ad

ad

The Last Breath (Pumzi ya Mwisho) - 7

Na Eric Shigongo
NDEGE imeanguka, watu wote wamekufa isipokuwa Johnson na mwanaye Melania pamoja na watu wengine kadhaa lakini mbele ya safari wakati wakijaribu kujiokoa, watu wengine wote wanakufa na wanabaki Johnson na mwanaye, hata hivyo Johnson naye anazimika ghafla,  Melania analia akijua baba yake amekufa.
Muda mfupi baadaye, binti huyo mdogo anaingia mikononi mwa waasi wa Kundi la Congoleze Patriotic Front,  ambao wanataka kumbaka lakini kiongozi wao anamnusuru na kumpeleka moja kwa moja hadi kambini ambako hivi sasa anaishi akiandaliwa kuwa muasi akiwa amekabidhiwa kwa kijana aitwaye Paul.
Mke wa Johnson (Loveness) baada ya kupewa taarifa za kuanguka kwa ndege mshipa ulipasuka kichwani mwake, akapoteza fahamu na hata baada ya upasuaji uliofanyika Dar es Salaam, kumbukumbu zake zimepotea! Hakumbuki chochote kilichotokea na inawezekana akabaki hivyo maisha yake yote.
Je, nini kitaendelea? SONGA NAYO…
MAKUBO Army Hospital  ilimilikiwa na Jeshi la Wananchi wa Congo, ilikuwa ni hospitali kubwa yenye vifaa vingi kwenye kutibu majeruhi, Kaskazini Magharibi mwa Nchi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo. Ndiyo iliyohusika sana na matibabu ya majeruhi wote walioumia katika mapigano kati ya Majeshi ya Serikali na Majeshi ya Waasi wa Kikundi cha Congolese Patriotic Front.

Asubuhi hiyo madaktari na wauguzi ambao pia walikuwa ni wanajeshi, walikuwa bize wakijaribu kuokoa maisha ya mgonjwa aliyeletwa na helkopta kutoka msitu wa   Kundelungu ambako mapigano kati ya jeshi na waasi yalikuwa makali kupita kiasi.

