ad

ad

MOYO WANGU BADO UNAVUJA DAMU - 01

Mama Mpendwa.
   Najua kwamba mlinionya mara kwa mara juu ya uamuzi ambao niliuchukua wa kuwa na mtu ambaye alionekana kwangu kuwa si sahihi, sikutaka kusikia kitu chochote kutoka kwenu, kila siku nilijisikia kufanya kile ambacho nilitamani kukifanya hata kama kilikuwa si sahihi.
   Kila kitu ambacho kilitokea katika maisha yangu, sitoweza kumlaumu mtu yeyote zaidi ya kujilaumu mimi mwenyewe. Nilijiona kuwa katika mapenzi mazito, nilijiona kuthaminiwa zaidi ya mtu yeyote yule ingawa kwa sasa nimefahamu kwamba kule nilipokuwa, kamwe haikuwa sehemu yangu sahihi.
   Sikuwa mtu wa furaha, huzuni ndio ilikuwa sehemu ya maisha yangu, kila siku nilikuwa mtu wa kuumia, furaha ikapotea katika maisha yangu. Nilijuta na milele nitaendelea kujutia uamuzi ambao niliamua kuuchukua wa kuishi na mwanaume ambaye nina uhakika hakuwa mwanaume wangu sahihi.
   Namkumbuka Simon ambaye siku zote alitamani sana kuwa pamoja nami, nilifahamu kwamba Simon alikuwa na mapenzi ya dhati kwangu na kila siku alikuwa akinihitaji kuliko kitu chochote kile. Pamoja na mapenzi yake yote aliyokuwa nayo, nilimkataa kwa kumuona hanifai.
   Kila siku Simon alikuwa akilia mbele yangu, alilililia penzi langu ambalo kamwe sikutaka kumpa. Niliijua hali yake ya maisha ambayo alikuwa akiishi, hakuwa akiishi katika familia iliyokuwa na fedha za kutosha kama ilivyokuwa familia ya Walter.
   Sikutaka kuwa na Simon japokuwa alinionyeshea ni jinsi gani alikuwa akinihitaji tangu kipindi kile shuleni, sikutaka kabisa kuwa na Simon. Alijitahidi kuniletea maua ambayo nilikuwa nikiyatupa katika pipa la takataka tena mbele ya macho yake. Nakumbuka vizuri sana hadi zile siku ambazo alikuwa akijitahidi kuniletea kadi mbalimbali za mapenzi, sikuona thamani yoyote ile zaidi ya kuzitupa na nyingine kuzichoma moto.
   Sikumuhitaji Simon kabisa na wala sidhani kama kulikuwa na msichana yeyote ambaye alikuwa akimuhitaji pale shuleni zaidi ya msichana Violeth ambaye kila siku nilikuwa nikimuona mjinga. Sikujua alikuwa akimpendea nini mvulana yule ambaye nilimuona kutokuwa na mvuto wowote ule.
   Sikuwa nikitaka kusikia kitu chochote kile kutoka kwa mtu yeyote juu ya Walter ambaye alinionyeshea mapenzi ya kweli ambayo kwa sasa ninaamini kwamba yalikuwa feki. Alinichezea alivyotaka, nilimkabidhi kila kitu katika maisha yangu, kwa sasa NINAJUTA.
   Nilimuonea huruma Simon ambaye kila siku alikuwa akiendelea kunifuatilia kila sehemu nilipokuwa, nilikuwa nikimchukia sana katika kipindi kile, nilikuwa nikimletea dharau kila siku lakini hakutaka kunielewa, kila siku alikuwa akiendelea kunifuatilia.
