ad

ad

BEYOND LOVE- (ZAIDI YA MAPENZI) SEHEMU YA 40 MPAKA YA 41




Beyond Love- 40
Kama mapenzi ni raha, basi kwa Mariam hayakuwa na maana yoyote, kwani siku zote yameendelea kuwa msumari wa moto katika maisha yake. Kila anapokaribia kupata faraja, lazima kuna kitu kinaingia na kuharibu furaha hiyo. Mariam anakuwa mtu wa kulia kila siku. Machozi hayakauki machoni mwake. Yote hayo yanasababishwa na mwanaume mmoja tu, Tom, ambaye hathamini wala kuheshimu penzi lake.
Anapata mateso makubwa, kusimangwa, kufukuzwa nyumbani na mengine mengi. Jambo linalosababisha aamue kukimbia mji na kwenda kwa bibi yake anayeishi Matombo, Morogoro. Akiwa huko anaanza maisha mapya na kufanikiwa kumsahau kabisa hadi pale alipoona gazeti mjini alipotumwa na bibi yake.
Matatizo yakafumuka! Akaanguka na kupoteza fahamu ambapo kijana Ramsey ndiye aliyejitolea kumsaidia hadi alipopata nafuu akasafiri naye hadi Dar es Salaam na kwenda kumwangalia Tom aliyekuwa amelazwa.
Mariam anakuwa tayari kugombana na wazazi wake kwa ajili ya Tom, anaamua kuishi hotelini na Ramsey ambaye baadaye anamtaka kimapenzi jambo lililopingwa vikali na Mariam. Hata hivyo baadaye anamkubalia, lakini hakuwa tayari kufanya naye mapenzi, kitu kilichomuudhi sana Ramsey aliyeamua kumuacha na kurudi zake Morogoro.
Mariam akaamua kujiua, lakini kabla ya hajafanya hivyo anajikuta akijisikia mwenye dhambi sana kujitoa uhai wake. Akaamua kuahirisha, hapo ndipo alipoona umuhimu wa kwenda kwa wazazi wake ambao walimpokea kwa mikono miwili.
Akiwa nyumbani kwa wazazi wake, anapanga safari ya uongo ya kwenda kwa rafiki yake Clara, lakini ukweli ni kwamba alikuwa anakwenda Muhimbili. Huo ukawa ndiyo utaratibu wake wa kila siku, hadi siku apoamua kusema ukweli mbele ya mama yake.
Mzozo mkubwa unaibuka lakini mwisho wake, Mariam anaamua kurudi nyumbani kwake Mbezi, anakuta nyumba chafu sana yenye mpangilio mbovu, anaweka vitu sawa na kufanya usafi kisha anaanza maisha upya huku jambo kubwa linalokuwa mbele yake likiwa ni kumhudumia  Tom.
Miaka minne badaye, Tom anazinduka mbele ya Mariam, anamfukuza akimwambia aondoke kwani Mayasa akifika ingekuwa ugomvi! Kwa kifupi Tom amekupoteza kumbukumbu kabisa, lakini baadaye anapata picha kwamba alivamiwa na majambazi usiku akiwa anarudi nyumbani.
Tom anapooza kuanzia shingoni hadi miguuni, taarifa ambazo Mariam alipewa! Mariam hamwelezi Tom ukweli juu ya kifo cha mama yake. Kila anapomuuliza, anajaribu kumficha! Lilikuwa jambo gumu sana kumweleza Tom kwamba mama yake alifariki dunia, tena alizikwa na Halmashauri ya Jiji. Je, nini kitatokea? SONGA NAYO....

 Hakukuwa na kitu kingine chenye thamani katika maisha ya Tom kama mama yake, hapakuwa na mtu muhimu zaidi maishani mwake kama mama yake! Kwa Tom, mama yake alikuwa kila kitu. Alikuwa uhai wake, furaha yake, kila kitu chake. Kumuona mama yake akiwa hai tu, ilitosha kabisa kumfanya mwenye furaha siku zote.