Alikuwa amevunjika mguu na mkono,  hakuwa na fahamu kabisa na kiasi kikubwa sana cha damu kilikuwa kimepotea. Kilichofanyika mwanzo ni kumwekea chupa za damu zisizopungua kumi, baada ya hapo akapelekwa chumba cha upasuaji ambako mifupa iliyovunjika ilirekebishwa ndipo akarejeshwa wodini na kuendelea na lishe kupitia kwenye mifupa yake, maana kiasi cha sukari katika mwili wake kilikuwa kimeshuka mno.
“He is terribly hypoglycemic, he needs 5% dextrose IV infusion, 30 drops per minute!”(ameishiwa sana na sukari kwenye damu, anahitaji  chupa za maji ya wanga 5%, matone thelathini kwa dakika!) Dk Linda Johnson kutoka Marekani ambaye alikuwa mfanyakazi wa shirika la madaktari wasio na mipaka alisema, alikuwa mmoja wa wafanyakazi kwenye hospitali hiyo wakiokoa maisha ya watu.
Maji yakaanza kuingia kwenye mishipa ya mgonjwa huyo kama daktari alivyoagiza, chupa zikawa zinabadilishwa kila moja ilipokwisha mpaka zikatimia chupa sita, damu yake ilipochukuliwa kwenda kupimwa kiasi cha damu kilionekana kuwa gramu 9.5, karibu kabisa na kawaida, daktari akaagiza chupa mbili zaidi ziwekwe.
Ghafla zilipomalizika hizo, mgonjwa akajitingisha na baadaye kufumbua macho, alichokifanya kiliwashtua watu wote waliokuwemo chumbani na hata waliokuwa kwenye ofisi ya wauguzi, alipiga kelele kwa nguvu kubwa akiita jina la Melania!
“Vipi?” Daktari mmoja aliuliza walipoingia chumbani.
“Ameita jina la Melania.”
“Labda ni mke wake?”
“Pengine, nashukuru angalau ameweza kuongea, hali yake ilikuwa mbaya mno, sikuwa na uhakika kama angeweza kufumbua macho na hatimaye kutoa neno, kwa jinsi sukari yake ilivyokuwa imeshuka, nilifikiri ubongo wake ungeweza kuwa umeharibika.”
“Mungu amemsaidia.”
“What is your name?” (jina lako ni nani?) daktari alimuuliza.
“Johnson!”
“Where are you from?” (umetokea wapi?)
“Tanzania.”
“What were you doing in the Congo forest? Are you a rebel?” (ulikuwa unafanya nini kwenye msitu wa Congo? Wewe ni Muasi?)
“No! I don’t know about that! The plane I was traveling with crashed, where is my daughter?” (Hapana! Sijui juu ya hilo! Ndege niliyokuwa nasafiri nayo ilianguka, binti yangu yuko wapi?)
“Who is your daughter?” (binti yako ni nani?)
“Melania.”
“She is not here, we found you alone in the forest, unconscious and dying, you have been here since yesterday!”(hayupo hapa,  tulikukuta wewe peke yako msituni, ukiwa hujitambui na unakufa, umekuwa hapa tangu jana!)
“Oh my God!”(Oh! Mungu wangu!) aliongea Johnson machozi yakianza kumlengalenga.
“What was your flight?” (ndege yako ilikuwa ni ipi?)
“Air Congo, flying from Kinshansa to Nairobi!” (ndege ya Shirika la Ndege la Congo,  iliyokuwa ikiruka kutoka Kinshasa kwenda Nairobi!)
Johnson akaenda mbele zaidi na kuwaeleza kila kitu kilichokuwa kimetokea, wote wakawa wameelewa kwamba ndege aliyokuwa akisafiri nayo ndiyo iliyoaminika na kutangazwa duniani kote kwamba ilidondoka baharini na kuzama mpaka kwenye sakafu ya bahari.
Zilikuwa habari mpya kabisa na zilipelekwa moja kwa moja kwa Mamlaka ya Anga ya Congo pamoja na shirika la ndege la nchi hiyo ambao walifika mara moja na kuonana na Johnson ambaye aliwasimulia kila kitu juu ya kilichotokea, hawakuamini!
Kilichofanyika ni kukubaliana kwamba apate nafuu ya afya yake kisha kabla hata hawajatangaza waende naye mpaka porini alikookotwa, huko ndiko angeweza kuwaonyesha mahali mabaki ya ndege yalipokuwa. Johnson akatuma taarifa zake Tanzania kuwajulisha juu ya kuwa kwake hai, ndugu, marafiki wakafunga safari kumfuata hadi kwenye hospitali hiyo iliyokuwepo katika Mji wa Marabakungu.
“Mke wangu yuko wapi?” alimuuliza kaka yake.
“Tanzania.”
“Mbona hamjaja naye?”
“Atakuja tu!”
“Au amekufa kwa mshtuko?”
“Hapana,”
“Nitaishije mimi? Bila mke na mtoto wangu?”
“Usiwe na wasiwasi, Melania atapatikana tu.”
“Wapi? Wakati tulikuwa naye pamoja porini? Lazima atakuwa amekufa.”
Wiki nne baadaye hali ya Johnson ilikuwa nzuri, kwa helikopta akarushwa mpaka katikati ya msitu wa Congo ambako helikopta ilitua, akashushwa na kubebwa begani mpaka eneo alikookotwa. Alipofikishwa hapo tu kumbukumbu zote zilimwijia kichwani mwake, akamkumbuka mtoto wake na watu wote waliokufa njiani wakijaribu kujiokoa.
“Unafahamu mahali ndege ilipoangukia?”
“Twendeni njia hii.”
Walitembea kwa saa tatu ndipo wakafika eneo hilo, mabaki ya ndege yalikuwepo na mifupa mingi ya watu, nyama zake zikiwa zimeliwa na ndege pamoja na wanyama. Kitu cha kwanza walichokifanya ni kukitafuta kisanduku cheusi, kikapatikana. Baada ya hapo wakaangalia sanduku lililokuwa na dhahabu pamoja na almasi, halikuwepo.

