ad

ad

MARIA - 03



      “Una ujauziti wa mwezi mmoja” Daktari alimwambia Maria mara baada ya vipimo vilivyochukua dakika kumi.
   “Najua dokta, sitaki wazazi wangu wafahamu... nisaidie dokta” Maria alimwambia dokta Semi.
   Tayari Maria akaanza kulia, alijua fika kwamba alikuwa mjauzito, moyo wake ulikuwa ukijifikiria juu ya uamuzi ambao wangechukua wazazi wake. Maria aliendelea kuomba msaada kwa dokta Semi lakini hakukuwa na msaada wowote ambao aliahidiwa.
   Dokta Semi alitamani kumsaidia Maria lakini alishindwa kujua ni kwa jinsi gani angeweza kumsaidia. Alimwangalia usoni, tayari machozi ambayo yalikuwa yakitiririka mashavuni mwake yalianza kuiloanisha blauzi aliyokuwa ameivaa.
   “Haina jinsi binti. Ni lazima wazazi wako wapate taarifa” Dokta Semi alisema na kuanza kutoka nje ya chumba kile cha vipimo.
   Dokta akaanza kuelekea ofisini mwake huku mkononi akiwa na karatasi za majibu ya vipimo alivyotoka kumpima Maria. Akaingia ofisini na moja kwa moja kuelekea nyuma ya meza yake na kutulia. Akachukua karatasi ile ya vipimo na kuiweka mezani.
   “Nimefanya vipimo vyote. Binti yenu ni ujauzito” Dokta Semi aliwaambia.
   Kila mmoja akaonekana kushtuka, hakukuwa na mtu ambaye aliamini kile ambacho alikuwa amekisikia. Walimwangalia dokta Semi mara mbili mbili huku wakionekana kutokuamini.
   “Umesemaje?” Mzee Bwaro aliuliza huku akichukua karatasi ile ya vipimo.
   “Ni mjauzito” Dokta alijibu.
   Mzee Bwaro akaonekana kuchanganyikiwa, akainuka kutoka katika kiti alichokuwa amekalia na moja kwa moja kuanza kupiga hatua kuelekea nje. Usoni alionekana kuwa na hasira kupita kiasi, mwili mzima ulimtetemeka kupita kawaida.
   Hakuamini kama Maria alikuwa mjauzito. Ushauri wote ambao alikuwa akiwapa, ulinzi wote ambao alikuwa akiwapa, hakuamini hata kidogo kama kulikuwa na mwanaume ambaye angeweza kumshawishi Maria kufanya mchezo ule.
   “Siamini... Siamini...” Mzee Bwaor alijisemea huku akipiga hatua kuelekea katika chumba kile cha vipimo.
   Bi Sara pamoja na dokta Semi hawakutaka kubaki ofisini, tayari walijua kuwa kwa hasira ambazo alikuwa nazo mzee Bwaro basi ni lazima angeweza kumjeruhi Maria ndani ya chumba kile.
   Mzee Bwaro akaingia ndani ya chumba kile kifujo fujo. Akaanza kuangalia katika kila kona, chumba kilikuwa kitupu. Mzee Bwaro akaanza kumtafuta Maria chumbani mule lakini Maria hakuonekana kabisa, chumba kilikuwa kitupu.
   “Yuko wapi...? Yuko wapi...?” Mzee Bwaro aliuliza huku akonekana kuchanganyikiwa.
   “Atakuwa ameondoka” Bi Sara alijibu huku akitetemeka.
   “Ni lazima tumfuate huko huko kijijini” Mzee Bwaro alimwambia mkewe huku akionekana kuwa na hasira.
   Mzee Bwaro na mkewe wakaanza kutoka nje jengo la hospitali ile, kila mmoja alionekana kuchanganyikiwa, aibu waliiona ikianza kuwasogelea, hawakujua wangeificha wapi aibu hiyo. Njiani walitembea kwa mwendo wa haraka haraka huku kila mmoja akiwaza lake. Ujauzito wa Maria ulikonekana kuwachanganya kupita kiasi.
                                                               ***********
                                                                
