MKUU wa Mkoa wa Arusha kubariki fainali nyama choma kesho General Tyre
MKUU wa Mkoa wa Arusha, Magesa Mulongo, anatarajiwa kuwa mgeni
rasmi katika fainali za shindano la nyama choma, zinazodhaminiwa na
Kampuni ya Bia Tanzania (TBL), kupitia bia ya Safari Lager,
itakayofanyika kesho kwenye viwanja vya General Tyre jijini humo.
Akizungumza kutoka mjini Arusha jana, Meneja wa Bia ya Safari Lager,
Oscar Shelukindo, alisema ni fahari kubwa kwa TBL kupitia Safari Lager
kufanikisha shindano hilo mkoani hapa, kabla ya kuhamia mikoa mingine.
Alizitaja baa zitakazochuana kesho kuwa ni Blue Line Park, VIP Lounge,
QX Pub, Royal Stop Over na Rombo Deluxe, ambako bendi ya Yekete, pamoja
na kikundi cha sarakasi vitatoa burudani katika fainali hiyo.
“Fainali ya Safari Lager Nyama Choma Mkoa wa Arusha, itafanyika
Jumamosi na hizo baa tano ndizo zitakazochuana, tulianza kwa kuwataka
watu wapige kura kupendekeza baa zinazofaa kuingia katika shindano.
Tunajua watu huwa wanakwenda katika baa na kula nyama, hivyo tukaona
ni vema tuanzishe mashindano haya ili walaji nyama choma wapate nyama
bora,” alisema Shelukindo.
Kwa upande wake, Jaji Mkuu wa fainali hizo, Douglas Sakibu, alisema
kabla ya shindano hilo, walitoa mafunzo kwa baa zote hizo juu ya mambo
wanayopaswa kuzingatia katika uchomaji nyama.
Alisema watatumia vigezo kumpata mshindi ambavyo ni usafi wa nyama,
vifaa na mazingira, maandalizi ya nyama kuanzia uchaguzi, uhifadhi wake
na wa vifaa, uchomaji na upangaji, ladha na ulaini wake, mtiririko wa
maji na uhifadhi wa taka.
Mshindi wa kwanza atajinyakulia sh 1, 000,000, wa pili sh 800,000, wa
tatu sh 600,000 wa nne sh 400,000, wakati mshindi wa tano atapata sh
200,000 na vyeti.

Post a Comment