ad

ad

The Last Breath (Pumzi ya Mwisho) - 11

MACHO yake yalikuwa yamezama kwenye albamu aliyoikuta ndani ya begi walilokamatwa nalo mateka, akitaka kufahamu picha ndani ya albamu zilikuwa ni za akina nani.
“No, stop!” (Hapana, acha!) lakini tayari alishachelewa risasi zilishaanza kurindima, macho yake yakatua kwa mwanaume aliyekuwa akihangaika kukata roho, risasi ilishapenya sehemu ya juu ya kifua upande wa moyo na damu nyingi ilikuwa ikimtoka.

Huku machozi yakimtoka, Kamanda Janette alimwamuru mwasi amfungulie na tayari Johnson alishakata roho. Ni majonzi, vilio hatimaye mazishi yakafanyika, Melania na mama yake wakabaki wakiomboleza.
Mpango mmoja tu uliokuwa juu yao, walitaka kutoroka na kurejea nyumbani. Je watafanikiwa kutoka katika kambi hiyo salama?
SONGA NAYO…
AWANIJUI!” Kamanda Janette aliongea akimwangalia mama yake.
“Akina nani?”
“Hawa waasi, nimeshaamua kuachana na ukatili, nataka kwenda Tanzania nikaishi maisha ya kawaida, kwanza sikuchagua kuwa hapa, wao ndiyo walinilazimisha! Nataka kutubu dhambi zangu zote, kisha nimrejee Mungu wangu!” aliongea Janette akimaanisha alichokuwa akikisema, macho yake yalionyesha hivyo.
“Ahsante mwanangu, kama unalifahamu hilo.”
“Nafahamu mama!”
“Sasa tutafanyaje?”
“Tutaondoka, lakini itakuwa ni safari ngumu sana, sijui kama utaiweza na maisha yetu yatakuwa hatarini, tunamhitaji Mungu ili tuweze kufika Tanzania, hapo katikati kama unavyojua ni pori lenye wanyama wakali, isitoshe hawa watu hawatakuwa tayari kuona ninaondoka, lazima watatufuata msituni kutusaka ili wanirudishe kambini, jambo ambalo sitakuwa tayari kulifanya.”
“Hakuna shida, Mungu atakuwa na sisi.”
“Basi acha niangalie nini cha kufanya.”
Kwa wiki nzima Kamanda Janette alijifanya kama vile ameahirisha kile alichokuwa akikifikiria, akaendelea kuongoza mipango ya mapambano. Mara mbili alikwenda msituni kupambana na majeshi ya serikali na kurejea akiwa salama, mara ya tatu alipokwenda nyakati za usiku, aliwachenga waasi na kurejea kambini ambako alimchukua mama yake kupitia mlango wa nyuma, pamoja na bunduki mbili aina ya SMG na mikanda ya kutosha ya risasi, wakijua kabisa mbele kungekuwa na mapambano.
Akielewa walikokuwa wenzake, Kamanda Janette aliamua kuchukua njia ya upande wa pili, kuelekea kaskazini, lengo lake likiwa ni kutembea kwa miguu msituni mpaka afike kwenye mji ulioitwa Bumba, karibu kabisa na mpaka wa Congo na nchi ya Jamhuri ya Afrika ya Kati, alitaka waingie katika nchi hiyo ambako wangeendelea na safari yao hadi Sudan, kisha Uganda na baadaye Tanzania.