   Maria alibaki katika chumba cha vipimo huku akitetemeka kwa wasiwasi. Kitendo cha dokta Semi kuelekea ofisini mwake kwa ajili ya kuwapelekea wazazi wake juu ya majibu ya vipimo vyake kulimaanisha hatari ingeweza kutokea muda wowote ule.
   Maria hakuonekana kuwa radhi kubaki ndani ya chumba kile, akasimama kutoka katika kiti alichokuwa na kuanza kuufuata mlango. Hakutaka kabisa wazazi wake wamkute ndani ya chumba kile, aliona ni bora kufanya kitu chochote cha hatari kwa wakati huo kuliko kuingia katika mikono ya baba yake mara ambapo angepewa majibu ya vipimo vile.
   Maria akaufungua mlango na kuanza kuangalia koridoni, hakukuwa na mtu yeyote zaidi ya mwanamke mmoja ambaye alikuwa akifanya usafi mahali hapo. Maria hakutaka kupoteza muda, moja kwa moja akaanza kupiga hatua kuufuata mlango wa kutokea nje na kuufungua.
   Maria hakutaka kuangalia nyuma, alianza kukimbia kwa mwendo wa kasi kuelekea kijijini. Njiani Maria alikuwa akilia tu, ujauzito ambao alikuwa ameupata ulionekana kumchanganya kabisa. Kadri alivyokimbia alijiona kutokukimbia kwa kasi kabisa hali iliyomfanya kukimbia kwa kasi zaidi.
   “Mbona hivyo Maria?” Agness alimuuliza mara baada ya kufika nyumbani.
   Maria hakujibu kitu chochote kile, akaingia ndani ambako akaanza kuweka nguo zake ndani ya mfuko na kisha kuelekea nje. Kila mtu akabaki akimwangalia Maria, macho yake yalikuwa mekundu kwa ajili ya kulia kwa kipindi kirefu.
   “Kuna nini dada, mbona umechukua nguo zako?” Agness alimuuliza.
   “Naondoka nyumbani Agness. Naelekea Dar es Salaam” Maria alimwambia Agness.
   “Unasemaje?”
   “Naondoka Agness”
   “Mbona sikuelewi. Unakwenda kufanya nini Dar es Salaam?” Agnes aliuliza huku akionekana kumshangaa dada yake, Maria.
   “Acha niondoke Agnes. Nina ujauzito” Maria alimwambia Agnes.
   “Unasemaje?” Agness aliuliza huku akionekana kushtuka.
   “Acha niondoke. Nitajifungulia mbele ya safari Agness. Kumbuka kuwa mtoto wangu ni wa kwako pia, siku atakapoletwa hapa, naomba umtunze kama mtoto wako wa kumzaa” Maria alimwambia Agness.
   “Mbona sikuel....” Agness aliuliza lakini hata kabla hajamaliza kuuliza swali lake, Maria akaanza kukimbia kuelekea uwanjani.
   Agnes hakutaka kubaki peke yake, nae akaanza kuimbia kumfuata Maria. Wote walionekana kuchanganyikiwa, Agnes alionekana kuchanganyikiwa kwa sababu hakuelewa kile ambacho aliambiwa huku Maria akionekana kuchanganyikiwa juu ya kile ambacho kilikuwa kimetokea.
   Maria alikimbia kwa kasi kubwa, mawazo yake katika kipindi hicho yalikuwa yakifikiria kufikia sehemu moja tu, ndani ya kijiji cha Mkuyuni. Hakuelewa maisha yake yangekuwa vipi, hakuelewa ni kwa jinsi gani angefika Dar es Salaam, lengo lake katika kipindi hicho lilikuwa ni kumtafuta Onesmo tu.
   “Mariaaaaaaa.... Mariaaaaaaa.....” Agnes aliita huku akikimbia lakini Maria hakusimama mpaka anapotea machoni mwa Agnes.
   Maria aliendelea kukimbia zaidi na zaidi, alipoona amechoka sana, akaanza kutembea. Jua lilikuwa kali sana lakini Maria hakutaka kujali, bado aliendelea na safari ya kuelekea katika kijiji cha Mkuyuni kabla ya kuedelea na safari ya kuelekea Dar es Salaam.
   Njiani, bado akili ya Maria ilikuwa ikimfikiria Onesmo. Hakujua ni mahali gani kijana huyo alikuwa akiishi ndani ya jiji la Dar es Salaam, hakujua angeanzia wapi kumtafuta Onesmo jijini Dar es Salaam. Akili yake haikutaka kuyajibu maswali yote, kitu ambacho alidhamiria kilikuwa ni kufika ndani ya jiji la Dar es Salaam tu.
   Maria alitembea mpaka jua likaanza kuzama. Hakusimama sehemu yoyote ile, bado safari yake iliendelea mbele. Kijiji cha Mkuyuni kilionekana kuwa mbali tofauti na siku ambazo alikuwa akielekea huko na mama yake. Kila alipozidi kwenda mbele, alijiona kutofika.
   Giza likaingia, bado Maria hakuwa amefika Mkuyuni, umbali ule ulimshangaza kupita kawaida, hakuwahi kutembea umbali mrefu namna ile. Kijiji cha Mkuyuni kilionekana kuwa mbali kwa siku hiyo, Maria akaonekana kuchoka, akatafuta sehemu ambayo ilikuwa na miti mingi pamoja na nyasi na kisha kulala.
                                                                     ***********
   “Umesemaje?”
