ad

ad

MASSACRE (MAUAJI YA HALAIKI) SEHEMU 01

Na Nyemo Chilongani
Kila aliyekuwa akizisoma taarifa ambazo zilikuwa zimeandikwa katika magazeti mbalimbali yaliyokuwa yakitoka katika siku hiyo alibaki akishangaa tu. Watu wakashtuka kupita kawaida, habari ile ilionekana kuwasisimua kupita kawaida. Imani juu ya wachungaji ikaanza kuondoka katika mioyo ya watu, hasa waumini wa dini ya Kikristo.
  
 Kanisa likaonekana kupotea njia, kila kitu ambacho kilikuwa kinaendelea hasa katika makanisa mbalimbali kilionekana kuwa kama maigizo juu ya jukwaa au ndani ya luninga. Shetani akaonekana kuliteka kanisa na kulifanya alivyotaka kulifanya. Dhambi ambayo ilionekana kufanyika kwa kiongozi mmoja wa kanisa moja ikaonekana kama imetokea katika makanisa yote nchini Tanzania. Watu wengine wakataka kujitoa kutoka katika imani ya Kikristo kwa kudai kwamba shetani alikuwa amemzidi nguvu kila mtu.
 Wokovu wote ambao ulikuwa ukiendelea katika makanisa yote ukaanza kuyumba. Watu wengine wakaahidi kutokuhudhuria tena makanisani mwao kutokana na imani juu ya viongozi wao kuanza kupotea. Idadi kubwa ya watu wakaanza kupoteza uaminifu wao juu ya wachungaji wa makanisa yao.

  MCHUNGAJI ATAKA KUMBAKA BINTI OFISINI’. Hicho kilikuwa ni kichwa cha habari ambacho kilikuwa kikisomekana katika magazeti mbalimbali jijini Dar es Salaam. Bado watu walikuwa wakiendelea kushangaa, hawakuamini kama mchungaji Matimya wa kanisa la Praise And Worship lililokuwa Mwenge angeweza kufanya kitu kama kile ambacho kilikuwa kimeonekana kuandikwa katika magazeti mengi.

  Habari ile ilionekana kuwa habari iliyokuwa na furaha kwa watu wote ambao walikuwa hawawapendi Watumishi wa Mungu. Watu wakaanza kupeana taarifa majumbani mwao huku kila aliyepewa taarifa ile akaanza kuelekea barabani kulinunua gazeti moja ambalo lilikuwa na habari ile.

  Katika mwaka mzima, habari ile ndio ambayo ilifanikiwa kuuza nakala nyingi kuliko habari yoyote iliyowahi kuandikwa katika mwaka huo. Mpaka inafika saa saba mchana, hakukuwa na gazeti lolote lililokuwa na habari ile ambalo lilikuwa katika meza ya wauza magazeti.
  
 Kila mtu ambaye alikuwa akiyaona magazeti yale, aliyanunua. Siku ya mwisho ikaonekana kukaribia kutokana na shetani kuonekana kulivamia kanisa hasa kwa viongozi mbalimbali wa makanisa. Aibu kubwa ikaanza kulikumba kanisa la Praise And Worship lililokuwa Mwenge.
  
 “Haiwezekani hata kidogo. Mbona huyu Mchungaji ni Mtumishi mzuri wa Mungu! Tena kwa sasa anataka kuwa Askofu Mkuu. Hawezi kufanya hivi” Sauti ya msichana mmoja ilisikika ikiwaambia wenzake huku mkononi akiwa ameshika Biblia katika kipindi ambacho walikuwa wakitoka kanisani siku hiyo ya Jumapili.
  
 “Kwa nini isiwezekane kwa mtu kama huyu kufanya hivi? Tumemkaribisha shetani sisi wenyewe. Acha awatumie watumishi wa Mungu anavyotaka” Mwanamke mmoja alisikika akisema huku akishika vizuri Biblia yake.

  Habari hiyo ndio ambayo ilikuwa imeshika hatamu katika kipindi hicho. Kila mtu ambaye alikuwa akiiona habari ile na kuisoma, alishtushwa kupita kiasi. Picha kubwa ya rangi ya mchungaji Matimya ilikuwa ikionekana vizuri katika kila gazeti ambalo lilikuwa na habari ile.
                                                            ****
   Mchungaji Matimya alikuwa amekaa katika kiti cha nyuma kabisa ndani ya kanisa lake. Uso wake alikuwa ameuinamisha chini huku machozi yakimtoka. Mbele yake aliiona aibu kubwa ikiwa imemkuta, hakuelewa ni kitu gani ambacho alitakiwa kukifanya ili Watanzania waelewe kwamba hakuwa amekifanya kile kitu ambacho kilikuwa kikitangazwa sana na vyombo vya habari.
  