Huo ndiyo mchoro aliokuwa ameutengeneza kwenye karatasi, ulikuwa ni rahisi kuusoma lakini mgumu kuutekeleza, halikuwa jambo rahisi kufika Bumba, kilometa elfu mbili ukiwa msituni mahali pasipo na barabara, lakini ilikuwa ni lazima wapitie njia hiyo ili kuwapoteza maboya waasi ambao Kamanda Janette alielewa kabisa lazima wangewafuata.
Hapakuwa na mbalamwezi, giza lilikuwa totoro, msaada wa tochi uliwasaidia kupita katikati ya vichaka na chini ya miti mikubwa, bunduki zikiwa tayari kushambulia yeyote ambaye angekuja mbele yao. Usiku mzima mpaka kunapambazuka walikuwa wametembea umbali wa kilometa zisizozidi tano kwa sababu ya unene wa msitu na miiba mingi iliyokuwa njiani.
Kulipokucha hawakutaka kupumzika, wao huo ndiyo ulikuwa wakati mzuri zaidi wa kutembea wakiwa wanaona kule walipokuwa wakielekea na mahali walipokuwa wakikanyaga, hii iliwasaidia kwenda umbali mrefu chini ya miti, mpaka giza linaingia tayari walishatembea kilometa ishirini na tano, hivyo kufanya jumla ya kilometa walizotembea kufikia thelatini, hii ilimaanisha bado mbele yao kulikuwa na kilometa elfu moja mia tisa na sabini mpaka kufika Bumba.
“Unajisikiaje mama?” Kamanda Janette aliuliza.
“Najisikia vizuri tu mwanangu Melania.”
“Kweli?”
“Kwani una wasiwasi?”
“Sana.”
“Miaka yote niliyokuwa na majeshi ya serikali nikikutafuta, mwili wangu umepata ukakamavu mkubwa mno, wala usiwe na wasiwasi.”
Mazungumzo hayo yakifanyika wote walikuwa juu ya mti, hawakutaka kuendelea na safari usiku huo, wakisubiri asubuhi jua litoke ndiyo wasonge mbele. Mvua kubwa ilikuwa ikinyesha tena ya radi na upepo mkali, walikumbatia mti ili wasiweze kudondoka chini.
Kulipokucha asubuhi, safari ikaendelea tena mpaka jioni. Huo ndiyo ukawa utaratibu wao wa kila siku, kutembea mchana na kulala usiku tena juu ya mti, kulipokucha asubuhi walisonga mbele wakipunguza kilometa kuelekea Bumba, kila mmoja akiwa na hamu ya kufika Tanzania ambako Kamanda Janette hakupakumbuka vizuri kwani alipoondoka alikuwa na umri wa miaka mitano.
Ilipofika jioni kama kawaida yao walipanda tena juu ya mti kulala, lakini kabla hata hawajapitiwa na usingizi, walishangaa kusikia mbwa akibweka chini yao! Haikuwa kawaida hata kidogo kukutana na mbwa wa kufugwa nyumbani katikati ya msitu usiku, kwa miaka yote ambayo waliishi msituni wakipigana vita, hata siku moja hawakuwahi kuona tukio la aina hiyo, Kamanda Janette akashtuka na kusogeza bunduki yake karibu akiwa tayari kuanza kuachia risasi.