   Ninajuta na kila siku nitaendelea kujuta katika maisha yangu. Nilipoteza bahati ambayo sidhani kama itaweza kurudi tena maisha mwangu. Sidhani kama Simon ataendelea kunipenda kama tu atakuja kuniona kwa jinsi nilivyokuwa sasa.
   Miguu yangu mizuri ambayo nilikuwa nikiiringia haipo tena, mataili ya baiskeli yangu ndio yamekuwa miguu yangu. Ninaonekana kuwa kama kinyago. Sitaki tena kutoka nje, kila siku ninajifungia chumbani kwangu nikilia, sijui nifanye nini tena.
   Namkumbuka sana Simon, nakumbuka mara ya mwisho kuonana nae, alikuwa mbele yangu pamoja na Walter. Simon alikuwa amepiga magoti chini akiendelea kulilia penzi langu. Muda wote nilikuwa nikimwangalia kwa dharau, sikutaka kusikia kitu chochote kutoka kwake.
   Simon alikuwa akizielezea hisia zake kali za mapenzi juu yangu, nilijikuta nikipata moyo wa ujasiri kumkataa kwa mara nyingine tena. Muda wote kicheko cha dharau kilikuwa kikisikika kutoka kwa Walter ambaye sidhani kama kuna siku ilitokea kumpenda Simon.
   Namchukia Walter na sidhani kama kuna siku nitakuja kumpenda au kumsamehe kwa haya ambayo amenifanyia, nimekuwa binadamu mpya, nimekuwa mtu nisiyejiweza tena. Kila siku nikimkumbuka Simon, bado moyo wangu unaendelea kujuta kwa kutokumpa kile ambacho alikuwa akikililia kila siku kutoka kwangu.
   MOYO WANGU BADO UNAVUJA DAMU kwa maumivu makali ambayo yametokea kuumiza moyo wangu. Sijui kama itatokea siku nitakuwa katika hali ya kawaida. Kila ninapoyakumbuka mambo mengi yaliyotokea katika kipindi changu cha nyuma, nabaki nikilia huku nikiendelea kumlaumu Walter ambaye alinitelekezi.
   Sijajua mahali ambapo Simon atakuwepo kwa sasa, sijajua ni kwa jinsi gani nitaweza kumuona. Na kama nikibahatika kuonana nae,  nitahitaji sana kuzungumza nae kwa kirefu, nitahitaji kumuomba msamaha juu ya yote ambayo nilikuwa nimemtendea katika maisha ya nyuma. Najua kwa sasa anaweza kuwa na msichana ambaye atakuwa anampenda, ila kama atakuwa na Violeth, moyo wangu utafurahi sana kwani naamini yule alikuwa msichana pekee ambaye ana mapenzi ya kweli kwake.
   Nimejaribu kuandika barua hii ndefu kwako mama kwa sababu nilitamani sana ufahamu mambo ambayo yalinitokea katika kipindi ambacho mlihama na kuelekea mkoani Shinyanga. Kwa sasa sijiwezi ila kumbukeni kwamba Walter ndiye alikuwa chanzo cha haya yote.
   Kama itatokea nikapata msaada wowote ule, basi naamini nitakuja huko kukaa nanyi mpaka pale kifo kitakaponikuta. Najua utakuwa umeshtuka sana kuyasoma haya ambayo nimekuandikia, ila amini kuwa hii ndio hali halisi niliyokuwa nayo na kamwe sitotakiwa kupingana nayo.
   Wasalimieni watu wote huko, msisahau kumsalimia mdogo wangu Paula, naomba umwambie mambo mengi kuhusiana na mapenzi ili yasimtokee haya ambayo yamenitokea.
   Nawapenda sana.
    Ni mimi
   Beatrice Sebastian.