Sasa mama yake hayupo tena duniani, mbaya zaidi hajui na wala hana taarifa zozote juu ya kutokuwepo kwa mama yake duniani. Pamoja na kutokujua hilo, moyo wake ulikuwa mzito kuliko kawaida, alihisi kama ganzi fulani ikizunguka moyoni mwake, alihisi kitu.
Tom akayatoa macho yake katika hali ambayo hata Mariam mwenyewe alishindwa kuelewa kilichokuwa akilini mwake. Midomo yake ikaanza kutingishika.
“Mariam!”
“Nakusikiliza mpenzi wangu!”
“Unanipenda?”
“Hata moyo wako unalitambua hilo!”
“Utakuwa tayari kuniacha niendelee kuumia?”
“Hapana!”
“Unaweza kumdanganya mpenzi wako?”
“Hapana!”
“Nahitaji kujua ukweli, mama yangu yupo wapi?!” Tom alisema akiwa hana chembe ya furaha usoni mwake.
“Unamaana gani?”
“Nataka kujua mama yangu alipo!”
“Ngoja nikuambie ukweli mpenzi wangu, jana nilienda nyumbani nikiwa na furaha sana, nilitamani sana kukutana na mama ili nimweleze kuhusu hali yako, lakini nilipofika nyumbani sikumkuta mama, aliacha maagizo kwamba anakwenda nyumbani Musoma, lakini majuzi alikuwa akinieleza nia yake ya kuanza kukushughulikia kienyeji, nadhani atakuwa huko,” Mariam akasema maneno hayo akiwa macho makavu.
Haikuwa rahisi kupingana naye, hasa kutokana na jinsi alivyokuwa akizungumza kwa kujiamini huku macho yake akiwa ameyatuliza usoni mwa Tom ambaye alianza kuamini maneno ya Mariam.
“Sawa mpenzi wangu, kama ni kweli, lakini kama ni uongo ni wazi kwamba hunipendi!”
“Nakupenda mpenzi wangu!”
“Lakini kuna kitu nahisi!”
“Ondoa hisia nyingine zozote nje ya penzi lako la kweli kwangu mpenzi wangu!”
“Ok!” Tom akajibu.
Jambo hilo likaisha wakiwa na maelewano kwa pamoja, Mariam akambusu Tom midomoni mwake, macho yake yalikuwa yanazungumza jambo, lakini bado akaongezea kwa kinywa chake.
“Nakupenda sana Tom!”
“Nakupenda pia Mariam wangu!”
******
Tom aliendelea kukaa hospitalini kwa mwezi mzima zaidi huku hali yake ikiendelea vizuri lakini hakuweza kuinuka kitandani. Marim alikuwa msaada pekee kwa Tom, lakini siku zote hakumweleza ukweli wa kifo cha mama yake.
Hiyo iliendelea kuwa siri iliyopo katikati ya moyo wake. Baada ya miezi miwili, Tom aliruhusiwa kurudi nyumbani kwa sharti la kupelekwa Kliniki kila baada ya mwezi mmoja kwa ajili ya kuangalia upya maendeleo ya afya yake.
Hilo ndilo lililofanyika, maisha hayakuwa mazuri nyumbani kwao kwani hawakuwa na uwezo kifedha wala vitega uchumi vya kuwaingizia kipato. Siku moja usiku wakati wa chakula cha usiku, Mariam alimweleza mumewe wazo alilokuwa nalo juu ya maisha yao.
Waliishi kwa upendo na Tom hakumkumbuka tena Mayasa, alimfananisha na shetani ambaye aliharibu maisha yake, kwake Mariam akawa ndiye kila kitu. Maisha yale magumu hayakumfurahisha kabisa Mariam, alitakiwa kufanya jambo moja muhimu sana ili kuyafanya maisha yao angalau yawe yenye furaha kutokana na kutengwa kwao na watu wanaowazunguka hasa wazazi wa Mariam ambao kwa wakati huo wangepaswa kuwa msaada pekee kwa maisha yao.