 Hakukuwa na mtu ambaye alionekana kumuamini Mchungaji Matimya, kila mtu kanisani humo alimuona kuwa kama Mwakilishi wa shetani ambaye aliletwa kanisani humo kwa ajili ya kulitia aibu kanisa. Ingawa ibada ilikuwa ikiendelea kanisani humo, macho ya washirika wengi walikuwa yalikuwa yakimwangalia Mchungaji Matimya.

   Machozi yale ambayo yalikuwa yakimtoka, yalionekana kuwa kama ya kinafiki machoni mwa washirika wa kanisa lile. Mchungaji Matimya hakuwa peke yake, familia yake ilikuwa pembeni yake. Mkewe, Bi Meriana alikuwa upande wake wa kushoto huku watoto wake wawili, Benedict na Angelina wakiwa katika upande wa kulia.

  Kilio cha chini chini kilikuwa kikisikika kutoka kwa Bi Meriana. Kila alipokuwa akikumbuka aibu ile ambayo ilikuwa imemkuta mumewe, alizidi kuumia. Hawakuonekana kufuatilia kitu chochote kilichokuwa kinaendelea kanisani mule. Vichwa vyao vilikuwa vikifikiria mbali.
  
 Ibada iliendelea kama kawaida. Mara baada ya muda wa matangazo kuingia, Askofu wa dhehebu hilo la Praise And Worship, Askofu Lugakingira akasimama na moja kwa moja kuelekea katika madhabau ya kanisa hilo na kuchukua kipaza sauti. Kabla hajaongea kitu chochote kile, alitulia kwa muda huku akiliangalia kanisa.
    
Kila mtu alikuwa kimya tayari kwa kusikiliza kile ambacho Askofu alitaka kukizungumza mahali hapo. Askofu alianzia mbali sana lakini huku lengo lake kubwa likiwa ni kufika katika kitu ambacho kilimfanya kuja katika kanisa lile katika siku hiyo ya Jumapili. Mara baada ya kutumia dakika kumi kuongea mambo tofauti tofauti, hapo hapo akamtaka Mchungaji Matimya kwenda mbele ya kanisa lile.
  
 Huku akionekana kuwa katika lindi la mawazo, Mchungaji Matimya akainuka kutoka katika kiti alichokuwa amekaa kule nyuma ya kanisa na moja kwa moja kuanza kuelekea mbele ya kanisa. Minong’ono ikaanza kusikika kutoka kwa washirika ndani ya kanisa lile, Mchungaji Matimya hakuonekana kujali, aliendelea kupiga hatua hadi mbele ya kanisa lile.
  
 “Nadhani hakuna mtu asiyejua kitu ambacho kimenifanya kuja ndani ya kanisa hili kwa siku ya leo. Lilikuwa ni suala ambalo lilihitaji kumuita Mchungaji Matimya. Niliongea nae kwa kirefu sana na kukiri kila kitu pasipo kuficha kitu chochote kile” Askofu Lugakingira aliliambia kanisa na kuendelea.
  
 “Ningependa kumpa nafasi ya kulieleza kanisa kama hiki kitu ambacho kimetawala kila sehemu ni kweli au kuna uongo wowote” Askofu Lugakingira alisema na kisha kumpa kipaza sauti mchungaji Matimya.

  Mchungaji Matimya hakuongea kitu chochote kile, alibaki kimya huku macho yake yakiangalia chini. Kila alipotaka kuongea kitu, aliuona mdomo wake kuwa mzito kufunguka, hakujua aseme kitu gani mbele ya kanisa na mbele ya familia yake. Kumbukumbu ya maisha yake ya nyuma ikaanza kujirudia kichwani mwake, katika hatua nyingine, alijuta kwa nini aliitwa kuwa Mchungaji.

  “Nalihitaji kanisa msamaha. Ni kweli nilitaka kumbaka Judith ndani ya of….” Mchungaji Matimya alisema lakini hata kabla hajamalizia sentensi yake, akaanza kulia. Sauti ya kilio chake kilisikika kanisa zima kutokana na kipaza sauti alichokuwa amekishika. Wanawake wakashindwa kuvumilia, nao wakaanza kulia.
  
 Mtoto wake, Benedict hakuweza kuvumilia kubaki kanisani hapo akasimama na moja kwa moja kuanza kuelekea nje ya kanisa lile. Moyo wake uliumia kupita kiasi, maneno ambayo aliongea baba yake mbele ya kanisa yalionekana kumuumiza kupita kawaida.
  
 Mara baada ya kufika nje ya kanisa, moja kwa moja akalifuata gari lao na kuingia ndani na kisha kuliwasha. Kila mtu ambaye alikuwa nje ya kanisa alikuwa akimwangalia Benedict ambaye akaliwasha gari lile na kuondoka katika eneo lile la kanisa.