   Beatrice alimaliza kuandika barua ile, machozi yalikuwa yameyaloanisha mashavu yake kupita kawaida. Hakuonekana kuridhika, akaanza kuirudia kuisoma zaidi na zaidi, kila alivyozidi kuisoma na ndivyo alivyozidi kuumia zaidi.
   Karatasi ya barua ile ikaanza kuloanishwa na machozi yake ambayo yalikuwa yakimtoka. Akaanza kuikunja karatasi ile na kisha kuiweka ndani ya bahasha na kuanza kukisukuma kibaiskeli chake mpaka karibu na kitanda huku bahasha ile akiwa ameiacha mezani.
   Alitumia muda wa dakika nzima mpaka kupanda kitandani. Akajifunika shuka na kuanza kulia. Kila alipokuwa akikumbuka maisha yake ya nyuma, moyo wake ulikuwa ukimuuma zaidi na zaidi. Miguu yake ambayo ilikuwa ikisifika kwa kila aliyekuwa akimwangalia wala haikuwapo tena zaidi ya kubaki vipingili tu.
   “MOYO WANGU BADO UNAVUJA DAMU” Beatrice alibaki akijisemea kitandani pale.
                                                                  ***********
Mwaka 2000
 “Kuna nini...mbona umeshtuka namna hiyo?” Bi Martina alimuuliza mtoto wake, Simon ambaye alikuwa ameshtuka kutoka usingizini katika hali ambayo ilionyesha kwamba alikuwa akiota ndoto mbaya.
   “Ndoto. Ndoto mama” Simon alimwambia mama yake huku akitokwa na jasho.
   “Ndoto? Ndoto gani? Ndoto mbaya?” Bi Martina aliuliza.
   “Sijui mama. Nilikuwa nikisikia tu sauti”
   “Ilikuwa inasemaje?”
   “Usimuache....kamwe usimuache, yeye ndiye mafanikio katika maisha yako” Simon alimwambia mama yake.
   “Usimuache nani?”
   “Sijui. Yaani sijui chochote mama”
   “Kwa hiyo ulikuwa unaisikia sauti tu? Hata haukumuona mtu yeyote?” Bi Martina alimuuliza Simon.
   “Nilimuona msichana. Sikumjua msichana gani. Alikuwa amevaa sketi ya shule, alionekana kuwa mrembo ingawa sikuwahi hata kumuona” Simon alimwambia mama yake.
   “Usijali mwanangu. Fumba macho tusali. Hizo ni ndoto tu” Bi Martina alimwambia mwanae na kisha kumshika mkono wake na kuanza kusali. Sala ilichukua dakika moja tu, wakamaliza na kulala.
   Hayo ndio yalikuwa maisha yao ya kila siku. Chumba ambacho walikuwa wakiishi kilikuwa kimoja, kila siku walikuwa wakilala pamoja. Maisha yao yalikuwa maisha ya dhiki ambayo kila siku hakukuwa na mtu ambaye alitamani kuyaishi.
   Kadri siku zilivyokuwa zikizidi kwenda mbele na ndivyo ambavyo ugumu wa maisha ulivyozidi kuongezeka. Chakula kwao kilikuwa kwa shida japokuwa walikuwa wakiishi watu wawili tu. Bi Martina alikuwa akihangaika kila siku kutafuta fedha kwa ajili ya kununulia chakula na kumlipia Simon ada shuleni.
   Kila siku Bi Martina alikuwa akitafuta fedha kwa nguvu zote kwa ajili ya kumtunza mtoto wake, Simon ambaye katika kipindi hicho alikuwa kidato cha kwanza katika shule ya Salma Kikwete. Bi Martina aliamini kwamba Simon ndiye alikuwa kila kitu katika maisha yake mara baada ya mumewe kumtelekeza katika kipindi ambacho Simon alikuwa na miezi miwili.
   Yeye ndiye ambaye alimlea Simon mpaka katika kipindi hicho, alijitahidi kumlea katika malezi mazuri ambayo kila mzazi alitamani kumlea mtoto wake namna ile. Kila siku ambazo alikuwa akihitajika kanisani,alikuwa akimpeleka huko. Simon akawa mtoto aliyekuwa akipenda dini kuliko kitu chochote kile maishani mwake.
   Kila siku alikuwa akisoma Biblia ambayo alikiona kuwa kitabu kilichokuwa kikimfariji kupita kiasi. Alipendelea sana kusoma kitabu cha Kumbukumbu La Torati, kitabu ambacho kiliandikwa ahadi nyingi kwa mtu ambaye alikuwa akifuatilia kila kitu kilichoandikwa katika kitabu hicho.
   “Sitokuwa mkia....nitakuwa kichwa...” Hayo ndiyo maneno ambayo kila siku Simon alikuwa akiyasema kila alipokuwa akilala.
   Mara kwa mara Simon alikuwa akielekea shuleni kwa miguu na ni mara chache sana alikuwa akipanda basi. Kutoka Mwembechai ambako alikuwa akiishi hakukuwa karibu kabisa mpaka shuleni kwao, lakini kutokana na ugumu wa maisha ambao ulikuwa katika familia yao, alijitahidi kuvumilia.
   Simon alikuwa mwanafunzi mkimya shuleni, umasikini wake ambao alikuwa nao ndio ambao ukaanzisha dharau shuleni pale. Wanafunzi wengi walikuwa wakimchukia Simon ambaye mara nyingi sana alikuwa akionekana mchafu.
   Muda wa mapumziko, Simon hakuwa akila kitu chochote kile, alikuwa akishinda bila kula kitu chochote shuleni mpaka katika kipindi ambacho alikuwa akirudi nyumbani. Siimon hakuwa na idadi kubwa ya marafiki shuleni, na hata hao ambao alikuwa nao katika kipindi hicho walikuwa nae kwa sababu tu uwezo wake darasani ulikuwa mkubwa.
Endelea kulike: www.facebook.com/2jiachie
Tembelea: www.2jiachie.com

No comments

Powered by Blogger.