***
Waasi waligundua kwamba Kamanda Janette alishaondoka, kiongozi aliyekuwa msaidizi wake, Kamanda Otimanya aliwaamuru wote warudi kambini baada ya mapigano kumalizika, huko hawakumkuta. Uamuzi uliofikiwa ni kumsaka kila upande wa msitu ili arejeshwe kambini na kuuawa maana waliamini kuondoka kwake ulikuwa ni usaliti na ungewaletea matatizo makubwa sana katika mapambano maana alifahamu siri zao nyingi.
“Hakikisheni anapatikana, mimi naondoka na kundi moja kuelekea upande wa kaskazini, tutampata tu!”
“Sawa kamanda!”
“Wewe Mrenge, elekea kusini, Kijoti elekea magharibi, Muyambi elekea mashariki, kila kundi liwe na mbwa ambaye atakuwa ananusa ardhini kufuata mahali walipopita, lazima tutawapata tu, hakuna kurudi hapa bila Janette na mama yake kupatikana, msiwaue huko, waleteni mpaka hapa kambini ili tuwaadhibu tunavyojua sisi.”
“Sawa Kamanda!”
Wote wakakubaliana na makundi manne ya waasi, kila moja likiwa na idadi ya waasi mia moja wenye silaha kali wakaondoka kuelekea upande walioamriwa kwenda, kila kundi likiwa na mbwa waliokuwa wataalam wa kunusa mahali walipopita wanadamu.
Kamanda Otimanya aliongoza kundi lake akiwa na mbwa wawili, hatua chache tu kutoka kambini, mbwa walibweka, kuashiria kwamba walikuwa wamesikia harufu ya binadamu aliyekuwa akitoroka, walikuwa ni mbwa wenye mafunzo ya kazi hiyo, wakainamisha pua zao ardhini na kuanza kusonga mbele wakipita katikati ya vichaka kuelekea kaskazini bila kusimama mahali popote isipokuwa wakati wa kupata chakula peke yake, baada ya hapo safari iliendelea, usiku na mchana.
Kadri walivyokuwa wakisonga mbele ndivyo sauti za kubweka zilivyoongezeka,hatimaye siku ya pili usiku, walifika chini ya mti ambako harufu haikuendelea mbele, wakaanza kubweka kwa nguvu! Kamanda Otimanya na kundi lake wakaja mbio wakikimbia kuelekea kwenye mti huo, walipofika kabla hawajafanya lolote walishangazwa na idadi ya risasi nyingi zilizomiminika kutoka mtini.
Kamanda Janette na mama yake walikuwa wamefanya kazi nzuri, hapo hapo wakaserereka hadi chini ambako walianza kukimbia wakipita katikati ya vichaka, huku wakisikia nyayo za watu wakiwakimbiza kwa nyuma.
“Mama ongeza mwendo!”
“Kuna kitu kimening’ata kwenye mguu.”
“Nini tena?” aliuliza Kamanda Janette akiogopa kuwasha tochi kwa hofu ya kuonekana mahali walipokuwa.
Haraka akarejea mpaka mahali mama yake alipokuwa ameketi, akasikia harufu ya wali katika eneo ambalo alikuwa na uhakika kabisa hapakuwa na binadamu, mara moja akaelewa mama yake alikuwa ameng’atwa na nyoka! Alichokifanya ni kuingiza mkono kwenye mfuko wake wa suruali na kutoa mpira ambao kila mwasi alitembea nao maana matukio ya nyoka yalikuwa kawaida, akamfunga mama yake kwenye mguu uliong’atwa kisha wakaanza kwenda mbele kwa kasi ndogo.
“Maumivu yanaongezeka!”
“Twende mama, jikaze, watatuua!”
“Sawa, lakini nashindwa kutembea.”
“Njoo!” alisema Kamanda Janette na kumpakata mama yake begani.
Safari ikaanza akikimbia kwenda mbele, ghafla akasikia kelele nyingi mbele yake,  walikuwa wamezingirwa na waasi! Haraka akalala chini na kumlaza mama yake kando, hatua za waasi wakitembea kuelekea mahali walipokuwa zikaendelea kusikika.
Waasi wakiwa mita chache mbele yake alinyanyuka ghafla na kuanza kumimina risasi, kwa utalaam wa kulenga shabaha aliokuwa nao, ingawa kulikuwa na giza, alishangaa kuona mbele yake watu wote waliokuwa wamesimama wamelaliana kimya.
Haraka akanyanyuka na kumbeba tena mama yake begani, kisha kugeuka na kuanza kukimbia kuwavuka watu alioamini kwamba ni maiti mbele yake, hakwenda mbele sana, akasikia mlio wa risasi kisha maumivu kwenye bega lake la kulia alilombebea mama yake, akalala chini tena na kumlaza mama yake kisha kutoka mbio akikwepa risasi na kumimina nyingi kutoka upande zilikotokea, kikundi cha watu  kilichokuwa upande huo kikadondoka chini,  akaamini kwa mara nyingine tena alikuwa ameondoa kizuizi, haraka akarudi mahali alipomwacha mama yake lakini hakumkuta!

Je, nini kitaendelea? Mama yake amekwenda wapi? Fuatilia wiki ijayo siku ya Jumatatu katika gazeti la Championi Jumatatu.

No comments

Powered by Blogger.