The Last Breath 6
Johnson na mwanaye Melania, wanapata ajali mbaya baada ya ndege waliyokuwa wakisafiria kutoka Kinshasa, Kongo kupata ajali mbaya wakiwa pamoja na abiria wengine.
Baada ya injini mbili za ndege hiyo kulipuka, ndege inashuka kwa kasi ya ajabu na kwenda kujibamiza ardhini katikati ya msitu mnene. Baada ya ajali hiyo, inaaminika kuwa watu wote wamekufa lakini haiwi hivyo kwani Johnson na mwanaye, wamenusurika.
Taarifa za ajali hiyo mbaya, zinamfikia Loveness, mwanamke wa Kitanzania aliyekuwa akifanya kazi katika Shirika la Kimataifa la Kuwahudumia Wakimbizi (UNHCR) ambaye pia alikuwa mke wa Johnson na mama wa Melania.

Baada ya injini mbili za ndege hiyo kulipuka, ndege inashuka kwa kasi ya ajabu na kwenda kujibamiza ardhini katikati ya msitu mnene. Baada ya ajali hiyo, inaaminika kuwa watu wote wamekufa lakini haiwi hivyo kwani Johnson na mwanaye, wamenusurika.
Taarifa za ajali hiyo mbaya, zinamfikia Loveness, mwanamke wa Kitanzania aliyekuwa akifanya kazi katika Shirika la Kimataifa la Kuwahudumia Wakimbizi (UNHCR) ambaye pia alikuwa mke wa Johnson na mama wa Melania.

Anapatwa na shinikizo la juu la damu ambalo baadaye linamsababishia kiharusi na anasafirishwa mpaka Dar es Salaam kwa ajili ya kufanyiwa upasuaji wa kichwa.
Johnson na Melania wanaporejewa na fahamu zao, wanajikuta katikati ya msitu mnene, wakiwa hawajui watasalimika vipi. Baadaye wanakutana na wenzao wawili ambao nao wanapoteza maisha.
Hali ya Johnson nayo inazidi kuwa mbaya na anaelekea kukata roho. Mara wanaibuka watu wa ajabu na kutaka kumbaka mtoto mdogo Melania, akiwa na umri wa miaka mitano tu.
Je, nini kitafuatia? “
Daaaady! Daaady! Daaaady!” (Babaaaa! Baabaaaa! Babaaa!) Melania aliita kwa sauti ya juu lakini hakupata msaada wowote.
“Dad dead! Se detendre, do something good with you” (Baba amekufa! Tulia, tufanye kitu kizuri na wewe) alisema mmoja wa watu hao akichanganya na maneno ya Lugha ya Kifaransa.
Melania alikuwa amelazwa ardhini, amekandamizwa vizuri, hakuwa na la kufanya, juhudi zake zote za kujinasua hazikuzaa matunda. Katika umri wa miaka mitano aliokuwa nao hakuwa na uwezo wa kujiokoa, alibaki akilia bila msaada wowote huku mwanaume mkubwa, zaidi hata ya baba yake akitaka kumlalia juu yake.
“Arretez, que faites-vous?” (Acha, mnafanya nini?) ilikuwa ni sauti nyingine nzito ikitokea kwenye kichaka.
Watu wote waliokuwa wamemlaza Melania ardhini, wakamwachia na kusimama wima huku wakipiga saluti! Ilivyoonekana aliyetoa sauti alikuwa ni kiongozi wao, Melania akakurupuka na kumkimbilia mwanaume huyo, akamshika miguuni akimwomba msaada, wengine wote wakasambaa.
“Qui etes-vous? Et que faites-vous ici?” (Wewe ni nani na unafanya nini hapa?) aliuliza mwanaume huyo kwa sauti ya kukwaruza.
Melania hakuelewa chochote kilichosemwa, yeye akaendelea kulia tu kwa uchungu huku akimwonesha mwanaume huyo mahali baba yake alipokuwa. Kwa sababu hawakuelewana, alichokifanya mwanaume huyo mwenye mwili wenye misuli ni kumbeba juujuu begani kwake na kuanza kuondoka naye kuelekea mahali ambako Melania hakupatambua.
Kilometa kama mbili hivi mbele, alishangaa kufika mahali kulikokuwa na vibanda vingi vya nyasi, kikubwa kikiwa katikati na kulikuwa na watu wengi waliobeba bunduki, miili yao ikiwa imezungukwa na mikanda ya risasi!
Kila kitu kilifanana kabisa na sinema ambayo Melania aliwahi kuiangalia nyumbani kwao iitwayo The Rebels in The Jungle ambayo iliwaonesha waasi walioishi porini huko Afrika Magharibi wakiwafundisha watoto kutumia bunduki na kufanya mauaji.
Baada ya kushushwa, Melania alipelekwa moja kwa moja kwenye kibanda cha katikati ambako alipewa chai na viazi, kisha kutandikiwa godoro pembeni mwa kitanda kikubwa na kulala. Hakuelewa kabisa mahali hapo palikuwa ni wapi na watu hao ni akina nani, kila alipomkumbuka baba yake alianza kulia kwa uchungu.
Chumba kilijaa bunduki na picha mbalimbali za viongozi, akatambua moja ilikuwa ni ya Laurent Kabila wa Kongo ambayo aliwahi kuiona nyumbani, akagundua pengine walikuwa nchini Kongo. Usiku ulipoingia alilala kwenye kibanda hichohicho kwenye godoro bila kuguswa na mtu yeyote, hakupata usingizi, usiku mzima alikuwa akimkumbuka baba yake na pia mama waliyemwacha Kinshasa.
