ad

ad

MASWALI 10 YA KUJIULIZA KABLA YA KUACHANA, TALAKA

Uhusiano wowote huanza kwa furaha na matarajio mengi. Hapa tuuweke ule wa watu wanaokutana kwa sababu za kingono na kumalizana ndani ya muda mfupi. Msemo wa mwana Bongo Flava, Ali Kiba katika wimbo Single Boy kwamba “ukinipenda tunamalizana leoleo”.

Hapa nauzungumzia ule uhusiano ambao hukua, yaani huanza mpaka hatua ya mtu kumwita mwenzake mpenzi! Huu ndiyo nauzungumzia kuwa huanza kwa bashasha nyingi na kujaa matarajio chanya kwa kila mmoja. Nyakati za mwanzo huwa haitokei kufikiria kuachana.
Hutokea kusimuliana matukio mabaya ambayo watu waliyapitia katika uhusiano uliopita, anayesimulia hujiaminisha kwamba atakuwa mzuri na hatafanya makosa kama ya mwenzake. Kwa kifupi ni kuwa ahadi chanya hutawala nyakati za mwanzoni kiasi ambacho imani kubwa hujengeka nyoyoni.
Ahadi za mwanzoni ni kilevi mithili ya bangi ambayo ikishamuingia mtu humpumbaza akili na kumfanya amwamini mwenzi wake kuliko chochote ndani ya muda mfupi. Hata mwenye matatizo ya moyo, ukipima mapigo yake yatakuwa mazuri kutokana na matumaini aliyonayo.
Siku zinavyokwenda mambo hubadilika. Maudhi yanapochukua nafasi hufanya tamu kugeuka shubiri. Wanafasihi wa Bendi ya African Stars ‘Twanga Pepeta’ waliimba katika wimbo wao Sumu ya Mapenzi kwamba “sumu ya mapenzi ni maudhi”.
Kwamba, maudhi yanapoingia kwenye uhusiano huigeuza ladha ya asali kuwa shubiri. Humsababishia mtu kumuona mpenzi wake ni mbaya kama Shetani wakati mwanzoni alimsifu kuwa ni mzuri mithili ya malaika. Hii ni namna ambavyo mapenzi yanavyoweza kubadilika.
Hata hivyo, lipo jambo linaloweza kutokea moja tu na likabadili sura ya mchezo. Uhusiano umekuwepo kwa miaka mingi lakini ukavunjwa/kuvurugwa na tukio moja. Mathalan, mtu kamfumania mwenzi wake, baada ya tendo hilo, kitakachofuata ni matamko ya kushushana hadhi na chuki.

Binadamu wametofautiana, wapo wenye mioyo yenye matarajio ya kuendelea, vilevile kuna wenye matarajio ya mgeuko au mabadiliko. Sitaki kutumia nyoyo ngumu kwa maana hata yule anayesemwa ana moyo mgumu huumia, pengine zaidi ya anayeitwa mwenye moyo mwepesi.
Mwenye moyo wenye matarajio ya kuendelea anakuwa na imani kwamba hata baada ya migogoro mingi na mwenzi wake, lipo penzi la kweli na maisha yenye furaha zaidi na upendo baadaye. Kwa maana hiyo husamehe akitarajia kupata kilicho bora baada ya misukosuko.
Aliye na matarajio mgeuko au kwa lugha nyingine anayeamini mabadiliko, baada ya maudhi na migogoro hushindwa kuvumilia. Imani yake humwambia kwamba akipata mpenzi mwingine, anaweza kuishi maisha ya furaha na maelewano zaidi kuliko kuendelea na aliyenaye.

Mara nyingi hutokea mtu anasuluhishwa na anakubali lakini akikaa peke yake anajikuta anajilaumu kwa kitendo chake cha kukubali suluhu. Kisaikolojia, ni bora kwa mtu huyu kuachiwa uwanja mweupe wa kwenda kuliko kung’ang’anizwa au kubembelezwa.
Katika pointi ya wazi na rahisi zaidi ni kuwa mtu huwa hang’ang’anizwi au kubembelezwa kuendelea na mwenzi wake. Isipokuwa hushauriwa kwa hoja ambazo humuingia mhusika na kuamua kubadili uamuzi. Kusamehe ni utashi wa mtu, maana yeye ndiye anayejua ubora na ubaya wa mtu.
Kusamehe ni ridhaa ya moyo kwa sababu kama umeshakinahi, hata ije mbeleko ipi, matokeo yake ni mabaya sana. Hutokea watu ugomvi mdogo kukumbushiana matukio mabaya yaliyopita. Hii husababishwa na kukosekana kwa msamaha wa kweli.
Yote kwa yote, ni vema kutambua kuwa inauma sana kuachana na mtu ambaye mwanzoni mlipendana. Anayeweza kutengana na mpenzi au mwanandoa mwenzake akiwa anatabasamu, huyo bila shaka atakuwa na ushawishi wa pembeni. Na kwa hakika, baadaye mtu wa aina hiyo hujuta sana yanapomrudia.

Somo letu linahusu maswali ya kujiuliza kabla ya kuchukua uamuzi wa kuachana au kupeana talaka (kwa wanandoa). Binadamu si kama mbuzi, kwa maana hiyo wanapokutana, kunakuwa na sababu ya kukutana kwao, hivyo haitakiwi kuamua kuachana bila angalizo.
Katika makala haya, utapata kujifunza au kujiongezea elimu kuhusu maswali 10 ambayo ama yanaweza kukufanya urudi nyuma na kuendelea kuujenga uhusiano wako au kushikilia msimamo wa kuachana lakini ukiwa na akili iliyo bora kabisa.  Ni maswali gani ya kujiuliza? TUKUTANE WIKI IJAYO

No comments

Powered by Blogger.