“Baby kuna kitu nimefikiria kwa muda mrefu sana na kupata ufumbuzi,” Mariam akamwambia Tom aliyekuwa ameegemea kwenye mto, akila.
“Ni nini hicho mpenzi wangu?”
“Tutaishi maisha haya hadi lini?”
“Unamaanisha nini mpenzi?”
“Maisha haya yasiyo na uhakika wa kesho, tutaendelea nayo hadi lini? Lazima nifanye kitu mpenzi wangu!”
“Umefikiria kufanya nini?”
“Nadhani ni bora nitafute kazi.”
“Sawa, naungana na wewe!”
Ndivyo ilivyokuwa, siku iliyofuata Mariam akaanza kutafuta kazi sehemu mbalimbali jijini Dar es Salaam, alituma maombi sehemu nyingi sana na mwishowe akaitwa katika Benki ya CRDB kwa ajili ya usaili. Baada ya kufanyiwa usaili akabahatika kuchaguliwa kuanza kazi rasmi kama Afisa Biashara wa Tawi la Vijana jijini Dar es Salaam.
Wiki moja baadaye Mariam akaanza kazi rasmi katika Benki ya CRDB Tawi la Vijana.  Maisha yakabadilika, alichokifanya ni kumuajiri msichana wa kazi ambaye alikuwa akimhudumia mumewe Tom. Waliishi maisha ya furaha sana, kwake kumuona Tom akitabasamu ilitosha kabisa kumfanya awe mwenye furaha.
Kila ifikapo mwisho wa mwezi alihakikisha anampeleka hospitalini kwa ajili ya kufanyiwa uchunguzi zaidi. Kila kitu kilikwenda sawa, lakini tatizo lilikuwa moja tu, kila Tom alipouliza kuhusu mama yake, alijibiwa kwamba yupo kijijini. Jioni moja, hali ilikuwa tofauti, Tom akamwambia kama ni kweli mama yake alikuwa amekwenda kijijini, basi aende akamfuate.
“Lakini alisema atakuja.”
“Kwani ni muda gani tangu nimetoka hospitalini?”
“Ni mrefu ndiyo!”
“Sasa kama ndivyo, unadhani mama anaweza kukaa muda mrefu kiasi hicho bila kuja kutizama hali yangu? Haiwezekani Mariam, kuna kitu unajaribu kunificha, naomba nieleze ukweli Mariam, mama yangu yupo wapi?” Tom alibadilika, alionyesha ukali ambao hata Mariam mwenyewe hakuutarajia kabisa.
Mariam akashindwa kuzungumza, akajikuta machozi yakianza kuchuruzika machoni mwake kama maji! Alianza pole pole, lakini akajikuta anaanza kulia kwa sauti kubwa zaidi huku akitaja jina la mama yake na Tom.
“Kwani kuna nini?”
Mariam hakujibu.
“Kuna kitu unajaribu kunificha Mariam, tafadhali naomba niambie ukweli!”
“Tom, sina sababu ya kuendelea kuificha siri hii!”
“Siri gani?”
“Juu ya mama!”
“Niambie basi, kuna nini?”
“Naomba usinifikirie vibaya Tom, ilikuwa lazima nitunze siri hii, lakini ni wazi kwamba isingewezekana kuendelea kukaa nayo kwa muda mrefu zaidi. Naomba upokee taarifa hii kama ilivyo. Uikubali, uiamini na uichukue kama ilivyo!”
“Mbona sikuelewi Mariam, hebu naomba nieleze kinachoendelea, achana na mafumbo ambayo ni giza kwangu!”
“Tom mpenzi wangu, nakuomba sana, usipaniki juu ya hili nitakalokuambia mume wangu!”
“Kama hutaki kusema acha...maana naona unanitibua sasa!”
“Siyo hivyo mpenzi, ni kwamba....mama alishafariki Tom!” Mariam akasema akihema kwa kasi sana.
“Unasemaje?”