  Mchungaji Matimya akashindwa kuendelea, akakikabidhi kipaza sauti kwa Askofu Lugakingira ambaye alikuwa akimbembeleza kwa kumpiga piga mgongoni. Mchungaji Matimya akazidi kulia zaidi na zaidi, akapiga magoti chini huku uso wake akiwa ameuinamisha chini kwa aibu huku machozi yaliyokuwa yakimtoka kuloanisha sakafu ya pale madhabahuni.

  “Kila kitu kina sheria zake. Na hili kama dhehebu la Praise And Worship, mchungaji Matimya hatokuwa mchungaji wa kanisa hili tena. Tunamfungia kufanya huduma yoyote kwa muda wa mwaka mmoja na nusu” Askofu Lugakingira aliliambia kanisa.

  Idadi kubwa ya washirika ikaonekana kufurahia. Thamani ya mchungaji Matimya ikaonekana kushuka. Pepo la uzinzi likaonekana kumvaa mchungaji Matimya ambaye bado alikuwa pale mbele ya kanisa akiendelea kulia kwa uchungu. Kila kitu ambacho kiliendelea katika maisha yake kilionekana kuwa kama ndoto ambapo baada ya muda fulani angeamka kutoka katika usingizi mzito.
****
   Uchaguzi wa Askofu mkuu ndio ambao ulikuwa ukikaribia, siku tano tu ndizo ambazo zilikuwa zimebaki kabla ya uchaguzi huo. Wachungaji wawili, mchungaji Matimya wa kanisa la Praise And Worship la Mwenge lililoko jijini Dar es Salaam pamoja na mchungaji Mwakipesile wa kanisa la Praise And Worship lililokuwa Morogoro ndio ambao walikuwa wakiwania nafasi ya kuwa Askofu mkuu nchini Tanzania.
  
 Kila mtu alionekana kuwa na nafasi nzuri ya kuchukua nafasi hiyo lakini mchungaji Matimya ndiye ambaye alionekana kuwa na nafasi kubwa zaidi. Kila kanisa la dhehebu la Praise And Worship lililokuwa nchini Tanzania, jina la mchungaji Matimya ndilo ambalo lilikuwa likitajwa mara kwa mara.
   Wachungaji wengi walikuwa wakitamani Mchungaji Matimya achukue nafasi hiyo kutokana na huduma nzuri ambayo alikuwa akiitoa katika kanisa lake na makanisa mengine mbalimbali nchini. Hakuwa na roho ya majivuno kama aliyokuwa nayo mchungaji Mwakipesile.

  Kila mtu alivutiwa nae, kila mtu akatamani mchungaji Matimya achukue nafasi ile na kuwa Askofu mkuu. Asilimia zaidi ya themanini ya wachungaji wote wa dhehebu hilo walitamani mchungaji Matimya achukue nafasi hiyo ambayo ilitarajiwa kuachwa na Askofu Lugakingira siku chache zijazo.
   “Ni lazima nifanye kitu” Mchungaji Mwakipesile alijisemea huku akionekana kukasirika.
   Mbele yake hakuona dalili zozote za ushindi katika nafasi ya Uaskofu. Baadhi ya wachungaji ambao walikuwa katika upande wake, katika kipindi hicho walikuwa wamemsaliti. Kila kitu katika kipindi hicho kilionekana kwenda tofauti na matarajio yake ya nyuma.

  “Nitamtumia hata mshirika wake mwenyewe” Mchungaji Mwakipesile aliendelea kujisemea.
   Hakutaka kuendelea kubaki Morogoro, kitu alichokifanya siku iliyofuata ni kuchukua ndege na moja kwa moja kuanza kuelekea jijini Dar es Salaam. Hakutaka mtu yeyote afahamu juu ya safari yake hiyo ya ghafla, hakumpa taarifa hizo mtu yeyote zaidi ya msichana mmoja tu, Judith Simon ambaye alikuwa akiishi ndani ya jiji la Dar es Salaam.
*****
   Jina la Judith Simon wala halikuwa geni masikioni mwa washirika wa kanisa la Praise And Worship lililokuwa Mwenge. Binti huyu alikuwa na sifa zote ambazo msichana wa kisasa na mrembo alitakiwa kuwa nazo. Alikuwa na wembamba kama waliokuwa nao wasichana ambao walikuwa wakigombania nafasi ya kuwa mrembo wa Tanzania.

   Uso wake ulikuwa mwembamba, alikuwa akitembea kwa mwendo wa mapozi kana kwamba alikuwa hakanyag ardhi. Kila aliyekuwa akiuangalia mwendo wa Judith alikiri kwamba binti huyo alikuwa akitembea mwendo uliokuwa na mvuto kanisani hapo.
   Mashavu yake yaipendezeshwa na vishimo viliwili vilivyokuwa mashavuni mwake ambavyo vilikuwa vikionekana vizuri katika kila wakati alipokuwa akicheka au kutabasamu. Kila wakati Judith alionekana kuvutia.

