ad

ad

MARIA - 06

 
 “Nashukuru mama. Niko tayari” Maria alimwambia mwanamke yule.
   Safari ya kuelekea nyumbani kwa mwanamke yule ikaanza. Muda wote Maria alikuwa akionekana kuwa na furaha isiyo kifani. Kupata nafasi ya kufanya kazi ndani ya jiji la Dar es Salaam kwake ilionekaa kuwa kama bahati kubwa.
Walichukua dakika kumi kutoka kutoka Ubungo mpaka Mwenge ambako wakaingia ndani ya nyumba kubwa na nzuri ambayo ilimvutia Maria kwa kuitazama. Hakuamini kama kungetokea siku yoyote ambayo angeishi ndani ya nyumba kubwa na nzuri kama ile.
 “Karibu” Mwanamke yule alimkaribisha.
“Asante” Maria aliitikia huku uso wake ukionyesha kubwa aliyokuwa nayo.
Maisha mapya yakaanza ndani ya jiji la Dar es Salaam. Maria alifanya kazi kwa moyo wake wote, kila kitu ambacho aliambiwa akifanye, alikifanya tena kwa haraka sana. Kila mtu ndani ya nyumba akaanza kumpenda Maria ambaye moyo wake ulikuwa katika mawazo mazito kadri siku zilivyozidi kwenda mbele.
Siku zikaendelea kukatika na hatimae miezi miwili kutimia. Maria hakuwa akiongea na mtu yeyote mtaani, kila siku alikuwa akishinda ndani na kuangalia runinga. Kazi kubwa ilikuwa kwa wavulana ambao walifanikiwa kumuona Maria, aliwavutia lakini hakukuwa na nafasi ya kumueleza ukweli juu ya kile ambach kilikuwa kinaendelea mioyoni mwao.
   “Sijisikii kwenda kanisani mama. Acha nikusaidie kazi za nyumbani” Maria alimwambia mwanamke aliyekuwa akiishi nae, Bi Lilian
   Maria hakutaka kwenda kanisani siku hiyo, alibaki nyumbani akifanya kazi pamoja na Bi Lilian. Maria alifanya kazi zake kwa haraka sana, alipomaliza akaelekea sebuleni na kuwasha runinga.
   Huku akiendelea kubadilisha baadhi ya chaneli mbalimbali, Maria akavutiwa na kituo cha Pasific Tv. Ibada ya kanisa la Praise And Worship ndio ambayo ilikuwa ikiendelea kanisani na ilikuwa ikirushwa moja kwa moja na kituo hicho.
   Ibada ya kusifu ambayo ilikuwa ikiendelea anisani pale ndio ambayo ilionekana kumfurahisha. Akaiweka pembeni rimoti ya runinga na kutuliza macho yake akiiangalia ibada ile. Dakika kadhaa zilipita mpaka katika kipindi cha matangazo.
   Tayari usingizi ukaanza kumnyemelea pale kochini, televisheni ilikuwa inawaka huku ibada ya kanisa la Praise And Worship ikiwa inaendelea. Ghafl, Maria akashtuka, akaikodolea macho televisheni ile vizuri huku akionekana kuwa makini.
   Jina ambalo alilisikia katika kipindi hicho likitajwa na mchungaji ndilo ambalo lilionekana kumshtua. Maria akajiona kuwa mbali na runinga hali iliyomfanya kusimama na kuisogelea kwa karibu ili aone vizuri.
   “Jumamosi kutakuwa na harusi kanisani hapa. Kama uchumba tulivyokuwa tukiutangaza kila Jumapili basi na hata tangazo la ndoa lilianza hivyo hivyo. Hili ni tangazo la mwisho kabisa la ndoa kati ya kijana wetu, Onesmo Samson na binti yetu Jesca Martin” Mchungaji alisikika akiongea na kuendelea.
   “Hata kabla sijaendelea, ningependa vijana hao wapite hapa mbele” Mchungaji alisema.
