TOROJO BAMIA (Winga teleza) - 05
“Nina imani elfu inakutosha, una jingine?” Suzy
alinyoosha mkono kumpa Shuku lakini hakupokea kitendo kilichomuuzi Suzy na
kumkazia macho kumuuliza.
“Kuna mtu kakutuma? Haya niambie.”
“Sivyo hivyo Suzy.”
“Sasa unashida gani Shuku? Unajua kuna sehemu nawahi kuna
ofa.”
“Nashida na wewe,” Shuku alijikakamua.
“Mimi?” Suzy alishtuka na kujishika kifuani.
“Eeh.”
“Shida gani?”
“Unajua Suzy nateseka kila nikuonapo.”
“Mmh! Makubwa, jamani mbona mapya, Shuku mimi nikutese wewe?
Nimegeuka mchawi nakuchukua usiku na kukugeuza fisi?”
“Hapana Suzy kimapenzi.”
“Unamaanisha unanitaka niwe mpenzi wako?”
“Ndi..ndi..yo Suzy.”
“Muone huna hata haya hata kuzungumza huwezi unajua
kabisa mimi si saizi yako. Shuku umenidharau kiasi gani kunisimamisha na
kunieleza ujinga wako?” Suzy alikuja juu na kupaza sauti iliyosikika umbali
mrefu.
“Si..si..hivyo..Su..su zy...na..na kupenda.”
“Shuku mbona unataka kunitia nuksi huko niendako mambo
yangu yaende ndivyo sivyo.”
“Lakini Suzy mpenzi hayapo hivyo nami nina haki ya
kuyasema mateso yangu kwako.”
“Hebu niangalie,” Suzy alisema kwa sauti huku akijigeuza
mbele ya Shuku kitu kilichomfanya Shuku ajute kumsimamisha mbele za watu na
kujiona kama kavuliwa nguo. Alitamani kukimbilia kuepuka aibu ile lakini miguu
ilikuwa mizito alibakia kasimama kama sanamu.
“Jamani mimi ni hadhi ya Shuku?” aliwauliza mashoga zake
kwa sauti ya juu waliokuwa mbali kidogo na yeye.
“Ha! Ndicho alichokusimamishia?” waliuliza.
“Eti jamani mbona leo kajua kunitia nuksi, najiona kama
nimekutana na paka mweusi.”
Yalikuwa maneno yaliyomdhalilisha Shuku na kujiona kama
kajipaka kinyesi, Shuku akiwa ndani ya gari aliyawaza yale yaliyomfanya
awaogope wanawake wazuri kama ukoma.
Alijiuliza siku ile yule demu na shoga zake waliomtoa nishai wakimuona yupo
vile watasemaje.
Alikwenda kupiga picha na
kuzipeleka kwa mkuu wa usalama barabarani, kisha alirudi uswazi kwake
kulipa kodi ya nyumba. Alipokaribia nyumba aliyokuwa akiishi alifungulia muziki
kwa sauti ya juu na kuwafanya wote kuliangalia lile gari.
Alilifunua na kuwafanya wote waliokuwa wamekaa akiwemo
Suzy kulishangaa lile gari lilionekana la ajabu mtaani,alilipaki pembeni ya
nyumba anayoishi.
Alitulia kidogo kabla hajateremka kuwaacha watu washangae
kwa muda kisha alilifunga na kutulia tena kabla ya kuteremka huku kila mmoja
akimtumbulia macho. Suzy na kampani yake walijiuliza zungu la unga limetoka
wapi. Baada ya kutembea kuelekea ndani wote walishtuka
kumuona Shuku.
“Suzy yule si Shuku?”
“Hapana Shuku awe vile labda ndugu yake.”
“Hapana ni Shuku.”
“Makubwa mbona tutakoma, gari na pamba kali
katoa wapi?”
“Najua?”
“Mmh! Inawezekana alinitongoza akijua mimi ni
hadhi yake, maskini sikujua,” Suzy alijikuta akijilaumu kumkataa Shuku.
“Dharau zako shoga, lakini bado una nafasi, sasa zamu
yako kujipendekeza kwake,” shoga yake
alimshauri.
“Naona aibu.”
“Aibu ya nini wakati ni jambo la kawaida bila kuwa kauzu
mjini hatukai.”
Wakati wakijadiliana na hali ya Shuku, ndani walimpokea
kwa mshtuko.
“Jamani hodi,” Shuku aliingia kwa mama mwenye nyumba.
“Ha! Shuku?” alishtuka kumuona alivyolipuka.
“Ndiyo mimi mama.”
“Ha! Mwanangu siamini!”
“Amini mama ni mimi.”
“Karibu mwanangu.”
