ad

ad

BEYOND LOVE- (ZAIDI YA MAPENZI) SEHEMU YA 20 MPAKA YA 39





KUPATA SIMULIZI TAMU ZAIDI JIUNGE NASI KATIKA PAGE YETU YA FACEBOOK
 LIKE HAPA >>>>>>>>www.facebook.com/2jiachie

Beyond Love -21

Tom au Papaa Bill kama alivyojulikana na wengi amekuwa tajiri mkubwa sana nchini Tanzania, pamoja na utajiri wake amejikuta akiwa mtu wa starehe kupita kiasi. Hakuona tabu kutumia fedha nyingi katika sterehe. Alidhamini Bendi nyingi za muziki jijini Dar es Salaam kwa kutumia fedha ili kulinda heshima yake!

Siku moja katika uzinduzi wa Albamu mpya ya Kigingi Music Band, ndani ya Ukumbi wa 56 Club, Kinondoni jijini Dar es Salaam, Tom alikutana na kitu ambacho  kiliuvuruga ubongo wake kwa muda! Macho yake yalikutana na msichana mrembo sana !

Huyu ni Mayasa, binti wa Mbagala jijini Dar es Salaam, anayejua kila aina ya utundu. Tom akaapa kuondoka naye, hakujua kama Mayasa naye alikuwa akimtega.

Je, nini kitatokea? Tom ataondoka na Mayasa? SONGA NAYO.....


Tom alibaki kimya kwa nukta kadhaa akizidi kumkodolea macho Mayasa ambaye kwa wakati huo vituko ilikuwa sawa na kiitikio kwenye nyimbo za Muziki wa Kizazi Kipya! Alihisi mapigo ya moyo wake kubadilika, alishasahau kwamba alikuwa jukwaani na alitakiwa kuwatambulisha wanamuziki wapya kutoka nchini Congo . Mayasa alishajua udhaifu wa Tom, alichokifanya ni kugeuka nyuma kisha akaanza kutembea kwa mwendo wa madoido akiacha sehemu kubwa ya miguu yake mizuri ikionekana kwa nyuma.

“Duh! Jamani hivi huyu mwanamke yupo katika dunia hii hii ya siku zote au ameshuka? Huyu lazima nitumie fedha zangu,” Papaa Bill akawaza kisha kwa taabu akajitahidi kuanza kuzungumza kwenye kipaza sauti.



KUPATA SIMULIZI TAMU ZAIDI JIUNGE NASI KATIKA PAGE YETU YA FACEBOOK
 LIKE HAPA >>>>>>>>www.facebook.com/2jiachie

“Samahanini sana kwa ukimya wa muda mfupi uliojitokeza, unajua nilikuwa nawaza ni kiasi gani tutakuwa na mashabiki wengi katika hii bendi yetu, wanamuziki niliokuja nao kutoka Congo ni wakali sana na bila shaka watafurahia mazingira ya Tanzania .

“Mimi sitakuwa na mengi sana ya kuzungumza, acha nimpishe Kiongozi wa Bendi, Abuu Sekidevi awakaribishe ili wapenzi wa bendi yetu wawaone,” Tom au Papaa Bill akasema kisha akakabidhi kipaza sauti kwa Mc wa siku hiyo.

Watu wakashangalia sana . Abuu ambaye alikuwa ndiye Kiongozi wa Bendi, akapewa kipaza sauti na kuwakaribisha wanamuziki wapya kutoka Congo .  Walishangiliwa sana .

“Kuna binti alikuwa amesimama pale,  mzuri-mzuri hivi, mweupe sana ni wa wapi?” Tom akamuuliza Jomba ambaye alikuwa mpambe wake.

“Yupi?”

“Alikuwa amesimama pale na wenzake!”

“Amevaa nguo za rangi gani?”

“Gauni jepesi!”

“Aaah! Nilimuona, vipi kwani?”

“Kanidatisha!”

“Kakudatisha?!”

“Ndiyo mkubwa, sasa ustaarabu unakuwaje?”

“Kwa mara ya kwanza nakuona ukianza kuzungumzia wanawake wa nje ya mkeo!”

“Ni kweli lakini leo nimezidiwa, lazima nikubali, sina ujanja!”

“Sasa vipi unamtaka?”

“Tena haraka sana !”

“Nipe dakika kumi tu!”

“Kweli?!”

“Nkuhakikishia!”

“Poa kaka, nakuaminia!”

“Ni kazi ndogo sana kwangu, msubiri sasa hivi anakuja kukaa na wewe meza moja, hayo mambo mengine nakuachia wewe!”

“Mambo gani tena?”

“Kumuimbisha!!”

“Sitazungumza kitu, fedha itanisaidia!”

“Nakuamini kaka!”

Jomba akaondoka akiwa anatembea kwa mbwebwe sana , alikuwa na uhakika wa kurudi na Mayasa, siyo kwa sababu anajiamini, bali alikuwa anamfahamu vizuri sana Mayasa. Siku zote msichana huyo alijua fedha na siyo mapenzi ya kweli.

Hakutembea sana , akakutana na Mayasa akiwa na kampani yake, akasimama mbele yao . Akatabasamu. Mayasa hakupata shida sana kujua kuwa Jomba alikuwa mpambe wa Papaa Bill. Alichokifanya na yeye ni kutabasamu.

“Mambo vipi warembo?” Jomba akasalimia.

“Poaaaaa....” Wote wakaitikia.

“Naona mpo!”

“ Kama unavyotuona!”

“Samahani mrembo, naweza kuzungumza na wewe kidogo?” Jomba akamwambia Mayasa.

“Kuna nini tena?”

“Nisikilize kwanza, mbona unakuwa na wasiwasi kiasi hicho?”

“Siyo wasiwasi, ni vyema nikajua hata dondoo kwanza!”

“Ni ujumbe wako!”

“Poa!” Mayasa akakubali. Wakaenda pembeni kuzungumza.

“Unamfahamu Papaa Bill?”

“Namsikia, kwani vipi?”

“Amesema nikuite!”

“Anataka nini?”

“Mtoto wa kike vipi? Mbona unakuwa na mashaka, twende umsikilize anasemaje?” Jomba akamwambia Mayasa ambaye hakubisha zaidi. Wakaongozana hadi kwenye meza aliyokuwa amekaa Papaa Bill.

Tom alipomuona alichanganyikiwa, kwanza hakuamini kabisa kwamba Jomba alifanikiwa kumleta Mayasa. Msichana huyo akakaa kwenye kiti akitabasamu kwa manjonjo ya kimahaba.

KUPATA SIMULIZI TAMU ZAIDI JIUNGE NASI KATIKA PAGE YETU YA FACEBOOK
 LIKE HAPA >>>>>>>>www.facebook.com/2jiachie
“Karibu mrembo!”

“Athante!” Mayasa akaitikia akijitahidi kuubana ulimi wake kwa mapozi ya kimahaba.

“Unatumia kinywaji gani?”

“Wine!”

“Sawa mwite Mhudumu akuletee!”

Muda mfupi baadaye Muhudumu alifika ambapo alimletea Mayasa wine aliyokuwa akiihitaji. Wakaanza kunywa pamoja. Papaa Bill alijikuta akishindwa kuzungumza kitu. Baadaye Mayasa akamwomba Papaa Bill, awaite marafiki zake ili wajumuike pamoja.

“Wako wapi?”

“Kulee!” Mayasa akasema akisonza kidole chake kuonyesha mahali marafiki zake walipo.

“Nenda kawaite hakuna tabu!”

“Hapana!” Jomba akadakia.

“Kwanini?” Papaa Bill akauliza akiwa na hofu sana .

“Acha niende nikiwalete mwenyewe. Si wale niliokukuta nao?”

“Ndiyo!”

“Acha nikawalete!”

“Poa!” Wakakubaliana.

Jomba akaondoka na kwenda moja kwa moja kuwaita wale marafiki zake na Mayasa. Muda mfupi baadaye, wakafika pale na kuketi pamoja, wakaagiza vinywaji na kunywa pamoja.

“Unajua muda wote huo tumekaa pamoja hapa, lakini hatujafahamiana!” Tom akasema akitabsamu.

“Lakini sisi tunakufahamu!”

“Mimi?”

“Ndiyo!”

“Naitwa nani?”

“Papaa Bill a.k.a  Nyamihela!” Mayasa akasema.

“Hamjakosea, lakini mimi siwafahamu!”

“Kabla hatujakuambia majina yetu, huyu rafiki yako anaitwa nani?”

“Labda mwenyewe aseme!” Tom akajibu.

“Mimi ni Jomba warembo!”

“Mjomba?!” Mayasa akauliza akitabasamu.

Siyo Mjomba, nimesema Jomba!”

“Ooh! Hapo sasa nimekupata...miye naitwa Mayasa, hawa marafiki zangu ni Angela na Monalisa!”

“Vizuri sana , sasa tunaweza kuendelea kuburika hadi tutakapotosheka!” Tom au Papaa Bill alisema akitabsamu.

Kama Tom alivyosema, kilichofuata baada ya pale ilikuwa ni kula na kunywa kwa kasi ya ajabu sana . Muda ukazidi kwenda, wakiendelea kunywa na kula, hadi ilipofika usiku wa saa tisa na nusu. Wakati huo Tom alikuwa ameshachangamka! Hakuwa na aibu aliyokuwa nayo awali.

“Mayasa....” Tom akaita.

“Abee!” Sauti ya Mayasa ilisikika, ilimchanganya sana Tom ambaye hakumini kama alikuwa akiisikiliza sauti ya Mayasa.

Kwa hakika mapenzi yalishauteka moyo wake, alishindwa kuelewa ni kwanini alijikuta akimpenda Mayasa kiasi kile. Tom akazama katikati ya dimbwi la mawazo, akasahau kwamba alikuwa akizungumza na Mayasa.

“Papaa nakusikiliza...” Mayasa akamzindua Tom katikati ya mawazo.

“Sorry kuna kitu kilikuwa kinanichanganya kidogo!” Papaa Bill akasema.

“Ni nini?”

“Mambo ya biashara zangu!”

“Pole, lakini watu kama nyie ni lazima muwe hivyo!”

“Ni kweli kabisa!”

“Enheee....nakusikiliza!” Mayasa alionekana kuwa na hamu sana na alichokuwa akitaka kuzungumza Tom.

“Hebu tusogee pembeni kidogo!”

“Sawa!” Wakasogea pembeni kwenye mwanga hafifu.

“Sikiliza Mayasa, sina sababu ya kuzungumza maneno mengi, mimi nina pesa na nimezunguka kila mahali, lakini sijawahi kukutana na mwanamke mzuri kama wewe, amini kwamba nimetokea kukupenda ghafla sana . Tafadhali naomba unipe moyo wako, nakupenda sana !” Tom akasema kwa hisia kali sana za mapenzi.

“Papaa unasema kweli?” Mayasa akasema akimtizama Tom kwa macho yaliyojaa matamanio ya mahaba.

“Niamini!”

“Papaa, unajua nyie wenye pesa, hamuwezi kuvumilia kuwa na mwanamke mmoja, akitokea mwanamke mwingine mzuri zaidi yangu, unaniacha na kwenda naye.” Mayasa akasema.

“Siyo Papaa Bill, mimi ni wa tofauti kabisa na matajiri wengine unaowajua!”

“Kweli unanihakikishia sitaumia?”

“Nakuhakikishia!”

“Sawa!” Tom akamsogelea Mayasa wakakumbatiana.

Kitu cha ajabu ni kwamba, Mayasa alionekana kama alikuwa na uhusiano na Tom kwa muda mrefu sana . Haraka aliusogeza ulimi wake ndani ya kinywa cha Tom, wakaanza kubadilishana mate!

“Bill nakupenda sana !”

“Hata mimi pia, sasa baby sioni kama kuna sababu ya kuendelea kuwepo hapa, twende zetu!” Tom akasema.

“Kwenda wapi?”

“Kupumzika!”

“Ni mapema sana Papaa Bill!”

“Hapana Mayasa, leo ni siku yetu, naomba tutumie usiku huu kufungua ukurasa mpya wa mapenzi!” Tom akazidi kumshawishi Mayasa.

“Sawa!” Mayasa akamjibu.

“Ahsante sana dear!”

Wakashikana mikono na kwenda walipokuwa wamekaa rafiki zake Mayasa na Jomba, wakawaaga.

“Jomba tutaonana kesho, mimi naondoka na mrembo wangu, stareheni salama!” Tom akasema akitoa noti ishirini za elfu kumi-kumi.

“Hizi zitawasaidia kwa ajili ya vinywaji na nauli!”

“Poa kaka!” Jomba akashukuru.

Tom akamshika mkono Mayasa na kwenda zao hadi alipoegesha gari lake, wakaingia.  Tom akawasha gari, wakaondoka maeneo ya Kinondoni. Walikuwa wanaelekea Ubungo katika moja ya hoteli nzuri ya kifahari. Tom alipanga kumsaliti mkewe Mariam kwa mara ya kwanza. Alilemewa na mapenzi mazito kwa Mayasa.

“Nitahakikisha natumia kila njia awe wangu wa moja kwa moja, hapo ndipo nitakapopata nafasi ya kuchuma ninavyotaka. Nani ampende huyu mjinga? Shida yangu ni mali tu, na wala siyo mapenzi!” Mayasa aliwaza wakiwa njiani kuelekea hotelini.
Je, nini kitatokea? Mayasa atafanikiwa kumteka Tom na kuchuma mali zake kama anavyotamani? Usikose
Beyond Love- 22
Hata hivyo, Mayasa anajisemea moyoni mwake kwamba, hana mapenzi na Tom na anajihakikishia kutumia kila njia ili aweze kuchuma sehemu ya utajiri wake. Je, atafanikiwa? Nini nkitatokea? SONGA NAYO...

Tom haamini kama msichana aliyekaa pembeni yake ndani ya gari lake alikuwa Mayasa. Hata yeye alijishangaa, kwani hakuwahi kupenda kama alivyompenda Mayasa. Msichana huyo alimwingia akilini mwake kwa kasi ambayo hata yeye mwenyewe alishindwa kupata majibu kila alipojiuliza.
“Yaani sijawahi kupenda katika maisha yangu kama ninavyompenda Mayasa, huyu mwanamke ameniingia hadi mimi nashangaa, sijui kuna nini bwana? Lakini hata hvyo ni mzuri sana, naamini uzuri wake ndiyo unanizuzua.”  Tom akawaza wakati akiwa anashuka katika bonde lililopo eneo la Mkwajuni, Barabara ya Kawawa, akiifuata barabara inayoelekea Magomeni.
“Papaa...” Mayasa akaita.
“Vipi baby?”
“Naona kama una mawazo, kuna nini?”
“Hapana, hakuna tatizo, nipo sawa kabisa!”
“Nahisi kuna kitu unajaribu kunificha!”
“Hapana...”
“Sawa kama hakuna kitu lakini nahisi kama kuna kitu kinakuchanganya akilini mwako, au unamuwaza mkeo?”
“Nimuwaze mke wangu wakati nipo na wewe?”
“Kwani haiwezekani?”
“Nitakuwa mwanaume wa ajabu sana.”
“Kwanini unasema hivyo Papaa Bill?”
“Kama nilikuwa naona ananifaa, ananitosha, ananiridhisha, ananivutia kwanini nihangaike kukusumbua? Lakini kwasababu kuna mapungufu katika maeneo kadhaa ndiyo maana nimeona wewe unaweza kusaidia kuziba hayo mapengo!”
“Kwahiyo mimi nipo na wewe kwa sababu ya kuziba mapengo tu?!”
“Hapana...amini kwamba nimekupenda lakini wakati huo huo, tambua kwamba nina mke. Wewe utakuwa na nafasi yako kwangu na yeye atakuwa na nafasi yake, pia ni vizuri kila mmoja akaheshimu nafasi ya mwenzake....hasa wewe...”  Tom alimwambia Mayasa akionyesha hana masihara kabisa na kilichokuwa kikitoka kinywani mwake.
Pamoja na usaliti ambao alikuwa anataka kumfanyia mkewe Mariam, lakini moyo wake ulikuwa na maumivu makali sana. Hakutaka Mariam wake adharauliwe kwa sababu ya mwanamke wa nje, tena aliyekutana naye Club.
Tom akaendesha gari kwa kasi alipofika Morocco, kwenye makutano ya Barabara ya Uzuri na Kawawa ambayo alikuwa anaitumia, alikata kulia na kuifuata Barabara ya Uzuri hadi Sinza Kijiweni ambapo alikata kushoto kufuata Barabara ya Shekilango.
Kasi ya gari ilikuwa ni ile ile, alibadilisha gia kila baada ya muda, hakuona haja ya kupunguza mwendo kwenye matuta ya barabarani, alikuwa akipita kwa mwendo ule ule. Alipofika kwenye mataa ya Shekilango, akakata kulia akifuata Barabara ya Morogoro ambapo aliendesha gari hadi kwenye mataa ya makutano ya Barabara za Morogoro, Sam Nujoma na Mandela, hapo alikata kushoto akiifuata Barabara ya Mandela.
Hakufika mbali sana, kabla ya kufika River Side, akaingiza gari ndani ya geti jekundu, katika hoteli moja nzuri sana. Moja kwa moja wakaenda hadi Mapokezi wakipitia mlango maalum, akalipia chumba na kiupandishwa ghorofa ya nne kwenye chumba chake.
“Karibuni sana.” Mhudumu akasema.
“Tunashukuru lakini zingatia maadili ya kazi yako.” Tom akamwambia.
“Kwanini unasema hivyo bosi?”
“Nafikiri unanifahamu vizuri!”
“ Ndiyo....”
“Ni nani?”
“Papaa Bill!”
“Sasa sitaki mtu yeyote ajue kuwa nimelala hapa, nenda na hilo kichwani mwako!”
“Naheshimu na kuzingatia sana maadili ya kazi yangu!”
“Usiku mwema!”
“Nawe pia.”
Tom aitumia muda mwingi sana kumwangalia Mayasa ambaye alikuwa na sura na umbo la kuvutia sana. Msichana hoyo, akipita sehemu yoyote ambapo kuna mwanaume asiye na matatizo yoyote katika via vyake vya uzazi basi lazima asisimke.
“Hebu simama.” Tom akamwambia Mayasa.
Mayasa akasimama.
“Zunguka nyuma!” Tom akamwambia huku akitabasamu na kutingisha kichwa. Mayasa akafanya hivyo.
“Sasa simama upande upande!”
“Kwani vipi?”
“Nataka kukuona vizuri!”
“Kwani hukuniona?”
“Ndiyo maana nimesema vizuri.”
“Sawa bwana!” Mayasa akageuka, safari hii alikuwa akigeuka kwa mapozi, huku akipandisha gauni lake na kuacha miguu yake wazi, ambayo ilianza kupandisha presha yake ya  mapenzi.
“Hakika wewe ni mwanamke mrembo sana, sema chochote unachotaka nikupe ili kuonyesha mapenzi yangu kwako!” Tom akamwambia Mayasa akitabasamu.
Mayasa akamfuata mahali Tom alipokuwa amekaa, akakaa na kupandisha mguu wake mmoja juu ya miguu ya Tom. Tom akahisi shoti ya umeme ikipita mwilini mwake. Mayasa alikuwa mwanamke aliyemchanganya sana ubongo wake.
Akasogeza kinywa chake karibu kabisa na sikio la kuume la Tom, kisha akaanza kuzungumza kama anamnong’oneza; “Ni kweli unanipenda Papaa?”
“Kwanini huniamini?”
“Siyo kama sikuamini Papaa!”
“Sasa kumbe nini?”
“Kama nilivyokuambia kule Club, wewe ni mwanaume tajiri na maarufu, kila mtu anakufahamu, nitawezaje kuwa na wewe kama sitanyang’anywa?”
“Mimi ndiyo mwamuzi, na ni mimi ndiye niliyekupenda. Ndiyo maana nimekuwambia chagu chochote utakacho nikupe ili kuonyesha penzi langu la kweli kwako!”
“Sawa, naona itakuwa vizuri sana kama ukinihamisha nyumbani!”
“Una maana gani?”
“Naishi na wazazi wangu na umri wote huu ni aibu sana, kwanza nina wadogo zangu wawili wa kike na wote wanaishi na mabwana zao, nimebaki mimi tu, nyumbani kwahiyo naona itakuwa vyema kama utanipangishia chumba!”
“Chumba au nyumba?”
“Utakavyoona mwenyewe Bill”
“Acha nikutafutie nyumba nzima, kuhusu samani za ndani niachie mimi, kila kitu utakikuta ndani ya nyumba!”
“Nitafurahi sana Papaa Bill!”
“Anza kufurahi kuanzia sasa!”
“Sawa mpenzi wangu.” Mayasa akasema akicheka kwa sauti kubwa sana.
“Nilitaka kusahau, unataka maeneo gani?”
“Utakayoona yanafaa!”
“Chagua mwenyewe!”
“Kinondoni au Mwananyamala.”
“Basi nipe muda mfupi sana, haitazidi mwezi mmoja!”
“Sawa baby!” Baada ya hapo, lugha ya Kiswahili haikutumika tena.
Hata hivyo lugha iliyozungumzwa badala ya Kiswahili haikuwa Kiingereza, Kifaransa wala lugha nyingine yoyote ambayo hutumika kama njia ya mawasiliano duniani. Walikuwa wakizungumza lugha ya mapenzi!
*******
 Pamoja na kwamba Tom alikuwa anapenda sana starehe, haikuwahi kutokea hata siku moja, akaacha kurudi nyumbani. Siku hiyo hadi kufikia saa tisa na dakika zake za usiku, Mariam alikuwa hajamtia machoni mwake mumewe.
Siku zote alikuwa mtu wa starehe sana lakini alipompigia simu alipopokea na kumweleza mahali alipo na wakati mwingine hadi muda aliokuwa akitarajia kurudi nyumbani. Siku hiyo ilikuwa tofauti sana, simu ya Tom ilikuwa haipatikani ka bisa!
“Masikini mume wangu, sijui atakuwa amekumbwa na balaa gani tena, siyo kawaida yake kuwa hajarudi nyumbani hadi muda huu, mbaya zaidi hata simu yake haipatikani,” Mariam akawaza akiwa amejilaza kwenye sofa kubwa sebuleni akiwa hoi kwa uchovu akimsubiria mume wake bila mafanikio.
Mapenzi yao sasa yalibadilika, hayakuwa sawa na ilivyokuwa awali, mara nyingi Mariam aliishia kulala mwenyewe nyumbani akiwa hana la kufanya. Hata alipotaka kutafuta kazi, Tom alikataa akidai kuwa uwezo wa fedha alionao, haumruhusu yeye kufanya kazi, kwani ana uwezo wa kumuachia fedha za matumizi kila siku bila matatizo.
Hakupata usingizi hadi asubuhi akiwa yupo sebuleni akimsubiria mumewe, hadi kufikia saa mbili za asubuhi, Tom alikuwa hajafika nyumbani, mawazo yakazidi kumjaa akilini mwake.
“Lazima nifanye jambo la ziada hapa, natakiwa kwenda kutoa taarifa Polisi kwanza!” Mariam anawaza kisha akaamua kwenda kubadilisha nguo haraka na kutoka nje.
Akiwa ndiyo kwanza, amewasha gari, anasikia honi ikipigwa mlangoni. Mlinzi anafungua mlango, gari la Tom linaingia na kuegeshwa pembeni. Mariam haamini macho yake. Alitegemea kumuona Tom akiwa na huzuni kutokana na matatizo aliyohisi kuwa  nayo, lakini alishuka akiwa na tabasamu pana.
Mariam akashuka garini, akiwa ameyatuliza macho yake kwa Tom ambaye hakuonekana kuwa na chembe ya wasiwasi. Akaingia ndani na kumuacha Mariam akiwa amesimama nje, ni jambo ambalo lilichukua muda mrefu sana kuaminika akilini mwa Mariam.
Mariam akamfuata Tom ndani, macho yake yakianza kupatwa na unyevunyevu na kubadilika rangi na kuwa mekundu. Akamkuta Tom akiwa amejilaza kwenye sofa kubwa.
“Vipi Tom mume wangu?”
“Salama, za tangu jana?”
“Mimi ndiyo natakiwa kukuuliza wewe!”
“Ooooh! Hivyooeh....mimi mzima, sina matatizo!”
“Lakini ulilala wapi?!”
“Kitandani!”
“Hayo ndiyo majibu gani Tom?”
“Nimekwambia nimelala kitandani!”
“Eti?”
“Hujasikia au hujapenda? Halafu we’ mwanamke...naona sasa unataka kunipanda kichwani, tafadhali naomba uniache, usipende kufuatilia sana mambo yangu!” Tom akasema kwa sauti kubwa iliyoonyesha kujaa hasira.
Mariam hakuwa na kitu kingine cha kuzungumza zaidi ya kwenda kujifungia chumbani, alichokifanya huko ilikuwa ni kulia akiamini alikuwa anapunguza hasira zake.
Tom ameshaanza kubadilika, sasa ameanza tabia ya kulala nje na anarudi nyumbani bila woga kwa mkewe.




Beyond Love- 23

Upande wa pili, Mariam anakuwa na wasiwasi sana kutokana na mume wake kutorejea nyumbani, usiku mzima anaweweseka sebuleni akilia. Asubuhi Tom anarejea lakini alipoulizwa kwanini hakurejea nyumbani alitoa majibu ya hovyo.
Mariam hakuwa na kitu kingine cha kufanya zaidi ya kurudi chumbani na kuanza kulia. Je, nini kitatokea? SONGA NAYO...

