TUKISEMA
staa wa filamu za Bongo, Vincent Kigosi ‘Ray’ yamemkuta ni sawa, kisa
ni ile ishu yake ya kutengeneza filamu inayoitwa Sister Marry ambapo
mapadri wamemtaka asiipeleke sokoni milele. Ishu hiyo ilitokea
kwenye kikao kizito cha saa 5 kilichofanyika Jumanne iliyopita katika
Ofisi za Utamaduni jijini Dar es Salaam.
Washiriki wa kikao hicho
walikuwa Ray, Mkurugenzi Mtendaji wa Utamaduni aliyetajwa kwa jina moja
la Mwansoke, mapadri wanne na mtu mmoja aliyedaiwa kuwa ni wa kutoka
Ofisi za Usalama wa Taifa.
Kikao hicho kilikuja baada ya hivi
karibuni viongozi wa Kanisa Katoliki Jimbo
Kuu la Dar es Salaam kumtaka
msanii huyo ajieleze kimaandishi ni kwa nini mtawa Sister Marry (Irene
Uwoya pichani) alikuwa akifanya matendo ambayo kiuhalisia, Wakatoliki
wenyewe huwa hawayafanyi. Kabla Ray hajajieleza kwa maandishi ndipo
alipoitwa huko na kukubaliana ana kwa ana na jopo hilo huku mashinikizo
kadhaa yakielekezwa kwake.
Awali,
wajumbe wote wakiwa wamekaa kwenye viti, filamu hiyo yenye saa 3
iliwekwa mwanzo mwisho huku mapadri hao wakiguna kila wakati, hasa
wakati Sister Marry akiwa anafanya mambo yake mabaya. Baada ya
kumalizika kwa filamu hiyo, hoja zikaanza. Mwansoke akasema vipande
vyote vichafu vinyofolewe na kubaki vile ambavyo wajumbe hawakuvigunia.
Baada ya bosi huyo kusema hayo, mapadri wakasema ‘noooo’. Filamu hiyo
isiende mitaani hata kidogo kwani imejaa udhalilishaji wa Wakatoliki.
Inasemekana Paroko wa Kanisa la Mtakatifu Maximilian Kolbe lililopo
Mwenge Kijijini (jina halikupatikana mara moja) yeye alipigilia msumari
wa mwisho kwa maneno aliyoyatoa. Alisema kwa kuwa filamu hiyo
ilirekodiwa kwenye kanisa lake hilo, anataka vipande vyote vya kanisa
hilo vitolewe ndipo iingie mtaani, jambo ambalo lilimtoa machozi Ray.
Ray sasa! Siku ya Alhamisi iliyopita, Ray alizungumza na gazeti hili na
kukiri kuwepo kwa kikao hicho. Akasema itakuwa vigumu kuviondoa vipande
vya kanisa hilo kwa sababu asilimia 85 ya filamu nzima imerekodiwa
Maximilian Kolbe.
“Asilimia 85 ya filamu imerekodiwa Maximilian
Kolbe, sasa wanaposema niviondoe ni kuimaliza filamu yote. Filamu ni ya
saa 3, ukivitoa vipande vya kanisa si itabaki dakika 5 tu,” alisema Ray.
Alisema kikao kiliisha kwa maamuzi hayo, kwamba mtu wa utamaduni
alisema vipande vichafu vinyofolewe huku mapadri wakitaka muvi nzima
isiende sokoni na paroko wa Maximilian Kolbe akitaka kanisa lake
lisionekane kwenye filamu hiyo.
Risasi: “Je, wewe Ray umeamuaje?” Ray: “Sijaamua chochote kwa kweli. Niponipo tu, nimetumia fedha nyingi sana.”
Post a Comment