   “Umeliona gari lile lililoelekea kule porini?”
   “Gari gani?”
   “Canter”
   “Mh..! Mimi mbona sijaliona”
   “Hujaliona? Hebu twende kule, kuna gari limeacha njia na limeelekea kule porini”
   Kwa kasi ya ajabu vijana hao wawili ambao walikuwa wakiongea huku wakiwa na kuni kadhaa wakaanza kukimbia kuelekea kule ambako gari aina ya Canter lilipokuwa limeelekea huku likionekana kuacha njia.
   Hakuna aliyeamini, gari lilikuwa limepinduka, mataili yalikuwa yakiangalia juu. Ajali ile ilionekana kutisha japokuwa kwa upande wa nyuma lilionekana kutokuharibika. Baadhi ya magunia ya mahindi yalikuwa yamerushwa mpaka katika nyasi ndefu huku magunia mengine yakiwa yametobolewa hali iliyoyafanya mahindi kumwagika.
   “Huku mbele ndipo kulipobondeka sana. Hivi dereva amepona kweli” Kijana mmoja aliuliza.
   Hakukuwa na mtu yeyote ambaye alichukua hatua yoyote kwa kipindi hicho mpaka pale baadhi ya wanakijiji wa kijiji hicho cha Semakwede kufika mahali pale. Kila mtu alibaki akishangaa tu, gari kwa nyuma lilikuwa salama kabisa ila kwa upande wa mbele, gari hilo lilionekana kuharibika kupita kawaida.
   Wanakijiji ambao walikuwa mahali hapo wakasaidiana kuwatoa majeruhi waliokuwa ndani ya gari lile na kisha kuelekea nao mpaka barabarani ambako wakasimamisha gari moja na kisha kuwapandisha.
   “Wafikisheni Hospitali ya Tumbi, Kibaha” Mweyekijiji wa kijiji hicho aliwaambia watu ambao walisimama mahali hapo na gari lao.
   Hakukuwa na maswali ya kuuliza, moja kwa dereva pamoja na wenzake ambao walikuwa ndani ya gari lile wakaanza safari ya kuelekea Kibaha katika hospitali ya Tumbi. Damu bado zilikuwa zikiwatoka majeruhi ambao walionekana kujeruhiwa vibaya.
   Kwa mwendo ambao dereva alikuwa akiiutumia, walitumia dakika thelathini wakawa wamekwishafika katika hospitali hiyo ya Tumbi ambako kwa haraka sana wauguzi wakafika mahali pale huku wakiwa na machela ambayo walikuwa wakiikokota.
   Kila muuguzi alionekana kusikitika, hali za wagonjwa zilionekana kuwatisha kupita kawaida. Majeraha makubwa ambayo yalikuwa yakitoa damu yalikuwa yakionekana vizuri machoni mwao. Hakukuonekana dalili yoyote kwa wagonjwa wale kupona, walionekana kufariki muda wowte kuanzia kipindi kile.
   “Nani amewaleta? Ndugu zao au?” Dokta Kimwinyi aliwauliza wauguzi.
   “Mhh! Wala hatufahamu, watu wenyewe waliondoka. Nafikiri hawakuwa ndugu zao” Muuguzi mmoja alisema huku machela zile zikianza kusukumwa hadi katika chumba cha upasuaji.
 Sauti za ndege zikaanza kusikika, kiubaridi cha asubuhi kikaanza kupiga hali ambayo ilimfanya Maria kuamka kutoka pale nyasini alipokuwa amelala. Kwanza alibaki na mshangao kujikuta mahali pale, hakuelewa ni kwa namna gani alikuwa amelala porini na wakati kulikuwa na nafasi kubwa ya kulala nyumbani kwao.
   Huku uso wake ukionekana kuwa na mshangao, kumbukumbu zikaanza kumrudia kichwani mwake, akakumuka kila kitu ambacho kilikuwa kimetokea katika usiku uliopita. Maria akaanza kulia. Akainuka na kisha kuendelea na safari yake kuelekea katika kijiji ambacho alikuwa na uhakika kuwa ni Mkuyuni.
   Maria alitembea kwa takribani saa moja, nyumba mbalimbali za udongo zikaanza kuonekana machoni mwake. Furaha ikaanza kurudi moyoni mwake, tabasamu pana likaanza kuonekana usoni mwake. Tayari alijiona kupata nguvu za ziada za kuendelea kusonga mbele, alijiona kuhitaji msaada wa chakula kutokana na njaa kali kumkamata.
   “Samahanini..” Maria aliwaambia wanawake ambao walikuwa wakichota maji katika kisima kimojawapo kijijini hapo.
   Wakinamama wote wakaacha kuchota maji, wakaanza kumwangalia Maria ambaye kwa muonekano tu alionekana kuchoka.
   “Naomba mnisaidie chakula. Nimetoka mbali, nimeshinda pasipo kula usiku kucha mpaka sasa hivi Maria aliwaambia wakinamama wale.
   Tayari machozi yalikwishaanza kumlenga na baada ya muda yakaanza kutiririka mashavuni mwake. Maria alionekana kuchoka na kuhitaji msaada wa chakula kwa wakti huo. Mwanamke mmoja akaanza kumsogelea Maria na kuanza kumwangalia usoni kana kwamba alikuwa akimfananisha na mtu fulani.
Endelea kulike ==>www.facebook.com/2jiachie
ITAENDELEAKESHO

No comments

Powered by Blogger.