CCM wainadi CHADEMA
LICHA ya wabunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), kuporomosha
matusi mazito bungeni na kuachwa bila kuchukuliwa hatua, bado hawajataka
kujirekebisha baada ya mbunge mwingine kuwadhalilisha mkutanoni wabunge
wa Viti Maalumu wa CHADEMA.
Hatua hiyo inakuja zikiwa ni siku chache tangu wabunge wa CCM, Juma
Nkamia (Kondoa Kusini) na Livingistone Lusinde (Mtera) kuwatukana wenzao
wa CHADEMA wakiwaita mbwa na kwamba wana mimba zisizotarajiwa.
Pia Mbunge wa Kigoma Mjini, Peter Serukamba naye aliwatukana wapinzani
mwishoni mwa wiki, tusi ambalo kimaadili haliwezi kuandikwa gazetini.
Matusi hayo yalionekena kumkera Mbunge wa Viti Maalumu, Anna Abdallah
(CCM) na kuwataka wabunge wanawake kwa niaba ya wanawake wengine wakatae
vitendo hivyo.
Abdallah ambaye ni mwenyekiti wa Jukwaa la Wabunge Wanawake (Ulingo)
pia alielezwa kukerwa na mifano ya Mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji
Peter Msigwa (CHADEMA) ya kwenye Biblia akidai inawadhalilisha wanawake.
Hata hivyo, katika hali ambayo haikutarajiwa, mbunge mkongwe wa Uzini,
Mohammed Seif Khatib (CCM), alirudia mtindo ule ule wa matusi kwa
kuwadhalilisha wabunge wa CHADEMA katika mkutano wa hadhara uliofanyika
mjini Morogoro jana.
Katika mkutano huo ambao ulirushwa moja kwa moja na kituo cha
Televisheni ya Taifa, Khatib ambaye pia ni Katibu wa Oganaizesheni ya
CCM, alisema CHADEMA ina wabunge wa kuchaguliwa na viti maalumu.
Alifafanua kuwa ukiacha wale wa kuchaguliwa, wabunge wa viti maalumu
walipatikana kutokana na kuwa wachumba, wake na wapenzi wa viongozi wa
CHADEMA Taifa.
Khatib huku akifahamu wazi kuwa wabunge hao wamepatikana kwa utaratibu
wa kikatiba ambao umeidhinishwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC),
aliongeza kuwa CHADEMA inaongozwa na wazinzi wenye dhambi wasiofaa
kwenda Ikulu.
Katika mkutano ambao kila kiongozi wa CCM aliyezungumza alitumia muda
wote kuijadili CHADEMA, Khatib vile vile aliwadanganya wananchi kuwa
Chama cha Wananchi (CUF) kina malengo mengine tofauti na siasa, hivyo
wasihangaike kujiunga nacho kwani kina wenyewe.
Katibu wa Halmashauri Kuu (NEC), Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye alidai
CHADEMA ni wachochezi wanaopanga mikakati ya ugaidi ili kuteka watu na
kuwang’oa kucha.
Katika kujenga hoja yake, Nape alimsingizia Waziri Mkuu mstaafu wa
Kenya, Raila Odinga kuwa ndiye aliyechochea vurugu za baada ya uchaguzi
wa nchi hiyo mwaka 2007/2008 na kuua watu zaidi ya 1,300 huku wengine
wakibaki bila makazi.
“Hawa CHADEMA ni kama Raila Odinga, huyu alishindwa urais mwaka 2007
na Rais Mwai Kibaki. Baada ya hapo akawachochea wafuasi wake waingie
mitaani kuua watu wakati mwenzake mzee Kibaki alikimbilia Tanzania
kwenye amani,” alisema.
Hata hivyo, licha ya Nape kumtaja Odinga, kauli hiyo haina ukweli
wowote kwani Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu wa Kivita (ICC) ya The
Hague, Uholanzi katika uchunguzi wake kuhusu vurugu hizo Odinga si mmoja
wa washukiwa wanaoshtakiwa.
Akihutubia mkutano huo, Katibu Mkuu wa CCM, Abdulraham Kinana naye
alitumia takribani saa nzima kwa kuichambua CHADEMA na viongozi wake
akidai ni waongo na wachochozi wasio na shukrani.
Kinana alizungumzia mchakato wa katiba mpya huku akitumia hotuba ya
Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe na kudai imejaa
matusi na uongo kwa viongozi.
“Hawa watu tumewalea sana, wanatukana hovyo, wamemtukana Rais Jakaya
Kikwete, wameitukana CCM, Usalama wa Taifa na majaji. Wanajiona wao ndio
kila kitu…hawafai kabisa hawa, ni wabinafsi,” alisema.
CHANZO TANZANIA DAIMA

Post a Comment