ad

ad

She is too young to die - 24



Fahamu za Salome  zimerejea na  kujikuta akiitambua familia yake tena,  furaha imerejea upya kwenye  nyumbani kwa Gilbert. Wakati  hayo yakitokea, ukatili  ambao  Tecla aliufanya  umempeleka yeye pamoja na wenzake  jela kwa miaka kumi na tano! Baada ya hapo kazi kubwa kwa Gilbert inakuwa ni  kuthibitisha kwamba mtoto wa Tecla hakuwa wake kama ilivyotangazwa kwenye vyombo vya habari na kuifanya jamii yote iamini, hivyo heshima yake kushuka vibaya mno.
Kazi hiyo anaifanya kwa kumtumia wakili wake  Johnson Tenga, ambaye anafanikiwa kupata vibali vyote vya Tecla na mtoto wake kuchukuliwa vipimo wakiwa jela kisha yeye Gilbert na mzee Toboatobo kuchukuliwa vipimo wakiwa hospitali ya Muhimbili, majibu yalipotoka yalionyesha kwamba mtoto  wa Tecla alikuwa ni wa mzee Toboatobo ambaye bila woga alijikuta akikiri kufanya tendo la ndoa Tecla kwa udanganyifu wa  kumwekea dawa ya mapenzi sehemu za siri.
“Hivyo ndivyo huwa tunafanya  ili nasi tuwapate wanawake wazuri!” alitamka mbele ya waandishi wa habari bila  kuelewa kwamba kitendo hicho kilikuwa ni ubakaji.

Hata hivyo ilibidi mzee huyo amwombe Gilbert amsaidie kumpata mtoto wake kutoka jela kwani hakuwa na sababu ya kuendelea kuteseka kwa makosa ya  mama yake, Gilbert akamwomba wakili wake ashughulikie jambo hilo,  haukupita muda mrefu mtoto akatoka na  mzee Toboatobo akamwomba Gilbert amsaidie katika malezi.
Je, nini kitaendelea?  SONGA NAYO…
Kwa furaha aliyokuwa nayo moyoni mwake, kumkubali mtoto wa mzee Toboatobo na Tecla halikuwa jambo baya, hata hivyo ilibidi kwanza akaongee na mke wake ili siku iliyofuata aweze kutoa jibu. Gilbert akafanya hivyo, Salome naye hakuwa na shida akiamini kabisa kwa maisha ambayo  mtoto huyo alikuwa amezoea na mama yake,  angeteseka sana kuanza maisha mapya kijijini Kimbiji baba yake akiwa mganga wa Kienyeji, lazima angepata shida sana, afya yake ingeharibika na pengine hata kupoteza maisha, wote wawili wakakubaliana kumchukua mtoto huyo.

Siku iliyofuata asubuhi, Gilbert alipigiwa simu kutoka ofisini WorldCom na kutaarifiwa kwamba  mzee Toboatobo alikuwa amefika ofisini hapo na mtoto na alitaka kumwona, lakini wakati akiwa hapo walifika maaskari wawili na kumkamata wakiongozana na  mawakili wa shirika la kutetea haki za wanawake, hivyo akalazimika kumwacha mtoto ofisini ili Gilbert aende kumchukua. Habari hizo zilimshtua Gilbert, akalazimika kumsimulia mke wake,    hawakuelewa sababu ya mzee huyo kukamatwa, ikabidi  Gilbert aondoke haraka hadi ofisini  ambako alimkuta mtoto yuko mapokezi akilia, alipojaribu kumbeba mtoto alikataa.
Tembelea tangazo la chini kujua mengi kwa ku clickujionee

