ad

ad

NANI ANAJALI? Tukiongozwa na wanasiasa uchwara

WIKI iliyopita niliandika kuhusu kichekesho cha wanandoa wawili walioingia katika aibu ya kufanya mapenzi na wafanyakazi wao wa nyumbani. Katika kichekesho hicho kilichoitwa UKIWA NDANI HUSIKII KITU, kijana wa kazi ambaye alikuwa amefanya kosa la kunywa mvinyo wa tajiri yake na kuweka maji, alimuumbua mume mbele ya mkewe kwa kuzini na dada wa kazi, na kisha kufichua siri ya yeye kuzaa na mke wa tajiri huyo.

Nikiri kwamba, nilipigiwa simu na kutumiwa ujumbe (sms) na wasomaji wengi. Kati ya hao, 17 kama sikukosei waliniomba niendeleze ‘mchapo’ huo kwa undani zaidi kwa sababu, ndoa nyingi zimejeruhiwa mno, na zinaishi katika mazingira mabaya. Baadhi, walitaka niwalekeze kule kinakopatikana kile kitabu changu cha NDOA YANGU, NINGEJUA nilichokitaja katika makala hiyo.
Kwa faida ya wale ambao hawakusoma kichekesho hicho, nawaomba radhi wale waliosoma wiki jana kwa kutekeleza ombi la wengi waliotaka nikirudie.

UKIWA JIKONI HUSIKII KITU...
Bosi mmoja alikuwa na mazoea ya kununua wine (mvinyo) anakunywa kidogo, kisha anaiacha juu ya kabati na kwenda kazini. Lakini kila siku kijana wa kazi alikuwa anakunywa kidogo alafu anaweka maji ili bosi asijue kama imepungua.
Bosi alipoinywa tena alikuta imebadilika ladha. Hivyo, siku moja akaweka mtego kwa kununua mvinyo ambao ukiwekwa maji unabadilika rangi na kuwa kama maziwa.
Kama kawaida, bosi akanywa kidogo akaenda kazini, na huku nyuma yule kijana kama kawaida yake akanywa kidogo alafu akaweka maji. Ghafla ukabadilika rangi na kuwa kama maziwa! Kijana Bakari akachanganyikiwa akaenda kujificha jikoni aliposikia bosi karudi na kukuta mvinyo wake umebadilika rangi. Akaanza kufoka, akimuita mke wake na kumwambia leo tumeshika mwizi.
Bosi: Bakari...wee Bakari!
Bakari: Yes boss.
Bosi: Kwanini umekunywa wine yangu na ukaweka maji?
Bakari: [Kimya]
Bosi: Kwanini umekunywa ‘wine’ yangu?
Bakari [Kimya]
Bosi akapandwa na hasira akamfuata Bakari jikoni huku mkewe akiwa nyuma.
Bosi: Nimekuita umeitika, lakini swali langu hujibu kwanini?
Bakari: Bosi ukiwa huku jikoni hausikii kitu chochote isipokuwa jina lako tu, kama huamini baki humu ndani ujionee.
Bakari akatoka nje na mke wa bosi na kumwacha bosi ndani.
Bakari: Boss.
Bosi: Yes Bakari.
Bakari: Nani hupenda kuingia chumba cha dada wa kazi wakati madam boss yuko kazini?
Boss: [Kimya]
Bakari: Nani hulala na dada wa kazi wakati madam boss amesafiri?
Boss: [Kimya] Bosi akafungua mlango wa jikoni, akatoka na kusema: “Walai maajabu, ukiwa humu ndani husikii chochote isipokuwa jina lako tu!”
Mke wa bosi akaja juu: “Pumbavu! Waongo wakubwa nyie...nini kinaendelea hapa enh?”
Bakari: Ukweli mama ukiwa ndani unasikia jina lako pekee...kama unabisha na wewe ingia utaamini!
Mke wa bosi akaingia jikoni na kumwacha mume wake pamoja na Bakari nje.
Bakari: Madam?
Mke: Yes Bakari?
Bakari: Sema ukweli, nani baba yake mtoto kati ya mimi na bosi?
Mke: [Kimya]
Bakari: Eeh…tuambie nani aliyekupa hiyo mimba?
Mke: [Kimya] Akafungua mlango akatoka: “Aaah...ni kweli, humu ndani kunahitaji maombi, yaani ukiwa ndani unasikia jina lako pekee!”
Katika makala ya wiki jana, nilihoji mambo mengi, machache kati ya hayo, ni juu ya sababu zilizowasukuma waheshimiwa hawa kutojali tena heshima yao, kubwaga chini hadhi yao kiasi cha kuwavulia nguo wafanyakazi wao wa ndani.