“Lazima waasi walifika hapa!” mmoja wa wapiganaji alisema:
“Inawezekana, wakachukua sanduku lenye mali na kuondoka.”
“Walipajuaje?”
“Inawezekana kabisa mtoto wa Johnson walimteka, baada ya mateso akasema ndege ilipoangukia.”
“Kwa hiyo mtoto wangu yuko mikononi mwao?”
“Kabisa, kama si hivyo basi inawezekana waasi waligundua tu kwa bahati na mwanao atakuwa ameliwa na wanyama wakali.”
“Hapana! Hapana! Usiseme hivyo, naumia moyo.”
Huku akilia machozi Johnson aliondolewa eneo hilo mpaka mahali helikopta ilipokuwa imetua, wakapanda na kuruka tena hadi Marabakungu ambako alirejeshwa hospitali kuendelea na matibabu, jioni ya siku hiyo Serikali ya Congo ilitangaza juu ya kupatikana kwa mabaki ya ndege iliyokuwa inaaminika kwamba ilizama katika bahari na mtu mmoja aliyenusurika alitajwa kuwa ni Johnson, picha yake ikionekana.

***
Loveness alikuwa wodini bado akiwa hajaweza kujitambua, muda wote alikaa na picha mbili mkononi mwake akiziangalia na kulia. Hilo lilionyesha kwamba kumbukumbu zake zilikuwa zimeanza kukaa sawasawa akili ndiyo ilikuwa bado haijatengemaa kama ilivyokuwa awali.
Ndani ya chumba cha wodi alichokuwa amelazwa, akiuguzwa na dada yake, kulikuwa na runinga kubwa ukutani, taarifa ya habari ya Shirika la Utangazaji la CNN ilikuwa hewani, mara ghafla taswira ya Johnson akihojiwa juu ya ajali ya ndege ilivyotokea ikaonekana.
“Johnsooooon! Johnsooon! My husband!”(Johnsoon!Johnsooon! Mume wangu!) kwa mara ya  kwanza baada ya muda mrefu kupita, Loveness alizungumza, dada yake aliyekuwa kando ya kitanda akanyanyuka ghafla akiwa katika mshangao na kutupa macho kwenye runinga.
“He! Ni yeye, umemtambua?”
“Ni mume wangu,  yupo Congo!”
“Kweli kabisa.”
Watu wakaingia wodini na kumkuta Loveness akiongea huku machozi yakimbubujika, kwa hali ilivyokuwa, daktari akihofia kwamba presha yake ingeweza kupanda, aliagiza achomwe dawa ya usingizi mara moja ili kupumzika.
Hilo likafanyika na akazinduka saa nne baadaye na kuelezwa kilichotokea.
“Nataka niende Congo, nikamwone Johnson, labda na mwanangu yuko palepale!”
“Haitawezekana kwa sasa.”
“Kwa nini isiwezekane?”
“Hali yako bado haijawa nzuri.”
“Lazima niondoke,  maisha yangu haya, maana ni kama sina watu wawili muhimu maishani mwangu; Johnson na Melania.”
“Tunaelewa.”
“Kama mnaelewa basi niacheni niende zangu.”
“Itabidi usubiri.”
“Siwezi kusubiri.”

Nisingependa kumaliza hadithi hii ya leo bila kukumbusha jambo muhimu la kutoa maisha yako kwa Mungu. Maisha tuliyonayo hapa duniani ni mafupi sana, yanapita kama maua yachanuavyo na kunyauka. Wengi unaowafahamu wamekufa lakini wewe unapumua, ni vyema basi kufikiria maisha baada ya kifo.
Kila siku jiulize: “Hivi nikifa leo nitakwenda jehanam au peponi?” Kila mmoja wetu analo jibu lake, bila shaka sote tungependa kwenda peponi. Kama hivyo ndivyo, basi tiketi ya kwenda huko ni matendo mema na kujiepusha na uovu.
Tukumbuke mshahara wa dhambi ni mauti, bali karama ya Mungu ni uzima wa milele.

Je, nini kitaendelea?  Fuatilia siku ya Ijumaa kwenye gazeti la Championi Ijumaa.

2 comments:

  1. Are you a business man or woman? Do you need funds to start up your own business? Do you need loan to settle your debt or pay off your bills or start a nice business? Do you need funds to finance your project? We Offers guaranteed loan services of any amount and to any part of the world for (Individuals, Companies, Realtor and Corporate Bodies) at Como puedo solicitar un crédito con ustedes ?our superb interest rate of 3%. For application and more information send replies to the following E-mail address: david.mutukufinance60@yahoo.com

    Thanks,
    Mr David Mutuku.

    ReplyDelete

Powered by Blogger.