Machozi ya Mariam yalikuwa na thamani kubwa, thamani hiyo ilitokana na kipimo cha mapenzi kilichokuwa ndani yake! Alimpenda sana Tom wake, lakini badiliko la tabia yake lilimkosesha raha moyoni mwake.
Mariam hakuwa na amani, alishindwa kuelewa ni shetani gani aliyemwingia mumewe na kumbadilisha kiasi kile. Hadi wakati huo hakuwa na uhakika kama aliyemjibu majibu machafu kiasi kile alikuwa Tom wake aliyemfahamu siku zote.
“Sasa amezidi! Amefikia hatua ya kulala nje, Tom kwanini unanitesa lakini?” Mariam alisema maneno hayo huku akilia kwa uchungu, chumbani alipokuwa amekimbilia.
Hasira zilipomzidi Mariam, alijikuta akizidisha kilio, jambo lililomuudhi sana Tom ambaye haraka alitoka na kwenda chumbani kumfuata kwa lengo la kumpa kipigo.
“Pumbaaaafu....hapa siyo Klinik, umeelewa? Naomba unyamaze haraka sana!”
“Sinyamazi.”
“Unasema?”
“Sinyamazi Tom, niache nilie hasira zangu ziishe. Unanitesa sana Tom lakini sasa umeona ili kunidhibitishia kwamba ni kweli hunipendi, umeamua kulala nje kabisa, sasa nina thamani gani kwako mimi?!”
“Hivi wewe mwanamke, nimekuoa au umenioa?”
“Tumeoana!” Mariam akajibu kwa kujiamini huku akifuta machozi machoni mwake.
Hakujua ni kiasi gani lilikuwa jibu baya kwa Tom. Alimwangalia kwa jicho la hasira kisha akamsogelea polepole huku akitetemeka kwa hasira zilizoonekana dhahiri.
“Hivi, hii jeuri unaipata wapi wewe mwanamke? Nakuuliza wewe...hii jeuri unaipata wapi?”
“Tom mpenzi wangu, kukuliza ulilala wapi imekuwa jeuri?”
“Hata kama, mimi ni mwanaume na nina mambo mengi, na kama nilikuwa nahangaika na biashara zangu, utajuaje?”
“Ni lini uliwahi kulala nje Tom, kama kuchelewa ulikuwa unanipa taarifa, iweje kwenye kulala nje ushindwe kuniambia?”
“Kwahiyo kila ninachokifanya lazima nikuambie siyo?”
“Mimi kama mkeo, natakiwa kufahamu hayo yote, kumbuka uliahidi nini siku ya ndoa, kumbuka Tom mume wangu!”
“Hata kama, lakini nimekuambia kuwa nina kazi nyingi na ndizo nilizokuwa nahangaika nazo, nilitegemea ungenipokea na kunipa pole, lakini mwenzangu ndiyo kwanza unaanza ugomvi!”
“Lakini simu zilikuwa hazipatikani!”
“Ziliisha chaji!”
“Hapakuwa na njia nyingine ya kunijulisha Tom!”
“Lakini mbona umeshikilia sana hilo jambo? Kitu kidogo unataka kiwe kikubwa?”
“Natetea uhai wangu Tom, hivi unafikiri kama ukizoa maradhi huko na kuyaleta hapa nyumbani itakuwaje kama siyo kuniua?”
“Unasemaje wewe mwanamke? Yaani mimi ni ukimwi? Sasa naona upole wangu unaniponza, unataka kunipanda kichwani sasa!” Tom akasema hayo huku akivua mkanda wake wa suruali.
Kilichofuata baada ya hapo ilikuwa ni kipigo cha nguvu, ambapo pamoja na Marim kuomba msamaha Tom aliendelea kumpiga!
“Nisamehe mume wangu utaniua, naomba msamaha, tafadhali Tom...nakufaaaaa...” Mariam alipiga kelele lakini Tom aliendelea kumpiga mpaka hamu yake ilipoisha akaamua kuachana naye.
******
BAADA YA MIEZI SITA
Mapenzi ya Tom na Mayasa yalizidi kushamiri huku mateso, manyanyaso na matusi kwa Mariam yakiwa ni vitu vya kawaida kila kukicha! Tom alibadilika sana, akawa hasikii wala haambiwi kwa Mayasa.
Kama ni mapenzi basi yalitakiwa kutafutiwa jina lingine maana katika penzi la wawili hao yalikuwa makali zaidi ya neno lenyewe! Walikuwa kama kumbikumbi, kila mahali walikuwa pamoja.
Tom alishindwa kuelewa kwanini alijikuta akizidisha mapenzi kwa yule mwanamke kwa kasi ambayo hata yeye mwenyewe hakujua ilipotokea. Alimuona Mariam kama kinyaa mbele yake, hakuwa na muda wa kukaa na Mariam hata kujadili kuhusu mambo mbalimbali ya familia yao.
Muda mwingi alikuwa na Mayasa, Tom hakujua siri ya kumpenda zaidi Mayasa, kulikuwa na kitu kilichosababisha mapenzi kati yao kuongezeka! Mayasa alikwenda kwa Mtalaamu wa Kienyeji ambaye alimuwekea mambo yote sawa! Tom alikuwa mkononi mwa Mayasa na hakuwa na uwezo wa kufurukuta kwa namna yoyote ile! Alikuwa kama bendera ambayo siku zote huwa inafuata upepo.
Siku moja Tom akiwa na Mayasa mjini, Tom alijikuta akifanya jambo la hatari sana. Baada ya kupungukiwa na fedha, waliamua kwenda kwenye mashine ya kutolea fedha ya CRDB Tawi la Azikiwe na kumtuma Mayasa aende akachukue pesa.
“Sasa nitawezaje wakati sifahamu namba zako za siri?”
“Hilo tu, nitakupa!”
“Lakini ni vizuri ukaenda mwenyewe, mambo ya pesa hasa akaunti ni siri ya mhusika mpenzi wangu! Hebu shuka kwenye gari uende ukachukue pesa, acha uvivu wako!” Mayasa alimwambia Tom lakini alikuwa anamtania kwani alikuwa anajua kwamba dawa ndizo zilizokuwa zikifanya kazi.
“Wewe ni mpenzi wangu siyo?” Tom akauliza.
“Hata hili gari linajua hivyo.”
“Umejibu vizuri sana, sasa sina haki ya kukutuma?”
“Unayo!”
“Namba za siri za hiyo kadi ni 1343, nenda katoe laki tano haraka!”
“Sawa baba, isiwe ugomvi!” Mayasa akasema kisha akatoka kwa mwendo wa maringo kuelekea kwenye mashine.
Tom alibaki hoi akikodolea macho makalio ya Mayasa, yaliyokuwa yanavutia sana. Watu waliomwona akipita, walishindwa kuzuia hisia zao na kujikuta wakimtimzama kwa macho ya matamanio.
Ilibaki kidogo Mayasa azimie baada ya kuona fedha zilizokuwa kwenye akaunti ya Tom, pamoja na kwamba alikuwa anafahamu Tom alikuwa na fedha nyingi sana, lakini hakuwahi kufikiria kwamba akanuti yake ingekuwa na fedha nyingi kile.
Akaunti ya Tom ilikuwa na zaidi ya bilioni thelathini, hata hivyo alikuwa na akaunti nyingine katika Benki za NBC na Barclays ukiachilia mbali akaunti nyingine zilizokuwa nje ya nchi. Mayasa akachukua kiasi kile cha fedha na kurudi kwenye gari.
“Umefanikiwa?”
“Ndiyo!”
“Twende!” Tom akawasha gari na kuondoka na Mayasa, safari yao iliishia katika moja ya Hoteli za sasa iliyokuwa ufukweni mwa Bahari ya Hindi.
Wakiwa huko Mayasa alikumbushia ahadi ya kupangishiwa nyumba, aliyoahidiwa na Tom.
“Haraka ya nini? Subiri kwanza!”
“Lakini dear nitaendelea kukaa Mbagala hadi lini? Sina hadhi ya kukaa kule tena!”
“Ni kweli lakini nimekuambia subiri mpenzi wangu, nakuandalia kitu cha maana na muda mfupi baadaye utafurahia!”
“Tutaona!” Walikula raha huko usiku mzima.
******
Wiki mbili baadaye Tom alimpigia simu Mayasa na kutaka wakutane kwa ajili ya kumpatia zawadi nzuri sana aliyoiandaa kwa ajili yake.
“Kwani we’ uko wapi?” Mayasa akamwuliza.
“Uwanja wa nyumbani 56 Club!”
“Mimi nipo Mwananyama, acha nichukue taxi mara moja nakuja hapo sasa hivi!”
“Nakusubiri mpenzi wangu!” Muda mfupi baadaye Mayasa akafika.
Bila kupoteza muda Tom akamwambia Mayasa aingie kwenye gari. Akaingia. Wakaangaliana kwa pamoja na kuachia matabasamu mapana sana usoni mwao.
“Leo ni siku ya furaha katika penzi letu, nataka kukuonyesha kwamba nakupenda, nakuthamini, nakuheshimu na nataka kuwa na wewe katika siku zote za maisha yangu!”
“Mbona unanitisha mpenzi, kuna nini?”
“Usijali, fumba macho yako, halafu nitakufunga kitambaa cheusi kisha nitakufungua baada ya kufika mahali zawadi ilipo, sawa?”
“Hakuna shida mpenzi wangu!” Tom akatoa kitambaa na kumfunga Mayasa usoni, kisha akaondoa gari.
Safari yao iliishia Kinondoni B, karibu kabisa na Shule ya Sekondari Biafra ambapo kulikuwa na nyumba nzuri ya kifahari iliyokuwa na kila kitu ndani! Nje ya nyumba hiyo, kulikuwa kumeegeshwa gari mpya aina ya Toyota Rav 4 la rangi la Buluu, ukoka ukiwa umechukua nafasi kubwa pamoja na bustani nzuri iliyokuwa pembeni ya bwawa la kuogelea.
Tom alipoegesha gari lake, akafungua mlango na kumtaka Mayasa atoke. Baada ya hapo akamfungua kitambaa usoni mwake na kumpa funguo mbili, moja wa gari na mwingine wa nyumba.
“Huu ni funguo wa nyumba yako, na huu ni wa gari lako, lile pale. Kuanzia leo, hii ni nyumba yako, ina kila kitu ndani, furahia maisha mpenzi wangu!” Tom akasema akitabasamu.
Mayasa hakuweza kuelewa kama yaliyokuwa yakitokea yalikuwa ni ndoto au tukio la kweli. Akamwangalia Tom huku akitetemeka kwa furaha, midomo yake ikaanza kutingishika!
“Ni nyumba ya kupanga au...” Tom hakumuacha Mayasa amalizie sentesi hiyo, akamkatisha.
“Nimeinunua na hati yake hii hapa, nimekuwa nikifanya ukarabati na kuifanya ya kisasa kwa miezi sita sasa, hii ni nyumba yako....mali yako!” Tom akamwambia Mayasa akitabasamu.
Tayari macho ya Mayasa yalishajaa machozi, akamsogelea Tom na kumkumbatia kwa nguvu, mabusu motomoto mashavuni mwa Tom yalitawala.
“Nimeamini unanipenda Tom!”
“Tena sana, kuliko hata Mariam!”
“Kweli?”
“Nakuhakikishia!”
“Leo ni siku ya furaha ya penzi letu, ili niamini vizuri kama kweli unanipenda, twende tukalale nyumbani kwako, hapo utanifanya nione unanithamini na kunipenda na humpendi mkeo!” Mayasa akasema akiwa ameyatuliza macho yake usoni mwa Tom.
Maneno yale yalizunguka kwenye ubongo wa Tom zaidi ya mara kumi bila kupata jibu la kumpa Mayasa.
“Tom, nahitaji jibu lako mpenzi wangu!”
Tom akafungua kichwa chake, macho yake yakitizama chini huku akionekana kuwa na mawazo mengi sana yaliyomkumba ghafla. Kila alipotaka kuzungumza alionekana kusita.  


Beyond Love – 24

Katika hali ya kushangaza sana, Mayasa anamwambia Tom akubali kwenda kulala nyumbani kwake, pamoja na kwamba alikuwa akifahamu kwamba ana mke. Linakuwa jambo zito sana kwa Tom, lakini Mayasa anaendelea kumng’ang’aniza.
Je, atakubali? Nini kitatokea? Ssa SONGA NAYO...

Kama ni mtihani, huu ulikuwa mkubwa kuliko yote kwa Tom! Pamoja na kumpenda sana Mayasa, lakini kitendo cha kumwambia akalale naye nyumbani kwake kilikuwa cha udhalilishaji mkubwa kwa mkewe wa ndoa Mariam.
Ni kweli Tom alikuwa katika mtihani mzito sana na hakuweza kufungua mdomo wake kusema chochote, hadi dakika mbili baadaye, Mayasa alimtingisha kwa nguvu na Tom kurejewa na kumbukumbu zake vizuri. Ni kama hakuwepo mahali pale.
“Mbona umenyamaza?”
“Unasema?”
“Mbona upo kimya, nahitaji jibu lako!”
“Najua Mayasa, lakini fahamu kwamba umenipa mtihani mkubwa sana!”
“Mtihani mkubwa kivipi?”
“Mayasa!” Tom akaita.
“Nakusikia mpenzi wangu!”
“Huoni kuwa huo ni mtihani mkubwa sana kwangu?”
“Labda nikuulize swali kabla ya kujibu lako!”
“Endelea...”
“Unanipenda?”
“Mayasa mpenzi wangu, hata wewe unaweza kunisaidia kujibu!”
“Pengine ninalo jibu, lakini yawezekana jibu nililonalo mimi ni tofauti na fikra zako!”
“Hapana...unavyowaza ndivyo nilivyo!”
“Kwahiyo sasa nikuambie ninavyowaza jibu yako?”
“Ndiyo!”
“Utaniamini?”
“Kwanini nishindwe?”
“Tom hunipendi, hunipen...” Mayasa akasema akilia.
Tom hakutaka kuyaona machozi ya Mayasa, haraka akaanza kumfuta machozi yake na kumbembeleza anyamaze.
“Niache nilie Tom, ni haki yangu!”
“Haki ya kuli? Kivipi?”
“Napenda nisipopendwa!”
“Usiseme hivyo mpenzi wangu, mimi nakupenda sana!”
“Kama unanipenda kwanini unanifanyia hivi?”
“Kumbe yote haya niliyoyafanya huoni thamani yake?”
“Sina maana hiyo, nataka udhihirishe penzi lako kwangu mbele ya mkeo, nataka mkeo afahamu kwamba yupo unayempenda zaidi, ambaye ni mimi. Kwanini unanitesa kiasi hicho Tom?” Mayasa alikuwa akizungumza kwa hisia sana huku machozi yakimtoka machoni mwake.
Tom hakujua kilichokuwa akilini mwa Mayasa, alifanya yote hayo kwa sababu alikuwa akihitaji Mariam afukuzwe ili aweze kuzitawala vizuri mali za Tom, hiyo ndiyo iliyokuwa ndoto yake siku zote. Kuchota mali za Tom ingewezekana kama Mariam angeondoka ndani ya nyumba ya Tom na hatua ya kwanza kwake ilikuwa ni kwenda nyumbani kwa Tom na kulala pale.
Aliamini kwa kufanya kungemchukiza Mariam na kuamua kundoka zake kwenda kwao. Wazo lake lilikuwa zuri sana ingawa hakujua ni kiasi gani lilikuwa sumu kwa mwenzake.
Ukimya wa mrefu ukapita, wote wakiwa hawazungumzi chochote hadi Tom alipoamua kuanzisha mazungumzo.
“Nina swali moja kwako!”
“Uliza!”
“Unanipenda?”
“Saaana!”
“Sasa sikiliza, mimi ni mwanamke na wewe ni mwanaume, sawa?”
“Ndivyo ilivyo!”
“Wewe una nafasi yako kama mke na mimi nina nafasi yangu kama mume ni kweli?”
“Hujakosea kitu!”
“Lakini pia unakubali kwamba, mwanaume ndiye kichwa cha nyumba?”
“Hata kwenye maandiko ipo!”
“Sasa mimi kama mumeo, kichwa cha nyumba, msemaji wa mwisho, naomba unielewe kwamba, kwa leo haitawezekana kwenda kulala nyumbani, lakini naweza kulala na wewe hapa kwa ajili ya kuizundua nyumba, umenielewa?” Tom akasema kwa kujiamini sana ingawa alitarajia kukutana na jibu la kukataliwa.
Kinyume na matarajio yake, Mayasa alimsogelea Tom na kukumbatia kwa nguvu, kisha akausogeza mdomo wake karibu kabisa na wa Tom, akautoa ulimi wake haraka na kuutumbukiza kinywani mwa Tom. Wakaanza kufurahia mapenzi.
“Nimekuelewa mpenzi wangu, hakuna shida!”
“Nami nimefurahi sana kwa uelewa wako mpenzi wangu, naona sasa umekuwa na unatambua nafasi ya mwanaume katika mapenzi.” Tom akasema akishangulia ushindi moyoni mwake.
“Ahsante mpenzi wangu!” Maneno hayo yalitoka kinywani mwa Mayasa lakini moyoni ilikuwa ni tofauti kabisa; “Huna ujanja wewe, nakulea-lea kwanza, lakini kuna siku utaingia mkenge tu.”
Tom akamshika mkono Mayasa, wakaingia ndani. Macho ya Mayasa hayakuwa tayari kuamini kilichokuwa mbele yake, ilikuwa sebule nzuri ya kisasa yenye kila kitu cha maana!
Kwanza kulikuwa na seti ya masofa mazuri, chumba maalumu cha chakula (dinning room), jokofu kubwa, redio kubwa, luninga na deki yake na kila aina ya anasa.
Hayo yangekuwa makazi mapya ya Mayasa baada ya kuishi muda mrefu katika maisha duni huko Mbagala. Hakuamini macho yake, kama kweli Tom alikuwa amedhamiria kumjengea nyumba nzuri nzuri kiasi kile. Macho yake yalizunguka kila kona ya sebele ile ya kisasa yakitizama vitu vizuri vilivyokuwepo.
“Ahsante sana mpenzi wangu, siamini macho yangu!” Mayasa akasema akimwaga machozi kama mvua.
“Amini, amini mpenzi wangu, wewe ndiye niliyekuchagua kutoka moyoni mwangu!”
“Nakuamini mpenzi!”
“Sasa twende nikakuonyeshe bed room!” Tom akamwambia na kumshika mkono kisha wote kwa pamoja wakaongozana hadi chumbani.
Huko Mayasa ndiyo alishindwa kuelewa namna gani atakavyotoa shukrani zake. Kilikuwa chumba kikubwa, kizuri na chenye kila kitu! Kwanza kulikuwa na kabati kubwa la nguo, kitanda kikubwa cha futi sita kwa sita ambacho kilitengenezwa kwa kutumia ngozi, meza ya vipodozi pamoja na vikorobwezo kibao!
Choo na bafu vyote vilikuwa ndani, kukiwa na bomba la maji ya mvua ambayo hutoka ya moto, baridi na ya mchanganyiko! Kilikuwa chumba cha kisasa sana. Mayasa akamwangalia Tom, kisha akajikuta hisia zake za mapenzi zikimpanda sana, akamsogelea na kumtupia kitandani. Kilichoendelea huko ilikuwa ni shughuli nzito iliyomalizika baada ya saa moja.
Wote wakiwa na furaha wakatoka na kwenda nje kuogelea katika bwawa la kuogelea. Hakika yalikuwa maisha ya kifahari sana, kila kitu kilikuwa kipya kwa Mayasa. Siku hiyo hawakutoka kabisa, kila kitu kilikuwa ndani. Vyakula vyote vilikuwa kwenye majokofu.
Walipomaliza Tom alijipumzisha nje, wakati Mayasa akiendelea kupika chakula ndani. Mayasa alijiona mshindi katika maisha mchezo ule hatari wa kuisambaratisha ndoa ya watu.
“Haya ndiyo maisha, lakini mambo bado, nitahakikisha ananyooka, mimi ndiyo Mayasa mtoto wa mjini, niliyezaliwa, kukulia na kusomea katika jiji la wanjanja, jiji la Dar es Salaam,” Mayasa alijisemea moyoni mwake wakati akipika chakula cha usiku.
Baadaye walikula na kulala usingizi wa mapenzi mazito.
******
Macho ya Mariam yaliganda katika saa ya ukutani iliyokuwa ikionyesha kuwa ilikuwa imeshatimia saa 7:55 usiku! Zilibaki dakika tano tu, kabla ya kufika saa 8:00, muda ambao kwa hakika, wanandoa wengi huwa katika harakati za kutafuta watoto!
Mariam alikuwa sebuleni akiwa anamsubiria mume wake bila mafanikio. Machozi yake sasa yalikuwa ya kawaida. Vituko na mateso kutoka kwa mumewe vilizidi, hakuona kama alikuwa na thamani kwa mumewe tena. Siku zote alikuwa wa kumangwa na kutukanwa kuwa yeye mgumba, neno lililomuuma sana.
“Kwahiyo kwasababu sijashika mimba ndiyo  anichukie kiasi hiki? Tom hanitendei haki, ananinyanyasa!” Mariam alisema kwa sauti kubwa na kuamua kwenda chumbani kulala, hapakuwa na matumaini ya Tom kurejea.
Asubuhi ya saa 4:30, gari la Tom lilikuwa likipiga honi nje, mlinzi akafungua na Tom akaingiza gari na kuegesha mahala pazuri. Akashuka na kuingia ndani. Alipokutana na Mariam sebuleni, hakuonyesha kama kuna kosa alilokosea, akamsalia katika hali ya kawaida kabisa.
“Umeamkaje Mariam?!” Tom akamsalimia huku akielekea chumbani.
“Salama!” Mariam alipojibu, Tom akaongeza mwendo kwenda chumbani.
Mariam hakuweza kuvumilia zaidi, akamfuata nyuma nyuma hadi chumbani. Hakuwa na ukali kwa mume wake, akamwacha akavua nguo na kwenda bafuni, aliporudi ndipo alipomwomba kuzungumza naye.
“Lakini mume wangu, kwanini umebadilika tabia kiasi hiki? Kila siku unalala nje, kwanini lakini?” Mariam akamwuliza Tom.
“Mazungumzo yenyewe ndiyo haya?”
“Ndiyo, kwani unaona ni madogo mume wangu?”
“Makubwa, tena makubwa sana!”
“Sasa una mpango gani?”
“Wa kuendelea kulala nje kila siku!”
“Naomba usifanye hivyo Tom wangu, unajua ninakupenda sana!”
“Hata mimi nakupenda sana, lakini kipo kinachokifanya nilale nje, sasa kama unataka nianze kulala nyumbani, basi niruhusu niwe nakuja na kinachokifanya nilale huko nje!”
“Hilo ni jambo dogo sana kwa mtu anayempenda mpenzi wake kama mimi. Hakuna tabu, nimekuruhusu!”
“Kweli?”
“Niamini mpenzi wangu!” Wakakumbatiana kwa furaha.
Siku nzima Tom alishinda nyumbani akiwa na mkewe, tena akijitahidi kumpa haki ya ndoa kwa kikamilifu, lakini jioni akamuaga Mariam kuwa anatoka kidogo.
“Unakwenda wapi tena?”
“Kuchukua hicho kinachonifanya nisilale nyumbani karibu kila siku!”
“Sawa!” Mariam alijibu akitabasamu.
******
Mariam alichukulia maneno ya Tom kama utani, hakujua kama mwenzake alikuwa akimaanisha alichokuwa akikizungumza. Tom alipoondoka, moja kwa moja alikwenda nyumbani kwa Mayasa ambaye alimkuta akitizama luninga sebuleni.
“Njoo chumbani nina habari njema mpenzi wangu!”
“Habari njema? Kuhusu nini tena?”
“Jiandae tuondoke!”
“Tunakwenda wapi?”
“Nimesema jiandae twende!” Ndani ya dakika kumi tu, Mayasa alikuwa ameshamaliza kuvaa na walikuwa njiani wakielekea nyumani kwa Tom, ingawa Mayasa alikuwa hajui.
“Tunakwenda wapi lakini?”
“Leo tunaenda kulala kwangu, nataka Mariam ajue nina akili na nilifunga naye ndoa kwa bahati mbaya, wewe ndiye unayefaa kuwa mke wangu wa ndoa na siyo yeye!”
“Sijakusikia vizuri, umesema tunaenda wapi?”
“Nyumbani kwangu!”
“Nakupenda sana Tom, kweli sasa umeamua kudhihirisha penzi lako kwangu, naomba ukanyage mafuta sawasawa tumuwahi huyo mwehu wako!” Mayasa alimwambia Tom kwa sauti iliyojaa mahaba mazito, kweli Tom akafuata maagizo aliyopewa na Mayasa, akakanyaga mafuta kisawa-sawa.
Alikuwa anamuwahi Mariam, hakika alidhamiria kumuumiza.


Beyond Love- 25

Masikini Mariam, hajui kilichokuwa kikimjia! Tom anakwenda kwa Mayasa na kumpa habari hizo njema, ambapo Mayasa anakuwa haamini kabisa alichosikia. Tom anamhakikishia kwamba, alichosikia kilikuwa yakini na kwamba walikuwa wanakwenda kulala nyumbani kwake.
Je, nini kitatokea? SONGA NAYO...

M
ayasa alikuwa akishangilia ushindi moyoni mwake, alijiona mwenye akili kuliko kawaida. Alimshukuru sana mganga wake kimoyomoyo, akiamini ndumba zilikuwa zinafanya kazi ipasavyo.
“Huu ni mwanzo mzuri sasa, naamini kila kitu kitakwenda sawa, utajiri wa Papaa Bill utakuwa wetu na siyo wake.
“Halafu inaonekana hicho kimwanamke chake hakijui mapenzi, sasa ngoja nimuonyeshe mji, mimi ndiyo mtoto wa mjini bwana!” Aliwaza Mayasa akimtizama machoni Tom.
“Tom...” Mayasa akaita.
“Nakusikiliza mpenzi wangu!”
“Nimeamini kwamba unanipenda sana, wewe ni mwanaume wangu wa maisha na sasa najihakikishia kuwa na wewe siku zote za maisha yangu.”
“Ni kweli kabisa, usiwe na wasiwasi Mayasa wangu, yaani mpaka najuta kumfahamu Mariam, sijui kwanini nilikutana na yule mjinga-mjinga, yaani nina mkosi wa ajabu sana, simpendi yule mwanamke hata chembe!”
“Pole sana, lakini mimi nipo kwa ajili ya kukupa furaha katika maisha yako, usiwe na wasiwasi mpenzi wangu, kila utachokitaka kwangu utakipata, sawa sweetie wangu?!” Sauti ya mahaba ilimtoka Mayasa, tena kwa kutokea puani.
Tom alikiri kwamba mwanamke yule alifanikiwa kwa kiasi kikubwa sana kuufanya moyo wake mateka. Hakuwa na la kufanya zaidi ya kukubali kuwa katika himaya ya mapenzi ya Mayasa.
“Naweza kukuliza!” Mayasa akamwuliza Tom.
“Maswali mangapi?”
“Moja tu!”
“Uliza.”
“Nataka kujua tutalala wapi?”
“Una swali la nyongeza?”
“Hapana.”
“Umesema unataka kujua mahali tutakapolala?”
“Ndiyo!”
“Hilo tu?”
“Kwani dogo?”
“Ok! Vizuri sana, acha nikujibu kwa vitendo!”
Alichokifanya Tom ni kuchukua simu yake kisha kubonyeza namba za Mariam, ikaita na baada ya muda ikapokelewa. Tom akaweka sauti ya juu ‘loud speaker’ kisha akaanza kuzungumza naye.
“Vipi Tom mume wangu?”
“Salama mama, habari za hapo nyumbani?”
“Nzuri, sijui wewe?”
“Mie ni mzima wa afya njema!”
“...ah Tom wangu, kama kuna siku umenifurahisha ni leo, yaani umenipa raha sana!”
“Kweli eh?!”
“Saaana, halafu naomba uwahi, usiku wa leo utakuwa kwa ajili yetu, nitakuonyesha mambo zaidi ya mchana!”
“Sawa mpenzi, hakuna shida, umepika nini?”
“Chakula chako ukipendacho!”
“Nini?”
“Bunia!”
“Kama siyo ndizi samaki, basi itakuwa ugali samaki!”
“Ni ugali samaki mpenzi wangu, mboga za majani na mtindi, najua leo utajilamba sana!”
“...hasa kama samaki wenyewe watakuwa sato!”
“Ni lini nimekupikia samaki wengine tofauti na sato?”
“Utakuwa mlo mzuri sana kwangu!”
“Basi uwahi Tom, angalau tuoge pamoja!”
“Hakuna tabu, lakini nitakuwa na mgeni, sasa ni vizuri kama utaandaa kile chumba cha wageni vizuri!”
“Hilo tu mume wangu, labda useme lingine!”
“Na chakula chake pia!”
“Hakuna shida!”
“Basi baadaye mpenzi wangu!”
“Sawa...mwaaaaaaa....”
“Mwaaaaaa...” baada ya mazungumzo hayo kwenye simu, Mariam alimuangushia busu mwanana Tom ambaye naye alijibu kisha akakata simu.
Baada ya hapo akamgeukia Mayasa akamwangalia kwa jicho lililojaa mahaba, huku akitabasamu kwa furaha. Alikuwa akishangilia ushindi!
“Nadhani umesikia kila kitu!”
“Sina la kuongeza mpenzi wangu, sasa moyo wangu mweupeeeee!”
“Leo ni siku yake, atajuta kukutana na mimi, mwanamke ananing’ang’ania utafikiri aliambiwa mwanaume nipo peke yangu? Nimeshafanya kila aina ya vituko lakini hasikii, sijui ni mwanamke wa aina gani yule?”
“Kwanza mwanamke gani mgumba? Subiri nikuzalie watoto haraka-haraka, upate warithi wa mali zako!” Mayasa akadakia.
Ilikuwa kauli ambayo ilimsisimua sana Tom, kuambiwa kwamba angezaliwa mtoto, tena haraka-haraka kulimpa faraja sana moyoni mwake, akawa na matumaini ya kuwa baba baadaye.
“Umenifurahisha sana Mayasa, hakuna kitu ninachokitamani kama kuwa baba, unanifanya nijisikie vizuri sana, ahsante sana mpenzi wangu, ahsante!”
“Tena nipe muda mfupi tu, kutoka sasa!”
“Tutaona!”
“Sasa?”
“Nini tena?”
“Tunakwenda moja kwa moja nyumbani au tunapitia mahali kwanza?”
“Wewe unaonaje?”
“Nilikuwa naona ingekuwa vizuri zaidi kama tutapitia mahali tuzungumze zaidi kwanza, kabla ya kwenda nyumbani. Nafikiri muda mzuri ni kuanzia saa tano au sita za usiku!”
“Tufanye saa saba!”
“Sawa, twende wapi?”
“Corner Bar!”
“Sawa!” Safari yao ikabadilika, wakaenda moja kwa moja Corner Bar, iliyopo Sinza, Afrika Sana, jijini Dar es Salaam.
******
Furaha iliyokuwa moyoni mwa Mariam, haikuwa rahisi kuelezeka, alimuona kama Tom wake alikuwa mpya kabisa, sasa alikuwa na imani kwamba Mungu wake alikuwa ameshamsikia na yake yalikuwa majibu.
Hakuwa na chembe ya hisia tofauti na hizo, hakujua kama muda huo, Tom alikuwa na mwanamke Bar, tena alikuwa akipanga kwenda kulala naye nyumbani kwao. Hilo halikuweza kuchukua nafasi kabisa katika moyo wake.
Alichokifanya ni kuhakikisha anamridhisha mumewe ipasavyo siku hiyo, kitu cha kwanza kabisa kufanya ilikuwa ni kupika chakula kizuri sana ambacho mumewe alikuwa akikipenda sana, ugali sato! Kitu kingine alichokifanya ni kuhakikisha chumba chao kinakuwa kisafi kuliko zote, baada ya hapo akafanya usafi katika chumba cha wageni.
Alipomaliza maandalizi yote hayo, akakaa sebuleni akimsubiria kwa hamu kubwa sana mumewe ambaye mpaka wakati huo, saa 2:00 za usiku, wakati taarifa ya habari ya Kituo cha Televisheni cha ITV ikianza, alikuwa hajafika!
Saa moja ikaondoka, ya pili, tatu na hatimaye ilifika saa 6:00 za usiku, Tom akiwa bado hajafika, hapo ndipo alipoanza kupatwa na wasiwasi ambapo aliamua kumpigia simu. Hata hivyo simu yake haikupatikana!
Hakuingia chumbani, akabaki pale pale sebuleni akimsubiria mumewe kwa shauku kubwa! Saa saba kasarobo za usiku, honi ilisikika getini, Mariam hakuwa na mashaka kwamba aliyekuwa mlangoni alikuwa mumewe. Mlinzi akafungua geti, Tom akaingia ndani na kuegesha mahala pazuri.
Akafungua mlango na kushuka garini, kisha akazunguka upande wa pili na kumfungulia Mayasa, akashuka.
“Karibu nyumbani mpenzi!”
“Ahsante sana.”
“Twende.”
“Tangulia.” Wakaongozana moja kwa moja, hadi ndani.
Mariam akawapokea kwa furaha sana, hakujua kilichokuwa nyuma ya pazia. Tofauti na matarajio yake, Tom alipita moja kwa moja na Mayasa hadi katika chumba anacholala yeye na Mariam kila siku.
Mariam akashindwa kuelewa kilichokuwa kikiendelea, kuna wakati alikuwa akifikiria labda mumewe aliamua kumfanyia mzaha. Alidumu sebuleni kwa dakika mbili tu, sebule haikukalika tena, akaondoka na kuwafuata chumbani. Dakika mbili zilikuwa nyingi sana kwa Tom na Mayasa.
Aliwakuta wakiwa kama walivyozaliwa, huku wakicheza michezo ya kimahaba bila wasiwasi!
“Tom!!!”
“Mariam!?”
“Nini unafanya na huyu mwanamke huku chumbani kwetu?”
“Sitaki kuamini kama macho yako yamepoteza uwezo wa kuona kiasi hiki!” Tom akasema kwa sauti tulivu sana, ambayo ilionekana dhahiri kabisa alidhamiria.
“Toooom...”
“Yes Mariam!”
“Umeona haifai kufanya uchafu wako huko nje, na sasa umeniletea hapa nyumbani kabisa!” Sauti ya Mariam sasa, ilianza kukata-kata, huku machozi yakifanana kabisa na maji machoni mwake.
“Lakini ukiona hivi ujue hutakiwi, kwanini unang’ang’ania? Mwanamke gani wewe, hata shepu huna, hebu ona wenzako tulivyojazia...hivi wakati wazuri tunaumbwa, we’ ulikuwa wapi mwenzetu? Hebu toka utuachie nafasi tujinafasi!” Mayasa akasema, akimtizama Mariam kwa dharau sana.
Wakati huo Mayasa alikuwa akijitingisha-tingisha akiwa kama alivyozaliwa. Mapigo ya moyo wa Mariam yaliongezeka kasi kuliko kawaida, akahisi kizunguzungu na kuanguka chini kama gunia la mchele.
“Haaaaah, Mariam?!” Tom akapiga kelele.
“Wa nini, mwache afe!” Mayasa akasema.
“Lazima tumsaidie!”
“Sasa amua kuwa na mkeo au mimi!” Mayasa akasema akianza kuvaa nguo zake tayari kwa kuondoka.
“Usifaye hivyo Mayasa, lakini tunatakiwa kumsaidia!”
“Inaonekana bado unampenda huyo mkeo, sasa baki naye!” Sasa Mayasa alikuwa anatoka nje ya chumba kile.
Tom hakutaka kuruhusu jambo lile litokee, akamfuata na kumrudisha chumbani, pamoja na kwamba moyo wake ulikuwa ukimuuma sana, lakini kwa kumridhisha Mayasa, Tom akaamua kumburuza Mariam hadi sebuleni kisha akarudi chumbani kulala na Mayasa. Hadi wakati huo, Mariam alikuwa hajazinduka.






