumwacha Lina katika mawazo kibao…
“Da! Nimeingia mkenge kwa kweli. Hapa sina cha kujitetea, siwezi kutengua ndoa tena. Imefungwa imefungwa tu. Kinachotakiwa ni kuamua moja, kusuka au kunyoa…
“Semi mume wangu akijua sijui nini kitatokea. Da! Balaa! Hivi kama ni tamaa, tamaa gani ya hivi mimi Lina mimi? Haya mambo si yanaweza kufika kwa wazazi? Yakifika nitajiteteaje?”
Lina alikosa ujasiri wa kufikiria kiasi kwamba alianza kutoa machozi mwenyewe…
“Mungu wangu, nisaidie mimi. Nimekwaa tatizo kubwa.”
Kwa upande wake James baada ya kumkatia simu Lina naye alizama kwenye maswali kibao huku akikosa majibu ya moja kwa moja…
“Ni kwa nini Lina anamuogopa dada yake kiasi hicho? Yeye si mke wangu wa ndoa? Sasa nini kitamfanya huyo dada azuie Lina kuondoka?
“Halafu, kwani mbona siku ya harusi ukumbini sikumwona huyo dada yake akitambulishwa? Maana kama ndiye ameishi naye alitakiwa kutambulishwa kama mzazi wa Lina kwa hapa Dar es Salaam.”
Kifupi wote walikuwa katika wakazi mgumu sana, kila mmoja alikuwa na maswali yake yaliyokosa majibu ya moja kwa moja kwa pale.
***
Mchana ulifika, Lina mapigo ya moyo yaliongezeka kwa sana. Kila dakika ilipokatika aliitupia macho simu yake akiamini James atapiga…
“Huyu atapiga sasa hivi,” alisema moyoni. Aliwaza amwambie nini mume wake, Semi ili aondoke kurudi hotelini aliko James lakini pia alijiuliza akienda bila nguo ataelewekaje kwa mumewe huyo?
Kama aliota, simu ya James iliita. Aliitupia macho kwa dakika moja nzima mpaka akakata. Ikapigwa tena ndipo akapokea…
“Baby…
“Mbona hufiki? Nikufuate?”
“Noo baby, nilikuwa naweka nguo zangu kwenye begi nakuja.”
“Poa.”
James akakata simu kwa dalili zote kwamba amekasirika na mwenendo wa Lina kwa siku ile.
Lina alimpigia simu mume wake ili amdanganye kitu…
“Baby…”
“Ee baby…”
“Kuna balaa juu ya balaa,” alisema Lina…
“Lipi tena baby?”
“Yaani Eg ana dada yake alikuwepo kwenye sherehe ya jana, amefika kwake ameumwa ghafla kakimbizwa Muhimbili…”
“Duu! Balaa. Sasa?”
“Sasa nakuomba ruhusa niende Muhimbili mchana huu maana Eg naye anakwenda.”
“Sawa! Lakini huyo atakuwa amekula kitu kibaya, unajua sherehe sherehe hizi mambo hayo hutokea. Ngoja nikupe namba ya Dokta Matingisha ukifika umpigie ili asaidie.”
“Itakuwa vizuri baby.”
Lina aliachia tabasamu, akapata akili. Alichukua begi, akatoa kwenye kabati lake nguo za zamani kibao na kuziweka kwenye begi.
Kama vile hiyo haitoshi, akafunua godoro ambapo pia mlikuwa na nguo nyingine, nazo akazitia kwenye begi mpaka likavimba. Akachukua Bajaj hadi hotelini alipo James.
***
Eg alikuwa hana hili wala lile, simu ya shemeji yake Semi ikaingia kwake…
“Mh! Huyu shemeji vipi, si kawaida yake kunipigia simu,” alisema moyoni Eg huku akiwaza apokee au la! Akaamua kuipokea…
“Haloo shem…”
“Shemeji poleni sana na mgonjwa jamani! Aisee,” alisema mume wa Lina…
“Mgonjwa?” alihoji Eg…
“Si Lina ameniambia kwamba…”
Eg alikata simu haraka sana. Akampigia Lina…
“Shoga…”
“Ee shoga vipi?” alisema Lina…
“Umemwambia shemeji nina mgonjwa?”
“Ha! Ndiyo Lina, kakupigia? Please mwambie unaye, nimemwambia ni dada yako amelazwa Muhimbili anaumwa sana tumbo la kuendesha na yuko hoi…”
“Oke, tena huyo anapiga ngoja nipokee…
“Haloo shem…”
“Shem, naona mtandao unasumbua…Lina kaniambie una mgonjwa.”
“Eee, unajua nilidhani unasema wewe ndiyo una mgonjwa ndiyo maana nikauliza mgonjwa gani?! Dada yangu bwana, anasumbuliwa na tumbo tukamkimbiza Muhimbili.”
“Da! Poleni sana, lakini Mungu atamsaidia.”
“Asante sana shemeji.”
“Oke shemeji. Sisi tupo, yeye kaniambia anakuja Muhimbili.”
“Ee, na mimi naelekea huko shemeji yangu.”
“Sawa, baadaye.”
***
Lina alifika hotelini, akasukuma mlango na kuzama kwenye chumba alichomo mume wake wa pili James…
“Hodi.”ITAENDELEASIKU YA KESHO.

Post a Comment