Tukio la kuanguka kwa ndege lililotokea halikuiacha akili yake, alishindwa kuelewa ni kitu gani hasa kilitokea mpaka akawa hai muda huo. Pamoja na umri mdogo alimshukuru Mungu kupindukia huku akimwomba amwondoe eneo hilo na kumrejesha nyumbani alikotokea na pia apokee roho ya marehemu baba yake.
Kulipokucha asubuhi, mtoto mmoja wa kiume, mweusi, mwenye macho mekundu aliitwa chumbani kwa mwanaume aliyemwokoa, ambaye watu wote walimwita Commandant na kumpigia saluti na kutakiwa kuongea na Melania kwa lugha ya Kiingereza.
“Who are you?” (Wewe ni nani?)
“Melania Johnson!”
“Where are you from?” (Unatokea wapi?)
“Tanzania.”
“I am Paul Ouma, from Uganda!”(Naitwa Paul Ouma, natokea Uganda!)
“I want to go home!”(Nataka kwenda nyumbani!)
“Home?”(Nyumbani?)
“There is no home for you, except here!”(Hakuna nyumbani kwingine isipokuwa hapa!) aliongea kijana huyo na kwenda mbele zaidi kwa kumsimulia jinsi ambavyo yeye na wazazi wake wawili walitekwa na waasi hao porini wakiwa na gari lao, wakauawa kinyama na yeye peke yake ndiye akachukuliwa na waasi akiwa na umri wa miaka mitatu, mpaka wakati huo alikuwa na umri wa miaka kumi na sita lakini hakuwahi kurejea nyumbani.
Melania akaangua kilio cha nguvu zaidi, ilikuwa haiwezekani kabisa amalizie maisha yake porini, alitaka kwenda kwa mama yake hata kama baba yake mzazi alikuwa marehemu. Alimsimulia kijana huyo kila kitu kilichotokea, ndege ilivyoanguka na watu walivyokufa, hatimaye baba yake alivyofia porini. Paul akamsimulia Commandant, kila kitu huku akionyesha msisimko na furaha.
“Peut-elle nous montrer ou I’ avion s’est ecrase?” (Anaweza kutuonesha mahali ndege ilipoangukia?) aliuliza Commandant na Paul akamuuliza Melania ambaye alikubali.
Kilichofanyika baada ya hapo ni Melania kubebwa begani na kuanza kuongoza kundi la watu kumi wenye silaha akiwemo Paul aliyebeba bunduki kubwa iliyomzidi urefu, wote walikuwa wakielekea mahali ambako ndege iliangukia. Kilichomshangaza Melania ni kwamba walipofika eneo ambalo alimwacha baba yake, maiti yake haikuwepo!
Alijiuliza maswali mengi bila kupata majibu lakini mwisho akawafikisha watu hao mahali ndege ilipoangukia, harufu ilikuwa kali, inzi zikiwa zimetapakaa kila mahali, miili ya watu waliokufa ikiwa imevimbiana na kunuka! Fisi walikuwepo wakila mizoga. Bunduki ya Paul ilifyatua risasi nyingi na kuwaua fisi wote.
Kilichofanyika baada ya hapo ni kuanza kupekua mabaki ya ndege hiyo, wakakutana na sanduku kubwa la chuma, wakalivunja na kukuta ndani yake kuna almasi na dhahabu nyingi kupindukia, kumbe ndege iliyowabeba Johnson na mtoto wake ilikuwa ikisafirisha almasi na dhahabu kuelekea Nairobi, makadirio ya chini ulikuwa ni mzigo wa tani mbili na nusu.
Watu wote walioambatana na Melania walishangilia kwa tukio hilo, wakabeba mzigo wao na kurejea kambini ambako watu wote walikusanywa na kuelezwa juu ya kilichotokea, Melania akatambulishwa kwa watu wote, alishangaa kuona kulikuwa na watoto wadogo ingawa yeye alionekana ndiye mwenye umri mdogo kuliko wengine. Akakabidhiwa kwa Paul kuwa ndiye mwenyeji wake.
Maisha msituni yakaanza, hatimaye Melania akaacha kuwa analia, akazoea! Ratiba za kambi hiyo ambayo baadaye alikuja kujua ni ya waasi wa kundi la Congolese Patriotic Front, wakiongozwa na Commandant Piere Kazimungu, ilikuwa ni asubuhi kujifunza Kifaransa, baadaye kujifunza matumizi ya bunduki na kulenga shabaha na mazoezi mbalimbali ya kijeshi.
Yalikuwa ni mateso makubwa sana kwa Melania, lakini ilibidi ayavumilie. Kitu kingine kilichomsikitisha zaidi ni chakula, kilikuwa kibaya mno, alikonda na kupoteza uzito mkubwa sana wa mwili. Akabadilika kabisa, hata siku moja hakuwasahau baba na mama yake na aliamini ipo siku angeondoka mahali hapo.
Paul alikuwa naye kila mahali, alimlinda asifanyiwe vitendo vibaya vya ubakaji ambavyo vilikuwa ni kawaida kwenye kambi hiyo. Kila mwanaume aliyetaka kumfanyia Melania ubaya alikutana na mkono wa Paul, ambaye pamoja na umri mdogo alikuwa katili kupindukia. Ndani ya muda wa mwezi mmoja tu ambao Melania alikaa kambini hapo, alishavunja miguu watu watano kwa risasi na kuua wawili waliotaka kumbaka.
Melania alijisikia salama sana mikononi mwa Paul, alimwona kama baba yake mlezi.
Je, nini kitafuata? Melania atafanikiwa kutoka porini? Mama yake anaendeleaje hospitali? Maiti ya Johnson imekwenda wapi? Imeliwa na wanyama? Fuatilia siku ya Jumatano katika gazeti la Championi Jumatano.
CHANZO CHA CHOMBEZO HILI NI GLOBAL PUBLISHERS
Post a Comment