Beyond Love- 26

Baada ya mzozo wa muda mrefu kati ya Tom na Mariam, kuhusu tabia ya  Tom kulala nje, hatimaye Tom anamweleza Mariam kwamba kuna kitu kilichomsababisha alale nje na kama angekuwa tayari aje nacho nyumbani!
Bila Mariam kuelewa kwamba alikuwa anakaribisha matatizo, akakubali. Tom anakwenda nyumbani kwake na Mayasa, anamfukuza Mariam chumbani kwake na kulala na Mayasa. Mariam anapatwa na mshtuko na kuanguka mlangoni.
Tom anamburuza hadi sebuleni na kumwacha huko kisha anarudi chumbani kulala na Mayasa. Je, nini kitatokea? Kwanini Tom anamchukia Mariam kiasi hicho? Anza sasa KUSONGA NAYO...


Kitendo cha Tom kukubali kumuacha Mariam akiteseka sebuleni na kwenda chumbani kulala na Mayasa, kilimfurahisha sana Mayasa, alijiona mwanamke mshindi ambaye ana nguvu ya ushawishi. Hali ilikuwa tofauti sana na Tom, yeye moyoni mwake alikuwa mwenye uchugu mwingi sana, ingawa ni kweli alikiri kwamba Mayasa alikuwa moyoni mwake zaidi kuliko Mariam.
“Umenifurahisha sana mpenzi wangu, sasa naamini kweli unanipenda kwa mapenzi ya dhati, wewe ndiye mwanaume wa maisha yangu, siwezi kukuacha hata siku moja!” Mayasa akasema akimkumbatia Tom aliyekuwa anaonekana dhahiri hana furara aliyokuwa nayo awali.
Jambo hilo liligundulika haraka sana na Mayasa, alijua wazi kwamba Tom hakuwa na furaha aliyokuwa nayo awali, jambo ambalo kwa kiasi kikubwa hakulipenda, siku zote alitaka kuibuka mshindi, kupotea kwa furaha ya Tom, kwa kiasi kikubwa kulimaanisha ushindi wake ulikuwa katika hati hati za kutoweka.
Ni jambo ambalo Mayasa alipingana nalo siku zote, kwake kulikuwa hakuna kitu kinachoitwa kushindwa, ushindi ndiyo kitu pekee ambacho kilikuwa na maana kubwa katika maisha yake, akili yake iliwaza ushindi pekee, bila kujali njia ambayo ushindi huo ungepatikana!
Alimwangalia Tom kwa jicho la hasira, kisha mkono wake akaupeleka moja kwa moja hadi kwenye sidiria yake alipokuwa amefunga hirizi yake na kuiminya kwa nguvu!
“Una nini Tom?” Mayasa akauliza kwa ukali sana.
Tom hakujibu!
“Hivi, nazungumza mwenyewe?”
“...hapana...” Tom akajibu kama alikuwa ametokea katika usingizi mzito.
“Bali?”
“Mbona upo hivyo?”
“Vipi Mayasa?”
“Umeniitaje?!”
“Mayasa!”
“Yaani umefikia hatua unaniita Mayasa?”
“...samahani mpenzi wangu, nilipitiwa kiudogo, unasemaje mpenzi wangu?”
“Inaonekana bado unampenda huyo mkeo, kama ndivyo ni bora uniambie niondoke zangu, sikulazimishi kuwa na mimi!”
“Hapana, kwani kuna nini?”
“Mbona sioni uchangamfu wako? Hukuwa hivyo Tom, naona una mawazo ya mkeo!”
“...hapana...nani? mariam? Mimi...ah no! Labda siyo Thomas, siwezi kabisa kuwa na mwanamke mbovu kama yule, tena sijui nilikutana naye usiku au vipi? Tena usikumbushe kuhusu hilo lijanamke, hebu tuzime taa tulale...” Tom akajikuta akiropoka bila kujua maneno yale yalitokea wapi.
Kwa Mayasa ulikuwa ushindi ambao alikuwa akiutegemea siku zote. Kama ni barabara, basi hiyo ilikuwa imenyooka! Hapakuwa na kitu kingine zaidi kupanda kitandani na kulala usingizi wa kiutu uzima!
***
Kila alipojaribu kuvuta kumbukumbu juu ya watu waliokuwa mbele yake, hakuweza kuwajua kabisa. Hilo halikuwa na maana sana kwake kwa wakati huo, lakini kwanini waliamua kumtesa na kumnyanyasa ndiyo jambo ambalo lilimnyima kabisa raha.
Huyu ni Tom, akiwa katikakati ya wanaume sita waliokuwa wamejazia vyema vifuani mwao, wakimwangalia kwa hasira huku wakimhakikishia kifo!
“Lazima ufe, we bweha!” Mmoja wa wanaume wale walioonekana kuwa na hasira sana akauliza.
“Nimefanya nini lakini?”
“Utajua mwenyewe, jiulize ni nani ambaye una ugomvi naye!”
“Ugomvi?”
“Ndiyo, ugomvi...ni nani ambaye huna maelewano naye?”
“Mbona naishi na watu vizuri sana!”
“Hata hivyo, hiyo siyo kazi yetu, tunachojua sisi ni kukuua tu na hiyo ndiyo kazi yetu ambayo tumelipwa kuifanya, hayo mambo mengine hatuna haja nayo!”
“Msiniue tafadhali!”
“Tutakuua tu lazima, hakuna kitu cha kubadilisha ukweli huu, lazima ufe.” Mtu mwingine ambaye alionekana kama ndiye mkuu wa wengine alisema kwa hasira.
Tom alishindwa kuelewa mahali pale palikuwa ni wapi na alifikaje? Alijaribu kuwaza kama kuna mtu alikosana naye, lakini hakumuona. Ghafla akashangaa amepoteza fahamu, alipozinduka baadaye, alikuwa katika katikati ya pori nene, mbele yake kukiwa na shimo kubwa, akiwa amezungukwa na wale vijana wenye silaha mikononi mwao.
Tom alikuwa amefungwa kamba mikono yote na miguu na hakuw ana uwezo wa kufanya jambo lolote. Tom alitetemeka sana.
“Naombeni mnisamehe tafadhali!”
“Hatuwezi kukusamehe, lakini tutafanya jambo moja kwa ajili yako!” Kiongozi wa lile kundi akasema.
“Ni nini?’
“Tutakuonyesha picha ya mtu ambaye ametuagiza tukuue!”
“Sawa, naombeni nimuone!” Tom akasema akiwa na hamu kubwa sana ya kujua ni nani ambaye aliamua kufanya njama za kumuua.
“...ambaye anataka ufe ni huyu hapa...halafu acha kufuatilia maisha ya watu...kufa salama...” Yule mtu akamwambia akimwonyesha ile picha.
Macho ya Tom hayakuwa tayari kuamini mtu wake wa karibu, mpenzi wake wa kweli ambaye aliamua kuachana na mkewe kwa sababu yake ndiye aliyekuwa akitaka auawe. Ilikuwa picha ya Mayasa. Tom akachanganyikiwa.
“Mayasa, nooooooooo.....” Tom akapiga kelele.
Katika hali ya kushangaza sana, wale wakaanguka mmoja mmoja baada ya kupigwa risisi kama mvua miilini mwao. Tom hakuweza kugundua ni nani aliyewapiga risasi. Ghafla akashangaa kumuona mtu mbele yake akiwa amevaa kininja, akijifunika hadi usoni.
Mtu huyo akaanza kuvua zile nguo za Kininja, kisha akavua ile kofia iliytofunika hadi uso wake, hapo ndipo Tom alipogundua alikuwa ni Mariam. Tom akashtuka sana.
“Mariam?!”
“Ndiyo ni mimi ninayekupenda, ambaye penzi langu halina mashaka kwako, nakupenda Tom ndiyo maana nimekuja kukuokoa...” Mariam akasema akitokwa na machozi kama mvua.
“Siamini macho yangu...Mariam....”
“Ni mimi!”
“Marimuuuuuuuuu....” Tom akapiga kelele kwa sauti ya juu sana. Muda huo huo akazinduka usingizini, alikuwa amelala kitandani na Mayasa, hapo ndipo alipogundua kwamba alikuwa ndotoni.
Ilikuwa ndoto ya ajabu sana, hakuweza kujua maana ya ile ndoto. Alipogeuza macho yake kumwangalia Mayasa, alimkuta akiwa anakoroma usingizini, akawasha taa na kunyanyuka polepole kitandani, kisha akaizima taa na kutoka hadi sebuleni kwenda kumfuata Mariam.
Moyo wake ulimuuma sana kumkuta Mariam hadi wakati ule hajazinduka, alichokifanya ilikuwa ni kumbeba hadi chumba cha wageni na kumlaza kitandani, akamfunika shuka na kumwekea chandarua. Moyo wake ulikuwa kama umepigwa ganzi, alishindwa kulewa ilikuwaje hadi akamchukia Mariam kiasi kile.
“Nashindwa kuelewa kwanini inakuwa hivi, ni kweli mimi siyo wa kwanza kuwa na mwanamke wa nje, lakini mbona mimi namfanyia mke wangu vituko kiasi hiki? Kuna nini lakini?” Tom akajikuta akijiuliza maswali mfululizo kichwani mwake bila kupata majibu yakinifu.
Akiwa anamwangalia Mariam aliyekuwa amelala pale kitandani kwa huruma, akashangaa mtu akimgusa mgongoni.
“Hivi we’ mwanaume una nini? Hutosheki? Umeona uje na huku?”
“Ah! Mayasa?!”
“Ndiyo mimi, unashangazwa na nini?”
“Samahani mpenzi wangu?”
“Imekuwaje tena?”
“Ah, hakuna kitu.”
“Unafanya nini hapa?”
“Nimeamua kumleta Mariam huku.”
“Kwanini?”
“Mbu zilikuwa zinamng’ata sebuleni.”
“Una uhakika hakuna zaidi ya hivyo?”
“Ndiyo, hakuna kitu.”
“Kwanini hukuniaga?”
“Sikuona sababu ya kukusumbua.”
“Haya twende chumbani.” Mayasa akamuamrisha Tom ambaye hakubisha.
Mayasa alikuwa mbabe kupitiliza, alikuwa na kitu kilichomfanya awe na jeuri aliyokuwa nayo, nguvu za giza alizokuwa akizitumia zilikuwa zinafanya kazi vyema bila ya Tom kugundua chochote. Walipofika chumbani, kazi ilikuwa moja tu, kupeana mapenzi motomoto hadi asubuhi.
Hawakulala tena, Tom hakuwa na kumbukumbu za Mariam tena, kichwani mwake kulikuwa na mtu mmoja tu, Mayasa. Alimuona mwanamke mzuri kuliko kawaida.
“Nakupenda sana Mayasa!” Tom akamwambia.
“Una uhakika?’
“Ndiyo, nakupenda sana, huoni mambo niliyokufanyia?”
“Mambo gani?”
“Nimekujengea nyumba nzuri, nimekupa gari na kila kitu utakacho nakupa, hiyo haitoshi kukufanya uamini kwamba nakupenda?”
“Haitoshi!!!”
“Unataka nifanye nini tena, sema chochote nitafanya!”
“Kweli?”
“Ndiyo, nakupenda sana na sitaki kukufanya uumie kwa ajili yangu!”
“Nataka umfukuze Mariam hapa nyumbani, tuishi kwa furaha!”
“Na kule kwako?”
“Nitaweka mpangaji, nataka kuishi na wewe hapa!”
Tom hakuwa na jibu.
*******
Jicho lake la kuume ndilo lilikuwa na kwanza kufumbuka, kisha likafuata la upande wa kushoto. Taratibu kumbukumbu zikaanza kumrejea Mariam. Kilikuwa chumba ambacho siyo alichokuwa akilala siku zote. Akapiga jicho kila upande na kujaribu kuvuta kumbukumbu zaidi, akatambua kwamba ni kweli siyo chumba anacholala siku zote.
Akakumbuka vyema kwamba kilikuwa chumba cha wageni, tena alichokiandaa jioni yake kwa ajili ya mgeni ambaye Tom alimwambia angekuja naye. Kufikia hapo, akakumbuka kila kitu. Alikuwa amelala katika chumba cha wageni. Hakuweza kukumbuka aliingia vipi na muda gani. Akaamka kichovu na kupiga hatua za taratibu kuelekea chumbani kwake.
Alipofika mlangoni, akasikia kelele za mahaba zikitokea chumbani. Walikuwa ni Tom na Mayasa wakipeana maraha chumbani. Mariam akachanganyikiwa, lilikuwa tukio la udhalilishaji sana. Mariam akachungulia kupitia tundu la ufunguo lililokuwa mlangoni, alichokiona humo ndani hakifai kuandikika hapa! Akaanza kulia.
“Tom mume wangu, ni nini unafanya na huyo mwanamke wako? Kwanini unakuwa hivi lakini? Yaani umeshindwa kufanya uchafu wako huko nje, unakuja kunifanyia hapa nyumbani, tena chumbani kwetu, katika kitanda ninacholala na wewe...Tom...Tom...Tom...kwanini unafanya hivi lakini?!” Mariam akapiga kelele akilia kwa uchungu.
Muda mfupi baadaye mlango ulifunguliwa, Mayasa akatoka akiwa amevaa upande wa kanga, tena kanga yake mwenyewe, uso wake ulikuwa umejaa makunyanzi, akamsogelea na kumzaba kibao kikali sana shavuni mwake.
“Koma kuharibu starehe za watu, ungekuwa na maana angenileta hapa? Huna jipya, mwanamke hujui mapenzi zaidi ya kufua na  kupika, unafikiri kwa mtindo huo ataacha kutafuta mtoto wa mjini anayeweza kumpa raha kama mimi? Na utalijua jiji na mitaa yake...” Mayasa akasema akibenua midomo yake.
Uso wa Mariam ulilowana kwa machozi, alishindwa kuelewa kwanini mateso yale yalikuwa kwake tu na siyo kwa mwingine.
“Halafu Mariam uwe na adabu, naomba usijaribu kumsumbua mpenzi wangu, nenda kalale chumbako kwako kule!” Tom naye akatoka na kumwambia Mariam.
Mariam alihisi alikuwa ndotoni, lakini ukweli ni kwamba haikuwa ndoto, kila kilichokuwa kikitokea katika maisha yake kilikuwa yakini kwa maana ya yakini haswa.




Beyond Love- 27

Yote haya yanasababishwa na mwanamke mmoja hatari sana, Mayasa! Huyu ni mtaalamu wa kwenda kwa waganga ambao walimtengeneza Tom na kumsahau kabisa Mariam. Sasa Mayasa ameshaingia nyumbani kwa Tom huku Mariam akilala katika chumba cha wageni. Mariam haamini kinachotokea katika maisha yake. Hajui hatma yake. Nini kitatokea katika maisha yake? SONGA NAYO...

Masikio ya Mariam yalikuwa hayataki kuamini yalichosikia wakati macho yake yakikataa katakata kukubaliana na kilichoonekana kupitia tundu la funguo, mambo yaliyofanyika chumbani yalikuwa mazito sana. Alishindwa kuelewa ni kosa gani kubwa alilomfanyia Mungu kiasi cha kumpa adhabu kubwa kiasi kile.
Ilikuwa lazima afikirie kitu cha kufanya, mawazo pekee yasingeweza kutosha kukabiliana na tatizo lililokuwa mbele yake. Alijua kitu kimoja moyoni mwake, kwamba alikuwa anampenda sana Tom, na mambo yote yaliyokuwa yakitokea ni juhudi za shetani kutaka kumharibia mume wake.
“Mungu ni wewe peke yako ndiye mwenye uwezo wa kunisaidia tatizo hili, naomba msaada wako baba, sina uwezo peke yangu, nisaidie mwanao...” Mariam aliomba moyoni mwake machozi machoni mwake yakitiririka.
Mara akapata wazo jipya, aliona ni bora aendelee kumuomba Tom abadili mawazo yeke. Aachane na huyo mwanamke kwani yeye ndiye mkewe wa ndoa aliyekuwa kwa ajili yake.
“Tom mume wangu, kwanini unanitesa kiasi hiki? Ni kosa gani nililokufanyia lakini mume wangu mpenzi? Kumbuka ahadi yako siku ya ndoa Tom, kumbuka!” Mariam alisema akitokwa na machozi.
“Huna kosa Mariam...” Tom akajibu akiwa chumbani.
“Sasa kwanini unanitenda hivi?”
“Huna mvuto mtoto wa kike, ndiyo maana ameona awe na mimi mwenye mvuto.” Mayasa akajibu.
“Sijakuuliza wewe!”
“Kumbe umemuuliza nani?”
“Mume wangu!”
“Unachekesha sana wewe, hivi Tom ni mumeo kweli wewe?”
“Kwani mume wa nani?”
“Yupo na nani chumbani? Hivi angekuwa anakuthamini angekulaza chumba cha wageni? Ameona huna jipya ndiyo maana amekususa, mwanamke usiye na haya, unayesubiri kutupiwa mabegi nje?! Kwani huoni kuwa hutakiwi humu ndani? Si uondoke...” Mayasa alisema maneno hayo macho makavu akiwa hana woga hata kidogo, alimchukia Mariam kuliko kitu chochote.
Mariam alikuwa ni kama anaharibu mambo yake, wazo la kwamba yeye ndiye aliyemwingilia mwenzake nyumbani kwake halikupata nafasi kabisa akilini mwake. Aliona kama Mariam ndiye aliyekuwa akimwingilia yeye.
Mariam alilia kwa uchungu mwingi sana, aliamini machozi yake pengene yangemuuma Tom na kubadilisha uamuzi wake, lakini ilikuwa tofauti kabisa, Tom alikuwa kimya chumbani akila raha na Mayasa, hakuonyesha kujali hata kidogo thamani ya chozi la Mariam.
Maisha yaliendelea kwa mtindo wa Mariam kulala chumba cha wageni na Tom kulala na Mayasa huku Mariam akishurutishwa kufanya kazi zote za nyumbani. Ni kama alikuwa mfanyakazi wa ndani! Kazi kubwa ya Mariam ilikuwa ni kusali, akimuomba Mungu wake amsaidie. Maisha yalikuwa ya shida sana.
Afya ya Mariam ikaanza kuzorota, kila siku kwake ilikuwa ni kilio. Tom hakuonyesha kujali, Mayasa alikuwa ndiye kila kitu nyumbani kwake, alipanga na kutoa amri ya kila jambo ndani ya nyumba. Usiku mmoja Mariam hakulala kabisa, alitumia kuwaza maisha yake, kwa muda wa miezi mitatu aliyovumilia, hakuna hata siku moja ambayo Tom alionyesha dalili za kubadilika tabia wala msimamo wake.
Tom alizidi kuwa mkali kwake na hakutaka kushirikiana naye kwa chochote, Mariam hakuona kama kuna sababu ya kuendelea kuteseka kwa mwanaume ambaye alikuwa hana mapenzi na yeye tena. Akapanga nguo zake usiku huo kwa safari ya kuondoka asubuhi yake. Alishachoshwa na vituko vya Tom.
*****
Saa kumi na mbili asubuhi, Mariam alikuwa ameshajiandaa kuondoka. Akiwa na begi lake la nguo, alikwenda hadi mlangoni mwa chumba cha Tom na Mayasa na kugonga. Alitumia muda wingi sana kugonga bila kufunguliwa.
“Nani?” Tom akauliza kwa ukali.
“Ni mimi!” Mariam akajibu kwa sauti ya unyonge sana.
“Sawa wewe, lakini nani?”
“Mariam!”
“Unataka nini asubuhi yote hii? Kwanini unatuharibia starehe zetu?”
“Samahani, sina nia mbaya!”
“Shida yako ni nini?”
“Nimekuja kukuaga Tom, naenda kwetu, nakuacha uendelee kuishi na mwanamke wako ambaye umeona anafaa kuliko mimi!”
“Siyo kwamba nimeona anafaa kuliko wewe, bali ndiyo uweli wenyewe ulivyo. Sasa unaondoka sasa hivi au baadaye?”
“Nimekuja kukuaga sasa hivi naondoka!”
“Hakuna neno wasalimie wote, waambie Tom au Papaa Bill sasa anakula bata na mtoto mzuri Mayasa!”
Mariam hakujibu tena, akaanza kulia akivuta mabegi yake kwenda nyumbani kwao.  Kwa Mariam ilikuwa siku mbaya sana ambayo kwa hakika isingeweza kufutika katika maisha yake, lakini kwa Mayasa na Tom, ilikuwa siku nzuri sana kwao, kwani walikuwa wanaachiwa uhuru wa kufanya kila kitu wanachotaka kwa nafasi!
*****
“Vipi tena mwanangu? Mbona hivyo?!”
“Mama acha tu!”
“Nini?”
“Matatizo!”
“Matatizo gani? Mbona sikuelewi?”
Mariam hakuweza kujibu kitu tena zaidi ya kulia. Mama yake akamfuata huku naye machozi yakimtoka, lakini kabla hajamfikia, Maram alianguka chini na kupoteza fahamu.
“Mungu wangu, mwanangu ana nini jamani? Nini kimempata tena jamani?” Mama yake na Mariam alipiga kelele, muda huo huo baba yake Mariam akatoka ndani.
“Vipi kuna nini?”
“Mariam amekuja analia...kaanguka chini kabla hata sijajua kinachomsumbua!”
“Amesema ana tatizo gani?”
“Hajasema chochote, tumpeleke hospitalini kwanza, hayo mambo mengine tutajua baadaye!”
“Sawa!”
Hawakuwa na muda wa kupoteza, wakamwingiza Mariam kwenye gari na kumpeleka katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili. Nusu saa baadaye tayari walishafika hospitalini na Mariam apelekwa katika chumba cha mapumziko kwanza kwa ajili ya kupewa huduma ya awali.
“Nini kimempata?” Daktari aliwauliza wazazi wa Mariam.
“Ameanguka ghafla!”
“Kabla ya hapo alikuwa anaumwa?”
“Kwakweli hatuna uhakika maana alitokea kwa mume wake asubuhi hii akiwa katika hali hii, inawezekana amegombana naye!”
“Mmejaribu kumtafuta kwenye simu?”
“Ndiyo, hapatikani.”    
“Ok! Subirini kidogo nje, acha sisi tufanye kazi yetu!” Daktari yule akasema akiwatizama wenzake ambao walitingisha vichwa kumuunga mkono alichokizungumza.
Wazazi wa Mariam wakatoka nje na kuwaacha madaktari wakijaribu kuokoa maisha ya Mariam.
“Sijui atakuwa amepatwa na nini mwanetu jamani!” Mama Mariam akamwambia mume wake.
“Inawezekana kuna kitu wamekorofishana na mume wake, maana naona hata afya yake siyo nzuri kabisa.”
“Mungu amsaidie apate nafuu kwanza, tutazungumza naye baadaye!”
Waliendelea kuzungumza juu ya afya ya mtoto wao hadi saa moja baadaye, mmoja wa madaktari waliyekuwa wakimhudumia Mariam alipotoka nje.
“Anaendeleaje sasa?” Mama Mariam alikuwa wa kwanza kumuuliza daktari.
“Msijali, inabidi mkubaliane na matokeo, maana hatuwezi kubadili kitu kilichopo!” Daktari akasema kwa utulivu sana.
“Dokta sema tu, nini kimetokea?”
“Punguzeni wasiwasi kwanza, tulieni...”

Beyond Love- 28

Anapelekwa Hospitali ya Taifa Muhimbili kwa ajili ya matibabu ambapo anaingizwa katika chumba cha wagonjwa wa awali kwa ajili ya kupatiwa huduma ya kwanza.
Ghafla daktari anatoka nje, uso wake ukionekana kuwa na jambo lililotokea. Je, nini kitatokea? SONGA NAYO mwenyewe...

