ad

ad

POLISI BADO WAMSAKA MBUNGE WA CHADEMA

POLISI Jijini Arusha bado inamsaka Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema Chadema, lakini Kamanda wa Polisi wa Mkoa, Liberatus Sabas, amesema ‘watampata tu.’
 Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema Chadema.
Juzi Sabas alisema wanamtafuta Lema na wenzake watatu kwa lengo la kuhojiwa kuhusiana na vurugu zilizotokea kwenye mikutano ya kampeni za uchaguzi wa udiwani Kata ya Sombetini, ambapo watu kadhaa walijeruhiwa.
 
Kamanda alisema jana kuwa kumekuwa na malalamiko kwa upande wa Chadema dhidi ya CCM, kuwa wafuasi wa chama hicho wamekuwa wakisababisha vurugu katika mikutano yao.
Alisema CCM nao wanawalalamikia wanachama wa Chadema kuwa wanasababisha vurugu katika mikutano yao. 

Alisema tayari polisi wamekwishafanya mahojiano kwa wanachama kadhaa wa CCM na sasa wanataka kufanya hivyo kwa Chadema.
 
Alisema kwa kuanzia wanamtaka Lema na wanachama watatu, Anorld Kamde, na wengine kwa jina moja moja tu la Frank na Daud, kwenda polisi kwa mahojiano.
 
Alisema wakishakamilisha mahojiano hayo, watapeleka majalada Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, ambayo ndiyo ndiyo yenye mamlakama ya kufungua mashtaka. Hata hivyo, kwa upande wake, Lema alisema hana taarifa za kutafutwa kwake na polisi.
 
Alisema kama wanania hiyo, basi wafuate utaratibu wa kumkamata mbunge. Mwandishi wa habari hii alishuhudia polisi wakiwa doria maeneo mbalimbali ya Jiji, kuangalia kama kuna wafuasi wa Chadema ambao wana nia ya kuandamana.
 
Lakini hakuna mtu aliyejitokeza kuandamana jana, kama walivyodai awali Chadema kuwa wangeandamana, kupinga kufanyiwa vurugu na wanachama wa CCM katika kata ya Sombetini, inayogombewa ili kupata mshindi katika uchaguzi utakaofanyika Jumapili Februari 9, mwaka huu.
 
Kata zingine zitakazofanya chaguzi ndogo za madiwani nchini siku hiyo Februari 9, mwaka huu, majina ya kata na mikoa yake kwenye mabano ni: Segela na Mpwayungu (Dodoma), Ukumbi, Ibumu na Nduli (Iringa), Malindo na Santilya (Mbeya),Tungi na Rudewa (Morogoro), Mkwiti, Kiwalala na Namikago (Lindi), Mkongolo (Kigoma), Mrijo (Dodoma), Magomeni na Kibindu (Pwani), Mtae na Kiomoni (Tanga), Ubagwe (Shinyanga), Partimbo na Loolera (Manyara), Kilelema(Kigoma), Kasanga (Rukwa, Kiborloni (Kilimanjaro), Njombe Mjini (Njombe) na Nyasura mkoani Mara.
CHANZO NI HABARI LEO
Powered by Blogger.