“Mama alishafariki....” Mariam hakuweza kumalizia sentesi yake, tayari mvua ya mchozi ilishafunika macho yake.
Huzuni ikatanda chumba kizima.

Je, nini kitatokea? Fuatilia 

 Beyond Love- 41

Baada ya Mariam kuitunza siri ya kifo cha mama yake Tom kwa muda mrefu, hatimaye ameamua kuanika ukweli hadharani! Amemweleza ukweli Tom, ambaye ameonyesha kushtuka sana. Je, nini kitatokea? Nini hatma ya wawili hawa? Hebu SONGA NAYO sasa katika sehemu hii ya mwisho ya simulizi hii yenye mafunzo makubwa kwa jamii...


“Kwanini ulinificha jambo hili siku zote?”
“Ilikuwa ni mapema sana kukuambia mpenzi wangu, lakini nakuomba sana tena sawa, piga moyo konde, huo ndiyo ukweli ambao hakuna kitu cha kuweza kuubadilisha!”
“Mama...umekufa nikiwa bado nakuhitaji mama yangu...bado nilikuwa nahitaji sana busara zako mama yangu...umeniacha na upweke mama! Sina la kufanya mama yangu, nenda mama nasi tupo njia moja na wewe!” Tom alisema maneno hayo akilia sana.
Kila alipokumbuka mapenzi ya mama yake kwake, alizidi kuchanganyikiwa, mama yake alikuwa kila kitu katika maisha yake, kila alipokumbuka shida na dhiki zote walizopitia ndivyo alivyozidi kupatwa na machungu. Tom alizidi kulia.
“Nyamaza mume wangu mpenzi, kashaenda huyo, Mungu amemwita katika ufalme wake, hakuna kinachoweza kumrudisha, mwache apumzike kwa amani. Kazi yetu kubwa kwa sasa ni kumwombea tu!”
“Mungu amlaze mahali pema peponi!”
“Amen!”
“Inabidi unipeleke mahali alipolala mama yangu, natakiwa kupaona, angalau ning’olee hata majani juu ya kaburi lake!”
“Naomba uvumilie na hili mpenzi wangu!”
“Lipi?”
“Mama amezikwa  na Halmashauri ya Jiji!”
“Unasema?”
“Huo ndiyo ukweli Tom, wakati mama anafariki sikuwa Dar, nilipata taarifa hizi nikiwa Morogoro kama nilivyokuambia mwanzoni!”
“Mama yangu anazikwa kama mbwa? Anakosa heshima anayostahili binadamu? Nimekukosea nini Mungu wangu mimi jamani? Kwanini mambo haya yanatokea kwangu tu jamani? Kwanini? Kwanini lakini?” Tom alipiga kelele, lakini Mariam akajitahidi kumnyamazisha.
Ilikuwa kazi ngumu sana, lakini mwisho wake Tom akanyamaza. Kila alipokumbuka sura ya mama yake, Tom alikuwa akimwaga machozi. Mama yake alikuwa ni kila kitu katika maisha yake. Maisha yaliendelea kama kawaida, kasoro kubwa ikiwa ni ulemavu alionao Tom pamoja na kumkosa mama yake mzazi.
Lingine kubwa zaidi ni kwamba, mpaka wakati huo, wazazi wa Mariam waliamua kumtenga, hawakutaka kushirikiana naye kwa jambo lolote. Walimwachia maisha yake na Tom, ambaye kwao alikuwa sawa na shetani. Yote hayo hakuwa aliyeyaweka akilini wala kuona kama kuna tofauti kubwa sana katika maisha yao. Kwako upendo wa kweli ndiyo ulikuwa kila kitu.

MWAKA MMOJA BAADAYE
Jambo kubwa lililofanyika ndani ya mwaka mmoja, ilikuwa ni kurudisha uhusiano kati ya wazazi wa Mariam na wao, ilikuwa kazi ngumu sana, lakini kwa kupitia wazee wenye hekima, suala hilo liliisha bila matatizo. Wazazi wa Mariam wakawasamehe Tom na Mariam kwa yote yaliyotokea, wakafungua ukurasa mpya.
