Wafuasi wa Ponda wafungwa mwaka mmoja
MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam, imewahukumu
kwenda jela mwaka mmoja wafuasi 53 wa Katibu wa Jumuiya na Taasisi za
Kiislamu, Sheikh Issa Ponda, waliokuwa wakikabiliwa na kesi ya kula
njama na kufanya maandamano haramu.
Hukumu hiyo ilitolewa jana na Hakimu Mkazi, Sundi Fimbo, ambapo
alianza kwa kuikumbusha mahakama kuwa mshtakiwa, Salum Bakari Makame, na
wenzake 52, wanaotetewa na wakili wa kujitegemea Mohamed Tibanyendera
walikuwa wakikabiliwa na makosa manne.
Makosa hayo ni ya kuandamana kwenda ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka
(DPP), Dk. Eliezer Feleshi, kumshinikiza ampatie dhamana Ponda kwa madai
kuwa ndiye alikuwa ameifunga dhamana hiyo.
Fimbo alilitaja kosa la kwanza kuwa ni kula njama kutenda kosa kinyume
na kifungu 384 cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu ya mwaka 2002, kosa la
pili ni la kufanya mkusanyiko haramu kinyume na kifungu cha 74 na 75 cha
sheria hiyo ambavyo vinasomwa pamoja na kifungu cha 43(2)(4) na 46 cha
Sheria ya Jeshi la Polisi ya mwaka 2002.
Kosa la tatu ni la kukaidi amri ya jeshi la polisi iliyowataka
watawanyike ambalo ni kinyume na kifungu 79 cha Sheria ya Kanuni ya
Adhabu kinachosomwa pamoja na kifungu cha 44 cha Sheria ya Jeshi la
Polisi ya mwaka 2002.
Alisema kosa la nne ni la uchochezi ambalo lilikuwa likiwakabili
washtakiwa watatu tu ambao ni Makame, Saidi Idd, Ally Nurdin Nandumbi,
ambao wote hawa DPP, aliwafungia dhamana tangu walipofikishwa kwa mara
ya kwanza mahakamani hapo Februali 18, mwaka huu.
Hakimu Fimbo alisema ili kuthibitisha kesi yao, upande wa jamhuri
uliokuwa ukiwakilishwa na mawakili waandamizi wa serikali, Bernad
Kongora, Peter Ndjike, Zuberi Mkakatu na Joseph Mahugo na Nassor Katuga
walileta jumla ya mashahidi 10 na upande wa utetezi walileta jumla ya
mashahidi 54.
Alisema mahakama yake kabla ya kutoa hukumu ilijiuliza maswali manne
kuwa je washtakiwa walikula njama kutenda kosa? Walifanya mkusanyiko
haramu? Walikaidi amri ya jeshi la polisi iliyowataka wasiandamane na je
walifanya uchochezi?
“Baada ya kujiuliza maswali hayo mahakama hii imefikia uamuzi wa
kuwaona washtakiwa 52 walitenda kosa la kula njama isipokuwa mshtakiwa
wa 48 (Waziri Omar Toli) hakutenda kosa hilo kwa sababu alikutwa akitoka
kununua mabeseni; mahakama hii imewatia hatiani kwa kosa hilo,”
alisema.
Alisema kuwa kwa vielelezo hivyo, mahakama hiyo imeridhika kwamba
walitenda kosa la kwanza, la pili na la tatu na kosa la nne ambalo ni la
uchochezi mahakama imeona upande wa jamhuri umeshindwa kulithibitisha.
Akilichambua kosa la pili ambalo ni la kufanya mkusanyiko haramu,
hakimu huyo alisema pia mahakama inamuachilia huru mshtakiwa wa 48,
isipokuwa washtakiwa wengine wote wametiwa hatiani kwa kosa hilo.
Hakimu Fimbo alisema kila kosa alilowatia nalo hatiani watalitumikia
kifungo gerezani kwa mwaka mmoja, hivyo washtakiwa hao watatumikia
adhabu ya mwaka mmoja jela.
Kwa upande wake hakimu Fimbo alisema amezingatia maombi ya pande zote
mbili na kwamba badala ya kuwahukumu kwenda jela miaka saba, anawahukumu
kwenda gerezani mwaka mmoja na akasema yeyote ambaye hajaridhika na
hukumu hiyo anaruhusiwa kwenda kukata rufaa mahakama ya juu.
Wakati huo huo mahakama hiyo, imesema kuwa Aprili 18, mwaka huu, itaoa
hukumu ya kesi ya uchochezi na wizi wa malighafi za sh milioni 59
inayomkabili, Sheikh Ponda na wenzake.
Hakimu Mkazi Victoria Nongwa aliyasema hayo jana muda mfupi baada ya
mashahidi watano wa upande wa utetezi waliopanda wote jana kizimbani
kutoa utetezi na hivyo kufanya upande wa utetezi kuleta mashahidi 52.
Hakimu Nongwa alizitaka pande mbili katika kesi hiyo kuwasilisha kwa
maandishi majumuisho ya mwisho ya kesi hiyo Aprili 3 na kwamba kesi hiyo
itatajwa Aprili 4.
Habari na na Happiness Katabazi

Post a Comment