Mwili wa mama yake na Mariam ghafla ulikuwa kama umemwagiwa maji ya baridi, alishahisi lazima mwanaye atakuwa amekubwa na matatizo makubwa sana, kitu pekee ambacho kilizunguka ubongoni mwake ilikuwa ni kiifo! Kwa vyovyote vile uso wa daktari yule ulisomeka kwamba taarifa zilizokuwa zikiwajia baadaye zilikuwa za msiba.
Machozi kama maji yalianza kutiririka ghafla machoni mwa mwanamke huyo ambaye uso wake ulishajaa makunyanzi. Machozi yake yalisbabisha hata baba yake na Mariam naye apatwe na wasiwasi mkubwa sana. Hisia za mwanaye alikuwa marehemu ziliutawala moyo wake kwa kasi ambayo hata yeye hakujua ilipotokea!
“Dokta kuna nini, mbona unatutisha?” Baba yake na Mariam akauliza akiwa na wasiwasi mwingi sana moyoni mwake.
“Sema tu, kama mwanangu amekufa, hakuna jambo jipya hapo na wala huna haja ya kujaribu kutuficha!”
“Hapana wazee wangu, hebu tulieni kwanza, hakuna jambo baya lililotokea, na kwa hakika tunahitaji sana msaada wenu katika tatizo hili!”
“Tatizo gani?”
“La binti yenu!”
“Sawa, kwani amekufa?”
“Hapana...Mariam ni mzima na kwa bahati nzuri ameshazinduka sasa, lakini kuna jambo limejitokeza ambalo ndilo lililosababisha nije kuwaona kwanza!”
“Ni nini dokta?” Mama Mariam alikuwa wa kwanza kuuliza kwa sauti iliyojaa wasiwasi mwingi sana.
Angalau sasa tabasamu la baba yake na Mariam sasa lilianza kuonekana, uso wenye makunyanzi ulianza kupotea taratibu na nuru kuanza kushamiri katika nyuso za wazee hawa ambao kwa hakika walikuwa na mapenzi mazito sana kwa mtoto wao.
“Enhee dokta, tatizo ni nini?”
“Binti yenu baada ya kuzinduka tu, ametaja jina la Tom, tena akipiga kelele akidai kwamba anamnyanyasa sana. Sasa sijui kama mnamfahamu huyo Tom!”
“Ndiyo tunamfahamu!”
“Ni nani?”
“Mumewe!”
“Ameachana naye?”
“Hapana, wanaishi pamoja ila leo asubuhi hii ndiyo amekuja nyumbani lakini kabla ya kuzungumza chochote tukashangaa amepoteza fahamu kwa inavyoonekana watakuwa wamekwaruzana kidogo!”
“Ok! Sasa hatua gani mmekwishachukua kama wazazi?”
“Kubwa ambalo kwetu sisi lilikuwa la maana zaidi ilikuwa ni kuhangaikia afya ya binti yetu kwanza, ingawa pia tumejaribu kumpigia mwenziye simu lakini hapatikani!” Baba yake na Mariam alisema.
“Ok! Poleni sana!”
“Tunashukuru, nini kinaendelea kwa muda huu?”
“Mariam itabidi abaki hapa hospitalini kwa siku tatu zaidi, tunahitaji kuwa naye karibu sana kwa kipindi hiki, anahitaji ushauri wa Kisaikolojia na baadaye tutawapa taratibu za kuzungumza naye kwa ukaribu zaidi ili kuweka haya mambo sawa!”
“Tunashukuru sana dokta, tunaweza kumuona?”
“Hakuna shida, lakini tunashauri msimuulize maswali magumu sana kwa kipindi hiki ambacho anaonekana kuwa na mawazo sana akilini mwake, msalimieni na mumpe pole tu, tafadhali msimuulize mambo magumu sana. Akili yake kwasasa inahitaji kupata wasaa wa kupumzika!”
“Hakuna tabu dokta!”
Dakika mbili baadaye wazazi wa Mariam walikuwa wameshaingia katika chumba kile ambapo walimkuta Mariam akiwa amelala juu ya kitanda, macho yake yakiwa yamejaa machozi.
“Mama....baba....” Mariam aliita akionekana kuwa na majonzi sana.
“Mwanangu, pole sana mama...utapona mama usijali!” Mama yake Mariam alisema akimwangalia mwanaye aliyekuwa ametulia kitandani.
Hakuwa na uwezo hata wa kukaa mwenyewe. Mariam alitia huruma sana, muda huo mama yake alipata nafasi ya kuweza kugundua kwamba Mariam alikwa amedhoofu sana, afya aliyokuwa nayo, haikuwa yake ya siku zote. Mariam alikuwa amepungua sana.
“Ahsante mama, lakinia alichonifanyia Tom kinauma sana mama yangu...nimevumilia lakini nimeshindwa!”
“Amekufanyia nini?” Baba yake Mariam akadakia.
“Tom ameamua kuwa na mwanamke mwingine sasa!”
“Umejuaje?”
“Anaishi naye pale nyumbani, mwanzoni alikuwa anafanya siri, lakini sasa ameweka kila kitu wazi, kaamua kuja naye nyumbani na ni muda mrefu sasa mimi nalala chumba cha wageni, Tom amebadilika, ananichukia sana sasa hivi!”
“Usijali mwanangu, kila kitu kinapangwa na Mungu, binadamu hatuwezi kupanga mambo mama, na hata kama tukipanga Mungu mwenyewe ndiye mwenye uwezo wa kubadilisha, kitu cha msingi kwako kwa sasa ni kutuliza akili yako na kumwachia Mungu kila kitu! Yeye ndiye atakayejua kitu cha kufanya, atakupigania na kukufanya huru tena, mkabidhi yeye kila kitu na maisha yako yatakuwa mapya mwanangu. Mungu ni kila kitu mama, asikudanganye mtu mwanangu!”  Mama yake Mariam alihakikisha anamuweka sawa mwanaye ili aweze kukabiliana na tatizo alilokuwa nalo.
“Lakini mama, hamuwezi kuzungumza naye, nampenda sana Tom wangu mama, nampenda Tom, nitawezaje kuishi bila yeye?”
“Sawa, acha tujaribu kwanza, lakini nakusihi tuliza akili yako mama, afya yako imezorota sana mwanangu, kumbuka sisi wazazi wako tupo na tunakupenda sana, hatutaweza kukubali tukuache uteseke, sawa mama?” Mama Mariam alizungumza kwa sauti ya upole iliyojaa mapenzi mazito.
“Sawa mama, lakini lazima mjaribu kuzungumza na Tom kwanza!”
“Sawa, usijali!”
Baada ya hayo, wazazi wa Mariam wakatoka nje ya chumba kile na kuwaacha Madaktari wakiendelea kumtibu Mariam.
******
“Karibuni sana, sijui mnamuhitaji nani?” Ilikuwa sauti ya Mayasa ambayo ilitokea puani huku ikiwa na sifa zote za ushangingi.
“Mwenye nyumba!” Mama yake na Mariam akasema kwa sauti tulivu sana.
“Hivi nyie ni kina nani?”
“Siyo kazi yako binti, nahitaji kuonana na mwenye nyumba!” Mama Mariam akasisitiza.
“Unajua nawashangaa sana, haiwezekani nyie mkawa wageni wa hapa halafu mnashindwa kujua kuwa mimi ndiyo mama mwenye nyumba!” Mayasa akasema kwa nyodo za wazi kabisa.
Ilikuwa kauli kali ambayo ilimnyomnyong’onyesha sana mama Mariam na mumewe.
“Sikiliza binti, tunahitaji kuonana na Tom!” Baba Mariam akasema kwa sauti ya ukali.
“Oh! Tom, sasa mtaingia ndani au nimuite hapa nje?”
“Mwite huku nje, tutazungumza naye hapa hapa!”
“Nimwambie ni akina nani?”
“Wageni wake wa kibiashara!”
“Ok!” Mayasa akaondoka na muda mfupi baadaye, Tom akaja akiwa ameongozana na Mayasa.
“Mnataka nini kwangu?” Tom akauliza kwa ukali sana.
“Unasemaje?” Baba yake Mariam akauliza kwa sauti iliyojaa mshangao mkubwa.
“Kwani masikio yako umeweka pamba? Kwanza ondokeni kwangu, sina muda wa kupoteza kuzungumza na nyie, mnanipotezea muda wangu wa kustarehe na mpenzi wangu!”
“We’ Tom umechanganyikiwa? Hujui kuwa sisi ni wakwe zako? Tumekuletea taarifa muhimu, mwenzako amelazwa Muhimbili!”
“Mwenzangu ndiyo nani?”
“Mariam!”
“Mariam siyo mwenzagu, siwezi kuishi na mwanamke kama yeye, mwenzangu ni Mayasa! Huyu mnayemuona hapa ndiye mke wangu ambaye ninampenda kuliko kitu chochote katika maisha yangu, sihitaji kusikia habari nyingine tofauti na Mayasa wangu. Nawaomba mtoke kwangu!” Tom alisema maneno hayo huku akibamiza geti na kufunga kwa komeo.
Mama Mariam na mumewe wakabaki wanaangaliana, machozi machoni mwao ndiyo faraja pekee ambayo ingewasaidia kwa wakati huo. Wakaangaliana kwa uchungu, wakasogeleana kisha wakakumbatiana na kuanza kulia. Walishindwa kuelewa ni mkosi wa aina gani uliompata binti yao.
“Binti yetu wa pekee Mariam, kwanini anapatwa na balaa kubwa kiasi hiki, kwanini lakini?!” Baba yake na Mariam alisema huku machozi yakilowanisha shingo ya mkewe aliyekuwa amelala kifuani mwake.
“Lakini naamini siyo Tom, yupo aliye nyuma ya akili zake, ni shetani pekee ndiye anayemsumbua!”
“Mungu adhihirishe utukufu wake!”
“Amen!” Wakatoka kwa pamoja wakiwa wameshikana mikono, wakalifuata gari lao, wakaingia na kuondoka taratibu. Msaada pekee uliobakia ulikuwa ni Mungu pekee.



Beyond Love- 29

Huko wanakutana na balaa juu ya balaa, wanaambulia matusi na kufukuzwa kama mbwa! Mfariji wao pekee aliyebakia anakuwa ni machozi! Kilio kinatawala! Machozi matupu. Je, nini kitatokea? SONGA NAYO...

Haikuwa rahisi kugundua kwamba kwa muda wote wa robo saa Dk. Joseph Kisanga aliuokuwa akiutumia kuzungumza na Mariam, alikuwa akizungumza mwenyewe! Dk. Kisanga alikuwa akizungumza kwa sauti ya taratibu, ukimya wa hali ya juu ukiwa umetawala na akihakikisha kwamba Mariama anarejea katika hali yake ya kawaida, lakini kumbe akili ya Mariam haikuwa pale!
Mapenzi yake kwa Tom ndiyo yaliyokuwa akilini mwake na siyo ushauri wa Dk. Kisanga ambao kwake ulikuwa sawa na porojo zisizo na maana yoyote. Kilikuwa chumba kimya, chenye mwanga hafifu, lakini kilichokuwa na hewa ya kutosha iliyozalishwa kwa mashine maalumu ya kisasa.
Mariam akiwa ameketi kwa mtindo wa kutazamana na Dk. Kisanga ambaye ni Mtaalamu wa Magonjwa ya Afya ya Akili na Mshauri wa Mambo ya Saikolojia na Maisha katika ofisi yake hii ambayo siku zote huwa ni tulivu sana akiwashauri watu wengi hasa waliokata tamaa. Ni Dk. Kisanga ndiye aliyemsaidia mzee Mallya, mfanyabiashara wa maarufu jijini Dar es Salaam, aliyetaka kujiua baada ya bohari lake la kuhifadhia mizigo muhimu kuungua na kumsababishia hasara ya mamilioni ya pesa!
Dk. Kisanga pia ndiye aliyemshauri msanii maarufu Bisongi ambaye aliathiriwa na dawa za kulevya lakini baada ya kuzungumza naye akimpa ushauri, akakubali kuacha na kubadilika kabisa! Naam. Dk. Kisanga ni mshauri maarufu ambaye amejizolea umaarufu mkubwa sana katika kutoa ushauri na kubadilisha maisha ya watu!
Hali ilikuwa tofauti sana kwa upande wa Mariam. Ilimchukua muda mrefu sana Dk. Kisanga kugundua kwamba muda wote huo alikuwa akizungumza peke yake.
“Mariam bila shaka tupo pamoja!” Dk. Kisanga akasema akimtizama Mariam usoni.
Mariam alikuwa kimya.
“Mariam...Mariam...we, Mariam...!” Dk. Kisanga akamwita kwa mara nyingine.
“Abee Dokta!”
“Mbona kama haupo hapa?”
“Tupo pamoja!”
“Unakumbuka nilizungumza nini mara ya mwisho?”
“Ndiyo!”
“Nilisemaje?”
“Ah! Dokta...nakuelewa vizuri sana!”
“Hapana lazima unisikilize vizuri Mariam, maisha yako yana thamani kubwa sana, hutakiwi kuyapa mapenzi kipaumbele zaidi kuliko maisha yako. Ni kweli mapenzi yana umuhimu mkubwa sana katika maisha yako lakini maisha yako yana thamani zaidi kuliko hayo mapenzi ambayo kwasasa yamekuwa tatizo kubwa kwako....” Dk. Kisanga aliendelea kumshauri Mariam kwa muda mrefu sana, akijitahidi kuzungumza naye kwa upole huku akihakikisha hali ya afya yake inarudi kuwa nzuri.
Mariam alionekana kumsikiliza Dk. Kisanga kwa makini sana, lakini kilichokuwa kikifanyika kilikuwa ni sawa na mchezo wa kuigiza, kwani alionekana kumsikiliza kwa umakini mkubwa lakini ndani ya moyo wake kulikuwa na kitu tofauti kabisa, moyoni mwa Mariam kulikuwa na maandishi makubwa yaliyosomeka; TOM! Ni yeye tu ndiye aliyekuwa wimbo moyoni mwake.
“Nimekuelewa Dk. Kisanga, nashukuru sana kwa kubadilisha maisha yangu, naamini sasa nimekuwa mpya na nitahakikisha natulia na kuishi maisha yangu bila matatizo wala kumuwaza Tom!” Mariam alisema kwa utulivu sana.
“Nimefurahi sana kusikia hivyo, amini kila kitu hupangwa na Mungu, hivyo ni wajibu kuhakikisha yeye anakuwa nguzo yako namba moja katika maisha yako. Nimefurahi sana Mariam, naona sasa unaweza kurudi nyumbani, hakikisha unafika hapa hospitalini kuonana na mimi kila mwezi hadi hali yako itakapokaa sawa.”
“Hakuna tabu Dokta, nashukuru sana!”
“Ahsante!”
Siku hiyo hiyo Mariam aliruhusiwa kurudi nyumbani akiwa ameonekana kuwa na nafuu kubwa. Wazazi wake walifika hospitalini na kumchukua kwenda naye nyumbani. Walikuwa na matumaini makubwa sana ya mwanao kuwa mpya, walimwamini sana Dk. Kisanga kutokana na uwezo wake mkubwa wa kushauri.
“Vipi mama, unajisikiaje sasa?!” Mama yake na Mariam alimwuliza akiwa anatizama usoni.
“Nina nafuu sasa mama!”
“Kweli?”
“Ndiyo mama.”
“Kwahiyo unataka kutuambia kwamba, sasa hivi hali yako imetengemaa.”  Baba yake akadakia.
Mariam hakuwa na jibu!
Alitulia kimya bila kuzungumza chochote, ni jambo lililowashtua sana, hawakutarajia kama mwanawo angekaa kimya kwa muda mrefu kiasi kile, hasa kutokana na ukweli kwamba alikuwa akionyesha ushirikiano wa kutosha kuanzia mwanzoni.
“Vipi mbona umenyamaza?”
“Kuna tatizo baba!”
“Tatizo? Tatizo gani tena, si umesema unaendelea vizuri mwanangu?”
“Baba bado mawazo juu ya Tom yananisumbua na kuna jambo ambalo ni bora kama ningelifanya ili kuepukana na haya matatizo.”
“Ni nini?”
“Nahitaji kuwa mbali na Dar es Salaam, mbali na Tom, mbali na Mayasa, mbali na Vyombo vya Habari. Sihitaji kusikia wala kujua chochote kinachohusiana na Tom, nimechoshwa na mambo yake, nataka kutulia sasa.” Mariam akasema huku akilia kwa uchungu.
“Mwanangu huwezi kuwakimbia watu na hata kama unaweza, utawakimbia hadi lini?” Mama yake akadakia.
“Naweza mama, inawezekana kabisa kuwakimbia, sina jinsi zaidi ya kuondoka hapa Dar es Salaam!”
“Uende wapi sasa, uende wapi mwanangu?” Baba yake akadakia.
“Nitakwenda kwa bibi!”
“Yupi?”
“Wa Morogoro, acha niende nikapumzike Matombo!”
“Lini?”
“Kesho!”
“Mbona haraka sana?”
“Kesho ni siku nzuri sana kwangu, acha nianze kujiandaa!”
******
Mapenzi ya Tom na Mayasa yalizidi kupamba moto, Tom akawa hashikiki wala hakamatiki, kila kitu ilikuwa ni Mayasa. Tayari alishamkabidhi kila kitu katika maisha yake. Siri zote za kibiashara alikuwa ameshampa, namba zote za siri za kadi zake za benki Mayasa alikuwa anazijua.
Tom alikuwa amechanganyikiwa! Penzi la Mayasa lilimchanganya sana kiasi kwamba, alikuwa kama chizi mwenye akili timamu! Hata yeye mwenyewe alishindwa kuelewa ni mapenzi ya aina gani yaliyokuwa na nguvu kiasi kile. Hata hivyo alipuuza na kuamini kwamba alikuwa akimpenda sana Mayasa na hapakuwa na kitu kingine zaidi ya hicho.
Kwa upande wa Mayasa ilikuwa tofauti sana, hata siku moja hakuwahi kuhisi kumpenda Tom, hilo hata yeye mwenyewe alilikiri moyoni mwake. Kama alikuwa akimpenda, basi ni kwasababu ya pesa alizokuwa nazo. Aifurahia kuishi maisha mazuri, huku akisiamia miradi mbalimbali ya Tom iliyokuwa jijini Dar es Salaam na mikoani. Mayasa alikuwa ni kila kitu.
Mara nyingi alikuwa akikutana na marafiki zake na kuzungumza nao juu ya mambo mbalimbali ya kimaisha, siku zote walishindwa kuelewa ni kwanini Tom alimpenda kiasi kile. Siku zote aliishia kuwaambia kwamba mapenzi yake ya kweli ndiyo nguzo kubwa inayomfanya aendelee kufaidi maisha mazuri kwa Tom.
“Shosti sema ukweli bwana, lazima kuna kitu kipo nyuma ya pazia!” Rukia, mmoja wa marafiki zake alimwuliza Mayasa.
“Zaidi ya penzi langu, nini kingine?”
“Sema shoga yetu na sisi tuwatulize wapenzi wetu, haiwezekani Papaa Bill mpaka anafikia hatua ya kumuacha mkewe kama hakuna kitu kingine nyuma ya pazia!”
“Aaaah! Bwana...kikubwa ni utaalamu kitandani...haya inatosha sana shoga zangu, nendeni mkajifunze mambo ya kitandani....tehe...tehe...tehe....” Mayasa alisema akicheka.
“Lakini ni vizuri ukatuambia ukweli bwana!”
“Sina ukweli mwingine zaidi ya huo...” Mayasa akazidi kusisitiza. Hakuwa tayari kutoa siri zake za ndani kiasi kile.
“Sawa shoga yetu lakini nina ushauri mzuri sana kwa ajili yako. Huwezi kuwa mjinga kiasi hicho, Papaa Bill ana pesa nyingi sana na tayari anakuamini kwa kiasi kikubwa, lakini kama hutakuwa makini, unaweza kuachana naye ukawa huna kitu!”
“Kwahiyo?”
“Lazima ufanye kitu fulani, uwe tajiri!”
“Kitu gani hicho shosti yangu?”
“KAMA UNATAKA UTAJIRI WA TOM, HUNA BUDI KUWA NA ROHO NGUMU! UNACHOTAKIWA WEWE KUFANYA NI KUMPOTEZA!”
“Kumpoteza? Unamaanisha nini?”
“PAPAA BILL ANATAKIWA AFE!” Rukia akambia Mayasa ambaye alikuwa kimya sana akiwasikiliza.
Lilionekana wazo lililomchanganya sana akili yake, alitumia kimya kwa muda mrefu sana bila kuzungumza kitu, lakini baadaye akafungua kinywa chake na kuzungumza; “Wazo lako ni zuri sana, lakini sasa nitamuuaje? Na watu wakijua?” Mayasa akasema akitetemeka kwa hofu.
“Acha ujinga Mayasa, wewe  ni mtoto wa mjini, kama ni kweli unataka utajiri wa Papaa Bill lazima umwondoe duniani, kama upo tayari sema nikupe njia nzuri ambazo zitakuwa katika mazingira ya usiri mkubwa, yeye afe akuache na utajiri wako!”
“Nipo tayari, nakusikiliza!”



Beyond Love- 30

Wakati yote hayo yakitokea, rafiki wa karibu wa Mayasa aliyeitwa Rukia anamshauri amwondoe Tom duniani ili aweze kumiliki mali zote, kikiwemo kiwanda cha madini cha Tom Minerals Ltd. Je, atafanikiwa? Nini kitatokea katika maisha ya Mariam? SONGA NAYO mwenyewe...

Pamoja na ushauri wa kitaalamu alioupata kutoka kwa Dk. Joseph Kisanga, bado Mariam hakuwa katika hali yake ya kawaida. Hata yeye mwenyewe alijishangaa, hapakuwa na kitu kingine akilini mwake zaidi ya Tom. Aliamini pasingetokea mwanaume atakayempenda kwa mapenzi yake yote kama ilivyokuwa kwa Tom!
Kwake Tom alikuwa ni kila kitu! Kilichomuumiza zaidi ni majibu ya wazazi wake, kwamba Tom aliwafukuza nyumbani kwake mbele ya mwanamke wake Mayasa, hilo lilimuumiza sana.
Hakika isingewezekana Mariam, akavumilia kumuona Tom akiendelea kutesa na Mayasa wake, mbele ya macho yake. Pengine angejifungia ndani, lakini bado angeweza kumuona kwenye magazeti na hata kwenye luninga akiwa katika shughuli mbalimbali za kijamii.
Tom asingekwepeka kirahisi! Kitu pekee kilichokuwa mbele yake ilikuwa ni lazima Mariam aondoke Dar es Salaam, aende mbali, kijijini, nje ya mji kusipokuwa na Teknolojia ya Mawasiliano kabisa. Hiyo ndiyo njia pekee ambayo Mariam alikuwa nayo.
“Ni bora niondoke, nihame kabisa, sina sababu ya kuendelea kuteseka, pengine ilikuwa lazima niteseke, niumie, nikose amani, lakini haya yote naamini Mungu wa mbinguni anaona na atanipigania kwa kila hali ili niweze kushindana na haya majaribu,” Mariam alimwambia mama yake kwa uchungu, muda mfupi kabla ya kuingia kwenye basi, eneo la Kituo Kikuu cha Mabasi ya Mikoani, Ubungo jijini Dar es Salaam.
“Usijali mwanangu, hakuna lenye mwanzo linalokosa mwisho, safiri salama mama, msalimie bibi yako. Hakikisha unatuliza akili yako mama, huna sababu ya kumfikiria mtu mbaya kama Tom tena katika maisha yako, fungua ukurasa mpya sasa mwanangu!”
“Nashukuru sana mama!”
“Usijali, lakini bado kuna kitu ambacho ni muhimu sana ukifahamu mwanangu!”
“Kitu gani mama?”
“Maombi! Unatakiwa uombe sana mwanangu, msaada pekee kwa sasa ambao upo mbele yako ni kuwa karibu na Mungu! Ukiweza kutimiza hilo itakuwa rahisi sana kushinda majaribu yaliyopo mbele yako.”
“Ahsante sana mama kwa ushauri wako, nafikiri unanijua vizuri sana kuhusu hilo mama yangu, nitakuwa karibu sana na Mungu wangu kwa kila kitu mama...nakuahidi na itakuwa hivyo kweli!”
“Nimefurahi sana, nakutakia safari njema!”
“Ahsante sana mama!”
“Halafu kitu kingine mwanangu, lazima ujue kwamba wewe bado ni mzuri sana, naamini kuna wanaume wengi ambao wanahitaji angalau kunywa soda na wewe, kwahiyo huna haja ya kuhuzunika sana!” Mama yake Mariam alisema akitabasamu.
Mariam naye akatabasamu, tabasamu la ushindi! Ulikuwa ushindi mkubwa sana kwa mama yake na Mariam, tangu alipoamka asubuhi, hakuwahi kumuona mwanaye akitabasamu, lakini tabasamu lake la muda ule, tena la ghafla lilikuwa faraja kubwa sana kwa mama Mariam, sasa alikuwa ana imani kwamba ufumbuzi umepatikana.
“Nafikiri umenielewa mwanangu!” Tabasamu la mama yake na Mariam, sasa liliongezeka.
“Mama, kwa utani na wewe!!!”
“Siyo utani mwanangu, wewe ni binti yangu na sina sababu ya kukutania, ninachokuambia ni kitu cha ukweli ambacho hata wewe utakidhibitisha, kama utaamua kutulia!”
“Ahsante mama, ahsante sana mama yangu kwa kuona uzuri wangu, lakini uzuri huu mama, ulikuwa kwa ajili ya Tom!”
“Tom?!” Mama Mariam akauliza akiwa ameukunja uso wake.
“Ndiyo mama, Tom!”
“Ndiyo hakutaki sasa mwanangu!”
“Najua siyo yeye!”
“Ni nani?”
“Shetani!”
“Hata kama ni shetani, ndiyo ampe nafasi kubwa kiasi kile? Wakati mwingine shetani huwa anakaribishwa na mtu mwenyewe, na ndivyo alivyofanya Tom, yeye ameamua kumkaribisha shetani, unafikiri kwanini asimchezee kama yeye mwenyewe amemruhusu?”
“Usiseme hivyo mama!”
“Kumbe niseme nini Mariam, niseme nini?”
“Tunatakiwa kumuombea, naamini kwa kufanya hivyo siku moja atabadilika, niamini mama!”
Mama Mariam hakujibu kitu zaidi ya kumtulizia macho mwanaye, macho ambayo hayakuweza kuficha hasira na chuki za wazi alizokuwa nazo dhidi ya Tom.
“Naomba kukuuliza kitu mama!”
“Uliza!”
“Unamwamini Mungu?”
“Ndiyo, hata yeye anajua hilo!”
“Vizuri, nina swali lingine!”
“Uliza!”
“Kuna mahali popote ambapo Mungu amewahi kushindwa?”
“Hapana, yeye ni mshindi siku zote!”
“Basi ataendelea kuwa mshindi hata katika hili linalonisumbua na kunitesa mama!”
“Aaaamen!”
“Kwahiyo bado naendelea kukuomba umuombee!”
“Nitamuombea!”
“Nimefurahi kusikia hivyo, nimefurahi pia kwa wewe kuwa upande wangu. Nakupenda sana mama...nakupenda sana!”
“Nakupenda pia mwanangu mpenzi, nakutakia safari njema!”
“Ahsante mama!” Baada ya hapo mama Mariam aliondoka kwani dakika moja tu, baadaye basi liliondoka kituoni na safari ya kwenda Morogoro ikaanza.
Mariam aliweza kuwa macho hadi alipofika Kibaha tu, baada ya hapo alisinzia kabla ya kupitiwa na usingizi mzito. Hakujua Chalinze walipita muda gani, hata gari lilipoingia kwenye mizani eneo la Mikese hakujua, alishtuliwa na abiria aliyekuwa ameketi naye siti moja gari lilipokuwa likiingia katika katika Kituo cha Mabasi cha Msamvu.
“Tumefika sister amka!” Kijana huyo akamwambia akimtingisha.
“Mmmmh!” Mariam akaitikia akionekana kuwa na usingizi.
“Tumefika, inaonekana umechoka sana!”
“Ah! Ni kawaida, siku zote huwa napenda kulala nikiwa safarini!”
“Unashukia hapa?”
“Hapana, nitakwenda kushukia mjini!”
“Sawa basi, mimi nashuka hapa!” Baada ya abiria waliokuwa wakishukia pale Msamvu kuisha, gari likaondoka na kuingia katikati ya Mji ya Morogoro likawashusha abiria wote, eneo la Masika.
Mariam akanyoosha moja kwa moja akifuata barabara iliyokuwa ikielekea katika Kituo cha Daladala kilichokuwa kituo cha zamani cha mabasi yanayokwenda mikoani. Kwa bahati nzuri akapata gari la kwenda kwao, tena lililokuwa likikaribia kuondoka. Akaketi siti ya dirishani akiwa mkimya sana.
Muda mfupi baadaye safari ya kwenda Matombo ikaanza. Matombo siyo mbali sana kutokea Morogoro mjini, lakini kwasababu ya ubovu wa barabara na milima, ilimchukua saa mbili na nusu Mariam kufika kijijini kwao. Aliposhuka kituoni akakodisha baiskeli ambayo ilimpeleka nyumbani kwa bibi yake, katikati ya mashamba na mapori makubwa, mwendo ambao uliwachukua saa nzima na nusu njiani.
Hatimaye Mariam alifika akiwa amechoka sana, bibi yake alipomuona alimkimbilia na kumkumbatia kwa furaha. Hata hivyo alishangazwa sana na hali ya afya yake ilivyokuwa imezorota! Baada ya salamu, bibi alianza kuuliza habari za mjini.
“Wazee hawajambo?”
“Wazima kabisa bibi, wanakusalimia sana!”
“Nimefurahi sana kusikia hivyo....enheee, vipi wewe na mwenzako?”
Mariam hakuweza kujibu kitu, ni kama alikuwa amechomwa na chuma chenye moto katikati ya kidonda kibichi! Machozi yakaanza kumiminika machoni mwake. Akaanza kulia kwa sauti ya chini.
“Vipi, mbona unalia tena?”
Mariam hakujibu zaidi ya kuendelea kulia, tena safari hii alilia kwa sauti kubwa zaidi ya awali.
“Sema basi mjukuu wangu, kuna nini? Au amepata matatizo? Niambie mimi ni bibi yako, nitakusaidia!” Kauli hiyo ya bibi yake ilizidi kumchoma Mariam ambaye sasa alizidisha kilio chake.
Kazi aliyokuwa nayo bibi yake, ilikuwa moja tu, kumbembeleza!
*******
Kwa muda mfupi sana, roho ya Mayasa ilibadilika! Roho yake ilikuwa mbaya kuliko hata ya muuza sumu! Mayasa alikuwa na roho mbaya kuliko kawaida, hata yeye mwenyewe alijishangaa na alishindwa kuelewa roho hiyo ya paka alipoipata.
Macho yake mawili yalikuwa yamemuelekea Rukia ambaye kwa mwonekano wake wa nje, haikuwa rahisi kuamini kwamba anaweza kumshawishi mtu aondoe uhai wa mtu mwingine kirahisi kiasi kile. Tamaa ya mali ilimvaa, heshima na umaarufu ulikuwa umemtawala moyoni mwake. Alikuwa tayari kwa lolote.
“Ni kweli upo tayari?” Rukia akamwuliza akimkazia macho.
“Nipo tayari kwa moyo wangu wote!”
“Sawa, sasa ipo njia, lakini lazima uwe makini sana!”
“Nimeshasema nipo tayari kwa lolote!”
“Hatutaki utusaliti Mayasa!”
“Ni kitu ambacho hakiwezi kutokea.”
“Tom anatakiwa kufa, ndani ya mwezi huu, hatutakiwi kuwa na haraka, unachotakiwa kufanya kwa sasa ni kuongeza mapenzi yako kwa nguvu, mchanganye kimapenzi sana, toka naye mara nyingi, jamii ione mapenzi yenu na ikiwezekana wadaku waandike, baada ya hapo kazi itafanyika kiulaini kabisa!”
“Sawa kabisa...” kila mmoja alimuunga mkono.
“Lakini nina wasiwasi na jambo moja!” Mayasa akasema akitetemeka, hakuweza kuificha hofu yake.
Rukia akamkata jicho la chuki lililojaa mashaka, kwa ilivyoonekana, kama Mayasa angeongea jambo lolote kupingana na uamuzi wake wa awali, basi hatari ambayo ingekuwa mbele yake asingeisahau hadi atakapoingia kaburini!




