ad

ad

Azam yawakabili FAR Rabat leo.

TIMU ya soka ya Azam leo inaikaribisha FAR Rabat ya Morocco katika mechi ya awali ya raundi ya pili ya Kombe la Shirikisho itakayochezwa Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam.

                                                                      FAR Rabat
Azam chini ya Kocha wake Stewart John Hall, leo itakuwa na kazi ya kusaka ushindi kujiweka kwenye nafasi nzuri ya kusonga mbele kabla ya mechi ya marudiano itakayochezwa wiki mbili zijazo mjini Rabat.

Hata hivyo, Azam wanapaswa kuwa makini zaidi dimbani kukabiliana na wapinzani wao wenye uwezo na rekodi ya kufanya vema kwenye michuano ya kimataifa.

Kati ya mafanikio ya timu hiyo iliyoanzishwa mwaka 1958, ni kutwaa ubingwa wa Kombe la Shirikisho mwaka 2005 na kuwahi kubeba taji la Ligi ya Mabingwa mwaka 1985.
Kwa kutambua umuhimu wa mechi ya leo, Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) limeitakia kila la kheri Azam katika mechi yake ambayo ni fursa nzuri ya kutumia uenyeji kupata matokeo mazuri kabla ya kurudiana wiki mbili zijazo.

Mazingira hayo yanaifanya mechi hiyo itakayochezeshwa na Emile Fred kutoka Shelisheli kuwa ya ushindani mkubwa kwani wakati Azam ikipambana kupata ushindi wa nyumbani, FAR Rabat, watakuwa wakipigana kupata matokeo mazuri kabla ya mechi ya nyumbani.

Aidha kwa kutambua nafasi ya hamasa katika kupigania ushindi, TFF imetoa wito kwa wapenzi wa soka kujitokeza kwa wingi uwanjani kuishangilia timu hiyo pekee kwa Tanzania iliyosalia kwenye michuano ya kimataifa.

Wakizungumzia mechi hiyo, makocha wasaidizi wa timu zote mbili, Kalimangonga Ongala wa Azam na Lahcen Ouadani wa AS FAR Rabat, kila mmoja amejigamba kuwa timu zao ziko tayari kwa mechi hiyo inayotarajiwa kuwa na ushindani mkubwa.

Ongala kwa upande wake, amesema wanawakabili FAR Rabat baada ya kuwasoma kupitia DVD za mechi tatu za mwisho ikiwemo dhidi ya Al Nasir ya Libya waliyokutana nayo kwenye raundi ya kwanza ya Kombe la Shirikisho.
DVD nyingine mbili za FAR Rabat zilizofanyiwa kazi na benchi la ufundi la Azam chini ya Hall, ni za Ligi Kuu ya Morocco na kusema wamefanikiwa kutambua mbinu za wapinzani wao.

Naye Ouadani amesema licha ya kutoifahamu vizuri Azam, wanaijua vizuri soka ya Tanzania hasa baada ya kuangalia mechi ya mchujo ya Kombe la Dunia kati ya Taifa Stars dhidi ya Morocco iliyochezwa Machi 24, kwenye Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam na Stars wakashinda 3-1.

Kwa upande mwingine, timu hizo zinakutana leo zikiwa nafasi ya pili kwenye misimamo ya Ligi Kuu katika nchi zao kwani wakati Azam wakiwa nafasi hiyo nyuma ya Yanga kutokana na pointi 43, FAR Rabat ya pili kwa pointi 49 nyuma ya Raja Casablanca.
Aidha, wakati Azam wakitoka kuvuna ushindi wa 3-1 na sare ya 2-2 dhidi ya Simba katika mechi zao mbili zilizopita, FAR Rabat wamevuna sare mbili dhidi ya Raja Casablanca na Olympic Safi.

Wakati Azam wakianzia kampeni yao tangu raundi ya awali wakiwatoa Al Nasr ya Sudan Kusini kwa jumla ya mabao 8-1 kisha kuwang’oa Barack Young Controllers ya Liberia kwa mabao 2-1, FAR Rabat wameanzia raundi ya kwanza.
Katika hatua hiyo, FAR Rabat walisonga mbele kwa ushindi wa jumla ya mabao 2-1 dhidi ya Al Nasri ya Libya ambapo ilipocheza nyumbani, FAR Rabat ilishinda bao 1-0 kabla ya kutoka sare ya bao 1-1 mjini Tripol.

Kwa upande wa Azam, kikosi kinaweza kuwa hivi: Aishi Manula, Mwadini Ally, Khamis Mcha, John Bocco na Salum Abubakar waliomo pia kwenye kikosi cha sasa cha Stars chini ya kocha wake Kim Poulsen.
FAR Rabat inaweza kuwa hivi: Younes Bellakhdar, Abderrahim Achchakir, Younnes Hammal, na viungo Salaheddine Said, Salaheddine Aqqal na Youssef Kaddioui.
Powered by Blogger.