Sitta amuokoa Nchimbi • Makombora ya Lissu yamtoa jasho.
WAZIRI wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Samuel Sitta, juzi
alimuokoa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk. Emmanuel Nchimbi, dhidi
ya makombora ya Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu (CHADEMA).
WAZIRI wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Samuel Sitta.
Busara za Sitta ndizo zilizomfanya Lissu abadilishe nia yake ya kuondoa shilingi kwenye bajeti ya Wizara ya Mambo ya Ndani.
Hatua hiyo ilikuja wakati Bunge limekaa kama kamati kupitia vifungu
vya wizara hiyo, ambapo Lissu alitaka Waziri Nchimbi afafanue serikali
imetekelezaje mapendekezo ya tume yake iliyoongowa na Jaji Ihema pamoja
na ile ya Haki za Binadamu zilizoshauri Jeshi la Polisi kusukwa upya ili
lifanye kazi bila kufuata matakwa ya wanasiasa wa chama tawala.
Lissu alitoa taarifa kwa Mwenyekiti wa kikao hicho, Anne Makinda, kuwa
anakusudia kuondoa shilingi kwenye mshahara wa Waziri Nchimbi endapo
majibu yake yataendelea kuwa mafupi na mepesi.
Hata hivyo, kama alivyokuwa amejibu mapema wakati akihitimisha hoja za
wabunge, Nchimbi alisema ni kweli kwamba Jeshi la Polisi halipaswi
kufanya kazi kwa maelekezo ya wanasiasa na kwamba ndiyo sababu Kamanda
wa Polisi wa Mkoa wa Iringa, Michael Kamuhanda, anaendelea kuwa kazini.
Nchimbi aliongeza kuwa ripoti hizo wamezisoma lakini wanajipa muda
kuzifanyia kazi, kwani endapo watakurupuka pasipo kuangalia mazingira
mwisho wake unaweza kuwa mbaya.
“Unajua ukikutana na mtu aliyetoka kuombwa rushwa na trafiki halafu
ukamuulizia utendaji wa jeshi hilo, atakwambia hakuna watu wabaya kama
hao. Lakini ukikutana na dereva aliyepata ajali akakatika mguu halafu
akaokolewa na trafiki, ukimuuliza kuhusu utendaji wa jeshi hili, atasema
hakuna watu wazuri kama hao,” alisema.
Hivyo, Dk. Nchimbi alisema ripoti hizo hawawezi kuzifanyia kazi moja
kwa moja bali wanapima kuona wakati zinafanyiwa kazi wajumbe waliegemea
kwenye nini.
Majibu hayo yalimwinua tena Lissu na kutoa hoja ya kuondoa shilingi
akisema Waziri Nchimbi ametoa maelezo ya mzaha wakati tume aliyoiunda
yeye na ile ya Haki za Binadamu iliyoundwa na rais ni kwanini
wameshindwa kuzifanyia kazi.
Hoja hiyo iliungwa mkono na wabunge wengi wa upinzani ambao walianza
kuichangia wakidai jeshi hilo linafanya kazi kwa maelekezo ya wanasiasa,
hata kufikia hatua ya kushindwa kuwachukulia hatua vigogo wa CCM kwa
amri za wakuu wa mikoa na wilaya.
Kabla ya Waziri Nchimbi kujibu hoja hizo, Makinda alimuita Waziri
Sitta ambaye alikuwa akikaimu nafasi ya waziri mkuu ili aweze kutoa
maelezo kuhusu sakata hilo.
Sitta alisema wanasiasa wanapaswa kuwatendea haki wananchi, akifafanua
kuwa: “Hapa kuna tuhuma nzito dhidi ya Jeshi la Polisi, kuna tuhuma
nzito dhidi ya serikali ya CCM na zinatolewa na wenzetu wabunge
tunaowaheshimu kutoka upande wa upinzani.
“Nataka kushauri mheshimiwa mwenyekiti, kanuni ya 103 si mahala pake
kuzungumza jambo zito namna hii, kwa sababu inahitaji hoja ikae vizuri,
iwe na ushahidi, majibu yawepo.”
“Sasa wakati wa kuondoa shilingi tuzungumze suala la polisi kutumiwa
na wanasiasa, na pande zote ziweze kupeana taarifa kulingana na mujibu
na pengine upande wa serikali wana jambo la kusema, maana tunakerwa na
kauli za viongozi wa vyama vingine wanaotoa eti saa 24 fulani aondoke,”
alisema.
Alisema kuwa kuna wanasiasa wanataka kuonesha serikali haifai, ni goigoi, kwamba hakuna serikali inayoendeshwa hivyo.
“Sasa haya ukiyachanganya ni furushi kubwa kwa wananchi wetu,
ningemshauri Mheshimiwa Lissu atumie kanuni nadhani ya 53, apewe nafasi
kwenye mkutano ujao alete hoja binafsi kwa mujibu wa kanuni, tuwe na
muda wa kuijadili vizuri na tutoe majibu yanayostahili,” alisema Sitta.
Hoja hiyo ilikubaliwa na Lissu akisema kuwa Sitta ametoa majibu
yanayoeleweka, ambayo si ya kuokoteza kama ya Dk. Nchimbi, maelezo
ambayo baadaye yaliruhusu kikao kuendelea na kupitisha vifungu na
hatimaye kuipitisha bajeti ya wizara hiyo.
CHANZO NI TANZANIA DAIMA

Post a Comment