Beyond Love- 31

Mariam anaamua uamuzi mpya, anakwenda kuishi kijijini Matombo, Morogoro, kwa bibi yake kwa nia ya kukaa mbali na Tom pamoja na vyombo  vya habari. Hakutaka kusikia kabisa habari za Tom. Wakati hayo yote yakitokea, shetani wa pesa anamwingia Mayasa, anapanga mipango ya kumuua Tom ili aweze kurithi mali zote!
Je, atafanikiwa? Vipi maisha ya Mariam huko kijijini Matombo? SONGA NAYO....
K
uulizwa habari za Tom, ilikuwa ni sawa na kumchoma kwa msumari wenye moto, katikati ya kidonda kibichi kilichokuwa moyoni mwake. Alitegemea kuulizwa na bibi yake juu ya Tom, lakini siyo mapema kiasi kile. Hata kama asingeulizwa, lazima angesema, kwani ndiyo sababu hasa iliyomfanya awe kule kijijini.
Moyo wa Mariam ulimuuma sana, alishindwa kuelewa ni mapenzi ya aina gani aliyokuwa kwa Tom, aliumizwa zaidi na jinsi alivyokuwa akimpenda kwa moyo wake mtu ambaye hakuonyesha kushtuka kabisa na penzi lake. Bibi yake alikuwa amemtonesha!
“Nyamaza mjukuu wangu, lakini lazima unieleze ukweli wa kilichotokea!” Baada ya Mariam kutulia, bibi yake akamwambia.
“Bibi kuna matatizo!”
“Ni nini?”
“Tom bibi, Tom ameniacha!”
“Amekuacha?””
“Ndiyo bibi!”
“Sababu?”
“Hakuna!”
“Haiwezekani, lazima kuna kitu umemuudhi mwenzako, lakini wazee wameshindwa kumaliza huko nyumbani?”
“Walikwenda kwake lakini walifukuzwa na Tom na mwanamke wake!”
“Mwanamke wake? Unataka kusema kwamba Tom ana mwanamke mwingine?”
“Tena anaishi naye pale nyumbani, mimi nilikuwa nalala chumba cha wageni, baada ya kuchoshwa na mambo yao, ndiyo nikaondoka kwenda nyumbani, huko napo ndiyo....” Mariam akamsimulia bibi yake kila kitu, hadi alipofikia hatua ya kulazwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.
“Pole sana mjukuu wangu, wewe baki hapa nyumbani, pumzika kwanza, utulize akili yako, mambo mengine yatafuata baadaye, naamini hali yako itarudi kuwa nzuri. Hapa utakula kambale na mboga za majani na afya yako itarudi kama zamani, sawa mama?!” Bibi yake akamwambia kwa sauti iliyojaa mapenzi mazito.
“Ahsante bibi, nimefurahi sana, umenifurahisha sana kwakweli, naanza kujiona mpya sasa.”
“Kama ndivyo kweli, basi Mungu wa Mbinguni ashukuriwe!”
“Amen!”
Maisha yaliendelea kijijini kama kawaida, Mariam akiwa anamsaidia bibi yake kazi za kilimo. Aliyafurahia mno maisha ya pale kijijini, kwani kama alivyotarajia awali, hapakuwa na mawasiliano ya aina yoyote, kitu ambacho ndiyo haswa alikuwa akikitegemea.
Afya yake ikaanza kurejea taratibu hadi ilipotengemaa kabisa, wazazi wake kila walipokwenda kumtembelea walikuta mabadiliko! Furaha ikarudi katika maisha yake. Ingawa ilikuwa kazi ngumu sana, lakini alijishangaa aliwezaje kumsahau Tom, mwanaume ambaye kwake alikuwa sawa na Wimbo wa Taifa!
Alifurahishwa sana na mabadiliko yake, kwa bahati nzuri bibi yake alishajua kwamba kutaja jina la Tom ni sawa na kuchochea matatizo aliyokuwa nayo, hivyo hakuthubutu kutaja jina la Tom katika mazungumzo yao. Siku zote alikuwa akimfundisha maisha ya kijijini na jinsi wazee wa zamani walivyoweza kuishi maisha marefu kijijini kutokana na aina ya vyakula wanavyokula.
“Kwahiyo bibi, unataka kuniambia kwamba hata mimi sasa nitaishi maisha marefu kwasababu nipo huku?”
“Bila shaka mjukuu wangu!”
“Lakini bibi ukiachana na vyakula, ni nini kingine kilichowafanya wazee wa zamani waishi miaka mingi zaidi kuliko hivi sasa?”
“Mazingira pia yanachangia, unajua Mariam, huku kijijini kila kitu ni cha asili. Hakuna kuvuta moshi wa dizeli wala petroli, hakuna mionzi ya minara ya simu, moshi wa viwandani wala dawa zenye kemikali, hizi ni sababu kubwa sana zilizowafanya wazee wa zamani waishi umri mrefu!”
“Sasa naanza kuelewa!”
Mariam alikubali maisha mapya, akajifunza vitu vipya kila siku. Hakika aliyafurahia maisha ya kijijini. Aliona ni bora kuishi maisha yale kijijini, kuliko kuishi Dar es Salaam lakini akiumizwa na kukosa amani ya kuendelea na maisha. Maisha ya kijijini yalikuwa chaguo lake la kweli na hakuwahi kuyajutia.
********
Kitendo cha Mayasa kusema kuna jambo lililompa wasiwasi, kilitoa tafsiri tofauti kwa Rukia. Msichana huyu ni katili na siku zote hakupenda kabisa msaliti katika mipango yake. Alimwangalia Mayasa kwa jicho la hasira akisubiria azungumze jambo lolote ambalo ni kinyume na makubaliano yao ili amuadhibu.
Mayasa akawaangalia wote kwa zamu, kisha akatingisha kichwa kama anayesikitishwa na jambo ambalo angelitamka.
“Una nini?”
“Nimeshasema kwamba kuna jambo linanitatiza kidogo!”
“Sema ni nini?”
“Hivi Rukia, askari hawawezi kujua kweli?”
“Labda uwaambie wewe, tena naomba nikuambie jambo moja, sina muda wa kupoteza zaidi juu ya jambo hili...ni hivi, leo jioni tutakutana katika kikao cha siri na vijana tutakaowapa kazi hii!”
“Ni wapi?”
“Mbezi!”
*******
Kilikuwa chumba kidogo, lakini nadhifu na kinachovutia, kikiwa na uwezo wa kuhudumia watu ishirini kwa wakati mmoja. Ndani ya chumba hicho kilichokuwa na kiyoyozi, kulikuwa na watu sita waliokutana katika kikao cha siri usiku huo.
Watu hao walikuwa ni Rukia, Mayasa na vijana wanne ambao walikuwa maalumu kwa kukodiwa kwa ajili ya kufanya mauaji. Wote walikuwa kimya, vinywani mwao, ukitoka moshi mzito wa sigara ambao wakati mwingine walikuwa wakiutolea puani na masikioni! Baada ya ukimya wa muda kupita, Rukia aligonga meza kwa nguvu!
“Tumekutana hapa kwa kazi moja muhimu iliyopo mbele yetu, kama nilivyotangulia kusema awali, Papaa Bill anatakiwa aondoke duniani, tena ndani ya mwezi huu! Malipo yenu ni mazuri sana na leo mtapata malipo ya utangulizi!” Alisema Rukia, akiwatazama wote kwa zamu.
“Hakuna tabu sister Rukia, nafikiri unatuamini katika michongo hii, sisi hatuna noma, tupeni cash, tufanye kazi!”
“Hakuna shida, suala la pesa siyo tatizo kwangu, chukueni hizi kwanza na ninaomba baada ya wiki mbili Papaa Bill awe na jina lingine! Marehemu nadhani ni jina litakalomfaa zaidi!” Mayasa alisema akitoa shilingi milioni tano kama fedha za utangulizi na kuwapatia wale vijana.
“Hakuna tabu, tunakuhakikishia kazi nzuri baada ya huo muda uliosema.” Mmoja wao ambaye ndiye aliyepokea zile fedha alisema.
“Kilichobaki ni utekelezaji tu!” Mayasa akasema.
“Kuhusu hilo, usijali kabisa, hawa vijana nawaaminia!” Rukia akasema.
“Sawa, tutaona!” Kikao kikaahirishwa.
******
Alichokifanya Mayasa ni kuwa karibu zaidi na mume wake kuliko kipindi kingine chochote walipokuwa wakiishi  na Tom. Alijifanya kumpenda zaidi, kuwa karibu naye zaidi kuliko kawaida. Tom akafurahi sana, akazidi kumpa siri zake za biashara akiamini alikuwa mke mwema wa maisha yake.
Hakujua kilichokuwa nyuma ya pazia, laiti kama angejua alikuwa katika hatari ya kufa wakati wowote, angeachana naye haraka sana, lakini jambo hilo hakulijua kwani lilikuwa siri kubwa sana. Maisha yaliendelea kama kawaida, Mayasa akiendelea kuwasiliana kwa karibu na vijana waliopewa kazi ya kumuua Tom na kuelekezekana kila kitu kwa hatua.
“Nadhani sasa kila kitu kipo tayari, mnaweza kukamilisha hiyo kazi!”
“Poa sister, ungependa iwe lini?”
“Kesho usiku, miye nitakuwa nyumbani, halafu nyie mtamtegea jirani na nyumbani mpaka atakapoingia, lakini muda wake mara nyingi ni saa mbili na madakika hivi, lakini haifiki saa tatu!”
“Umesomoka!”
Siku iliyofuata, kuanzia saa moja na nusu jioni, nyumba ya Tom ilikuwa imezungukwa na vijana sita wenye silaha, wakisubiria muda atakaorudi! Kama kawaida yake, saa mbili na robo alikuwa getini akipiga honi mfululizo  ili afunguliwe lakini cha ajabu hakuna aliyetokea kumfungulia!
“Shiiit! Huyu mwanamke vipi, kwanini hanifungulii, ngoja nishuke nikagonge mwenyewe!” Tom akasema akifungua mlango wa mbele ili atoke, lakini kabla hajafanya hivyo akashangaa akihisi kitu cha baridi kikigusa shingoni mwake.
“Tulia hivyo hivyo, nyoosha mikono yako juu na ufuate maagizo yote tutakayokuambia!” Alisikia sauti ya mtu ikimuamrisha nyuma yake.
“Kuna nini tena jamani?”
“Hatubishani, lakini kama utaleta ubishi wa aina yoyote nakulipua sasa hivi!”
Sekunde chache baadaye, Tom alikuwa amezungukwa na watu sita waliokuwa wanaonekana dhahiri kuwa ni watu wa mazoezi. Alishajua kwamba kifo chake kilikuwa kimekaribia! Isingekuwa rahisi akubali kufa kijinga kiasi kile, alitakiwa kufanya jambo fulani ili aokoe roho yake.
“Jamani kama ni pesa au kitu chochote cha thamani mnataka, niambieni niwape lakini mniachie roho yangu, nawaombeni sana!”
“Hatuna shida na pesa zako!”
“Sasa kumbe mnataka nini jamani?!” Tom akasema akitetemeka kwa woga.
“Tunahitaji roho yako!”
“Roho yangu?”
“Ndiyo, unatakiwa kufa Tom!” Tom akachanganyikiwa zaidi.
“Sikilizeni ndugu zangu, mnajua...” hakupewa nafasi ya kumalizia sentesi yake.
“Hivi kwanini tunamkawiza?”
“Mlipue!” Mwingine akadakia.
Hakuna aliyezungumza tena baada ya hapo, muda mfupi baadaye ulisikika mlio wa risasi. Wale vijana wakatoweka na kumuacha Tom akiwa ameanguka chini hoi, damu zikimvuja mwilini. Tom alikuwa hajitambui!


Beyond Love- 32

Alipopona akaamua kwenda kupumzika kwa bibi yake, Matombo, Morogoro. Huko nyuma, Mayasa anapanga mauaji ya Tom. Siku ya tukio Tom alishangaa anapiga honi lakini hafunguliwi, alipoamua kushuka ili akagonge geti, ndipo alipokutana na mdomo wa bastola na kuwekwa chini ya ulinzi! Sekunde chache baadaye, Tom alikuwa chini, akivuja damu baada ya kupigwa risasi!
Je, nini kitatokea? SONGA NAYO....

M
lio wa risasi ulisikika mara tatu, lakini baada ya hapo muungurumo wa gari ukasikika. Hiyo ilimaanisha tayari wauaji walikuwa wameshatoweka eneo la tukio. Ndani ya dakika tatu tu, watu walikuwa wamejaa getini mwa nyumba ya Tom wakishuhudia Tom alikiwa hajigusi chini, huku damu zikimtoka kwa wigi!
“Mume wangu oh! Mume wangu jamani...” Mayasa naye alitoka nje na kuanza kulia, akamlalia Tom, huku akisikilizia mapigo yake ya moyo kuhakikisha kwamba alikuwa amekufa au lah!
“Nitabaki na nani miye...Tom wangu jamani...” Mayasa alizidi kupiga kelele.
Watu walimuonea huruma sana, walijua ni kaisi gani alikuwa anaumia kutokana na matatizo aliyopata mumewe. Hakuna aliyejua kwamba yote aliyokuwa akiyafanya ilikuwa ni maigizo tu! Siri hiyo aliijua yeye mwenyewe.
“Lakini wezi gani wa mapema hivi?’ Mtu mmoja aliyekuwa kwenye tukio lile aliuliza.
“Hata mimi nashangaa...” mwingine akadakia.
“Mnashangazwa na nini jamani, kama watu wanaiba kwenye benki mchana inashindikana vipi kwa muda huu?”
“Lakini mbona hawajachukua kitu?”
“Hata mimi nashangaa!”
Kila mmoja alikuwa anaongea lake, lakini wengi walishangazwa sana na majambazi hao, ambao hawakuiba kitu chcohote zaidi ya kumdhuru Tom na kuondoka zao. Ilionekana kuwepo kwa kitu kilichojificha, kitu ambacho hakuna ambaye alikuwa anakijua.
Muda mfupi baadaye watu walijadiliana na kuamua kumkimbiza Tom katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili. Akalazwa kwa ajili ya kupatiwa matibabu. Muda wote huo Mayasa alikuwa analia sana, alionyesha huzuni kubwa, lakini moyoni mwake alikuwa akitamani sana Tom afe, hilo ndilo lililokuwa akilini mwake.
Kilichoonekana usoni mwa Mayasa kilikuwa tofauti kabisa na kilichokuwa moyoni mwake. Mayasa alikuwa na roho mbaya  kuliko hata ya muuza sumu! Aliweka mbele masilahi yake baada ya kifo cha Tom.
“Samahani Dokta naweza kumuona mume wangu?”
“Hapana, yupo kwenye uangalizi maalum kwa sasa, tafadhali nenda urudi kesho asubuhi!”
“Lakini atapona?”
“Tumuombe Mungu, tutajitahidi kufanya kila tutakaloweza, lakini nguvu za Mungu ndizo zinazohitajika zaidi katika hili.”
“Ahsante sana Dokta.”
*****
Kilikuwa chumba kidogo, kizuri, chenye hewa safi ya kiyoyozi, ndani ya chumba hicho kulikuwa na vijana wanne na wasichana watatu, hiyo ndiyo ilikuwa Kamati nzima ya mauaji ya Tom. Wote walikuwa kimya, wakimtizama Rukia ambaye alikuwa ndiye Kiongozi wa Kamati hiyo. Rukia akapiga meza kwa nguvu!
“Nina furaha sana, nina furaha kwasababu kazi ambayo tuliwatuma, mmeikamilisha ingawa siyo kwa kiasi kikubwa!” Rukia alianza kuzungumza.
“Samahani sister!” Mmoja wa vijana wale akasema.
“Nakusikiliza!”
“Kwanini unasema siyo kwa kiasi kikubwa?”
“Acha wasiwasi kijana, nimesema siyo kwa kiwango kikubwa kwakuwa hajafa lakini nafikiri Mayasa atakuwa na majibu mazuri juu ya hilo kwakuwa yeye ndiye aliyeenda naye hospitalini!”
“Ni kweli Rukia, hali yake siyo nzuri, hana dalili za kupona kabisa, hadi sasa hivi hajazinduka, naona lazima atakufa tu!”
“Ni kweli kabisa!”
“Na hilo ndiyo lengo letu.”
“Kikubwa zaidi kilichotukutanisha hapa ni kuwalipa pesa zenu zilizobakia, lakini kama tukihitaji msaada wenu baadaye tutawajulisha na tafadhali mtoe ushirikiano.”
“Hakuna tabu sister Rukia.”
“Sawa.. Mayasa...” Rukia akaita.
“Nakusikiliza.”
“Wapatie mzigo wao uliobakia.”
Mayasa hakuwa na kitu cha kuzungumza zaidi ya kuchukua fedha kwenye pochi yake na kuwakabidhi.
“Tunashukuru sana kwa msaada wenu, lakini lazima jambo hili liwe siri,” Mayasa akasema.
“Siyo tu, siri bali kama tutaisikia mahali popote, basi mjue kuwa kifo kitakuwa jirani zaidi na nyie!”
“Kuhusu hilo huna sababu ya kuwa na wasiwasi nalo, kwani ni kazi ya kwanza tunafanya na wewe?”
“Lakini watu wanabadilika!”
‘Watakuwepo ila siyo sisi!”
“Nimefurahi kusikia hivyo!” Baada ya hapo kikao kikaahirishwa.
Siku iliyofuata, asubuhi na mapema Mayasa alikuwa ameshafika hospitalini, alikuwa makini sana na Tom, akihakikisha anamhudumia kwa karibu, lakini nia yake ya moyoni ilikuwa ni Tom afe, alichukia sana kumuona Tom akiwa bado anaendelea kuwa hai, ingawa alikuwa anapumua kwa msaada wa mashine.
Aliendelea kuwa karibu na Tom siku zote, hakuna aliyejua kilichokuwa akilini mwa Mayasa, kilichokuwa kikifanyika ilikuwa ni mchezo wa kuigiza tu, siri ambayo aliitunza moyoni mwake.
Wiki moja baadaye hakuona sababu ya kuendelea kumficha mama yake Tom juu ya hali ya mwanaye. Akafanya mawasiliano haraka, ambapo siku iliyofuata mama Tom alikuwa ameshafika Dar es Salaam, akipokelewa na Mayasa. Siku zote mama yake Tom, hakuwa akimpenda Mayasa, lakini kwasababu alishamuomba sana mwanaye aachane naye na akakataa, hakuwa na sababu ya kuendelea kuingilia mapenzi yao.
“Enhee vipi hali yake?” Mama Tom aliuliza mara baada ya kufika nyumbani na kuketi sofani.
“Pumzika kwanza mama!”
“Hapana, lazima nijue hali ya mwanangu!”
“Hana hali mbaya sana mama, lakini kesho asubuhi tutaongozana pamoja kwenda kumtizama, ila nimewasiliana na daktari wake amesema hali yake sasa siyo mbaya sana!”
“Fahamu zake zimesharudi?”
“Bado, lakini ana nafuu kubwa!”
Mama Tom alimpenda sana mwanaye, hakuwa tayari kumuona anakufa akiwa mdogo kiasi kile, kwa maisha ya shida ambayo amekulia, aliamini alipaswa kuendelea kuwa hai ili ale matunda ya jasho lake.
Kila alipokumbuka siku aliyotoka kwenye mgodi unaotitia akiwa na madini kwenye mfuko wake wa salufeti, alitokwa machozi. Kwake Tom alitakiwa aendelee kuyafaidi maisha! Kufa mapema kiasi kile ilikuwa ni pigo kubwa sana kwake. Mayasa alipata kazi ya kumbembeleza mama Tom, ambaye hakunyamaza mpaka sauti ilipoanza kukauka ndipo akanyamza na kupitiwa na usingizi.
Yeye ndiye aliyemwamsha Mayasa asubuhi, akimkumbusha kuwahi hospitani kumwona Tom. Walipoingia wodini na mama Tom kumuona mwanaye akiwa amefungwa mashine za kupumua, alichanganyikiwa! Tom alikuwa na hali mbaya sana na hadi wakati huo alikuwa hajitambui!
Ghafla mama Tom akaanza kuhisi kizunguzungu kikali, mwili wake ukaanza kupoteza nguvu taratibu, kisha akaanguka chini kama mzigo! Muda huo huo akakimbizwa wodini na kuanza kushughulikiwa. Hata hivyo hali yake ilizidi kuwa mbaya, usiku wa siku ile ile, mama Tom alifariki dunia!
“Pole sana dada, mgonjwa ni nani wako?” Daktari aliyekuwa akimhudumia alimwuliza Mayasa akifikiria jinsi ya kumweleza juu ya kifo cha mama huyo.
“Mama mkwe wangu, kwani vipi?”
“Kwa bahati mbaya sana, ameshafariki dunia!”
“Unasema?”
“Usijali ni mambo ya kawaida ambayo unapaswa kukubaliana nayo, hata kama ukilia, machozi yako hayataweza kumrudisha mama duniani, zaidi utakuwa unajiumiza mwenyewe.”
“Lakini kwanini inakuwa kwangu, nina mkosi gani mimi jamani! Mume wangu amelazwa na mpaka sasa hivi hajarejewa na fahamu, mama naye amefariki, nitakuwa mgeni wa nani mimi?”
“Usijali dada yangu, kubaliana na hali halisi, hatuwezi kubadilisha kilichotokea, zaidi unapaswa kumshukuru Mungu maana ameagiza tushukuru kwa kila jambo.”
“Ahsante sana Dokta, nashukuru. Acha nikawapashe habari ndugu zetu na kuandaa taratibu za mazishi.” Mayasa akasema na kuondoka.
“Sawa.”
Mayasa aliondoka akiwa na mawazo mengi sana kichwani mwake, hakuona sababu ya kuendelea kuishi nyumbani kwa Tom, alishachuma mali za kutosha kwa kipindi kifupi sana ambacho Tom alikuwa amelazwa hospitalini. Aliweza kufanya hivyo kwasababu Tom alikuwa akiweka mambo yake wazi.
Alishachukua fedha katika akaunti zote na kuziacha nyeupe kabisa, madini yaliyokuwa yakihifadhiwa chumbani nayo aliyachukua na kuyauza. Hakurudi tena hospitalini kumuangalia Tom wala kuuchukua mwili wa mama mkwe wake kwa ajili ya mazishi.
Wiki moja baadaye, kila kitu kilikuwa tayari na kilichokuwa mbele yake ilikuwa ni kuondoka nchini, kwenda zake kujichimbia Uingereza. Hilo ndilo lililofanyika, Mayasa akapanda ndege na kwenda zake Uingereza, akiwa hajui kabisa kilichoendelea huku nyuma.
******
Maisha ya kijijini Matombo, yalianza kumzoea Mariam, kama ilivyokuwa nia yake, kujitenga mbali na mji ili asiweze kujua habari zinazomhusu Tom na Mayasa. Alifurahia sana kuishi kijijini na aliyapenda maisha ya kule. Hata afya yake ilianza kuridhisha. Siku moja alitumwa na bibi yake mjini. Alipokuwa akikatiza eneo la Nunge akaona meza ya magazeti, hakutaka kuisogelea, maana alijua pengine angekutana na habari za Tom, jambo ambalo hakutaka litokee.
Katika hali ya kushangaza sana, akajikuta kuna kitu kinamlazimisha kwenda kwenye meza ile ya magazeti. Baadaye akaamua kwenda, akijipa moyo kwamba hata kama ataona habari zake, hazitamuuma sana kwasababu tayari ameshaanza kumzoea!
Magazeti karibu yote ya siku hiyo, yaliandika habari juu ya kifo cha mama yake Tom, Mariam alihisi kuchanganyikiwa! Macho yake yakatua juu ya gazeti la Ijumaa. Gazeti hilo lilikuwa limeandika kwa maandishi yaliyosomeka; ...wakati hali ya Papaa Bill ikizidi kuwa mbaya, MAMA YAKE MZAZI  AFARIKI DUNIA! Chini ya maneno hayo, kulikuwa na maneno mengine yaliyosomeka; Mwenyewe yupo hoi Muhimbili, bado hajapata fahamu, mkewe amkimbia...soma habari kamili uk. 2
Zilikuwa habari mbaya sana kwa Mariam, akajikuta akipoteza nguvu taratibu, giza totoro likaanza kupita mbele ya macho yake. Akaanguka chini na kupoteza fahamu.




Beyond Love- 33

Magazeti yote yaliandika, juu ya taarifa za kifo cha mama yake na Tom, huku Tom mwenyewe akiwa amelazwa! Mariam anapoteza fahamu.
Je, nini kitatokea? SONGA NAYO...