Wakawa wanatoa ushirikiano kwa kila kitu, hata katika mambo yaliyohusu fedha, kila kitu kikawa kimepita, wakawa karibu wakihangaikia afya ya Tom pamoja. Mpaka muda huo Tom alikuwa bado hajaamka kitandani, mwili wake ulikuwa umepooza.
Pamoja na juhudi za mkewe na wazazi wake kumuhangaikia katika Hospitali mbalimbali, ndani na nje ya nchi, lakini mafanikio yalikuwa hakuna. Mariam alifikia hatua ya kuchukua mkopo kazini kwao ili aweze kumhangaikia Tom wake, angalau aweze kuamka, lakini ilishindikana.
Hilo lilizidi kuongeza maumivu katika ndoa yao, ambayo yeye aliifananisha na ndoa ya mateso. Hata hivyo, mara zote Tom alikuwa akimkataza juu ya matumizi makubwa ya fedha kwa ajili ya kuhangaikia afya yake, akisisitiza kwamba haikuwa rahisi kupona.
“Lakini kwanini unasema hivyo mpenzi wangu? Napenda sana kukuona ukiamka tena!”
“Sawa, lakini naamini nitaamka siku ambayo Mungu mwenyewe atakuwa ameichagua!”
“Hapana darling, hupaswi kukata tamaa mapema kiasi hicho!”
“Lakini pia hupaswi kutumia fedha nyingi kiasi hiki katika jambo ambalo linaonekana dhahiri kuwa ni gumu kufanikiwa!”
“Unanikatisha tamaa tu mpenzi wangu!”
Hayo ndiyo yalikuwa maisha yao, kila kukicha Mariam alikuwa akihangaika kutafuta dawa hadi za kienyeji kwa ajili ya kurudisha afya ya Tom, lakini haikuwezekana. Pamoja na hayo, kuna jambo moja ambalo lilimshangaza sana Mariam.
Tom, alikuwa na kawaida ya kumuita Mariam akionyesha kutaka kumwambia jambo, lakini akifika ghafla anaonekana kusahau. Tatizo hilo liliendelea kwa mwaka mmoja zaidi, kiasi kwamba Mariam akawa anampuuza, kwani kila anapotaka kusema anajikuta amesahau.
“Lakini  una nini Tom? Mbona kila unapotaka kusema jambo unasahau?”
“Hata mimi nashindwa kuelewa, ila ni jambo muhimu sana, kila nikitaka kusema nashangaa nasahau, lakini kuna siku nitakumbuka, na utaona jinsi jambo hilo lilivyo kubwa na muhimu!”
“Haya hebu tungoje huo muujiza!”
Hiyo ikaendelea kuwa kawaida ya Tom, kila mara alimwita mkewe na anapotaka kusema anaonekana kusahau. Mariam alihuzunika sana, alishindwa kuelewa mumewe alikuwa na jambo gani kubwa kiasi kile, na analisahau kila anapotaka kusema. Mariam akaamua kwenda kwa Dokta wake, ambaye alimwambia kwamba ile ilikuwa hali ya kawaida na kumbukumbu zake zitaendelea kurejea taratibu.
“Kweli Dokta?”
“Ndivyo ilivyo, inaonekana aliumia kidogo, sehemu ya ubongo wake, ndiyo maana anapoteza kumbukumbu, lakini zitaendelea kurudi polepole!”
“Kweli kabisa?”
“Nakuhakikishia!”
“Nashukuru sana Dokta!”
“Ok!”
**********
Ilikuwa ni Jumamosi usiku, tayari Tom na mkewe walikuwa wameshalala. Ulikuwa ni usiku wa saa saba na dakika zake. Mariam akashtuliwa na Tom ambaye alikuwa akimvuta kwa nguvu.
“Kuna nini?”
“Amka, amka haraka sana!”