“Asante, sasa mama mi si mkaaji kile chumba alichohama
mtu jana kina mtu?”
“Hakina baba.”
“Sasa mama, sasa hivi nitalipia miaka miwili na deni ulilokuwa
ukinidai.”
“Hakuna tatizo baba, tena utakuwa amenisaidi maana hali
ilikuwa tata.”
“Ila chumba changu kitakuwa na vitu vyangu nami nitakuja
siku moja moja, lakini sasa hivi nina maisha mengine kabisa.”
“Jamani Shuku sasa hivi unaishi wapi?”
“Utajua muda si mrefu mama.”
Shuku alimuhesabia fedha ya miaka miwili na deni kisha
alimpa elfu ishirini ya soda.
“Asante mwanangu, Mungu akuzidishie huku uliko.”
“Atuzidishie wote, ila baada ya muda nitakuja kubadili
vitu vya ndani, na hii fedha atampa salmini amihamishie vitu vyangu.”
Shuku baada ya kulipia pango miaka miwili aliagana na
mama mwenye nyumba na kuelekea kwenye gari lake. Wakati anatoka aliwakuta wale
wanawake wakisumbiri kwa hamu wamuone kwa mara nyingine, Shuku aliyelipuka
pamba za nguvu na kamba nzito shingoni, chini alikuwa na raba kali. Kwa jinsi
alivyokuwa hakukuwa na mwanamke yeyote anayeweza kusimamishwa na Shuku
akakataa.
Kabla ya kutoka nje alivaa miwani ili aweze kuwasanifu
waliombele yake, alipofika mbele ya gari lake aliwatazama wale wasichana macho
yalivyowatoka kama wameona meli barabarani, Shuku alichekea moyoni. Kabla ya
kuondoka walitokea washkaji zake waliokuwa wakirudi toka kwenye mihangaiko,
kwanza walimpita bila kumjua alipowaita ndipo waliposhtuka na kushangazwa na
maajabu ya dunia.
“Shuku ni wewe?”
“Ni mimi ndugu zangu.”
“Mbona kama njozi ni asubuhi tulikuwa pamoja ajabu sasa
hivi umekuwa kama mtu wa hadithini?”
“Ni historia ndefu ila tutazungumza wiki endi.”
“Sasa tuachie basi mshiko, yaani baada ya kuachana
asubuhi siku ya leo imekuwa na gundu tupu.”
“Poa wangu,” Shuku aliingiza mkono mfukoni na kutoa fedha
alizozihesabu kwa kuzionesha ili wale wasichana waone na kuhesabu elfu
therasini na kumpa kila mmoja elfu kumi kisha aliwaaga rafiki zake.
“Sasa washikaji ngoja nirudi nikapumzike, nilikuja
kulipia chumba changu pia nilipitia kwa mkuu wa trafiki kwa ajili ya leseni si
mnajua sina gamba sitaki nikitembea na gari nipate usumbufu.”
“Mmh! Hatukuwezi, sasa ndo upo anga zipi?”
“Mtajua tu washikaji zangu nikija jumapili mtaelewa.”
Baada ya kusema vile aliingia kwenye gari, kabla ya
kuondoka alilifunua gari na kuwafanya rafiki zake wapige kelele za mshangao.
“Wawooo, si mchezo mwana una kitu cha nguvu mwaka huu
wanga lazima wazime zao.”
“Poa washkaji baadaye,” Shuku alisema huku akiwasha gari
aondoke. Wakati Shuku akiagana na rafiki zake ili aondoke zake Suzy na shoga
zake walikuwa kwenye kigagaziko kikubwa wafanye nini ili kumnasa Shuku.
“Sasa jamani nitafanyaje na Shuku ndio anaondoka?” ITAENDELEA KESHO HAPAHAPA
KAMA ULIKOSA SEHEMU ZA NYUMA SOMAHAPA
1.SOMA SEHEU YA KWANZA >>>www.2jiachie.com/2014/06/torojo-bamia-winga-teleza-01.html
2. SEHEU YA 2: >>www.2jiachie.com/2014/06/torojo-bamia-winga-teleza-02.html
3. SEHEU YA 3: >>www.2jiachie.com/2014/06/torojo-bamia-winga-teleza-03.html
KAMA ULIKOSA SEHEMU ZA NYUMA SOMAHAPA
1.SOMA SEHEU YA KWANZA >>>www.2jiachie.com/2014/06/torojo-bamia-winga-teleza-01.html
2. SEHEU YA 2: >>www.2jiachie.com/2014/06/torojo-bamia-winga-teleza-02.html
3. SEHEU YA 3: >>www.2jiachie.com/2014/06/torojo-bamia-winga-teleza-03.html

Post a Comment