Meya ampoza DC Bukoba
MKUU wa Wilaya ya Bukoba mkoani Kagera, Zipora Pangani, juzi
alijikuta katika wakati mgumu baada ya wafanyabiashara wa mjini humo
kumuumbua mbele ya tume iliyoundwa kuchunguza tuhuma za Meya wa Manispaa
huyo, Anatory Amani.
Wazo la kuundwa tume ya kumchunguza meya lilitolewa na Chama Cha
Mapinduzi (CCM) Taifa baada ya kutokea msuguano mkali kati yakr na
madiwani wa chama hicho.
Tayari tume hiyo inaendelea na uchunguzi wake mjini humo ambapo juzi
ilikutana na wafanyabishara wa soko kuu ambalo ni moja ya mradi
unaolalamikiwa kuingiwa mkataba na meya bila kuwashirikisha madiwani.
Tume hiyo inaundwa na wajumbe wanne; Abbas Kandoro (Mkuu wa Mkoa wa
Mbeya), Dk. Rehema Nchimbi (Dodoma), Naibu Katibu Mkuu wa Tamisemi na
Naibu Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali.
Taarifa kutoka mjini Bukoba zilisema kuwa kikao hicho kati ya tume na
wafanyabiashara kilipamba moto huku wakishinikiza kuwa meya Amani lazima
ang’oke kutokana na kutumia mabavu na hivyo kuisababishia halmashauri
hasara.
Wakizungumza kwa simu na gazeti hili jana, baadhi ya washiriki wa
kikao hicho walisema kuwa hata mkuu wa wilaya, Pangani alilazimika
kuwaomba radhi wafanyabishara hao kwa kile alichodai kuwa alidanganywa
na meya kuhusu mradi huo.
“Huyu mkuu wa wilaya alidanganywa maana baada ya sisi kukataa ubabe wa
meya kutaka kutuondoa kwa nguvu sokoni hapo, alikaribishwa katika
mkutano kwenye Uwanja wa Kataba ambao meya alidai kuwa umeweka uongozi
mpya wa soko,” alisema mtoa taarifa wetu.
Kwamba baada ya Pangani kuelezwa ukweli huo mbele ya tume kuwa
alidanganywa, alilazimika kusimama na kuwaomba radhi wafanyabiashara
hao.
Katika kikao hicho kilichochukua takribani saa tano, inaelezwa kuwa
wafanyabishara walisema kuwa hawapingi mradi huo wa ujenzi wa soko la
kisasa bali wanakataa ubabe wa meya Amani.
“Tumeieleza tume kuwa tuko tayari kufuta kesi tuliyoifungua dhidi ya
meya ikiwa atang’olewa na kuchaguliwa mwingine. Maana tangu kuanza kwa
vitisho vyake vya kutaka kutuondoa, biashara imeyumba. Tulichukua mikopo
lakini tumepata hasara.
“Baada ya kufungua kesi, halmashauri imekuwa haikusanyi chochote
kutoka kwetu na hivyo imepoteza mapato ya zaidi ya sh milioni 100. Meya
alikurupuka kutufukuza wakati hakukuwa na maandalizi yoyote ya ujenzi
kwani fedha za kutekeleza mradi huo hakuwa nazo,” alisema mfanyabiashara
mmoja.
Jana asubuhi tume hiyo ilikutana na Baraza la Madiwani na mchana
ilifanya kikao na wadau wengine wa sekta ya ardhi kusikiliza maoni yao
kuhusu utekelezaji wa mradi wa upimaji na uuzaji viwanja zaidi ya 5,000.
Hata hivyo, habari kutoka Bukoba zilidai kuwa tume hiyo imekuwa
ikifanya kazi yake kwa usiri mkubwa na hivyo kutotoa nafasi kwa wananchi
wengi kutoa maoni yao kuhusu sakata la tuhuma hizo.
Chimbuko la mgogoro lilitokana na madiwani wanane wa CCM akiwemo na
mbunge wa Bukoba Mjini, Balozi Khamis Kagasheki na wawili wa CUF kusaini
hati ya dharura kumtaka mkurugenzi wa halmashauri kuitisha kikao cha
kumng’oa meya Amani.
Hatua hiyo ilisababisha uongozi wa CCM Taifa kuingilia kati na
kuwaamuru madiwani wake waondoe tuhuma zao na hivyo kuiomba Tamisemi
iunde tume kuchunguza miradi hiyo mitatu ya uuzwaji wa viwanja, ujenzi
wa soko na stendi ya kisasi.
Mwishoni mwa wiki, tume hiyo ilikutana na madiwani wa CCM na wajumbe
wa kamati ya siasa ya wilaya, jambo lililodaiwa na baadhi ya madiwani
kuwa ni mkakati wa kutaka kuwalainisha ili kumbeba meya Amani.
Chanzo chetu kilidokeza kuwa wiki moja kabla ya tume kuanza kazi yake,
meya Amani kwa kushirikiana na mkurugenzi aliyehamishwa, Hamis Kaputa,
walimuita kazini katibu wa vikao vya madiwani mstaafu, Tukelia Kagumisa
kwa muda wa wiki moja.
“Huyu mama alistaafu Januari mwaka huu, sasa kitendo cha kumwita na
kujifungia naye ofisini kwa wiki nzima kinatia shaka kuwa huenda
walikuwa wakibadilisha mihutasari ya vikao vilivyopita ili kupoteza
ushahidi,” alisema mtoa taarifa.

Post a Comment