Alishaumia vya kutosha, alishateseka kiasi cha kutosha, aliamua kuishi kijijini Matombo ili asizidi kuteseka, alitaka kuwa mbali na maumivu ya mapenzi. Ni kweli alikuwa akimpenda sana Tom, hata moyo wake ulimhakikishia jambo hilo, lakini ilikuwa lazima awe mbali na matatizo!
Kumpenda mtu si tatizo, lakini kwa Mariam ilikuwa tatizo! Alikuwa na kila sababu ya kujitenga na matatizo. Hakutaka kuzidi kujipa mateso ambayo anaweza kuwa nayo mbali.
Mariam hakuwa na penzi la kinafiki, alikuwa na penzi la dhati ambalo siku zote lilikuwa hai, lakini hakutaka kumwaga machozi tena, hakutaka kuumia zaidi, lakini kwasababu tayari alishatambua kwamba moyo wake ulimpenda sana, akaona njia pekee ilikuwa ni kumkimbia!
Pengine ulikuwa uamuzi wa busara, lakini safari yake ya mjini ya siku hiyo, ilisababisha matatizo makubwa, ikatonesha kidonda kilichoanza kukauka. Mambo yakawa yale yale! Hakuweza kuvumilia kusoma habari za Tom akiwa amelazwa hospitalini, tena akiwa hana msaada wowote, mbaya zaidi mama mkwe wake akiwa amefariki! Hilo lilimuuma sana na kujikuta akianguka chini na kupoteza fahamu!
Hakuna aliyekuwa na taarifa za Mariam.
“Vipi jamani?!” Mmoja wa watu waliokuwa wamesimama mbele ya meza ile ya magazeti alisema.
“Siyo suala la kuuliza, kilichobaki hapa ni kumsaidia tu!”
“Lete gari bro,” jamaa mmoja alijitolea kumchukulia na teksi.
“Mshike huko...tusaidiane jamani...” watu wakasaidiana kumwingiza Mariam kwenye gari na safari ya kwenda Hospitali ya Mkoa wa Morogoro ikaanza.
Kutoka Nunge hadi Hospitali ya Mkoa, hapakuwa mbali, dakika tano tu tayari gari lilikuwa limeshaingia ndani ya Jengo la Hospitali hiyo. Walipofika mapokezi, waliruhusiwa kwenda moja kwa moja Chumba cha Mapumziko, akapokelewa vizuri na kuanzishiwa tiba haraka.
“Poleni sana jamani,” Dokta akawaambia wale watu waliompeleka Mariam hospitalini.
“Tunashukuru sana Dokta.”
“Nani anayehusika zaidi na huyu mgonjwa, nataka kufanya naye mazungumzo kidogo!”
“Kwakweli hakuna!”
“Hakuna?!”
“Ndiyo hakuna daktari!”
“Unamaanisha nini kusema hivyo, kwahiyo kati ya ninyi nyote hakuna ndugu wa huyu mgonjwa?”
“Hakuna!”
“Kivipi?!”
“Sisi ni wasamaria wema tu, ambao tumeamua kumsaidia baada ya kumuona ameanguka na kupoteza fahamu!”
“Ilikuwaje?”
“Kwakweli hatujui, lakini ilikuwa ni mbele ya meza ya magazeti!”
“Basi hakuna tabu, lakini mnaweza kujitolea pia kumsaidia malipo ya matibabu yake!”
“Hilo halina tabu.”
“Mungu akubariki kwa hilo, acha sisi tuendelee!”
“Sawa, sijui wewe ni dokta nani?”
“Naitwa Dk. Ringo, tena nilisahau kukufahamisha, sijui na wewe mwenzangu nani?”
“Naitwa Ramsey Muhando.”
“Nashukuru sana kukufahamu.”
“Nami pia.”
Kazi ya kumtibu Mariam ikaanza, huku gharama zote zikilipwa na Ramsey ambaye alijitolea.
******
“Sikiliza shoga yangu, mimi sijazoea mambo ya nuksi nyumbani kwangu, kama nilivyokuambia, mama yake Tom amefariki na sitaki kujihusisha na jambo lolote linalomuhusu yeye!” Mayasa alikuwa akimwambia Rukia katika kikao chao kilichofanyika usiku, ndani ya hoteli moja ya kifahari katikati ya Jiji la Dar es Salaam.
“Kwahiyo sasa utafanyaje?”
“Nawaachia watu wa Halmashauri ya Jiji wazike!”
“Lakini huoni kwamba mambo yanaweza kushtukiwa?”
“Kwanini?”
“Magazeti yameshaandika, halafu nyumbani hakuna msiba, unadhani utaelewekaje?”
“Kila kitu nimeshakamilisha, nimeshauza vitu vyote, fedha zilizokuwa benki pia nimekomba zote tena kwenye akaunti zake zote, kuna madini aliyokuwa akiyahifadhi ndani nayo nimeyachukua. Sina kinachonifanya niendelee kubaki kwenye ile nyumba, waache wenye moyo mwema watamzika, wakikosekana basi, bahati mbaya!”
“Safi sana, sasa vipi kuhusu mimi, naambulia nini?” Rukia akamwuliza Mayasa akiwa anamtizama kwa macho yenye kusubiria jambo fulani.
Mayasa hakumjibu kitu, zaidi ya kumwangalia kuanzia chini hadi juu, ni kama alikuwa akimchambua!
“Twende!” Mayasa akasema.
“Wapi? Mi’ nataka kujua changu!”
“Ndiyo maana nimekuambia twende!”
“Wapi sasa?”
“Nikakupe chako!”
“Ni nini?”
“Surprise!”
“Okay!” Wote kwa pamoja wakaondoka na kushuka chini ambapo walipanda kwenye gari la Mayasa na safari ya kwenda kusipojulikana ikaanza.
Rukia alikuwa kimya muda wote wa safari, akiwa hajui ni wapi hasa walipokuwa wakielekea, maswali tele kichwani mwake yalibaki yanazunguka. Baadaye gari likasimama nje ya geti jeusi, lenye nyumba moja nzuri sana. Mayasa akapiga honi mfululizo, mlango ukafunguliwa.
Wakaegesha gari kisha Mayasa akamshika mkono Rukia na kumtembeza kila kona ya nyumba ile. Ilikuwa nyumba ya kisasa iliyokuwa na kila kitu ndani, bwawa la kuogelea, gari ndogo ya kutembelea, samani ndani na bustani nzuri sana iliyokuwa nje.
“Sikiliza rafiki yangu...wewe ni rafiki yangu mpenzi, nakupenda na ninaheshimu sana msaada wako katika kufanikisha zoezi hili, kuanzia leo hii ni nyumba yako na kila kitu kilichomo ndani.
“Kwa bahati nzuri, hii nyumba nilijengewa na Tom mwenyewe, na hati zote zina majina yangu, kwahiyo usiwe na wasiwasi kabisa, hapa ni kwako na kila kilichomo ndani, kuanzia gari na samani zote, kuishi hapa au kuuza ni hiyari yako!” Mayasa akamwambia Rukia.
Rukia hakutegemea kama angepewa zawadi kubwa kiasi kile, kwanza alitumia muda mwingi kuwa kimya akijaribu kutafakari kama ni kweli kilichokuwa mbele yake kilikuwa yakini, Mayasa akampatia hati zote na kumtoa wasiwasi kwamba pale palikuwa ni nyumbani kwake na alikuwa na uhuru wa kufanya jambo lolote apendalo.
“Ahsante sana Mayasa shoga yangu, huu ndiyo urafiki wa kweli, ni wachache sana wanaweza  kuwa kama wewe!”
“Usijali...sasa sijui utaishi hapa au utauza?”
“Nitauza, siwezi kuishi hapa!”
Ndivyo ilivyokuwa, siku iliyofuata nyumba ilitafutiwa mteja wa chapchap, ikauzwa kwa bei ya kutupwa! Jioni ya siku hiyo hiyo, Mayasa akaondoka kwenda zake Uingereza. Hakutaka kuendelea kuishi Tanzania tena, haikuwa sehemu salama kwake!
Hadi wiki moja baada ya mama yake Tom kufariki bila kutokea kwa ndugu yeyote, mwili huo ulichukuliwa na Halmashauri ya Jiji na kwenda kuzikwa. Kama kawaida, magazeti yaliripoti kila kitu, haikueleweka ni wapi Mayasa, mwanamke aliyekuwa akiishi naye baada ya Tom kumuacha mkewe Mariam, alipokwenda.
Kwakuwa hapakuwa na ndugu mwingine yeyote, mambo yaliendelea kuwa giza nene, mwenye majibu alikuwa ni Tom ambaye kwa wakati huo ni kama alikuwa nusu-mfu!
*******
“Toooom....Toom...Tooom, usife, bado nakupenda, bado nakuhitaji Tom wangu usife...” Ndiyo maneno aliyozungumza Mariam baada ya kuzinduka siku tatu baadaye katika Hospitali ya Mkoa wa Morogoro alipokuwa amelazwa.
“Vipi dada yangu, naomba utulie kwanza...tulia...” Ilikuwa sauti ya muuguzi ambaye alimwita mwenzake mara moja, ambapo alimuagiza akamwite dokta haraka.
“Afadhali amezinduka, vipi dada unaendeleaje sasa?” Dokta akamwuliza akiwa anamtizama usoni.
Mariam hakuwa na la kuongea, alianza kushangaa hadi aliporudisha fahamu vizuri, hapo ndipo Daktari alipomsimulia kila kitu. Bahati nzuri, Ramsey mmoja wa watu walioshuhudia tukio la yeye  kuanguka, ambaye ndiye aliyekuwa akigharamia matibabu yake, akatokea. Alifurahi sana kumkuta katika hali nzuri. Akamsimulia kila kitu kilichotokea, Mariam naye hakuficha chochote kuhusu Papaa Bill ‘Tom’. Alizungumza kila ukweli unaohusu uhusiano wake na Tom. Historia yake ilihuzunisha sana, haikuwa rahisi kuamini kama msichana mdogo kama yeye aliwahi kupitia historia ngumu kiasi kile.
“Pole sana dada yangu, sasa nafikiri ni vyema nikurudishe nyumbani ukapumzike kwanza!” Ramsey akasema.
“Wapi?”
“Matombo, kwa bibi yako.”
“Haiwezekani!”
“Kwanini?”
“Sitaki!”
“Unataka kwenda wapi?’
“Kama ni kweli unataka kunisaidia, kwasasa nataka kwenda Muhimbili kuonana na Tom, pili kushughulikia mazishi ya mama mkwe wangu! Nampenda sana mama...nampenda, najua alikuwa akitamani sana niishi na mwanaye, lakini Tom alimpuuza mama yake. Lazima nionyeshe mapenzi yangu kwake hata kama amekufa!”
“Sawa nitakusaidia, lakini lazima hali yako itengemae kidogo!”
“Sawa!”
Siku tatu baadaye, hali ya Mariam ilipokuwa nzuri akaruhusiwa kutoka Hospitalini. Kama Ramsey alivyoahidi ndivyo alivyofanya, alifika Hospitalini akiwa amemnunulia nguo mpya na viatu. Mariam akaoga na kubadili nguo zake kisha wakaondoka na kwenda Msamvu ambapo walipanda basi la Hood kwa safari ya kwenda Dar es Salaam.
Safari ilikuwa ndefu sana kwa Mariam, lakini hatimaye walifika Ubungo, Ramsey akakodi teksi iliyowafikisha Muhimbili. Kutokana na umaarufu wa Tom ‘Papaa Bill’, haikuwa kazi kubwa kufahamu wodi aliyokuwa amelazwa. Ramsey na Mariam wakaongozana hadi kwenye kitanda cha Tom.
Mariam hakuamini macho yake, Tom alikuwa amelala kimya kitandani huku akipumua kwa kutumia mashine. Tom alikuwa hajitambui! Mariam akaanza kulia, hadi muuguzi alipofika eneo hilo na kumwita ofisini kwake.
“Vipi dada, wewe ni ndugu yake na Papaa Bill?”
“Ndiyo!”
“Nani wake?”
“Mume wangu.”
“Mumeo?
“Ndiyo!”
“Wewe ndiye Mariam, tunayekusoma kwenye magazeti?”
“Ndiyo!”
‘Pole sana mdogo wangu, una moyo wa peke yako kwakweli!”
“Ahsante sana sister, vipi maiti ya mama Tom? Nataka kushughulikia taratibu za mazishi!”
“Pole sana, ni juzi tu alizikwa na Halmashauri ya Jiji baada ya ndugu zake kutoonekana!”
“What?!” Mariam alitamka maneno hayo, macho yakimtoka.
Hakuwa tayari kuamini alichosikia.






Beyond Love- 34

Huko anakutana na habari za kusikitisha sana, anakuta mama yake Tom, ameshazikwa na Halmashauri ya Jiji, huku hali ya Tom ikiwa mbaya sana. Mariam anachanganyikiwa.
Je, nini kitatokea? Kwanini Ramsey ameamua kumsaidia Mariam kwa karibu? SONGA NAYO...

M
arehemu mama Tom alikuwa akimpenda sana Mariam, alimpenda kwa mapenzi yake yote. Alimfahamu vizuri sana Mariam, wema wake ulikuwa mkubwa sana, alikumbuka kila kitu alichokuwa akikifanya kwa ajili ya marehemu mume wake.
Alijua yote hayo yalifanyika kutokana na mapenzi ya kweli aliyokuwa nayo kwa mwanaye! Hilo pekee lilimfanya ajitahidi kumshauri mwanaye kwa kila hali aachane na wazo la kutoishi na Mariam. Alishazungumza sana, alionyesha kila dalili ya kuchukizwa na vitendo vya Tom, lakini kijana wake hakubadilika!
Pamoja na kwamba Mariam aliamua kwenda kujificha kijijini Matombo kwa ajili ya kukaa mbali na Tom, lakini hakuwa akimchukia mama yake! Siku alipoona habari kwenye gazeti la Ijumaa kuwa amefariki dunia, aliona fadhila aliyokuwa akitakiwa kufanya ni kumzika mama huyo kwa heshima!
Pengine angeumia sana baada ya kukuta amezikwa na jambo pekee ambalo lingefuata ingekuwa ni kwenda kutizama kaburi lake na kusoma dua pembeni ya kaburi lake, lakini sasa ndoto hizo zimezimika kama mshumaa!
Mama Tom amezikwa na Halmashauri ya Jiji, ni jambo ambalo lilimuumiza sana moyo wake. Machozi kama maji yakazidi kumiminika machoni mwake.
“Nyamaza Mariam, huna sababu ya kulia dada yangu, shukuru kwa kila jambo!” Ramsey, msamaria mwema aliyemsadia kuanzia Morogoro alimwambia.
“Siyo rahisi Ramsey, ni vigumu sana  kaka yangu!”
“Kwanini....kubali kilichotokea, unajua hakuna kitakachobadilishwa na machozi yako!”
“Najua, lakini naamini machozi yangu yatakuwa yanaonyesha kujali kwangu!”
“Kwa mtu aliyekufa?”
“Ndiyo!”
“Ndiyo nasikia kwako...lakini Mariam, nyamaza kulia, huna sababu ya kulia kiasi hicho, utakuwa unajiumiza tu mdogo wangu!” Nesi naye akamwambia Mariam.
“Ahsante!”
“Pole sana!”
“Nashukuru!” Sasa Mariam akatulia kidogo.
Ramsey akamwangalia Mariam aliyekuwa akiendelea kutokwa na machozi mepesi, akachukua kitambaa chake na kumfuta machozi.
“Kwahiyo Sister ni nani anayemuuguza Tom kwa sasa?”
“Papaa Bill?”
“Ndiyo!”
“Hakuna mtu yeyote anayemhudumia, yupo peke yake!”
“Hali yake?”
“Kama ulivyomuona, hali yake siyo nzuri na amepoteza fahamu tangu siku aliyoletwa hapa!”
“Nini zaidi kinachomsumbua?”
“Kwani Mariam ulikuwa wapi hadi usijue yote hayo?”
“Acha tu dada’ngu, ni stori ndefu lakini fahamu kwamba sijui chochote kinachoendelea, nitakusimulia baadaye, lakini nafikiri ni vyema ukanieleza.”
“Alivamiwa na majambazi na kumpiga risasi, kwa bahati mbaya amepooza kuanzia shingoni kushuka chini, mbaya zaidi hajapata fahamu na anapumua kwa msaada wa mashine!”
“Mungu wangu!”
“Usijali Mariam, maadam unajua kuna Mungu, basi huyo ndiye msaada pekee uliobakia kwa sasa!”
“Nitaendelea kumuomba yeye siku zote!”
“Amen!”
“Sasa Mariam, kwahiyo utakuwa ukimuuguza Tom siyo?”
“Ndiyo, lazima nifanye hivyo!”
“Vizuri sana!”
Baada ya hayo, Ramsey na Mariam wakarudi tena wodini kumuangalia Tom, bado hakuwa amefumbua macho, hali yake ilikuwa mbaya sana. Mariam akamsogelea na kumbusu mashavuni mwake, kisha akamshika Ramsey mkono na kuondoka naye.
“Tunakwenda wapi?” Mariam akamwuliza Ramsey.
“Unamaanisha nini?”
“Namaanisha tunapokwenda!”
“Mariam kwani hujui nyumbani kwangu ni Morogoro?”
“Najua!”
“Sasa?”
“Nilikuwa nataka kujua kama unakwenda huko!”
“Ndiyo jibu lake!”
“Ramsey nashukuru sana kwa msaada wako, napenda kukuambia wazi kwamba wewe ni binadamu kamili, mwenye utu na unayetambua thamani ya ubinadamu. Mungu akubariki sana kwa hilo, lakini nilikuwa na ombi lingine!”
“Nini?”
“Sitaki kwenda nyumbani leo, nahitaji kulala hotelini kwa wiki nzima, unaweza kunisaidia fedha za kulipia pango na chakula kwa muda huo?”
“Hilo linawezekana, lakini kwanini hutaki kwenda nyumbani?”
“Nataka akili yangu ipumzike kidogo kwanza, nina mawazo mengi sana Ramsey!”
“Usijali lakini sioni kama ni busara kukuacha peke yako katika kipindi hiki kigumu, nafikiri tutafute hoteli kisha nitalipia vyumba viwili, niendelee kukupa kampani zaidi au unaonaje?”
“Sawa!” Ndivyo ilivyokuwa, wakaongozana hadi katika hoteli moja nzuri iliyopo Magomeni, wakalipia na kuingia ndani.
*****
Magazeti yote ya siku iliyofuata yalikuwa yamepambwa na habari ya Mariam kuonekana Muhimbili. Yaliandika habari ile kwa undani sana tena yakiwa na picha mbalimbali zinazomwonyesha Mariam akilia wodini na nyingine akimbusu Tom aliyekuwa amelala hoi kitandani!
Walielezea kitendo kile kuwa ni cha kijasiri na kwamba Mariam alikuwa na penzi la kweli. Habari hizo ziliwafikia wazazi wa Mariam ambao walikasirika sana. Kwanza walishindwa kuelewa ni kwanini mtoto wao alikuwa anaendelea kumsaidia Tom, mwanaume ambaye alimtesa, mbaya zaidi aliwatukana hata wao!
“Unaona mama Mariam, huyu mtoto ana akili kweli?”
“Sijui amempa nini mwanangu huyu Tom? Huyo mwanamke aliyemuona anafaa, amemkimbia na nasikia ameuza kila kitu, sasa kipindi cha matatizo ndiyo Mariam awe msaada kwake, haiwezekani!”
“Haiwezekani kabisa!”
“Sasa tutafanyaje?”
“Kilichopo hapa ni kwenda Muhimbili hadi kwenye wodi aliyolazwa, lazima tutamwona Mariam!” Wazo hilo liliungwa mkono na wote wawili ambapo waliingia kwenye gari na kwenda moja kwa moja Muhimbili.
Walipofika wakaingia katika wodi aliyolazwa Tom, kama walivyokuwa wakitarajia ndivyo ilivyokuwa. Walimkuta Mariam akimhudumia Tom, machozi mengi yakimtoka. Mama yake Mariam alipomuona mwanaye alikuwa na hasira sana, akamfuata na kumvuta pembeni uso wake ukiwa na makunyazi.
“Hivi we’ mtoto umelogwa? Una akili kweli? Kwani huyu hana ndugu, hana marafiki? Mabaya yote aliyokufanyia huyaoni? Matusi aliyotutukana sisi wazazi wako hayakuuma?
“Umelazwa mara ngapi kwa ajili yake, lakini leo wewe ndiyo unakuwa wa kumsaidia..sasa sisi kama wazazi wako, tunakuambia toka haraka sana hapo,  unatakiwa tuongozane pamoja nyumbani!”
“Najua nyie ni wazazi wangu, najua kuwa mnanipenda, lakini lazima mzifahamu na kuheshimu hisia zangu. Mimi nampenda Tom kwa mapenzi yangu yote, siwezi kwenda na nyie nyumbani nikaamuacha Tom katika hali hii!”
“Unasemaje wewe mtoto, hivi una akili kweli wewe?” Baba yake Mariam akamwuliza kwa hasira sana.
“Akili ninazo tena nyingi sana, lakini penzi langu kwa Tom litaendelea kudumu siku zote za maisha yangu!”
“Sasa kama hujatoka kwenye tumbo langu mimi mama yako, endelea kubaki hapa hospitalini, lakini kama mimi ni mama yako, niliyekuzaa, urudi mwenyewe nyumbani!” Mama Mariam akasema kwa sauti ya ukali sana, kisha akamshika mumewe mkono na kutoka nje.
Baba Mariam alikuwa na hasira sana, hakuweza kuongea neno lolote zaidi ya kuwa msikilizaji! Baadaye Mariam naye alitoka kwa hasira, akachukua taxi na kwenda hotelini.
******
Mariam alipofika hotelini, aliingia chumbani kwake akiwa amechanganyikiwa sana. Kila alichokifanya aliona kama anakosea! Mawazo mengi yalimchanya kichwani.
Zaidi ya kufikiria kuhusu wazazi wake ambao walikuwa wanamzuia kumhudumia Tom, lakini pia aliumizwa na wema wa Ramsey. Hakutaka maumivu tena baadaye, alianza kuhisi kwamba Ramsey angehitaji kulipwa fadhila.
Hapo ndipo alipoamua kumpigia simu Ramsey, hakutaka kubaki na mawazo kichwani mwake. Akachukua mkonge wa simu, kisha akabonyeza namba za chumbani kwa Ramsey, simu ikaanza kuita, baadaye ikapokelewa na sauti tulivu sana ya Ramsey.
“Yes, Mariam hapa, naomba uje chumbani kwangu Ramsey!”
“Chumbani kwako?”  Ramsey akauliza kwa mshangao.
“Ndiyo!”
“Kuna nini?”
“Njoo tu!” Dakika mbili baadaye Ramsey alikuwa chumbani kwa Mariam akiwa amevaa bukta na fulana nyepesi, uso wake ukionyesha wazi wasiwasi aliokuwa nao.
“Kuna nini dada Mariam?”
“Nataka kujua kwanini unanifanyia yote haya?”
Ramsey hakuwa na jibu la haraka. Aliangalia juu, kisha akarudisha macho yake chini kabla ya kuyatuliza usoni mwa Mariam.
“Unasema?” Ramsey akauliza.
“Kwanini umekuwa mwema kwangu kwa kiasi kikubwa namna hii?”
Ramsey alikuwa kimya.







Beyond Love- 35

Huko anakutana na habari za kusikitisha sana! Anakuta mama yake Tom, ameshazikwa na Halmashauri ya Jiji huku hali ya Tom ikiwa mbaya sana. Anaamua kumhudumia Tom kwa moyo wote, lakini wazazi wake wanapingana naye, wakidai kuwa hakuwa mwanaume mwenye mapenzi ya kweli kwani alimtesa sana.
Mariam anaachana na wazazi wake na kurudi hotelini ambapo alikutana na Ramsey, anamlazimisha amwambie ni kwanini aliamua kumsaidia kwa kiwango kikuwa kiasi kile. Haijulikani nia ya yeye kuuliza swali hilo.
Je, nini kitaendelea?  SONGA NAYO...