   Maria akazidisha umakini wake katika kuangalia runinga. Kamera ikaanza kumuonyesha Jesca ambaye alionekana kupendezeshwa na gauni refu alilokuwa amelivaa. Mara baada ya Jesca kufika mbele, kamera ikaanza kumuonyesha Onesmo ambaye alikuwa amevaa suti nyeusi.
   Maria akaonekana kushtuka kupita kawaida, alimwangalia Onesmo mara mbili mbili huku akionekana kutokuamini kile ambacho alikuwa akikiangalia. Akajikuta machozi yakianza kumtoka, hakuamini kama kweli Onesmo alikuwa amefikia uamuzi wa kumuoa msichana mwingine badala yake.
   “Haiwezekaniiiiii.... Haiwezekaniiiii.....” Maia alisema kwa sauti huku akinekana kuchanganyikiwa.
   Akainuka kutoka kochini na moja kwa moja kuelekea nje. Maria akaanza kukimbia kuelekea kituoni huku lengo ake kuu likiwa ni kuelekea kituoni ambako angechukua daladala na kumfikisha Magomeni Mapipa, mahali ambako kanisa lile lilipokuwa.
   Maria hakutaka kuona Onesmo akimuoa msichana mwingine zaidi yake hasa ukizingatia kuwa tayari alikuwa na mtoto wake. Mara baada ya kufika kituoni, akachukua daladala na safari ya kuelekea katika kanisa lile kuanza huku lengo lake likiwa ni kuzuia harusi ile ambayo ingetarajiwa kufanyika wiki moja baadae isifanyike.
   “Nina mtoto wake. Ananisaliti, Onesmo...Onesmo....Onesmo....” Maria alikuwa akijisemea peke yake huku akiiona daladala ile ikiendeshwa kwa mwendo wa taratibu.
   Muda wote Maria alikuwa akilia, hakuamini kama Onesmo angeamua kuchukua uamuzi kama ule ambao alichagua kuufanya. Njia nzima alikuwa akijuta kwa kuchukua uamuzi wake wa kukubali kufanya nae mapenzi.
   Alikuwa na ndoto nyingi katika maisha yake lakini Onesmo huyo huyo ndiye ambaye alizizima ndoto zote ambazo alikuwa nazo katika maisha yake. Hakutaka kumuona Onesmo akimuoa msichana mwingine zaidi yake, alijiona kuwa yeye ndiye alikuwa mke halali wa Onesmo.
   “Ni lazima nimwambie ukweli. Sikubali kumuona akimuoa msichana mwingine” Maria alisema huku daladala ikiendelea na safari.
                                                                     ********
                                                                              
   Maisha yaliendelea kila siku. Onesmo akaanzisha uhusino wa mapenzi pamoja na binti wa shemasi wa kanisa hilo, Jesca Martin. Hakukuwa na muda wa kuchezeana, kitu ambacho Onesmo alikuwa akikifikiria ni ndoa tu, alihitaji kuwa na mke katika kipindi hicho.
   Harakati za uchumba zikaanza mara moja huku kamati ya harusi ikianza kazi yake. Kila mtu kanisani alikuwa na furaha mara baada ya tangazo la kwanza la uchumba kutangazwa kanisani. Watu wakawa wanaisubiria harusi ambayo ilitarajiwa kufanyika baada ya miezi mitatu.
  Kila Jumapili tangazo la uchumba lilikuwa likitangazwa kanisani hapo. Kila kitu kilionekana kwenda kama vile kilivyotakiwa kwenda. Mikakati ilikuwa ikiendelea kila siku, kilamtu alitaka kufanya kitu katika harusi hiyo.
   Siku ziliendelea kwenda mbele mpaka kufikia siku ambayo ilikuwa ni ya mwisho kutangazwakwa harusi hiyo ambayo ilikuwa imebakia wiki moja ifanyike.
   Tangazo a mwisho likatangazwa kanisani, hakukuwa na mtu yeyote amaye aliongea chochote juu ya harusi hiyo, kila mtu aliitolea maneno yake ya baraka.