“Nini saa hizi Tom?”
“Amka nimeshakumbuka, amka haraka kabla sijasahau!”
“Enhee sema!” Mariam akasema akiwa ameshawasha taa.
“Sikiliza kwa makini sana!”
“Nakusikiliza!”
“Nenda nje sasa hivi, pale kwenye ule mlimao, fukua chini kisha utoe kiroba utakachokiona!”
“Kina nini?”
“Kina madini, nilikuwa najitahidi sana kuvuta kumbukumbu, afadhali sasa nimekumbuka!”
“Unasema kweli Tom?”
“Huo ndiyo ukweli, nenda haraka kaangalie kama bado kipo!” Tom alisema haraka haraka huku akihema kwa kasi sana.
Mariam akatoka na jembe usiku huo bila kuogopa, kukuta kile kiroba kungemaanisha kuachana na maisha ya umasikini tena. Maisha yao yangekuwa mapya yasiyo na chembe ya dhiki. Alipofika nje, zoezi la kuchimba eneo la kuzunguka ule mlimao lilianza haraka sana.
Hakufika mbali sana, akaanza kuhisi kitu kigumu, aliendelea kidogo, akaona mfuko wa salufeti, akauvuta kwa nguvu, ukatoka ukiwa na madini ndani yake. Akatoka nao mbio hadi chumbani kwa mumewe. Hakusema kitu, walipoufungua walihisi kuchanganyikiwa! Kile kiroba kilikuwa kimejaa dhahabu tupu!
“Umasikini kwaheri....kwaheri umasikini...” Tom alipiga kelele akiwa haamini kilichotokea.
“Ndiyo maana ulikuwa unasahau kila wakati? Yaani unasahau utajiri?” Marim akamwambia Tom akicheka.
“Yaani acha tu, Mungu mkubwa mke wangu! Sasa andaa safari kabisa, kesho nenda Nairobi ukauze sehemu ya haya madini ili upate nauli ya kwenda Marekani ukaeze dhahabu yote huko!”
“Sawa!”
Usiku huo hawakuweza kulala, walikuwa wakipanga mipango mbalimbali juu ya maisha yao yajayo ambayo yangerejea kwenye utajiri kama kawaida.
“Mayasa alikuwa hafahamu kama pale uliweka hizi dhahabu?”
“Nilimuamini kwa kila kitu, lakini sijui ni kwanini sikumweleza kuhusu pale, ilikuwa ni siri yangu mwenyewe!”
“Hakuna mwingine zaidi ya Mungu mume wangu!”
“Na ni kweli ni Mungu mwenyewe ndiye aliyefanya yote haya!”
Walizungumza mambo mengi sana hatimaye wakalala, masaa manne baadaye walikuwa macho, Mariam akijiandaa kwa safari ya kwenda Nairobi. Saa kumi na mbili kamili, Mariam aliondoka na kwenda Uwanja wa Ndege, kwakuwa alishapanga mipango ya tiketi mapema, haikuwa kazi kubwa sana, alifika na kuondoka na ndege ya saa moja kamili.
Alifanikiwa kufanya mauzo vizuri kisha akarejea Tanzania kabla ya safari nyingine ya kwenda Los Angeles, Marekani. Huko akauza dhahabu yote na kurejea Tanzania akiwa na mabioni yake.
“Pole sana mke wangu!”
“Ahsante baby, sasa ni wakati wa kupanga mipango yetu, hatuna muda wa kupoteza zaidi!”
“Ni kweli!”
Ndicho kilichofanyika, halikuwa jambo gumu sana kwao, kikubwa kilichofanyika ilikuwa ni kununua majengo marefu (Towers) mengi jijini Dar es Salaam, Tanga, Arusha na Mwanza. Hiyo ndiyo ikawa biashara yao kubwa. Fedha zilizobakia wakahifadhi kwenye akaunti. Maisha yao sasa yakawa ya furaha, magazeti yakaanza kuandika habari zao kwa fujo!