  Uzuri wake ulikuwa ukionekana wakati wote. Haijalishi alikuwa amekarika, amenuna au ametabasamu, muda wote huo uzuri wake wa asili ndio ulikuwa ukionekana machoni mwa watu wengi.
  
 Judith alionekana kuwa mcha Mungu. Karama ya Uimbaji ambayo alikuwa nayo ndio ambayo ilimfanya kuzidi kukubalika katika kanisa hilo lililokuwa likiongozwa na mchungaji Matimya. Judith akaamua kujiunga na kwaya mojawapo iliyokuwa kanisani hapo. Kila mtu alionekana kubarikiwa katika vipindi vyote ambavyo Judith alikuwa akimsifu Mungu. Judith alikubalika na kila mtu kanisani hapo.

  Vijana hawakutaka kubaki nyuma kanisani hapo, harakati za kumtaka Judith zilikuwa zikiendelea kimya kimya kanisani hapo. Judith hakutaka kujirahisisha kwa wavulana kitu ambacho kiliwapelekea vijana wengi kusimamishwa huduma kanisani humo.
   “Watu wakijua?” Judith alimuuliza mchungaji Mwakipesile huku akionekana kuwa na hofu. Mchungaji Mwakipesile hakuongea kitu chochote, alibaki akimwangalia Judith na kisha kutoa tabasamu.
  
 “Utawaambia au?” Mchungaji Mwakipesile alimuuliza.
   Swali lile likaonekana kuwa gumu kwa Judith, alibaki kimya huku akimwangalia mchungaji Mwakipesile ambaye alionekana kumaanisha kile alichokuwa akikiongea kwa wakati huo. Alipoona Judith amekaa kimya, akachukua glasi iliyokuwa na juisi ya maembe na kisha kupiga fundo moja.
   “Kama hautowaambia nina uhakika hawatojua” Mchungaji Mwakipesile alimwambia Judith ambaye kwa kiasi fulani woga wake ukaonekana kupungua.
   “Na vipi kuhusu malipo?” Judith aliuliza.
   “Milioni tano baada ya kukamilisha kazi hii” Mchungaji Mwakipesile alijibu.
   “Sawa” Judith aiitikia na moja kwa moja kuondoka huku akijiandaa na kazi ambayo alitakiwa kuifanya.
****
   Alipomaliza kuongea na viongozi mbalimbali wa kanisa lake, mchungaji Matimya akaanza kuelekea katika ofisi yake iliyokuwa pembeni ya kanisa hilo. Alipoingia ofisini mwake, akaanza kuifuata kiti chake na kukalia, akaichukua Biblia ambayo ilikuwa mezani na kuanza kusoma baadhi ya maandiko.
  
 Alitulia kimya huku akiendelea kupitia baadhi ya maandiko. Mara kwa mara uso wake ulikuwa ukionyesha tabasamu kila alipokuwa akisoma andiko ambalo lilionekana kumvutia. Alitumia muda wa dakika thelathini kuyasoma baadhi ya maandiko ambayo alikuwa ameyadhamiria kuyasoma katika kipindi hicho. Alipomaliza kuyasoma maandiko hayo, akaifunika Biblia yake na kuanza kusali.

   Huku akiwa katikati ya sala, mara mlango ukasikika ukianza kugongwa kitu ambacho kilimpelekea kukatisha sala yake na kumkaribisha mgongaji. Mlango ukafunguiwa na msichana Judith kuingia. Mchungaji Matimya akaonekana kushtuka kwani halikuwa jambo la kwaida kwa mgeni kuingia ndani ya ofisi yake katika kipindi hicho ambacho alijiandaa kufunga ofisi yake.
  
 Judith akaanza kupiga hatua kukifuata kiti cha wageni na kisha kutulia huku kikiwa mbele ya meza ile pale ofisini. Judith hakuongea kitu chochote kile, alibaki akimwangalia mchungaji kwa kutumia macho ambayo yalionyesha mshtuo mkubwa kwa mchungaji Matimya. Mchungaji Matimya akasimama na kuanza kumsogelea Judith ambaye alibaki kimya akijifikiria namna ya kufanya kile ambacho alitakiwa kukifanya kwa wakati ule.
   
 “Kuna nini tena judith?” Mchungaji Matimya alimuuliza Judith.
   “Nina kiu mchungaji” Judith alijibu.
   “Kiu ya Neno la Mungu au?”
 Unataka niwe nakutumia CHOMEZO watu 200 wa kwanza kulike PAGE YA 2JIACHIE Mtatumiwa imbox chomezo LIKE PAGE YETU HAPA ==>www.facebook.com/2jiachie

ITAENDELEA KESHO HAPA HAPA

No comments

Powered by Blogger.