Ramsey aliendelea kuwa kimya, katika siku ambazo alishangazwa sana na Mariam basi ni pamoja na siku ile. Swali aliloulizwa lilikuwa gumu sana, gumu kwa sababu hata mazingira ya swali lenyewe yalikuwa tata! Kuna wakati alianza kuwaza kwamba, inawezekana Mariam alikuwa akimtaka ndiyo maana akamwuliza swali lile kama mtego.
Macho ya Ramsey yalibaki usoni mwa Mariam kwa muda mrefu, akimtizama kwa makini na kumsoma uso wake kama ulifanana na aliyokuwa anayazungumza. Kwa kiasi kikubwa hakuweza kujua nia hasa ya Mariam ilikluwa nini kwani katika uso wake hapakuwa na kitu hata kimoja kilichoonekana kushabihiana na maneno yake.
Hakujua kama alikuwa anamtania au alikuwa anamwekea mitego! Ramsey akabaki anamwangalia Mariam bila kufungua kinywa chake kusema neno lolote. Sasa Ramsey akaamua kumwangalia Mariam kwa umakini zaidi, macho yake yalishuka hadi miguuni mwa Mariam, akaikagua.
Akayapandisha taratibu hadi kiunoni, hapo akakubali kwamba kweli Mariam alikuwa mwanamke mwenye mvuto wa kike! Akamwangalia macho yake ya mviringo ambayo yalikuwa pambo tosha katika chumba kile. Ramsey akahema kwa kasi, kisha akatizama “lips” za Mariam, hakika zilipendeza sana.
Lakini alikuwa na maswali yaliyomchanganya kichwani mwake, anaweza kuonekana mwenye tabasamu wakati alikuwa kwenye kipindi kigumu cha matatizo? Hilo lilizunguka ubongoni mwake bila kuwa na majibu ya moja kwa moja.
Kila kitu kilikuwa gizani. Maswali yote hayakuwa na majibu. Mariam ambaye muda wote alionekana kuwa kimya, sasa alifungua kinywa chake akionekana kuwa na jambo la msingi sana la kuzungumza naye. Akayatoa macho yake kwa kasi, kama alikuwa haoni vizuri, akameza fundo moja la mate ambayo bila shaka aliyakusanya kwa muda mrefu sana mdomoni mwake.
Akawa mtulivu sana, akaanza kuzungumza: “Nimekuuliza swali Ramsey!”
“Swali?”
“Ndiyo!”
“Mh!”
“Mbona unaguna?”
“Naguna sababu ya maneno yako Mariam!”
“Yanachekesha au hayana maana?”
“Siyo kwamba yanachekesha na wala siyo kwamba hayana maana.”
“Bali?”
“Nina wasiwasi na wewe.”
“Juu ya nini?”
“Ya ulipotoka, sijui kama umetoka sehemu salama.”
“Nini maana yako?”
“Siyo kawaida yako kuwa hivi Mariam, nahisi kuna tabia nyingine ambazo unazifanya ambazo mimi nilikuwa sizijui.”
“Kwanini unasema hivyo Ramsey?”
“Naweza kukuuliza kitu?”
“Uliza tu!”
“Unakunywa pombe?”
“Hapana.”
“Kweli?”
“Nakuhakikishia, kwani naonekana nimekunywa?”
“Hapana ila yanayotoka kinywani mwako ndiyo yanayosababisha nihisi hivyo.”
“Anyway...nisikilize Ramsey, tufanye hivi, mimi ni mnywaji wa pombe na leo nimekunywa. Halafu baada ya hapo jibu maswali yangu hata kama ni ya mlevi sawa?”
“Usiseme hivyo...”
“Sasa niseme nini? Inawezekana umesahau swali, nitakukumbusha...wewe ni kijana mzuri sana, ambaye roho yako inafanana na tabia yako! Nashukuru kwa hilo, lakini naamini una kazi nyingi za kufanya umeziacha na kuamua kunisaidia mimi katika kipindi hiki kigumu, je kwanini umeamua kufanya hivyo?” Mariam aliongea maneno hayo huku machozi yakimlengalenga machoni mwake.
“Mariam acha kulia, naomba ufahamu kitu kimoja, nimefanya yote hayo kwa sababu ya mapenzi tu, sina kitu kingine chochote ambacho kimenifanya nikaamua kukusaidia!”
“Unanipenda?”
“Ndiyo...kama dada yangu, rafiki yangu wa karibu lakini kubwa zaidi natimiza moja ya amri muhimu tulizopewa na Mungu, tuliagizwa tupendane Mariam, kwanini nisikusaidie kwa upendo huo?”
“Kweli?”
“Niamini!”
“Hakuna lingine?”
“Lipi tena?”
“Basi nashukuru sana kama ni kweli hakuna lingine zaidi ya hilo, umenifurahisha sana Ramsey.”
“Usijali.”
Wakaendelea kuzungumzia mambo mengine, hadi baadaye Ramsey alipoaga na kurudi chumbani mwake. Hata hivyo Ramsey aligundua kwamba lazima Mariam alikuwa na kitu kilichomchanganya hasa kutokana na maswali aliyokuwa akiuliza.
Jioni walikutana kwa ajili ya chakula cha jioni, baada ya kula Ramsey alishindwa kuvumilia kubaki na maswali mengi kichwani mwake, akaamua kumuuliza Mariam ili kupata ukweli. Mariam hakuona sababu ya kuficha jambo, akamweleza ukweli jinsi alivyokwaruzana na wazazi wake hadi kufikia hatua ya kuondoka wodini bila kuwepo kwa maelewano.
“Lakini wale ni wazazi wako Mariam, lazima uwasikilize!”
“Hujakosea Ramsey, lakini na wao hawawezi kunichangulia mtu nitakayeishi naye.”
“Ungewapa nafasi kwanza, hata kama unampenda huyo Tom kiasi gani lakini waliyokuambia yana maana, unampenda vipi mtu ambaye alikufukuza na kuwatukana wazazi wako?”
“Najua siyo yeye, ni yule shetani Mayasa niliyekupa habari zake.”
“Hata kama, lakini wazazi wako walikuwa na hoja ya msingi.”
“Sasa naona unataka kuniudhi,” Mariam akasema akionyesha hasira.
“Basi Mariam yaishe,” Ramsey akaamua kuwa mpole.
*******
Mariam akaendelea kumhudumia Tom kwa karibu sana, kila siku alikuwa akishinda Muhimbili na kurudi hotelini usiku. Hakutaka mpenzi wake apate shida, alikiri wazi kwamba hatatokea mwanaume ambaye atampenda kama alivyompenda Tom.
Tom alikuwa kila kitu kwake, alimkabidhi maisha yake yote, hakujali mateso na manyanyaso yote aliyompa. Imani kubwa aliyokuwa nayo moyoni mwake ni siku moja Tom angeamka na kuwa naye kama mke na mume maana Mayasa ambaye kwake alikuwa ni shetani alikuwa ameshatoroka.
Hakutaka kusikia kuhusu wazazi wake, aliamua kuishi maisha yake peke yake, huku mtu muhimu aliyekuwa mbele yake akiwa ni Tom pekee.
Siku moja Ramsey alimtoa Mariam na kwenda naye ufukweni, hiyo ni baada ya kumweleza alikuwa na mazungumzo ya muhimu sana ambayo yalihitaji sehemu iliyotulia ili aweze kumweleza vizuri jambo ambalo Mariam hakulipinga.
Wakiwa katika hoteli moja, ufukweni mwa Bahari ya Hindi, Mariam ndiye aliyeanzisha mazungumzo baada ya kuona Ramsey hazungumzi chochote.
“Enheee Ramsey, ulisema una mazungumzo muhimu na mimi, muda unazidi kwenda, naona ni bora ukaniambia.”
“Ni kweli, tena ni muhimu sana.”
“Nakusikiliza, bila shaka huu ndiyo muda muafaka.”
“Mariam nataka kukuambia jambo moja muhimu sana, muhimu kwako na kwangu, muhimu kwa maisha yako,” Ramsey alisema kwa sauti ya utulivu sana.
“Nakusikiliza Ramsey.”
“Nafikiri unakumbuka kuwa mimi ndiye niliyekuokota Morogoro na kukupeleka hospitalini kwa ajili ya matibabu!”
“Ndiyo nafahamu.”
“Pia mimi ndiye niliyekuleta Dar ba kukupeleka hadi hospitalini!”
“Ni kweli.”
“Kwamba mpaka sasa hivi mimi ndiye ninayegharamia mahitaji yote ya Tom na wewe.”
“Ndiyo!”
“Nimekufanyia mambo mengi sana ili kukufanya mwenye furaha!”
“Hilo halipingiki.”
“Unajua ni kwanini nimekufanyia yote haya?”
“Hilo litakuwa moyoni mwako.”
“Kipo kitu kilichonisukuma mimi kufanya yote hayo Mariam, kipo! Tangu nilipokuona siku ya kwanza, niliona kitu kwako Mariam, nakumbuka uliwahi kuniuliza sababu ya kukufanyia wema wote huu lakini nilikujibu jibu la uongo kwa sababu muda wa kukuambia haya ninayokuambia ulikuwa haujafika.
“Nisikilize kwa makini Mariam, wewe ni msichana mrembo sana, ambaye unahitaji matunzo, unatakiwa ukae mahali utulie ukila na kunywa kila unachokitaka. Hupaswi kuwa na huzuni wala mateso kama uliyonayo hivi sasa, hutakiwi kuwa na msiba mzito moyoni mwako kama ulionao sasa hivi. Urembo wako haufanani na matatizo uliyonayo. Mariam unatakiwa kubembelezwa!” Ramsey alipofika hapo alitulia kwa muda kisha akapeleka glasi yake ya maji ya matunda kinywani kabla ya kuanza tena kuzungumza.
“Mariam mimi nakupenda, tena nakupenda kwa mapenzi ya dhati kutoka moyoni mwangu, nipe nafasi nikuonyeshe raha za ulimwengu. Achana na yule mlemavu kule Muhimbili, kwanza inawezekana baada ya kupata fahamu akakufukuza, kwanini uumize moyo wako? Nipe nafasi nikuonyeshe ninavyokupenda Mariam,” Ramsey alizungumza kwa sauti ya upole sana, akiamini Mariam angemsikiliza.
“Umemaliza?” Mariam akamwuliza akivuta midomo.”
“Tayari...”
“Sikiliza....tena sikiliza kwa makini sana, hivyo vijimsaada vyako visiwe sababu ya kunitongoza. Mwili wangu una thamani sana, tena ni maalum kwa ajili ya mtu mmoja tu, Tom!  Huyo ambaye kwako wewe umeona ni mlemavu lakini kwangu ni mwanaume, tena mume wa ndoa. Kama umechoka kunisaidia, acha! Sikulazimishi, lakini mwili wangu, sahau!” Mariam akasema kwa kujiamini sana.
Ramsey akavimba kwa hasira, hakuzungumza neno lolote zaidi ya kusimama na kuanza kupiga hatua moja baada ya nyingine akimwacha Mariam mwenyewe ufukweni.
Mariam akafikiria kwa haraka, akaona giza nene lililokuwa mbele yake, kumuacha Ramsey aondoke kulimaanisha yeye kutokuwa na mahali pa kulala kuanzia siku hiyo, pia asingeweza kumuhudumia Tom wake, achilia chakula chake yeye mwenyewe.
Mariam akaanza kulia. Ramsey aliendelea kutembea bila kugeuka nyuma, akiwa amedhamiria kabisa kuondoka na kumwacha Mariam pale ufukweni. Mariam akasimama na kuanza kumkimbilia Ramsey huku akiita jina lake kwa sauti kubwa.
“Ramseeeeeeeyyyy.....” Mariam aliita kwa sauti kubwa sana.
Ramsey akageuka nyuma, akasimama akiwa tayari kumsikiliza Mariam, hakuhitaji kitu kingine chochote zaidi ya penzi lake, vinginevyo aliamua kucha kusaidia tena Mariam. 


Beyond Love- 36

Je, anataka kuwambia nini? Atakubali kumsaliti Tom wake? SONGA NAYO...

Ni kama alikuwa amewahi kukimbia mbio za marathon, lakini haikuwa hivyo. Mariam hakuwahi kufanya mazoezi ya riadha hata mara moja, lakini siku hiyo alikimbia kwa mwendo wa ajabu. Hata yeye alijishangaa.
Alimfikia Ramsey akiwa anahema kwa kasi ya ajabu, akasimama mbele yake huku akiwa ameyatoa macho yake kama alikuwa akikimbizwa na mnyama hatari. Ghafla macho yake yakaanza kupatwa na unyevunyevu, baadaye kidogo machozi yakaanza kumiminika machoni mwake.
“Nyamaza Mariam, nyamaza...kulia kwako hakutasaidia kitu kama...”
“Kama sitakuambia nakupenda pia...”
“Ndiyo Mariam, kwanini unataka kuutesa moyo wangu kiasi hiki? Ni nani ambaye angeweza kufanya yote haya kwa ajili yako? Ni mimi ninayekupenda pekee ndiye niwezaye kufanya mambo haya.
“Lakini sasa, unadhani unafanya vyema kufanyiwa yote haya kwa mapenzi halafu wewe ulipe mabaya? Angalia mara mbili Mariam,” Ramsey alikuwa akizungumza kwa sauti laini, taratibu na macho yake yakiwa yameganda usoni mwa Mariam aliyekuwa akilia wakati wote.
Mariam hakuzungumza kitu, alitulia kwa muda kabla ya kwenda kujilaza kifuani mwa Ramsey. Ramsey alisikia raha sana kusikia pumzi za Mariam zikitoka kwa shida akiwa amelala juu ya kifua chake.
“Najua unanipenda sana Ramsey, najua...nafahamu kwamba ulifanya yote yale kwa sababu ya mapenzi yako kwangu...lakini pia unatakiwa kufahamu kwamba sikuwa nafahamu haya mambo mpaka leo uliponiambia, sikujua kama ulikuwa na jambo hilo moyoni mwako.
“Nashukuru sana kwa kunipenda na kunipa nafasi ya kwanza moyoni mwako, lakini unatakiwa kufahamu kwamba moyo wangu una makovu, kama ni sumu nilipewa kali, yenye kuua na kukausha kabisa! Hali yangu siyo nzuri kihisia....
“Najisikia kumpenda mtu mmoja tu, Tom! Lakini wema unaonipa nashindwa kujua nitakulipa vipi? Najua ni kiasi gani unavyoumia juu ya penzi lako kwangu, lakini nitafanyaje?” Mariam aliongea kwa sauti iliyojaa kwikwi huku machozi yakimiminika mgongoni mwa Ramsey aliyekuwa kimya akimsikiliza kwa makini sana.
“Kipo kitu cha kufanya Mariam, kipo...”
“Nini?”
“Kunipenda!”
“Ingeweza kuwa rahisi kukupenda, lakini siyo kukupenda wewe tu, Ramsey hata mwanaume mwingine yeyote. Ni kweli wewe ni kijana mzuri sana unayevutia kwa kila kitu, lakini moyo wangu una sumu, hauwezi tena kumpenda mtu mwingine zaidi ya Tom.
“Tafadhali usiumizwe na kauli zangu, ni hisia za kweli zinazotoka moyoni mwangu, naomba uzipokee kama zilivyo, nakupenda kama kaka yangu lakini siyo kimapenzi.”
“Kama hunipendi Mariam?”
“Nakupenda sana, tena sana lakini siyo kimapenzi, labda kama utanisaidia katika hilo!”
“Kukusaidia nini?”
“Kukupenda!”
“Unamaanisha nini?”
“Nisaidie niweze kupenda tena, moyo wangu sijui una matatizo gani?”
“Una uhakika na kauli yako?”
“Ndiyo!”
“Kweli?”
“Ndiyo...mbona unaniuliza mara mbilimbili, kwani huniamini?”
“Nakuamini sana...”
“Sema nakupenda sana Ramsey!”
“Nakupenda sana Ramsey!”
“Hebu niangalie!” Ramsey akamwambia Mariam ambaye alijitoa kifuani mwake na kusimama mbele yake huku akiwa ameyatuliza macho yake kwa Ramsey.
Ramsey akatabasamu, Mariam naye akatabasamu pia.
“Unahisi nini?”
“Kukupenda!”
“Kwahiyo mimi sasa ni mpenzi wako siyo?”
“Ndiyo, lakini nitaomba msaada mwingine kutoka kwako!”
“Unahitaji kiasi gani cha pesa?”
“Siyo pesa Ramsey, sizungumzii pesa!”
“Bali nini?”
“Tom!”
“Tom? Ameingia vipi tena kwenye mazungumzo yetu?”
“Naomba uniruhusu niendelee kumsaidia mpaka atakapopona!”
“Akifa je?”
“Hiyo itakuwa mipango ya Mungu!”
“Ok, hakuna tatizo katika hilo.”
Wakasogeleana tena, wakakumbatiana kwa nguvu, wakaanza kupeana mvua ya mabusu motomoto. Wakafungua ukurasa wa mapenzi. Hapo sasa wakarudi tena ufukweni ambapo walicheza michezo ya kimahaba mpaka usiku waliporudi zao hotelini.
*******
Moyo wa Mariam ulikuwa na maumivu makali sana, alikubali machoni tu kuwa na Ramsey lakini moyoni hakuwa na hata chembe ya mapenzi kwake. Moyoni mwake kulikuwa na mtu mmoja, Tom. Hakuwahi na wala hakufikiria kuwa na mtu mwingine zaidi ya Tom.
Alikubali ili aweze kuendelea kupata misaada yake kwani asingeweza kumhudumia Tom akiwa hana fedha. Kumkubalia ulikuwa mtihani wa kwanza, lakini mtihani wa pili ambao ungekuwa mgumu zaidi kwake ni kufanya mapenzi na Ramsey.
Alijiapiza kukabiliana na hilo mpaka mwisho wa pumzi zake. Ni kweli hakuwa na mapenzi naye, lakini asingeshindwa kujifanya kuonyesha mapenzi yake kwa kila njia, lakini tatizo kubwa kwake likawa ni mapenzi, hakutaka kabisa kuruhusu mwili wake uguswe na mwanaume mwingine zaidi ya Tom wake.
Jioni walikuwa wanakula pamoja hotelini, Mariam akimlisha na kumbusu kila wakati, alionyesha kila dalili za wao kuwa wapenzi, ingawa Mariam alikuwa makini sana na kamera za waandishi wa habari hasa za waandishi wa magazeti ya udaku.
“Angalia bwana, haya maeneo siyo kabisa. Kuna mwandishi mmoja anaitwa Issa Mnally akituona tu, lazima atatupiga picha na utashangaa tumetoka kwenye gazeti la Risasi!”
“Issa Mnally?”
“Ndiyo...huyu ni mdaku balaa, hakuna asiyemjua hapa Bongo. Habari nyingi za Tom amekuwa akiziripoti yeye na kama siyo yeye basi ni Senchawa, hawa wadaku hawafai kabisa!”
“Usijali mpenzi wangu, tupo kwenye chimbo hapa hawawezi kutuona.”
“Lakini ni vyema tukichukua tahadhari.”
“Hakuna shida.”
Wakaendelea kula na kunywa kwa furaha hadi usiku kabisa, walipoamua kuondoka na kwenda vyumbani mwao kulala. Mariam aliingia chumbani kwake na Ramsey naye akaenda chumbani mwake. Muda mfupi baada ya Mariam kuingia chumbani kwake, simu ya mezani ikaita. Haraka akapokea akijua ni lazima angekuwa ni Ramsey.
“Vipi mpenzi wangu, si tumeachana muda huu tu,” Mariam alisema maneno hayo mara baada ya kupokea simu.
“Siyo shwari darling!”
“Kwanini?”
“Kuna baridi sana, siwezi kulala mwenyewe, nahitaji sana joto lako!”
“Lakini mbona bado mapema sana?”
“Mapema kupata joto lako? Mbona sikuelewi Mariam, naomba uje chumbani kwangu!”
“Sawa,” Mariam akajibu na kuamka haraka kisha akavaa na kwenda chumbani kwa Ramsey.
Hakutaka kumuudhi tena, lakini kikubwa ambacho kilikuwa akilini mwake ni kutomuachia kabisa mwili wake. Hilo alijihakikishia kabisa kwamba lilikuwa ndani ya uwezo wake. Akatoka nje, kisha akafunga mlango wake na kwenda chumbani kwa Ramsey.
“Karibu mpenzi wangu!”
“Ahsante sana!” Mariam akaingia na kwenda moja kwa moja kitandani.
Wakalala wakiwa wamekumbatiana. Katikati ya usiku, Mariam akiwa amelala fofofo, alisikia mikono laini ya Ramsey ikipita mwilini mwake. Mwanzoni alihisi alikuwa usingizini, lakini muda ulivyozidi kwenda ndivyo alivyogundua kwamba kila kilichokuwa kinatokea kilikuwa yakini!
Akashtuka zaidi alipogundua, Ramsey alikuwa ameshamvua nguo zake zote na alikuwa mtupu kabisa.
“Ramsey unataka kufanya nini?” Mariam akasema kwa ukali sana.
“Mbona hivyo mpenzi wangu? Kwani wewe ni nani wangu enheee? Sisi si ni wapenzi, sasa kuna ubaya gani kufanya mapenzi?”
“Ubaya upo!”
“Kivipi?”
“Hatujajuana vizuri Ramsey, lazima tupime kwanza kabla ya kuanza haya mambo!”
“Ninazo kondom!”
“Sipo tayari....kwanza huwa situmii kondom!”
“Mbona unakuwa hivyo?”
“Nooooo...haiwezekani Ramsey, naomba uelewe!” Mariam akajitoa kitandani kisha akavaa nguo zake haraka na kutoka nje, akarudi chumbani mwake.
*******
Hadi inafika saa moja kamili asubuhi, Mariam alikuwa hajafumba macho yake kulala. Alitumia usiku mzima kuwaza maisha yake. Hakuwa tayari kumsaliti Tom wake, lakini pia hakuwa tayari kupoteza misaada ya Ramsey.
“Nitafanya nini mimi jamani? Mbona dunia inanigeuka kiasi hiki?” Mariam akawaza akilia.
Usiku mzima alikuwa hapokei simu ya Ramsey, baadaye akaamua kuweka mkonge wa simu pembeni ili kukwepa usumbufu. Alipoanza kupiga simu yake ya mkononi akaamua kuizima kabisa. Akili yake ikawa ni juu ya mpenzi wake wa moyo wa Tom.
Akiwa anaendelea kuwaza, ghafla akasikia mlango ukigongwa, akaenda kufungua. Akakutana na Ramsey akiwa amebeba begi lake. Akamwangalia Mariam akionekana kuwa na chuki za wazi. Akaingiza mkono mfukoni kisha akatoa burungutu la pesa na kumrushia kitandani, baada ya hapo akaingiza tena mkono katika mfuko wa shati kisha akatoa karatasi iliyokuwa na maandishi na kumpatia.
“Maisha mema!” Ramsey akasema kisha akafunga mlango kwa nguvu na kuondoka.
Haraka Mariam akafungua lile karatasi kisha akaanza kusoma kwa makini. Ilikuwa imeandika hivi; Nilikupenda kwa mapenzi ya dhati, nikakupa kila kitu lakini hukuthamini penzi langu. Nilikuwa tayari kukupa kila aina ya msaada uliotaka, lakini ukanilipa machungu.
Kuondoka chumbani kwangu usiku, kumenipa taswira kwamba hunipendi, unanionea kinyaa na ni mwaume ambaye sina uwezo wa kuwa na wewe. Ahsante sana kwa hilo, naomba na mimi niishie hapa. 
Nimekuachia hizo lakini tano, nikusaidie katika mwanzo mpya wa maisha yako, maana najua ni kiasi gani utakuwa katika hali ngumu. Maisha ya hapo hotelini hutayaweza, hivyo nakushauri rudi nyumbani, ukawaangukie wazazi wako, uwaombe radhi.
Hata hivyo, bado nakupenda, siku ukiona utaweza kuwa na mimi, basi nipigie simu kwa namba zangu nilizokuachia. Sina kingine zaidi ya kuendelea kukuambia nakupenda na sitaacha kukupenda. Huyo Tom ni msumari wako wa milele, lakini mwenye uamuzi wa kuutoa huo msumari ni wewe mwenyewe.
Akupendaye kwa dhati,
Ramsey.
Mariam alirudia kusoma yale maneno zaidi ya mara kumi na hakuna sehemu hata moja iliyobadilika! Yalikuwa maneno makali sana ambayo yaliuchoma moyo wake. Hakuwa na kitu kingine cha kufanya zaidi ya kulia. Mariam akaanza kulia.
“Lakini nimekumbuka, ipo njia ya kuepukana na haya matatizo yote, ipo...hapa natakiwa kufa tu, hakuna kingine. Nife, niende zangu kwa Mungu, yeye mwenyewe anajua kwanini nimeamua kwenda kwake mapema kabla yeye hajaniita. Nataka kufa, tena leo hii hii!” Mariam akasema maneno hayo kwa sauti ya chini huku akitokwa na machozi.




Beyond Love- 37

Uamuzi ambao kwa hakika ulikuwa mbaya sana, lakini kwake ulikuwa uamuzi makini ambao aliamini baada ya hapo angepumzika! Aliamua kufa. Hilo pekee ndilo lingekuwa pumziko lake la kweli! Machozi yakaanza kutiririka machoni mwake! Alidhamiria kufa. Je, ni kweli atajiua? Nini kitatokea katika maisha ya Mariam? SONGA NAYO...

CHUMBA kilikuwa kichungu kwake, asingeweza kuendelea kuishi pale bila msaada wowote. Bado akilini mwake hakuweza kujua nini cha kufanya tofauti na uamuzi wa kufa ambao aliuona kuwa ni bora zaidi.
“Nitakuwa nimepotea kabisa, sitaonana na mtu yeyote tena, nitakuwa nimepumzika kwa Mungu, mateso na shida zote yatakuwa yameisha. Kwanini niendelee kuishi kwa shida kiasi hiki? Wazazi wangu hawanitaki, Ramsey amenikimbia, Tom naye ni mgonjwa, pamoja na kwamba nampenda lakini bado anaweza akapona na akaendelea kuwa na msimamo wake ule ule, sasa kwanini nijitese? Kwanini niendelee kuteseka?
“Ni bora kufa, ni bora niondoke, hiyo ndiyo inaweza kuwa salama yangu, sina kitu kingine cha kufanya zaidi ya hivyo, acha nikapumzike,” Mariam akawaza akilini mwake huku machozi mithili ya maji yakimiminika machoni mwake.
Alitulia kwa muda mrefu pale kitandani, akiendelea kulia, muda ukizidi kwenda. Alitumia muda mwingi akiwaza maisha yake, hapo ndipo alipokumbuka kwamba hakuwahi kufurahi kabisa katika maisha yake ya kimapenzi.
Mchana mzima alikuwa akilia, hakukumbuka kula siku hiyo, usiku akaamua kwenda kununua sumu ya panya ili ajitoe uhai. Alidhamiria kufa, baada ya kununua sumu yake ya panya, alirudi hotelini na kutulia kwa muda akijaribu kufikiria maisha yake baada ya kifo chake.
“Hakuna kitakachoharibika, sina thamani ya maisha hapa duniani, naamini kwa Mungu kuna afadhali, najua nitakuwa na dhambi ya kujiua lakini Mungu mwenyewe naamini atanisamehe kutokana na haya mateso niliyonayo. Sijapenda kufa, ila nalazimika kukimbia matatizo ya hapa duniani, siwezi kukabiliana nayo, yamenishinda,” Mariam alijisemea moyoni.
Mariam alibadilika sana, hakuona thamani yake tena duniani, aliamini kwa kufa pekee ndiyo angeweza kupumzika na kuepukana na matatizo anayoyapata. Alichokifanya ni kuchukua mkonge wa simu, kisha akabonyeza namba za hotelini.
“Hotelini!”
“Ndiyo habari yako?”
“Salama.”
“Naomba kukusikiliza!”
“Nahitaji soda ya badiri sana!”
“Soda gani?”
“Yoyote isiyo na gesi sana!”
“Soda gani sasa?”
“Yoyote.”
“Upo chumba namba ngapi?”
“206.”
“Ghorofa ya ngapi?”
“Tatu.”


KUPATA SIMULIZI TAMU ZAIDI JIUNGE NASI KATIKA PAGE YETU YA FACEBOOK
 LIKE HAPA >>>>>>>>www.facebook.com/2jiachie

“Ok! Baada ya muda mfupi utaletewa.”
Mariam akachukua kalamu na karatasi akaanza kuandika ujumbe ambao ungewasaidia wahudumu kufahamu alikuwa ni nani na ndugu zake ni akina nani. Ulikuwa ujumbe unaosikitisha sana, muda wote aliokuwa akiandika alikuwa akilia machozi.
Ujumbe huo, ulisomeka hivi; ‘Nimeamua kufa ili kukwepa fedheha ninayoipata hapa duniani, naamini kifo pekee ndicho kitakachoweza kunitenganisha na kero na matatizo yote ninayoyapata hapa duniani. Nimeteseka vya kutosha, ninayempenda hanipendi, wazazi wangu wamenifukuza nyumbani, sina msaada wowote.
Sioni thamani wala faida yangu duniani, ni heri nife tu, ni wengi wananifahamu, mimi ni mke halali wa Tom ambaye wengi wamekuwa wakimfahamu kwa jina la Papaa Bill. Naamini kwa utambulisho huu utawarahisishia kuwapa taarifa wazazi wangu ambao watakuja kuuchukua mwili wangu na kuuzika.
Naamini kifo ni safari ya kwenda mbinguni, hivyo basi ni imani yangu kwamba siku moja tutakutana katika enzi yake Mungu wa mbinguni. Kwaherini ya kuonana.
Mariam.’

 KUPATA SIMULIZI TAMU ZAIDI JIUNGE NASI KATIKA PAGE YETU YA FACEBOOK
 LIKE HAPA >>>>>>>>www.facebook.com/2jiachie

