ad

ad

Papa ajiuzulu

KIONGOZI wa Kanisa Katoliki Duniani, Baba Mtakatifu Benedict wa 16, mwenye miaka 85, ameomba kujiuzulu wadhifa huo kwa sababu ya umri wake kuwa mkubwa hali inayompa ugumu katika kutekeleza majukumu yake.
Katika taarifa rasmi iliyotolewa na makao makuu ya kanisa hilo mjini Vatican, Papa Benedict atajiuzulu rasmi Februari 28 mwaka huu.

Papa Benedict wa 16 alichaguliwa kushika wadhifa huo mwaka 2005, kufuatia kifo cha mtangulizi wake Papa Yohane Paulo II.
Kustaafu kwa Papa si jambo la kawaida kwani Baba Mtakatifu mwingine aliyewahi kustaafu ni Celestine V mwaka 1415.

Sheria ya kanisa kifungu cha 333(2) ya mwaka 1983, inamruhuru Baba Mtakatifu kustaafu kwa hiari kwa sababu zikiwemo za kuzorota kwa afya na umri mkubwa kama wa Papa Benedict.
Kiongozi huyo alichaguliwa kushika wadhifa huo akiwa na miaka 78, akijulikana kwa jina lake halisi la Joseph Cardinal Ratzinger, na hivyo kuwa miongoni mwa mababa watakatifu waliochaguliwa akiwa na umri mkubwa.

Baba Mtakatifu amenukuliwa katika ujumbe wake akisema: “Ndugu zangu naomba kuwafikishia ujumbe muhimu kwa maisha ya kanisa, baada ya kutathmini dhamira yangu mbele ya Mungu, nimepata uhakika kuwa nimetindikiwa nguvu kwa sababu ya umri mkubwa, naona sasa sitaweza kuendelea na wadhifa wa Baba Mtakatifu.”
Aliongeza, “Natambua vema utume huu, kwa kuwa ni wa kiroho kwa asili, ni lazima utekelezwe sio kwa maneno tu bali kwa matendo, sala na mateso.

“Hata hivyo katika dunia ya sasa inayokumbwa na mabadiliko makubwa na ya haraka yanayotikisa kwa nguvu maisha ya imani, ili kuweza kutawala vema utume wa Mtakatifu Petro na kutangaza vema Injili, uimara wa akili na mwili vyote ni vya muhimu, uimara ninaouzungumzia ni wa kimwili uliosababisha miezi michache iliyopita hali yangu ya afya kuyumba sana hadi kufikia uamuzi wa kusema siwezi kutekeleza vema utume huu mkubwa niliokabidhiwa,” alisema.
Papa aliongeza katika waraka huo: “Ndugu zangu, nawashukuru sana kwa upendo na kazi zenu mlizonisaidia sana kutekeleza utume huu na niwaombe radhi pale ambapo nilikosea.”

“Na sasa tuliweke Kanisa Takatifu chini ya ulinzi wa Mchungaji Mkuu, Bwana wetu Yesu Kristo, na kwa maombezi ya Mama Maria Mtakatifu ili awasaidie Makadinali waweze kuchagua Baba Mtakatifu mpya,” alisema.
Alisema kuwa kwa sababu hiyo akiwa na ufahamu kabisa na kwa umuhimu wa hili tendo, kwa uhuru kabisa anatangaza kustaafu utume wa Askofu wa Roma, mrithi wa Mtakatifu Petro aliokabidhiwa na makardinali Aprili 19, 2005.

“Katika maana kwamba Februari 28, 2013, saa mbili kamili usiku, kiti cha Baba Mtakatifu kitakuwa wazi na wenye mamlaka ya kuteua Baba Mtakatifu mpya watapaswa kuitwa na wenye mamlaka na suala hilo,” alisema.

Papa Benedict wa 16, alizaliwa Marktl Jimbo Katoliki la Passau nchini Ujerumani April 16, 1927 (Jumamosi Kuu). Alibatizwa siku hiyo hiyo, baba yake alikuwa askari polisi katika eneo la Bavaria, na mama yake alikuwa mpishi wa hotelini.
Kuanzia mwaka 1946 hadi 1951 alisoma Falsafa na Tauhidi katika Chuo Kikuu cha Munich na Juni 29 mwaka 1951 alipata daraja la upadri. Mwaka 1953 alipata shahada za uzamivu katika Tauhidi. Machi 25, 1977, Baba Mtatifu Paul VI alimteua kuwa Askofu Mkuu wa Munich na Freising na 28 Mei 28 aliwekwa wakfu kuwa Askofu Mkuu.

Mwaka 1978 alikuwa ni mmoja wa makadinali walioshiriki kumchagua Baba Mtakatifu Yohane Paulo II, ambaye yeye alimrithi baada ya kifo chake mwaka 2005.
Papa Benedict wa 16 anaheshimika sana katika Kanisa Katoliki kati ya wasomi wakubwa na ameandika vitabu vingi sana vya maadili na imani ya kanisa hilo vinavyotumika kufundishia katika vyuo vikuu mbalimbali vya kanisa duniani kote.
Powered by Blogger.