Wanaomiliki silaha waonywa
JESHI la Polisi nchini limetoa onyo kali kwa watu wanaotumia vibaya silaha walizomilikishwa.
Onyo hilo lilitolewa jana na Msemaji wa Jeshi la Polisi, Mrakibu
Mwandamizi wa Polisi (SSP), Advera Senso, katika taarifa yake kwa vyombo
vya habari na kuwataka watu hao kuacha mara moja tabia hiyo na badala
yake wazingatie sheria na masharti waliyopewa wakati wa umilikishwaji.
Alisema kutokana na kushamiri kwa vitendo hivyo katika jamii, jeshi
hilo linaanza operesheni kali ya kuwabaini wote wanaofanya vitendo
hivyo, ikiwa ni pamoja na kuwanyang’anya silaha hizo kwa wale
watakaobainika kwenda kinyume cha sheria na matumizi ya silaha zao.
“Katika siku za hivi karibuni, imebainika baadhi ya watu
waliomilikishwa silaha kihalali wamekuwa wakitumia silaha hizo kinyume
cha malengo mazuri ya umilikishwaji.
Baadhi yao wamekuwa wakitoa vitisho kwa wananchi kwa kutumia silaha
hizo bila sababu za msingi wawapo katika maeneo mbalimbali, kama vile
kwenye mabaa, kumbi za starehe na hata kulipizana visasi, jambo ambalo
ni kinyume cha sheria na malengo ya umilikishwaji.
“Jeshi la Polisi linatoa wito kwa wananchi wote wazalendo na wenye
mapenzi mema na nchi yetu kutoa taarifa zitakazosaidia kuwabaini watu
wanaojihusisha na vitendo hivyo, ili waweze kukamatwa na kufikishwa
kwenye vyombo vya sheria,” alisema Advera katia taarifa yake hiyo.
Alisema wananchi wanaweza kutoa taarifa kupitia namba ya simu
0754785557 pamoja na namba za simu za makamanda wa mikoa au kwenye kituo
chochote cha Polisi.

Post a Comment