MABOSI wa Kamati ya Rufani ya Uchaguzi na ile ya Uchaguzi ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) - wagoma kujiuzulu.
MABOSI wa Kamati ya Rufani ya Uchaguzi na ile ya Uchaguzi ya
Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), wamedai hawatojiuzulu kama baadhi ya
wadau wanavyowashinikiza, kwani walitenda haki wakati wa mchakato wa
uchaguzi mkuu wa shirikisho hilo ulioingia dosari.
Kamati hizo zinaongozwa na Idd Mtiginjola (Rufani ya Uchaguzi) na Deo Lyato (Uchaguzi).
Hivi karibuni, Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA), lilituma ujumbe
wake hapa nchini kushughulikia mtafaruku ulioibuka baada ya baadhi ya
wagombea kukatwa na kamati hizo ambapo liliamuru mchakato huo uanze upya
baada ya kugundua dosari kadhaa.
Kutokana na hali hiyo, wadau hao wamekuwa wakidai kamati hizo ndizo
chanzo cha kuharibu mchakato huo na kusababisha uanze upya.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, wadau hao wakiwemo baadhi ya
viongozi wa TFF, ambao hawakutaka majina yao kutajwa kwa madai kuwa wao
ndio wahusika wakubwa kusimamia uchaguzi huo, walieleza kukerwa na
maamuzi ya kamati hizo.
Kiongozi huyo wa TFF alisema hakuridhishwa na bado haridhishwi na
uwepo wa Lyatto, kwa madai kuwa sio mwanasheria kama katiba inavyotaka
mwenyekiti wa kamati hiyo kuwa na kudai kuwa ni vizuri akaachia ngazi na
shirikisho likasaka mtu ambaye anakidhi vigezo hivyo.
“Mimi nashangaa sana kuona Lyatto sio mwanasheria na anaongoza kamati
hiyo; ni ubabaishaji wa viongozi wetu wa juu hapa TFF, na pia
haijaniingia akilini, eti wanamuondoa Jamal Malinzi kwa madai hana
uzoefu wa miaka mitano katika soka, halafu wanamuacha Yusuph Manji
ambaye hana hata mwaka mmoja, hii sio haki kabisa,” alisema mmoja wa
wajumbe wa Kamati ya Utendaji ya TFF.
Akizungumzia tuhuma hizo, Lyatto alikiri kuwa yeye si mwanasheria na
wala hatamani kuwa mwanasheria na kudai ni kazi ya waliomuweka
kumuondoa, kwani alifanya maamuzi yake kama sheria na katiba
inavyomruhusu.
Kwa upande wake, Mtiginjola alisema yeye anajiamini na anaiamini
kamati yake na kudai kuwa hana mpango wa kujiuzulu, labda kama waliompa
dhamana hiyo watamuondoa, lakini sio matakwa ya watu wachache, kwa kuwa
alifanya maamuzi sahihi kutokana na katiba na kanuni zinavyomruhusu.
“Wao hawawezi kunitaka mimi kujiuzulu, kwani aliyeniweka ndiye ana
mamlaka ya kuniondoa, kwanza mimi nina kazi zangu nyingi za kufanya na
pia kamati yangu ina watu makini, ambao hawawezi kuendeshwa kimaamuzi na
ndiyo maana hata nilikataa kufanya ‘Review’ kwa kuwa iko nje ya katiba,
sheria na kanuni katika kamati yangu,” alisema Mtiginjola.

Post a Comment