CHADEMA WAFUNGA MDOMO, DK. SLAA ASEMA CHAMA KINA MAMBO MENGI YA KUFANYA
ATIMAYE Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kimesema kuwa
mjadala kuhusu viongozi wake waliovuliwa nyadhifa zao kwa madai ya
kukisaliti chama umefungwa.
Viongozi waliovuliwa nyadhifa zao ni Mbunge wa Kigoma Kaskazini,
Zitto Kabwe, aliyevuliwa nafasi ya Naibu Katibu Mkuu, Mhadhiri wa Chuo
Kikuu cha Dar es Salaam, Dk. Kitila Mkumbo, aliyevuliwa ujumbe wa Kamati
Kuu (CC) na Samson Mwigamba, aliyevuliwa uenyekiti wa Mkoa wa Arusha.
Kauli ya kufunga mjadala huo ulioshika kasi kwa takribani wiki moja
sasa, ilitangazwa jana na Katibu Mkuu wa CHADEMA, Dk. Willibrod Slaa.
Akizungumza na gazeti hili jana, Dk. Slaa alisema mjadala huo
umefungwa, na tayari barua za mashitaka 11 kwenda kwa watuhumiwa
zimeshatumwa.
“Nataka niwaambie wana CHADEMA wote wanaotumia mitandao na njia
nyingine za mawasiliano kwamba mjadala huo sasa umefungwa, hatutaki
kusikia, kuona mwanachama yeyote anauendeleza, lakini tutajibu tu pale
itakapoonekana kuna upotoshaji,” alisema Dk. Slaa.
Kwa mujibu wa Dk. Slaa, kazi iliyobaki ni kwa watuhumiwa kujibu
mashitaka yao ndani ya siku 14 na hatma yao itajulikana kwenye kikao cha
Kamati Kuu (CC).
Dk. Slaa ambaye amepata kuwa mgombea urais wa CHADEMA mwaka 2010 na
kutoa upinzani mkali kwa mgombea wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Jakaya
Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano, alisema kuna mambo mengi mazito ya
kujadili kuliko hilo la mzozo wa Zitto na wenzake.
“Tumekumbwa na tatizo la umeme hapa ambao hatujui chanzo, kuna
wenzetu wanaendelea kupigwa na kufanyiwa vitendo vya unyanyasaji,
hatuwezi kuendelea na malumbano ambayo hayana tija, CHADEMA ni chama
makini na bado kiko imara,” alisema Dk. Slaa.
Kauli ya Dk. Slaa itahitimisha mjadala huo ambao tangu watuhumiwa hao
walipotangazwa kuvuliwa madaraka, kumekuwa na majibishano kati ya
viongozi wa CHADEMA na watuhumiwa hao.
Mara baada ya mkutano na waandishi wa habari wa kutangaza uamuzi wa
kuwavua madaraka viongozi hao, Zitto na Dk. Kitila kwa mara ya kwanza
walijibu mapigo katika mkutano wao na waandishi wa habari uliofanyika
katika hoteli ya Serena, jijini Dar es Salaam.
Katika mkutano huo, Zitto na Kitila walitaja sababu walizodai ndizo
zimewafanya kuvuliwa nyadhifa zao, ikiwemo suala la ukaguzi wa hesabu za
fedha za ruzuku inayotolewa kwa vyama vyenye wabunge, kikiwemo CHADEMA.
Zitto alidai kwa muda mrefu amekuwa akizushiwa kupokea rushwa na
kukisaliti chama, na kwamba hatoki ndani ya chama hicho kwani nusu ya
maisha yake tangu alipojiunga akiwa na miaka 16, hadi sasa ana miaka 37,
maisha yake yapo CHADEMA.
Kutokana na maelezo hayo ya Zitto na Kitila, CHADEMA juzi
walilazimika kuitisha mkutano na kudai kuwa viongozi hao waliovuliwa
madaraka, walishindwa kusema ukweli mbele ya waandishi wa habari wiki
iliyopita wa kile kilichowafanya wavuliwe nafasi zao.
Akizungumza katika mkutano huo, Mwanasheria Mkuu wa CHADEMA, Tundu
Lissu, alisema Zitto na Dk. Kitila hawakusimamishwa nyadhifa zao kwa
masuala ya PAC, uchaguzi wa mwaka 2010, wala kutoshiriki kwenye
operesheni za chama au sababu nyingine, na kwamba walitaja sababu hizo
ili kupotosha tuhuma zinazowakabili kwa jamii.
“Walichokifanya kina Zitto na Kitila ni “Diversion” (kubadili
mwelekeo) wa mashitaka yao yanayotokana na waraka wa kihaini wa
mabadiliko, ambao ni kinyume na katiba, kanuni na maadili na itifaki ya
chama,” alisema Lissu.
Aliongeza kuwa CHADEMA ina mwongozo wa uchaguzi uliopitishwa na
Kamati Kuu, na Zitto na Kitila wanaufahamu ingawa haijulikani ni kwanini
wao walienda kinyume na mambo yanayojadiliwa katika Kamati Kuu.
Aidha, Lissu alieleza kuwa Dk. Kitila anapotosha umma kwa kauli yake
kuwa Kamati Kuu haina mamlaka ya kumvua nafasi yake ya ujumbe wa Kamati
Kuu maana amechaguliwa na Baraza Kuu.CREDIT TANZANIA DAIMA
Post a Comment