Nikahoji sababu ipi hasa iliyowafikisha wanandoa hawa, kutojali na kulinda utu wao hadi kuwavulia nguo watu ambao kwa namna yoyote walikuwa sawa na watoto wao, nakadhalika. Sasa tuendelee.
Kawaida ya wanandoa wengi, hususan wanaume, hudhani kwamba wao wanayo haki ya ziada kuliko wake zao. Hufikiri kwamba wanayo haki ya kuondoka na kurudi muda wowote. Wana haki ya kuwa na vimada kuliko wake zao kuwa na wanaume wengine wa pembeni. Ndiyo maana haishangazi kuona mwanaume anazaa nje na kisha anaomba radhi kwa mkewe kwamba aliteleza. Subiri mkewe naye abebe mimba na atumie lugha ileile ya kuteleza. Mwanaume gani atapokea hayo?
Katika kisa hiki, mke na mume wote wamefikia hatua ya kuumbuliwa na kijana wa kazi, tena mpita njia tu kwa sababu wote hawakujali. Mwanaume, hakujali kwamba alioa mke aliyeacha wazazi wake, na ndugu kuja kuwa mke.

Kitendo cha mkewe kufikia hatua ya kumtamani kijana wa kazi, akakubali kubaki tupu, kumpa hadhi ya kuwa mume kijana huyo, kulitokana na kutojali kwa mumewe katika mambo mengi, hapa niyataje mawili. Kwanza, mume hakujali kwamba mkewe alihitaji uwepo wake kwa wakati unaofaa na hata usiofaa. Mume alifiriki kuwa kwa sababu alishaoa, kazi yake imekwisha na hivyo, yuko huru kuendesha maisha kana kwamba hajaoa. Mke alibaki pweke wakati mwingi, pindi alipotoka kazini, alitamani kusikia sauti nzito ya kiume ikitawala ndani ya nyumba, lakini mume hakujali.

Jambo la pili kubwa ni hili. Kwa kiasi gani mume alitimiza wajibu wake wa kumpa furaha na faraja mkewe wakati wa tendo la ndoa. Yawezekana mara kadhaa alirudi amechoka, na hapo alipolazimika kuhitaji tendo la ndoa, alifanya kwa nia ya kujifurahisha mwenyewe. Hakujali kwamba mkewe katika tendo hilo, anafika katika kilele cha furaha. Alijali furaha yake, na kisha kuishia usingizi. Hakujali!

Katika kuhangaika, mke anajikuta anamtazama kijana wa kazi anayeshinda naye muda mrefu awapo nyumbani. Anamtazama sasa kwa jicho tofauti; jicho la mapenzi. Bila kujua, anafunikwa na wingu la mahaba. Mke hajali tena, anatamani kushibisha njaa yake ya siku nyingi. Njaa ambayo inaondolewa kama utani na kijana anayejua kujali! Sasa mke kwa furaha aipatayo, anaweza kwenda kazini na kurudi mapema ili aipate furaha ile aliyoikosa kwa mume. Hajali tena kama kaolewa na wala hana muda wa kumkumbuka mume ambaye kwa miaka mingi amemgeuza kama jalala. Mume ambaye amekuwa hajali kuona mkewe anafurahi. Kosa la nani hapa?

Lakini mke naye hana hatia? Ni wanawake wangapi wameondoa mapenzi kwa waume zao na hasa baada ya kuzaa na kuyaelekeza kwa watoto? Ni wanawake wangapi wameona kazi kuwa muhimu kuliko waume zao? Fikiri ni akina mama wangapi wenye madaraka kazini, wamekuwa wakirudi na vyeo vyao nyumbani, wakitaka mume amheshimu mkewe, kama waziri, RC, DC nakadhalika, bila kujua kuwa kwa mumewe ana cheo cha mke tu? Majigambo na kauli ngumu zimekuwa chanzo cha kuwafanya waume zao kutotamani kurudi nyumbani mapema.

Mara ngapi kina mama nao wamekuwa mabingwa wa wimbo wa ‘leo nimechoka’ kila wanapotakiwa kutimiza wajibu wao wa ndoa? Ni wanawake wangapi ambao, ukiacha kulala kitanda kimoja na waume zao, wameacha majukumu yote ya nyumba mikononi mwa dada wa kazi? Mume kama huyu anayeishi na mke mwenye sifa za kamanda wa sungusungu; mume ambaye hakumbuki kuambiwa neno la upendo toka kwa mke, anayekaribishwa chakula kwa mguu, atashindwaje kuvutiwa na binti anayemkaribisha kwa sauti laini, heshima na hata kumnawisha? Atashindwaje kuvutiwa na binti ambaye daima yu macho kumfungulia baba arudipo nyumbani? Atashindwaje kuwa kipofu kwa binti ambaye hajui kusema ‘leo nimechoka’ katika mambo hayo?
Katika hali kama hii, kwanini wote wasibebe lawama ya kutojali kiapo chao, heshima yao na hadhi yao? Wajali kwa lipi ikiwa kila mmoja anaamini asingefanya hivyo kama mwenzake angemjali?
Powered by Blogger.