Sunzu kuikosa JKT Oljoro
LIGI Kuu Bara inaendelea tena leo kwa mechi tatu, huku mabingwa
watetezi, Simba wakiwa Uwanja wa Sheikh Amri Abeid Arusha kucheza na JKT
Oljoro.
Mbali na mechi hiyo, ligi hiyo iliyofikia hatua ya 16 pia itashuhudi mechi nyingine kwenye Uwanja Kaitaba Bukoba kati ya wenyeji Kagera dhidi ya JKT Mgambo.
Aidha, Toto Africans wanaoshika nafasi ya 12 kwenye msimamo wakiwa na pointi 12, watakuwa uwanja wa nyumbani, CCM Kirumba, Mwanza kuikaribisha Coastal Union ya Tanga.Mabingwa watetezi wako nyuma kwa pointi sita dhidi ya mahasimu wao wakubwa Yanga wanaoongoza kwa kuwa na pointi 30, wakifuatiwa na Azam pointi 30.
Ushindi kwenye mchezo wa leo ni muhimu kwa Simba, kwani kinyume chake watazidi kuongeza pengo la pointi dhidi ya mahasimu wao. Kwa upande wao Yanga, wanashuka dimbani Jumatano ijayo.
Tayari Simba imewasili jijini Arusha ikiwa na kikosi kamili na kuweka kambi kwenye Hoteli ya Bristol ambayo hufikia mara kwa mara.Msemaji wa Simba, Ezekiel Kamwaga alisema timu yake itakosa huduma ya mshambuliaji Felix Sunzu ambaye ni majeruhi.
Hiyo ni mara ya pili kwa mshambuliaji huyo wa kimataifa kutoka Zambia kukosa mechi, ambapo hakuwapo kwenye mchezo dhidi ya JKT Ruvu.Kamwaga alisema pamoja na kukosekana kwa mshambuliaji huyo, ana imani timu yake itafanya vizuri kwani bado ina wachezaji wengi wazuri.
Hata hivyo, Kamwaga alisema kuwa wamejiandaa kwa namna yoyote ile kukabiliana na maafande hao na hawatarajii kuupoteza mchezo huo kwa namna yoyote.

Post a Comment