Hakutaka kumlazimisha, akanyoosha moja kwa moja  kwa meneja wake Davis na kuulizia kilichotokea,  akaonyeshwa gazeti lililoandika habari ya mzee  Toboatobo chini ya kichwa cha habari  “Wanaharakati wamwijia juu mzee Toboatobo”  alipoendelea kusoma zaidi aligundua kwamba kilichomponza mzee huyo ni kauli yake ya kujitapa kwamba alimwingia Tecla na kumpa mimba bila ridhaa yake kwa kisingizio cha kupaka dawa ya mapenzi kwenye uume na kumwingizia ukeni.
“Mungu wangu! Mzee kapata tatizo huyu?”
“Kabisa!”
“Hebu twende kituoni tukafuatilie” Gilbert alimwambia Davis, wote wakatoka hadi mapokezi na kumwomba msichana wa mapokezi aendelee kubaki na mtoto  mpaka watakaporejea kutoka polisi.
Hali waliyoikuta kituo cha polisi iliwashangaza na kuwakatisha tamaa, kulikuwa na wanawake wengi wenye mabango yaliyoandikwa maandishi ya kumtaka mzee Toboatobo achukuliwe hatua kali za kisheria kwa kitendo alichokifanya,  wakaingia ndani kutaka kuonana naye lakini walizuiliwa, mpaka wanaondoka kituoni saa nane mchana walikuwa hawajamwona.  Gilbert akamchukua mtoto huku akilia kwenda nyumbani kwake kuanza maisha mapya, familia nzima ilimfurahia na Faith akapata mtoto wa kucheza naye.
“Anaitwa nani?” Faith aliuliza.
“Festo!” Gilbert akajibu jina lililomwijia kichwani kwani hakuwa  ametajiwa jina la mtoto, likanasa hapo hapo, kila mtu akaanza kumwita mtoto huyo kwa jina la Festo.
Siku iliyofuata mzee Toboatobo alifikishwa mahakamani kwa kosa la ubakaji,  Gilbert pamoja na wakili wake walikuwepo  kufuatilia kesi hiyo iliyokuwa imeshikiwa bango na Wanaharakati wa kutetea wanawake. Hapakuwa na dhamana, akatajiwa shtaka lake na kupelekwa moja kwa moja mahabusu Segerea. Gilbert alipomuuliza wakili wake kuhusu kesi hiyo na alivyoiona, alielezwa wazi kwamba hapakuwa na namna yoyote ya kumsaidia mzee Toboatobo kwa sababu yeye mwenyewe alikiri kufanya kosa hilo akirekodiwa na  waandishi wa habari,  maneno ambayo kama yangetolewa mahakamani kama ushahidi lazima angekwenda jela si chini ya miaka thelathini.
“Kwa hiyo hakuna namna?”
“Sikushauri upoteze muda wako kwenye kesi hii,  mwache avune alichopanda!”  wakili alishauri na Gilbert akakubaliana na ushauri  wake.
Mwezi mmoja baadaye alifanya tafrija kubwa nyumbani kwake   kuwashukuru  ndugu, jamaa na marafiki wote walioshirikiana naye katika matatizo yote aliyoyapitia,   watu maarufu wengi jijini Dar es Salaam walialikwa pamoja na wafanyakazi wote wa WorldCom, kila mtu alifurahia kuwepo hapo, pia Salome alipewa nafasi ya kutoa shukrani zake akiwa ameketi kwenye kiti cha matairi, hayo ndiyo yaligeuka kuwa maisha yake.
Baadaye walipata nafasi ya kuongea na waandishi wa habari kwa ajili ya kutoa habari hiyo kwenye vyombo vya habari siku iliyofuata, maswali yalikuwa mengi lakini kubwa likawa ni kwanini Salome alijitoa kiasi hicho kwa ajili ya mume na mwanae mpaka akajikuta akipata kilema cha maisha, jibu lake liliwashangaza.
“They were too young to die!” (Walikuwa wadogo mno kufa!)
“What about you Gilbert?” (Vipi kuhusu wewe Gilbert?)
“My wife was too young to die”! (Mke wangu alikuwa mdogo mno kufa!)
Wote wakatoa jibu la aina moja, wakakumbatiana na kucheka kwa furaha ambayo iliendelea kuwemo katika maisha yao siku zote baada ya hapo, wakiwa na watoto wawili, Faith na Festo ambaye pia walimhesabu kuwa mtoto wao baada ya mama yake kufa kwa kipindupindu gerezani.
MWISHO.
MTUNZI: ERIC SHIGONGO

No comments

Powered by Blogger.