   Mchungaji Samuel hakutaka kuhubiri kwa muda mrefu siku hiyo, dakika kumi zilimtosha vilivyo. Ibada ilipokwisha, washirika wote wakatoka nje na kikao cha mwisho cha kamati ya harusi kufanyika.
   “Utaniambia kilichoendelea Benjamin. Kwa sasa sijisikii vizuri, acha niende nyumbani” Onesmo alimwambia mwenyekiti wa kamati ya harusi.
   “Usijali” Benjamini alimwambia Onesmo ambaye aianza kupiga hatua kuelekea nje ya kanisa.
   “Onesmooooo....” Ilisikika sauti ya kike ikiita kwa sauti kubwa.
   Onesmo akaunyanyua uso wake na kuangalia mbele, msichana mmoaja alikuwa akimfuata kule alipokuwa huku akikimbia. Alipokuwa kwa mbali hakuwa akimfahamu lakini alipokaribia, Onesmo akashtuka kupita kiasi kwani hakuamini kama msichana yule angekuwa ndani ya jiji la Dar es Salaam.
   “Maria....” Onesmo alijikuta akiita huku akiwa haamini macho yake.
                                                                              ****
   Safari ya kuelekea Magomeni bado ilikuwa ikiendelea. Maria hakuwa katika hali ya kawaida, muda wote alionekana akiwa na mawazo. Jina la Onesmo ndilo ambalo lilikuwa limemtawala zaidi katika kipindi hicho.
   Moyoni hakuelewa kwa nini Onesmo aliamua kutaka kumuoa msichana mwingine badala yake, Maria alijiona kusalitiwa, alijiona akiachwa mpweke katika maisha yake. Aliliona gari likiendeshwa taratibu sana, alitamani ashuke ili aanze kukimbia kwani aliamini angewahi zaidi kuliko kuendelea kubaki ndani ya daladala.
   Hata kabla daladala haijafika Ubungo, foeni kubwa ikaanza kuonekana, magari hayakuwa yakitembea tena, madereva walianza kuendesha taratibu huku muda mwingine wakismama kwa muda. Maria akaonekana kukasirika zaidi, foleni ilionekana kumuudhi.
   Walikaa kwa dakika zaidi ya nane, magari hayakuwa yamesogea kwa hatua yoyote ile. Ingawa Ubungo kulikuwa na foleni kubwa lakini siku hiyo ilionekana kuwa kubwa zaidi. Magari yaliendelea kubaki katika foleni, dakika ishirini baadae, magari yakaruhusiwa.
   Maria alikwishajiona kuwa amechelewa, hakuwa na uhakika kama muda huo angewahi kufika kanisani hata kabla ibada haijakwisha. Daladala ikakata kona kulia na kuchukua barabara ya Morogoro. Hapo dereva hakutaka kuchelewa, akaongeza kasi zaidi na baada ya dakika chache wakafika Mwembechai.
   Magari yote ambayo yalikuwa yakipita kwa wakati huo yakaamriwa kupaki pembeni. Kila mmoja alionekana kutokuelewa sababu iliyowafanya matrafki kuwaambia wapaki pembeni. Maria akazidi kuchukia zaidi na zaidi, alitamani ashuke chini na kumpiga trafki kibao.
   “Kuna nini tena?” Dereva alimuuliza trafki.
   “Kuna msafara wa Waziri Mkuu unapita” Trafki alimjibu.
   Magari yalisimama kwa dakika kumi zaidi, msafara wa Waziri Mkuu ulipopita, nao wakaruhusiwa kuendelea na safari. Daladala ilipoingia katika kituo cha Magomeni Mapipa, Maria akateremka na kuanza kukimbia kuelekea kanisani.
   Maria alionekana akikimbia kama mtu ambaye alichanganikiwa, kasi yake ilikuwa kubwa kama mtu ambaye alikuwa akikimbia miripuko ya mabomu. Jasho lilikuwa likimtoka lakini wala hakujali, bado alikimbia zaidi na zaidi.
   Maria akayapeleka macho yake mbele, kanisa kubwa lililoandikwa Praise And Worship kwa juu lilikuwa likionekana mbele yake. Maria akaacha kukimbia, akaanza kutembea lakini kwa mwendo uliojaa haraka.