“Lakini kuna jambo moja bado!” Mariam akamwambia Tom.
“Jambo gani?”
“Lazima usimame tena!”
“Unamaanisha nini?”
“Pesa itaongea, lazima tutafute tiba mpenzi wangu!”
“Hapana, sitaki!”
“Kwanini?”
“Nilishasema kabla, nitasimama siku Mungu mwenyewe akiamua!”
“Lakini Mungu alisema jisaidie nami nitakusaidia!”
“Mimi sitaki hivyo, nataka anisaidie yeye mwenyewe akitaka!”
“Haya na tusubiri!”
Wiki moja baadaye, Tom akamwagiza Mariam akamwite Mchungaji wa Kanisa wanaloabudu, alitaka kufanyiwa maombi maalumu nyumbani kwake. Zoezi hilo lilifanyika haraka sana, kila Jumapili yule Mchungaji alikuwa akifika nyumbani kwa akina Tom na kusali pamoja naye.
Wiki nne tu baadaye, wakiwa katikati ya maombi, Tom alishangaa akipata nguvu za ajabu sana, akasimama. Halikuwa jambo jepesi kuamini, hata Mchungaji mwenyewe hakuwa anaelewa jambo hilo kwasababu alikuwa amefumba macho.
“Yesu ahsante, nasema ahsante sana Mungu wangu...siamini kama kweli leo nimesimama tena!” Tom akapiga kelele huku akiimba.
Mchungaji akafumbua macho, hakuamini macho yake, akaendelea kumuomba Mungu bila kukoma. Mariam aliyekuwa nje, aliingia ndani baada ya kusikia kelele za Tom ndani. Naye akashangazwa sana na jambo hilo, akaungana na mumewe kumshukuru Mungu.
“Mungu wa ajabu jamani, leo ameamua kumuamsha mume wangu kitandani!”
“Amen!”
Ilikuwa ni furaha kubwa kuliko kawaida, Jumapili iliyofuata Tom alikwenda Kanisani, akapanda Madhabahuni kutoa sadaka ya shukrani kwa Mungu. Hapakuwa na machozi tena baada ya pale, wakaishi kwa amani na furaha katika maisha yao. Mapenzi ya kweli ndiyo yaliyotawala maisha yao.
“Nakushukuru kwa yote mke wangu, umenivumilia katika kila hali Mariam. Sitaki kukumbuka tena maisha yetu ya nyuma, lakini Mungu ni shahidi wa hilo kwamba wewe ni mwanamke sahihi wa maisha yangu, mkombozi wangu. Naamini uliandaliwa kwa ajili yangu, nakushukuru sana mke wangu, wewe ndiye wangu wa milele, nakuahidi sitakusaliti tena, tuyaache yaliyopita yaende zake, tuanze maisha mapya yaliyojaa mapenzi! Uliyonionyesha ni Zaidi ya Mapenzi, ahsante sana Mariam,” Tom alisema akiwa kifuani mwa Mariam, huku machozi yakimiminika kama maji machoni mwake.
“Nilipanga kukupa mapenzi ya kweli kama zawadi yangu kwako, wewe ndiye mwanaume wangu wa kweli, nakupenda sana!” Mariam akasema, naye akishindwa kuzuia hisia zake, akajikuta akimwaga machozi.
Haya yalifanyika nyumbani kwao Mbezi, muda mfupi baada ya kutoka Kanisani. Wakaendelea kukumbatiana zaidi, hawakuwa na kitu kingine vichwani mwao zaidi ya penzi la kweli.

Mwisho.
N:B Nawashukuru sana wasomaji wangu kwa kufuatilia hadithi hii kuanzia mwanzo hadi mwisho, naamini mmejifunza mambo mengi sana, kubwa zaidi likiwa ni umuhimu wa penzi la kweli! Nawashukuru kwa kuniunga mkono. Usikose katika hadithi mpya na nzuri kuliko kawaida.
Mungu wangu awabariki sana. Ahsateni. 

No comments

Powered by Blogger.