Muhongo ‘avuliwa’ nguo
MABILIONEA
wanne waliotajwa na Jarida la Forbes la nchini Marekani wiki hii,
wamemuumbua Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo,
ambaye amekuwa akiwabeza kwamba hawana uwezo wa kuwekeza kwenye sekta ya
gesi.
Kwa mujibu wa jarida hilo, Rostam Aziz, ametajwa kuwa kinara kwa
kumiliki utajiri wa dola za Marekani bilioni moja (sh trilioni 1.6),
hivyo kuwa na uwezo wa kumiliki vitalu zaidi ya vitano vya gesi.
Mwenyekiti Mtendaji wa kampuni za IPP, Reginald Mengi, ametajwa
kushika nafasi ya pili katika orodha ya mabilionea hao kwani ana uwezo
wa kumiliki pia visima zaidi ya vinne kutokana na utajiri wake wa dola
milioni 550 (sh bilioni 861).
Jarida hilo limeonyesha Mbunge wa Singida Mjini (CCM), Mohamed Dewji
‘Mo’, anashikilia nafasi ya tatu kwa kuwa na utajiri wa dola milioni 500
(sh bilioni 783), akifungana na Said Bakhressa katika nafasi hiyo (ya
tatu) ya orodha ya matajiri wa Tanzania na ya 38 kwa Afrika.
Mo na Bakhressa nao wametajwa kuwa na uwezo wa kumiliki vitalu vya gesi zaidi ya vitatu.
Wataalamu wa mambo ya uchumi, waliliambia gazeti hili jana kuwa kwa
viwango hivyo vya utajiri, mabilionea hao si tu kwamba wana uwezo wa
kuwekeza kwenye sekta ya gesi, bali pia wana sifa ya kuwekeza kwa pamoja
na wawekezaji wa nje.
Taarifa ya jarida hilo na kauli ya wachumi ni dhahiri kwamba imemvua
nguo Waziri Muhongo ambaye siku za hivi karibuni amekuwa akibeza uwezo
wa wafanyabiashara hao kwamba wanaweza kuwekeza kwenye juisi na soda,
akimlenga Mengi anayemiliki viwanda vya soda na Bakhressa viwanda vya
juisi.
Kauli hiyo ilimfanya waziri huyo kuingia katika mzozo na Dk. Mengi,
ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taasisi ya Uwekezaji nchini (TPSF).
Dk. Mengi amekuwa akisisitiza umuhimu wa ushirikishwaji wa Watanzania
katika uchumi wa gesi na kuishauri serikali kusitisha ugawaji wa vitalu
hadi sera ya gesi itakapokuwa tayari.
Rais Jakaya Kikwete naye aliwahi kusema uchimbaji wa kisima kimoja
cha gesi, unagharimu dola milioni 100, sawa na sh bilioni 150, hivyo
hakuna mzawa anayeweza kumudu gharama hiyo na kuwataka kujiunga katika
vikundi ili kuweza kumiliki ugawaji wa vitalu hivyo uliozinduliwa
mwishoni mwa Oktoba mwaka huu.
Kwa mujibu wa utafiti wa jarida hilo, ni wazi kuwa iwapo Rostam Aziz
ana nia ya kuwekeza katika sekta hiyo, anaweza kumiliki vitalu zaidi ya
vinne kutokana na kutajwa kuwa ndiye tajiri namba moja Tanzania kwa
sasa.
Utajiri wa Rostam unachangiwa zaidi na biashara ya mawasiliano ya simu za mkononi, ujenzi na uchimbaji wa madini.
Anamiliki asilimia 35 ya hisa katika Kampuni ya simu za mkononi ya
Vodacom. Ni kampuni inayoongoza kwa biashara ya simu za mikononi nchini
Tanzania, ikiwa na wateja zaidi ya milioni 9.5.
Pia anamiliki Kampuni ya Caspian, ambayo inafanya kazi za kuchimba
madini katika migodi inayomilikiwa na Kampuni za BHP Billiton na Barrick
Gold.
Vilevile ana hisa katika Kampuni ya Hutchison Wampoa, inayofanya kazi
za kupakua mizigo bandarini na anamiliki majumba nchini na katika nchi
za Mashariki ya Kati.
Mwingine mwenye uwezo wa kuwekeza kwenye sekta ya gesi ni Dk. Mengi
ambaye anaelezwa kuwa na uwezo wa kumiliki visima zaidi ya vinne
kutokana na utajiri wa dola 550 milioni (sh bilioni 861).
Utajiri wake unatokana na kumiliki vyombo vya habari, kiwanda cha vinywaji baridi na madini.
Mengi anamiliki magazeti kumi na moja, vituo vitatu vya televisheni
na takriban vituo 10 vya redio. Pia ana mgodi wa madini ya dhahabu na
viwanda vya soda aina ya Coca-Cola.
Bakhressa kwa upande wake, pia ana uwezo wa kumiliki rasilimali hiyo.
Ana kampuni kubwa inayoajiri zaidi ya watu 2,000 ikijishughulisha zaidi
katika kusaga nafaka, kusindika matunda, usafiri wa meli na biashara ya
mafuta. Pia hutengeneza pipi na ice cream.
Mo, ambaye anafungana na Bakhressa kwa utajiri wa dola milioni 500
(sh bilioni 783), mafanikio yake yamechangiwa zaidi baada ya kuendeleza
mali ya wazazi wake.
Anafanya biashara ya nyumba, kuuza mazao na viwanda vya mafuta.
Alinufaika baada ya kununua viwanda vilivyobinafsishwa na serikali.
Alivifanya viwanda hivyo kutengeneza faida na kuinyanyua Kampuni ya
Mohamed Enterprises (MeTL) kuwa miongoni mwa kampuni zenye mafanikio
makubwa Tanzania.
CHANZO TANZANIA DAIMA
CHANZO TANZANIA DAIMA
Post a Comment