   “Onesmooooo....” Maria alianza kuita mara baada ya kumuona mtu akishuka ngazi za kanisa.
   Alikuwa na uhakika wa asilimia zote kwamba mtu yule ambaye alikuwa akimuona alikuwa Onesmo. Kila kitu alifanana nae, kuanzia mwendo mpaka umbo. Maria akaanza kumsogelea mtu, alipomfikia, fikra zake zilikuwa sawa, alikuwa Onesmo.
   Onesmo alibaki akimshangaa Maria kana kwamba alikuwa akiangalia muujiza. Alitamani kuongea kitu lakini akajiona akishindwa kuongea. Maria akamsogelea zaidi Onesmo, machozi yalikuwa yakimtoka. Kitendo cha kumuona Onesmo tu, alijiona akiumia zaidi hasa kila alipokuwa akifikiria kile alichokioa kwenye runinga.
   “Onesmo...Onesmo...Onesmo unanisaliti!...” Maria alimwambia Onesmo huku machozi yakimtoka.
   Hata kabla hajaongea kitu chochote Onesmo akaanza kuangalia katika kila uande mahali pale, alipoona kwamba hakukuwa na mtu, akamvuta Maria pembeni kabisa nje ya eneo la kanisa lile.
   “Maria. Umefika vipi Dar es Salaam?” Onesmo alimuuliza Maria huku akionekana kutokuamini.
   “Nimekuja kwa ajili yako Onesmo. Onesmo, unanisaliti kwa kutaka kumuoa msichana mwingine. Msichana mwingine zaidi yangu” Maria alimwambia Onesmo huku machzi yakiendelea kumtoka.
   “Nani amekwambia kwamba ninataka kuoa?”
   “Nimeona kwa macho yangu Onesmo. Nimekuona katika teevisheni. Nimekuona Onesmo” Maria alimwambia Onesmo.
   Onesmo alikaa kimya kwa muda, tayari alikwishajua kuwa alionekana kweli kutkana na ibada za kanisa lile kurushwa katika kituo cha televisheni cha Pasific. Onesmo hakuongea kitu, moyoni akajiona akilaumiwa. Kitu ambacho alikifanya mahali hapo ni kumuomba Mungu amuongoze katika maneno ambayo angemwambia Maria.
   “Kwa nini umenisaliti Onesmo?” Maria alimuuliza Onesmo.
   “Sikiliza Maria. Naomba usahau kilichopita, najua kwamba nilikuahidi mambo mengi kipindi cha nyuma. Kwa sasa nimebadilika Maria, maisha yangu yamebadilika Maria. Sahau kila kitu kilichotokea kati yangu na wewe” Onesmo alimwambia Maria.
   Maria hakuonekana kuamini, maneno ambayo aliyaongea Onesmo yalionekana kumuumiza kuliko kawaida. Hakuamini kama Onesmo yule aliyekutana nae kijijini ndiye ambaye alikuwa akiongea maneno yale. Moyoni alijisikia maumivu makali hata zaidi ya kuchomwa na msumari wa moto.
   “Unasemaje Onesmo?” Maria aliuliza kwa mshtuko.
   “Sahau kila kitu Maria. Mungu ameyabadilisha maisha yangu. Mimi ni Onesmo mpya” Onesmo alimwambia Maria.
   Maria akajiona akiishiwa nguvu za miguu, akakaa chini, machozi yalikuwa yakimtoka, hakuamini kama kukutana kwake na Onesmo kungekuwa kama vile, alitarajia furaha lakini furaha yote akaiona ikitoweka. Onesmo alikuwa ameuumia moyo wake kupita kiasi.
   “Usilie Maria. Itakubidi ukubaliane na ukweli” Onesmo alimwambia Maria maneno ambayo yalimuumiza zaidi.
Endelea kulike ==>www.facebook.com/2jiachie
ITAENDELEA SIKU YA KESHO


No comments

Powered by Blogger.