SHIBUDA ATIMULIWA KATIKA KIKAO CHA NDANI YA CHAMA HICHO KANDA YA ZIWA

MBUNGE wa Maswa Magharibi, John Shibuda (CHADEMA), ametimuliwa
katika kikao cha ndani ya chama hicho Kanda ya Ziwa Mashariki kwa madai
ya usaliti.
Uamuzi wa kutimuliwa kwa mwanasiasa huyo ulifikiwa juzi jioni mkoani
Shinyanga wakati Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe, alipokutana na
viongozi wa kanda hiyo katika kikao cha ndani kwa ajili ya mikakati ya
ujenzi wa chama.
Akizungumzia tukio hilo, Mwenyekiti wa CHADEMA Kanda ya Ziwa
Mashariki, Silvester Kasulumbai, alisema kuwa katika mkutano huo
uliowahusisha viongozi wa mikoa ya Shinyanga, Simiyu na Mara, kabla ya
Shibuda kutimuliwa, Mbowe alimpa nafasi ya kutetea tuhuma zilizotolewa
dhidi yake ikiwamo sababu ya kuhudhuria majukwaa ya mikutano ya Chama
Cha Mapinduzi (CCM).
“Mmoja wa wajumbe alisimama na kutoa hoja ya kuwa kikao hicho
hakiwezi kuendelea kujadili masuala ya msingi ya chama ilhali kukiwa na
watu wanaotoa taarifa kwa CCM na ghafla akamtaja mtu huyo kuwa ni
Shibuda,” alisema.
Kasulumbai aliongeza kuwa mtoa hoja alisisitiza kuwa Shibuda alipanda
katika jukwaa moja na viongozi wa CCM na kudai kuwa vyama vya upinzani
havina kitu, kwamba CCM ndicho chama tawala, hali aliyoeleza kuwa hata
mikakati itakayopangwa katika mkutano huo anaweza kuivujisha na hivyo
kumtaka Mbowe amtoe nje ya kikao hicho.
Kwa mujibu wa Kasulumbai ambaye pia ni Mbunge wa Maswa Mashariki,
baada ya hoja hiyo Mbowe aliwataka wajumbe wasiwe na jazba na wampe
nafasi Shibuda ili aweze kujitetea dhidi ya tuhuma zilizoelekezwa kwake.
Alisema baada ya Shibuda kupewa nafasi alieleza kuwa yeye kupanda
katika jukwaa la CCM si jambo la ajabu katika masuala ya kisiasa na
kutolea mfano hatua ya wenyeviti wa vyama vitatu vya CHADEMA,
NCCR-Mageuzi na CUF kukutana na Rais Jakaya Kikwete Ikulu huku wakijua
kuwa ni mwenyekiti wa CCM.
Kasulumbai alisema katika utetezi wake, Shibuda alisema kwamba mtu
mzima anapokuwa na shida yoyote hukimbilia kwa baba yake na kumaainisha
baba huyo ni chama kinachotawala yaani CCM.
Aliongeza kuwa kauli ya Shibuda iliwakasirisha wajumbe na kuwaudhi
zaidi, hivyo kuanza kumshambulia kwa maneno hali iliyomfanya Mbowe
kuingilia kati na kuwataka wajumbe kupiga kura kwa ajili ya kufikia
hitimisho juu ya uwepo wake katika kikao hicho.
“Zilipigwa kura akapata kura 38 zilizotaka aendelee kubaki ndani,
tano ziliharibika na 90 zilitaka aondolewe katika kikao na wajumbe
wakamuomba Mbowe afanye utaratibu wa kumuondoa kwa amani,” alisema
Kasulumbai.
Alipotafutwa kwa simu jana kuzungumzia tuki hilo, Shibuda alisema
wanachama na wafuasi wa CHADEMA walimuelewa vibaya alipopanda jukwaani
katika mkutano wa CCM mjini Geita.
Alisema wakati alipopanda jukwaani na kuonana na viongozi wa CCM,
alikuwa akiwakilisha kilio cha wakulima wa pamba wa Kanda ya Ziwa.
“Mimi ni mlezi wa wakulima wa pamba Kanda ya Ziwa na pale nilimfuata
Katibu wa CCM nikamueleza kuwa akamwambie mwenyekiti wake, Rais wa nchi
kwamba tunapata taabu na masilahi kidogo kwa kuwa tunanyonywa na
wajanja katika kilimo cha pamba,” alisema.
Kwa mujibu wa Shibuda, kitendo hicho angekifanya kwa kiongozi wa
chama chochote kilicho madarakani kwa kile alichoeleza kuwa ilani ya
wakati itakayokuwa inatekelezwa ni ya chama husika.
Aliongeza kuwa kwa nafasi yake ya mbunge anayetokana na CHADEMA hoja
yoyote atakayoipeleka serikalini na kufanikiwa zitakuwa ni juhudi za
chama badala ya watu kumfikiria kuwa msaliti.
“Kuna waganga njaa ndio wanaendekeza mifarakano ndani ya chama na hii
ipo katika vyama vyote, wanafanya hivi si kwa sababu ya masilahi ya
chama na nchi bali kuhakikisha matumbo yao yanashiba wakati wote kwa
kuendekeza misigano isiyo na ulazima,” alisema.
Aliongeza kuwa kama hatua ya kutaka kuwatetea wakulima wa pamba Kanda
ya Ziwa ni usaliti atakuwa tayari kuhukumiwa na kufukuzwa kwa hatua
hiyo.
CHANZO TANZANIA DAIMA.
Post a Comment