Alipomaliza kuandika ujumbe huo, alirudia kuusoma mara mbili mbili huku akilia. Akiwa anarudia kwa mara ya tatu, mlango wa chumba chake ukagongwa, alijua lazima alikuwa mhudumu. Haraka akafuta machozi yake kisha akaficha karatasi yake, akasogea mlangoni, akafungua mlango.
“Vipi sister?”
“Salama.”
“Mbona kama ulikuwa unalia? Kuna tatizo?” mhudumu akamwuliza.
“Hapana macho yananisumbua kaka yangu!” Mariam akadanganya.
“Pole sana!”
“Ahsante!” Wakati Mariam anajibu hivyo, alijikuta machozi yakimwagika usoni mwake kama maji yanayotiririka kutoka mferejini.
“Mh! Dada inaonekana una tatizo, lakini unajaribu kunificha, kwanini usiseme ukweli, naweza kukusaidia mawazo,” yule mhudumu akamsisitizia.
“Kaka nimeshakuambia macho yananisumbua lakini kwanini unazidi kuning’ang’aniza niwe na matatizo? Kwanza siyo kazi yako kujua matatizo yangu, tafadhali fungua soda uondoke!” Mariam aliongea kwa ukali sana, alionyesha kudhamiria alichokuwa akizungumza.
Yule mhudumu hakuwa na maneno mengi, akafungua soda kisha akaondoka zake. Mariam akaimimina soda kwenye glasi kisha akachanganya na ile sumu aliyoinunua, baada ya hapo akaanza kuikoroga kwa pamoja. Akasimama mwili ukimsisimka, kisha akaiangalia ile glasi, baada ya hapo akaielekeza mdomoni mwake.
“Eeeh baba naomba upokee roho yangu,” Mariam akasema maneno hayo glasi ikikaribia kufika kinywani.
Aliamua kufa!
******
Nyumba ilipoteza amani, furaha yao haikuwepo tena, walishamtafuta Mariam hadi wamechoka na hawakufanikiwa kumpata. Mama yake Mariam alikuwa akilia muda wote.
Kila walipoenda Muhimbili kumtafuta Mariam, waliambiwa kuwa huwa anakwenda mara moja moja, jibu ambalo lilizidi kuwachanganya. Walishaamua kumchukua mtoto wao ili wafanye mazungumzo na kumuweka sawa, lakini waliumia sana walipomtafuta bila mafanikio.
“Lakini nina wazo mume wangu,” mama yake Mariam akamwambia mumewe.
“Wazo gani mama Mariam?”
“Tunahangaika na tutahangaika sana, lakini ipo njia moja tu tunayopaswa kuitumia!”
“Ipi?”
“Tumesahau kumuomba Mungu, nakuhakikishia kama tukimshirikisha yeye kila kitu kitakuwa sawa, ni lazima tuwe karibu na Mungu baba Mariam.”
“Ni kweli, tumefanya kosa kubwa sana mke wangu, hatuna haja ya kupoteza muda, tunatakiwa kuanza kusali sasa hivi.”
“Haya simama tuombe mume wangu.” Wote wakasimama, kisha wakashikana mikono, mama Marim akaongoza sala.
Walianza na nyimbo za kuabudu, ambazo waliimba kwa robo saa kabla ya kuingia kwenye maombi yaliyowachukua saa nzima! Kila mmoja alikuwa akimuomba Mungu wake, amuepushie Mariam kwenye mateso na shida zote na hata kama alikuwa na mawazo mabaya ambayo yalikuwa yanateka akili yake, yashindwe!
“Katika jina la Yesu Kristo wa Nazareth tumeomba na kushukuru...” 
“Aaamen...” baba Mariam akaitikia. 
“Mungu ndiyo kila kitu mume wangu, nakuhakikishia tutaona majibu yake, Mungu wetu siyo mwongo, maana yeye mwenyewe tumuombe naye atatujibu, hawezi kutoa ahadi ya uongo, lazima atatujibu tu, lazima.”
“Ni kweli mke wangu, twende chumbani tukalale.”
Wakaongozana hadi chumbani kulala, angalau sasa mioyo yao ilikuwa na amani baada ya kufanya maombi.
*******
“Acha!” Mariam alisikia sauti hiyo ambayo hakuelewa ilitokea wapi.
Alihisi alikuwa ndotoni, hivyo akapuuza, akaamua kuipandisha glasi yake hadi kinywani, akiwa anataka kuanza kunywa, ghafla akahisi mkono wake ukitetemeka kwa kasi, ukazidisha kasi hadi glasi ikaanguka chini.
Mariam hakuelewa kilichotokea, chumba kizima kikawa kinanuka harufu ya sumu ya panya. Ilikuwa harufu mbaya sana, Mariam alichanganyikiwa, hakujua kwanini jambo lile lilitokea, alichoamua kwa muda huo, ilikuwa ni kurudi tena dukani na kununua sumu nyingine ili aweze kuendelea na zoezi lake.
Akiwa ndiyo anataka kufungua mlango ili atoke nje, akashangaa miguu yake inakuwa mizito, sauti nyingine tena ikasisika, tena kwa sauti ya juu na ya msisitizo zaidi; “Wewe ni msichana mzuri sana, unayevutia na ambaye una mpenzi mzuri sana, siyo kweli kwamba baada ya kufa utakuwa umekimbia matatizo, achana na mawazo hayo.
“Unachotakiwa kufanya sasa ni kwenda kwa wazazi wako, uwaangukie na kuwaomba radhi, bado una nafasi ya kuendelea kuishi. Mariam badili uamuzi wako...” Mariam alizidi kuchanganyikiwa, hakuweza kuelewa ilikuwa sauti ya nani na wapi ilipotokea.
Katika hali ambayo hata yeye mwenyewe hakuitegemea, alijikuta akiahirisha kujiua, moyo wake ukawa umekunjamana  na kuhisi uhitaji wa radhi za wazazi wake.
“Lazima nirudi nyumbani, lazima tena usiku huu huu wa leo,” Mariam akawaza na kuchukua begi lake dogo lililokuwa na nguo zake chache kisha akafunga chumba na kushuka hadi chini ambapo aliingia kwenye taxi.
“Wapi sister?”
“Jeti, Lumo!”
“Poa.” Dereva akawasha gari na safari ya kwenda nyumbani kwa wazazi wake ikaanza.
Kwa kuwa hakukuwa na foleni, dakika ishirini zilitosha kabisa kutoka Magomeni Mapipa katika hoteli aliyokuwa akiishi hadi Jeti, Lumo. Tayari ilikuwa imeshafika saa saba kasoro za usiku. Kwa bahati nzuri, nyumba yao ilikuwa barabarani, hivyo alimlipa dereva akashuka na kuanza kugonga geti.
Muda mfupi baadaye baba yake akafika getini.
“Nani usiku wote huu?”
“Ni mimi baba!”
“Mariam!”
“Ndiyo!”
“Karibu mwanangu, ngoja nikufungulie!” Mlango ukafunguliwa na Mariam akaingia.
Mapokezi aliyokutana nayo hakuyategemea kabisa, baba yake akampokea begi na kuingia naye hadi ndani ambapo alimwita mama Mariam ambaye hakuamini kilichokuwa mbele yake.
“Mariam ni wewe mwanangu? Karibu nyumbani mama...” mama yake alisema huku machozi yakianza kumlengalenga.
“Ahsante sana mama, nawaombeni msamaha wazazi wangu, najua ni kiasi gani nimewavunjia heshima, nimewakosea adabu na hata kuwadhalilisha mbele ya jamii. Nawaahidi nitakuwa mtoto mwema kwenu, naachana na mambo yote ya kale na sasa naanza upya maisha yangu.
“Kama siyo Mungu, kesho mngepata taarifa za kifo changu, tayari nilikuwa na sumu ambayo niliitayarisha kwa ajili ya kujiua, nikasikia sauti ya ajabu ikiniambia niache, hapo ndipo nilipoamua kurudi kwenu wazazi wangu.
“Naamini mkinisamehe na kunibariki nitaishi maisha mapya,” Mariam alikuwa akisema huku akilia. Mama yake naye alikuwa akilia sana, maneno ya mwanaye yalikuwa makali sana na hakuamini kuwa mwanaye alipitia mateso makali kiasi kile.
“Mwanangu, sisi tumekwishakusamehe siku nyingi sana, huna haja ya kuwa na wasiwasi juu ya hilo,” baba yake Mariam akasema.
“Nashukuru kusikia hivyo wazazi wangu, lakini nilikuwa na ombi moja ambalo nawaomba sana mnikubalie!”
“Ombi gani mwanangu, we sema tu!”
“Naomba mniahidi kwanza kuwa mtanikubalia!”
“Sema tu!”
“Au basi, tuache tu...” Mariam akasema akionekana kuwa na wasiwasi sana.
“Akha! Kwanini tena.”
“Basi tu!” Mariam akaanza kulia, tena kwa sauti ya juu kama ambaye alikuwa amefiwa.
Wazazi wake walishindwa kuelewa alikuwa na tatizo gani kubwa kiasi cha kushindwa kusema. Vichwa vyao vikawaka moto, mwenye siri hiyo alikuwa ni Mariam mwenyewe.


KUPATA SIMULIZI TAMU ZAIDI JIUNGE NASI KATIKA PAGE YETU YA FACEBOOK
 LIKE HAPA >>>>>>>>www.facebook.com/2jiachie

Beyond Love- 38

Mariam akaamua kujiua, lakini kabla ya hajafanya hivyo anajikuta akijisikia mwenye dhambi sana kujitoa uhai wake. Akaamua kuahirisha, hapo ndipo alipoona umuhimu wa kwenda kwa wazazi wake ambao walimpokea kwa mikono miwili.
Mariam alionekana kuwa na kitu alichotaka kuwaomba wazazi wake, aliporuhusiwa kusema akasita! Je, ni kitu gani hicho? Atasema? SONGA NAYO...

Furaha waliyokuwa nayo wazazi wa Mariam ilikuwa haielezeki, lakini sasa ilianza kuyeyuka taratibu. Kutokuwa na mwanao kwa muda mrefu kiasi kile tena wakiwa hawafahamu mahali alipo lilikuwa pigo kubwa sana kwao, lakini kilichowachanganya zaidi vichwa vyao ni Mariam kusema ana jambo alilotaka kuwaomba wazazi wake lakini ghafla anakataa.
Vichwa vyao vikawaza upande wa mabaya zaidi, kwamba yawezekana alikuwa katika hali ya matatizo makubwa na alikuwa akiogopa kuwashtua wazazi wake. Mama akaanza kulia kwa uchungu akiamini lazima Mariam alikuwa na tatizo kubwa lililomkabili.
“Lakini Mariam ni nini? Sema kinachokusumbua basi mwanangu!” Baba yake akasema kwa uchungu sana akimwangalia Mariam usoni.
“Acha tu baba, naona niachane na hayo mambo!”
“Kwani kuna tatizo?”
“Halijawa tatizo baba!”
“Halijawa tatizo? Unamaanisha nini kusema hivyo?”
“Yaani halijafikia kuwa tatizo na ndiyo nimeona niliache ili lisiwe tatizo!”
“Hapana, wewe ni mtoto wetu wa pekee, na mimi na mama yako hatutaki kukuona unasononeka, kama kuna kitu kinakusumbua ni bora ukaeleza kwa uwazi ili tujue jinsi ya kukusaidia!”
“Baba ni usiku saa hizi, naomba tuzungumze kesho.”
“Lakini ingekuwa ni afadhali tulale tukijua mzigo ulionao umeshautua!”
“Basi baba, acha niwaambie lakini naomba mniahidi kitu kimoja kwanza.”
“Nini?”
“Kwamba mtanikubalia.”
“Sema tu mwanangu, kama nilivyokuambia, hatupendi kukuona ukiwa huna furaha kwa mambo ambayo yapo ndani ya uwezo wetu...eleza nini tatizo mwanangu!”
 “Baba ni kweli niliwakosea kwa mambo mengi, lakini pia napenda kuwaeleza kilichopo moyoni mwangu!”
“Enheee...”
“Nakubali Tom alinitesa, alininyanyasa na kunifanyia kila aina ya ubaya lakini mama na baba yangu, bado kuna kitu moyoni mwangu. Bado nahisi kumpenda sana Tom!” Mariam alizungumza kwa sauti iliyojaa huruma sana.
“Bado unafanya nini? Hivi una akili kweli Mariam? Ni mangapi amekufanyia yule mpuuzi, una sababu ya kuendelea kuona kwamba eti ana nafasi kwako, kwanini hutaki kutumia akili yako mwanangu?” Mama yake akamwambia akiwa ameukunja uso kwa hasira.
“Lakini mama nampenda!”
“Unapenda matatizo? Hivi we’ mtoto una akili gani?”
“Basi mama, tuachane nayo...nimekubali kuachana na Tom, lakini naomba mniruhusu kufanya jambo moja!”
“Jambo gani?”
“Naombeni mniruhusu nimhudumie mpaka apone, lakini sitakuwa na uhusiano naye kabisa!”
“Hilo haliwezekani.”
“Sasa nini kinawezekana?”
“Hakuna kinachowezekana.”
Walizozana kwa muda mrefu sana, hadi saa tisa za usiku walipoingia vyumbani kulala bila kuwepo na maafikiano. Asubuhi hakuna aliyezungumzia juu ya jambo hilo, lakini akilini Mariam aliamua kukaa kimya  akiwaza jinsi atakavyomhudumia Tom bila wazazi wake kufahamu.
Tom alikuwa kila kitu katika maisha ya Mariam, alimpenda kwa mapenzi yake yote na wala hakuweza kujua ni kwanini alijikuta akimpenda Tom kwa kiasi kile. Hata hivyo hakutaka kujiuliza maswali hayo, alichojua yeye ni kumpenda Tom tu.
“Nampenda sana Tom wangu, ukweli huu nitausimamia siku zote na ni lazima nihakikishe naulinda msimamo wangu huu. Najua siku moja Tom ataujua ukweli kwamba mimi ndiye mwanamke wa maisha yake, mimi pekee ndiye ninayempenda na wala siyo Mayasa kama anavyofikiria, hili litadhihirika!” Mayasa akawaza.
Kwa wiki nzima Mariam alikuwa anashinda nyumbani bila kwenda hospitalini, moyo wake ulimuuma sana lakini aliamua kufanya hivyo ili kuwapumbaza wazazi wake wasahau kabisa kuhusu Tom. Siku moja asubuhi baada ya baba yake kwenda kazini, Mariam alimuomba mama yake ruhusa ya kwenda kumuona rafiki yake.
“Nani?”
“Clara mama!”
“Lakini kwanini yeye asije?”
“Mama yake ni mgonjwa, amenipigia simu jana kunipa taarifa na kama unavyojua sisi ni marafiki, naona hii ni nafasi yangu ya kuonyesha ninavyomjali kwa kumfariji mama!” Mariam akadanganya.



KUPATA SIMULIZI TAMU ZAIDI JIUNGE NASI KATIKA PAGE YETU YA FACEBOOK
 LIKE HAPA >>>>>>>>www.facebook.com/2jiachie

“Sawa mwanangu, lakini jitahidi basi kuwahi!”
“Usijali mama!”
Mariam akajiandaa kisha akatoka na kwenda zake Muhimbili tena akitumia gari la mama yake. Aliingia wodini na kumkuta Tom akiwa amelala kimya kitadani, bado alikuwa akipumulia mashine. Mariam akapiga magoti pembeni ya kitanda chake, akambusu usoni huku akitamka; “Nakupenda sana Tom wangu, najua yote uliyonifanyia ni kwa sababu ya shetani tu, wewe na akili yako huwezi kufanya hayo.
“Namwomba Mungu akujalie, siku moja usimame tena, uone jinsi ninavyokupenda, naamini siku hiyo itafika na utajua ukweli kwamba mimi ndiye mwanamke pekee ambaye nakupenda kwa moyo wangu wote.”
Mariam alijikuta akilia akimtizama Tom.  Zilikuwa kumbukumbu za kuhuzunisha sana katika maisha yake, alitamani sana siku moja Tom aamke na warudiane tena kama mtu na mke wake. Hilo aliamini lazima siku moja litatokea. Baadaye akatoka na kwenda ofisini kwa daktari wake ili kupata maelezo ya maendeleo ya Tom.
“Ndiyo Dokta anaendeleaje sasa?”
“Matumaini yapo, lakini kama ulivyomuona bado hajazinduka.”
“Unadhani itamchukua muda gani?”
“Kwa kweli siyo rahisi kukuambia maana bado kuna vipimo vingine vinaendelea kufanyika, ila tunashukuru kidogo mapigo yake yanaanza kurudi vizuri, nafikiri baada ya wiki mbili tatu, ataweza kuanza kupumua mwenyewe.”
“Nitashukuru sana dokta, kwa hiyo atapona?”
“Mategemeo yetu yapo kwa Mungu dada yangu, nafikiri ni vyema kama tutamwachia yeye!”
“Nashukuru sana dokta!”
“Ok!”
Mariam aliendelea kukaa pale hospitalini hadi usiku kabisa, baada ya kuhakikisha Tom alikuwa ameshaoga na kula kwa kupitia mpira. Akarudi nyumbani usiku sana, maelewano na mama yake hayakuwa mazuri lakini alisingizia kwamba hali ya mama wa rafiki yake haikuwa nzuri, hivyo asingeweza kumuacha akiwa katika hali mbaya peke yake.
“Lakini kwanini hukutoa taarifa?”
“Nilipitiwa mama!”
“Ndiyo na simu uzime?”
“Iliisha chaji mama!”
“Angalia sana Mariam, sitaki unigombanishe na baba yako!”
“Nisamehe mama.”
Mariam aliendelea kumhudumia Tom kila siku, alifanya hivyo kwa siri kubwa hadi siku mama yake alipogundua na kumwambia baba yake. Mariam akatakiwa kuamua jambo moja, kuondoka nyumbani aendelee kumhudumia Tom au abaki nyumbani lakini aachane na Tom.
“Mama nimechoka na haya masimango yenu, sili chakuka kikashuka...basi bora niondoke hapa kwenu, nikamsaidie Tom wangu, kwanza kumbukeni nimefunga naye ndoa. Yule ni mume wangu halali, na nilimuahidi kuwa nitaishi naye katika shida na raha, sasa kwanini nimtese?”
“Kama unayajua hayo, mbona yeye alikusaliti? Mbona yeye alikutesa?”
“Umeshasema yeye...kwani huoni kama kuna tofauti kubwa kati ya yeye na mimi, ninafanya kile nilichoahidi na yeye kwa nafasi yake anatakiwa kufanya alichoniahidi.”
“Kwahiyo?”
“Narudi Mbezi, nyumbani kwangu, nitaishi maisha yoyote na nitaendelea kumhudumia mpaka atakapopona, hayo ndiyo maamuzi yangu,” Mariam alionyesha msimamo wa hali ya juu sana, ilifikia hatua wazazi wake wakashindwa kumzuia zaidi.
Mariam akaondoka na kwenda zake Mbezi katika nyumba ya Tom waliyokuwa wakiishi. Nyumba ilikuwa chafu na haikuwa katika mpangilio mzuri, baadhi ya vitu vilikuwa havipo. Hakusumbua sana kichwa kugundua kwamba ilikuwa ni kazi ya Mayasa.
Alichokifanya ni kuhakikisha nyumba inakuwa safi, kisha kazi yake kubwa ikawa ni kumhudumia Tom.
********
MIAKA MINNE BAADAYE
Kama kawaida, asubuhi hiyo Mariam alikwenda Muhimbili, hiyo ilikuwa ni kama ndiyo kazi yake. Siku hiyo alihisi moyo wake ukienda kasi sana, alijaribu kujiuliza sababu za hali hiyo kumtokea lakini hakupata majibu. Akaingia wodini kisha akaketi kitandani akimtizama Tom aliyekuwa akipumua kwa kutumia mashine.
Kwa miaka minne sasa alilala kitandani bila kujitambua! Hata hali ya afya yake haikuwa nzuri tena, Tom alitia huruma! Katika hali ya kushangaza sana, akaona macho ya Tom yanafumbuka taratibu. Tom akatabasamu, lakini alipogundua kwamba aliyekaa mbele yake alikuwa ni Mariam akakasirika sana.
“We’ mwanamke umefuata nini hapa? Ondoka utakuja kupigwa na Mayasa wewe...Mayasa ni mkorofi, kwanini unaendelea kunifuatafuata? Toka...toka Mariam usije kunisababishia matatizo...” Tom akazungumza kwa sauti kubwa huku akiyatoa macho.
Hakujua kilichotokea katika maisha yake tena, hakuwa na habari kwamba alilala kitandania kwa zaidi ya miaka minne. Aliendelea kufoka huku akimuamrisha Mariam aondoke. Mariam alijikuta akishindwa kuzungumza, machozi yakaanza kumtoka.
“Tom mume wangu, Mayasa hayupo hapa na wala hawezi kutokea Tom...mimi ndiye Mariam, mwanamke wa maisha yako, ambaye nakupenda kwa mapenzi yangu yote. Nakupenda kwa mapenzi ya kweli, sikujali pesa wala utajiri wako Tom, lakini Mayasa uliyemuona anafaa, leo hayupo unateseka na mimi kwa miaka yote uliyokuwa umelala.
“Mayasa ameuza kila kitu, amekuachia kibanda cha kulala tu, hakuna kitu tena mpenzi wangu. Lakini yote hayo najua ni shetani, ndiyo maana nipo hapa leo kukuonyesha kwamba mimi nina mapenzi ya dhati kwako,” Mariam aliongea akilia.
Tom alishindwa kuelewa alichokuwa akizungumza Mariam, ni kama alikuwa akizungumza vitu vigeni. Amelala miaka minne kitandani? Kivipi? Hilo hakulielewa na wala hakutaka kulipa nafasi kabisa akilini mwake.
“Hivi una kichaa Mariam? Unavyosema Mayasa ameuza vitu vyangu unamaanisha nini? Nimekuambia toka hapa Mayasa atakukuta na kukufanyia fujo...ni bora ukaondoka Mariam...” Tom alisema maneno hayo kisha akajitahidi kuamka, lakini akashindwa!
Hapo akagundua kwamba alikuwa amelazwa hospitalini tena alikuwa akipumua kwa kutumia mashine! Hakujua kilichotokea, lakini alivyotulia kwa muda akakumbuka alivyovamiwa na majambazi na kurushiwa risasi akiwa getini kwake!
Tom akaanza kulia. Mariam naye akaungana naye. Machozi yakatawala wodini.
“Tom unanipenda?” Mariam akamwuliza Tom, lakini hakujibu zaidi ya kuendelea kulia.


KUPATA SIMULIZI TAMU ZAIDI JIUNGE NASI KATIKA PAGE YETU YA FACEBOOK
 LIKE HAPA >>>>>>>>www.facebook.com/2jiachie

Beyond Love- 39

Anaanza kulia, Mariam naye analia, wote wanaungana kulia kwa furaha. Mariam anamwuliza Tom kama anampenda, Tom hajibu badala yake anaendelea kulia. Je, nini kitatokea kati ya Tom na Mariam? SONGA NAYO...

“Tom niambie basi kama unanipenda?” Mariam anazidi kumkazania Tom swali hilo huku mvua ya machozi ikiendelea machoni mwake.
Tom hajibu kitu zaidi ya kuendelea kulia kama mtoto mdogo!
“Tazama ninavyokupenda Tom, umenisaliti, ukaniletea mwanamke mpaka ndani, ukanifukuza lakini yote hayo nilishayasahemehe, kilichokuwa ndani ya moyo wangu ni upendo wa dhati, upendo ambao siku zote umekuwa silaha yangu ya kweli, umeniwezesha kuwa mvumilivu na mwenye ahadi za kweli, niliuahidi moyo wangu kutokukusaliti asilani na ndivyo nilivyofanya mpenzi wangu.
“Ni miaka minne umelala hapa hospitalini, ukiwa huna kumbukumbu ya jambo lolote lile, nikihangaika na wewe kwa kila hali, nikawa tayari kugombana na wazazi wangu kwa ajili yako Tom, naomba uamini kwamba nakupenda, upendo wa dhati kutoka katikati ya moyo wangu...nakupenda sana Tom, naomba uniamini kwa hilo.”
Mariam alikuwa na uchungu mwingi sana moyoni mwake, pamoja na uchungu aliokuwa nao, ilikuwa ni siku ya furaha kubwa katika maisha yake, hakutegemea kuisikia tena sauti ya Tom, kumuona akifumbua macho yake mazuri na kumtizama uso wake. Alijisikia furaha isiyo na kifani, kwake Tom alikuwa mpenzi mwema, awe mgonjwa au katika hali yoyote, alichojali ni kumuona Tom wake akiwa mzima!
“Hujanijibu bado Tom wangu, niambie basi unanipenda?” Mariam akamwuliza tena.
“Nakupenda Mariam!”
“Nashukuru kusikia hivyo,” Mariam akasema kisha akambusu katikati ya midomo yake.
“Nakupenda pia mpenzi wangu, wewe ni wangu wa maisha, nilijua Mayasa alikuwa anakupoteza na nina imani haikuwa akili yako mume wangu, lazima yule malaya atakuwa alikuwekea kitu.
“Hata hao majambazi waliokuvamia, nina wasiwasi nao sana, yawezekana ikawa Mayasa alitengeneza mchezo!”
“Huna haja ya kuwaza sana mambo yaliyopita mpenzi, tuyaache kama yalivyo. Enhee Mayasa yupo wapi?”
“Mayasa?”
“Ndiyo!”
“Ngoja nikupe stori!” Mariam akaanza kumsimulia Tom kila kitu baada ya yeye kuamua kwenda kijijini kwao Matombo, Morogoro, akamweka wazi kwamba alisikia Mayasa alitoroka na aliuza mali zote akiwa mgonjwa.
Hakumficha kitu chochote, aliweka wazi jinsi alivyoteseka kwa ajili yake. Wote walilia sana. Tom akaona thamani ya penzi la Mariam kwake, akauahidi moyo wake kuwa mtulivu na kuendelea kuwa na Mariam pekee, hakutaka kuhaingaika tena.
“Enhee na mama yuko wapi?”
“Mama?”
“Ndiyo!”
“...Yupo nyumbani!” Baada ya kufikiria sana, Mariam akaamua kudanganya, hakuona sababu ya kumweleza ukweli juu ya kifo cha mama yake, kwani alijua wazi ni kiasi gani angemuumiza.
“Mbona hukuja naye?”
“Huwa tunakuja kwa zamu, wiki hii ni yangu, wiki ijayo ni yake, ila akijua kwamba umeshapata fahamu lazima atakuja!”
“Nitafurahi sana!”
“Pole sana mpenzi wangu, najua ni kiasi gani ulivyokuwa katika mateso makali kwa muda mrefu!”
“Usijali Mariam wangu, nashukuru pia kwa kuonyesha penzi lako la dhati, hakika haya ni zaidi ya mapenzi, wewe ni mpenzi wangu wa kweli!” Tom akasema akitoa machozi.
“Nashukuru kwa kutambua hilo mpenzi, nitakupenda milele!”
“Hata mimi pia!”
Wakiwa katikati ya maongezi, Muuguzi alifika na kushangazwa na hali aliyomkuta nayo Tom, hakutarajia kumuona mgonjwa wake akiwa amerejewa na fahamu baada ya kulala kitandani kwa siku zote hizo. Akakimbia ofisini kwa daktari haraka kwenda kumpa taarifa hizo.
“Yule mgonjwa amezinduka!”
“Yupi?”
“Tom!”
“Kweli?”
“Ndiyo dokta!”
“Hebu twende!” Dokta akaongozana na Muuguzi hadi kitandani kwa Tom.
Alipomkuta akizungumza  na Mariam, akamkataza.
“Mariam mwache kwanza apumzike, bado hajawa na nguvu ya kuzungumza sana kwa wakati huu, anahitaji muda mwingi wa kupumzika kwanza!”
“Sawa dokta!”
“Hebu tupishe kidogo!”
“Sawa!”
“Enhee Tom, unajisikiaje?”
“Nina nafuu sasa, Mungu amenipigania!”
“Ni kweli lazima umshukuru sana Mungu maana yeye ndiye aliyekupa uzima ulionao!”
“Amen!”
“Pole sana!”
“Nashukuru sana dokta!”
Baada ya pale Daktari alimwita Mariam ofisini kwake, kumpa taarifa za maendeleo ya Tom.
“Mariam kwanza tunamshukuru sana Mungu kwa kumuwezesha Tom kurejewa na fahamu tena, lakini kuna jambo moja lazima ulijue, mgonjwa wako amepooza kuanzia shingoni hadi miguuni, kwasasa kinachofanya kazi ni kichwa tu, lakini napenda kukutoa wasiwasi kwamba, kama Mungu huyo huyo ndiye aliyemzindua leo baada ya kulala miaka minne kitandani, basi Mungu huyo huyo ndiye atakayempa nafuu tena. Kifupi tutegemee muujiza wa Mungu!” Daktari akasema kwa utulivu sana.
Mariam alikaa kimya kwa muda akifikiria, ni kweli Tom alikuwa na tatizo, lakini kwake halikuwa tatizo kubwa sana kama angekufa kabisa! Akamshukuru Mungu kwa kumzindua Tom wake, tegemeo kubwa lilikuwa kwake.
“Hakuna shida daktari, nimefurahi kumuona akifumbua macho yake tena, mambo mengine hayo, nayaacha mikononi mwa Mungu mwenyewe!”
“Mungu atawasaidia!”
“Nashukuru sana, kazi njema.”
Magazeti ya mchana ya siku hiyo yalipambwa na habari ya Tom kuzinduka, haikujulikana ni muda gani waliingia wodini na kuwapiga picha Mariam na Tom, wakati Mariam alipokuwa akimbusu Tom mashavuni.
Gazeti la Za Leo ndilo lililokuwa na picha hiyo, pamoja na kichwa kikubwa cha habari kilichosomeka; HAYA NI ZAIDI YA MAPENZI! Lilikuwa gazeti pekee lililouzika zaidi kutokana na kuwa na picha ya wapenzi hao wakiwa pamoja hospitalini asubuhi ya siku hiyo.
*******
Usiku Mariam alishindwa kulala, alikuwa anawaza ni jinsi gani angeweza kumdanganya Tom kuhusu mama yake, hakika alikuwa na kazi kubwa sana ya kuzungumza naye na kumweleza ukweli.
Hata hivyo, pamoja na kuwaza kwa muda mrefu, baadaye alipitiwa na usingizi mzito. Asubuhi yake aliamka na kujiandaa kama kawaida kisha akaenda zake hospitalini. Akamkuta Tom akiwa amelala kitandani macho yake yakiangalia juu.
“Vipi sweetie?”
“Salama mama vipi?”
“Shwari lakini siyo shwari!”
“Kwanini?”
“Sijielewielewi kabisa, mwili wangu kama umekufa ganzi hivi!”
“Ni kawaida mpenzi, umelala kitandani kwa muda mrefu sasa, tena nilikuwa nazungumza na Dokta jana, kasema hali hiyo ni ya kawaida na itapotea polepole ingawa itachukua muda kidogo!”
“Siamini...” Tom akasema.
“Naomba kukuliza Tom, unaamini kama kuna Mungu?”
“Ndiyo!”
“Unaamini yupo Roho Mtakatifu?”
“Ndiyo!”
“Pia unaamini kwamba Mungu alimtuma mwanaye mpendwa Yesu Kristo ili afe msalabani kwa ajili ya dhambi zetu?”
“Ndiyo!”
“Kwahiyo unaamini juu ya Utatu Mtakatifu?”
“Hakika!”
“Basi mwachie haya mambo Mungu mwenyewe, naamini utukufu wake utadhihrika!”
“Ni kweli mpenzi wangu, ahsante sana kwa kunipa moyo, acha Mungu afanye awezavyo, najua hataniacha nikaabika!”
“Nashukuru kwa kutambua hilo mpenzi!”
“Enhee mama yupo wapi?”
“Unasema?”
“Mama yupo wapi?”
Mariam hakujibu, alikaa kimya akiwa ameyatuliza macho yake usoni mwa Tom, huku machozi yakianza kumtiririka machoni mwake. Tom alishindwa kuelewa maana ya machozi ya Mariam.
“Sasa unalia nini mpenzi wangu, Mungu atanisaidia, huna sababu ya kulia... kwanini hujaja na mama? Nina hamu sana na mama yangu!” Maneno ya Tom yalikuwa msumari wa moto moyoni mwa Mariam, kwani alikuwa na siri nzito sana ambayo kuitoa kwake lazima awe amejiandaa vya kutosha!
Haikuwa jambo jepesi kumwambia Tom, moja kwa moja kwamba mama yake alishafariki, tena alizikwa na Halmashauri ya Jiji. Hilo lilikuwa jambo gumu sana.
Je, nini kitatokea? Mariam atamweleza ukweli? Nini kitafuata katika maisha yao?


KUPATA SIMULIZI TAMU ZAIDI JIUNGE NASI KATIKA PAGE YETU YA FACEBOOK
 LIKE HAPA >>>>>>>>www.facebook.com/2jiachie

No comments

Powered by Blogger.