ad

ad

Mbwembwe zakolea Uchaguzi TFF

UCHAGUZI Mkuu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), hauna tofauti na uchaguzi za vyama vya siasa kwa jinsi mbwembwe na vituko vinavyotawala hasa wakati wa uchukuaji na urejeshwaji wa fomu za kugombea uongozi.

Hali hiyo ilionekana jana katika Ofisi za TFF wakati baadhi ya wagombea wa nafasi mbalimbali za uongozi walipokuwa wakichukua fomu tayari kwa uchaguzi huo mwezi ujao.
Kama kawaida, mbwembwe zilitangulia mbele na vituko nyuma, huku wagombea wakisindikizwa kuchukua fomu na kundi la watu kama vile tayari wameshashinda kiti kwenye uchaguzi huo.

Kazi ya kuchukua fomu ilianza mwanzoni mwa wiki hii na inatarajiwa kufikia tamati kesho, tayari kwa kinyang’anyiro hicho cha Februari 24.

Saa tano asubuhi, Athuman Nyamlani (Makamu wa Kwanza Rais TFF) anayemaliza muda wake, aliwasili katika Ofisi za TFF kuchukua fomu ya kugombea urais wa TFF.
Nyamlani ambaye alikuwa wa kwanza kufungua pazia la uchukuaji fomu nafasi ya urais, aliingia na wapambe wake kadhaa waliokuwa kwenye magari.

Baada ya kuingia kuchukua fomu hiyo na kuijaza na kisha kurudisha alitoka na nje kulikuwa na wapambe wake wakimsubiri.

Kabla ya kuondoka, Nyamlani alielezea kile kilichomsukuma kuchukua fomu ya kugombea urais. Alisema: “Nimejitosa kuwania nafasi hii ili niweze kuleta maendeleo nikiamini pale alipofikia Tenga (Rais anayemaliza muda wake) siyo pabaya.”
Alisema amekaa kipindi kirefu TFF na anaamini amepata uzoefu wa kutosha na anafahamu nini anapaswa kufanya.

Saa moja baada ya Nyamlani yaani 12:00 aliwasili Mwenyekiti wa Chama cha Soka Kagera (KRFA), Jamal Emil Malinzi, huku wapambe wake wakiwa wanamsubiri katika ofisi za TFF.
Walimpokea na kumsalimia kisha wakaingia ofisi za TFF, kuchukua fomu za urais akiwa ni mtu wa pili na baada ya kujaza na kurudisha fomu hiyo alisema kuwa hana maneno ya kuzungumza kwa vile kipindi cha kampeni hakijaanza.

Hata hivyo, alitumia fursa ndogo kumshukuru Rais wa TFF, Leodegar Tenga kwa uamuzi wake wa kutangaza kutogombea tena nafasi hiyo pamoja na kwamba katiba inamruhusu.
“Nampongeza Tenga kwa kufanya uamuzi mgumu. Ameonyesha kweli ni mpenda soka kwa kuacha na wengine waongoze. Naamini utamaduni huu utaendelea kwa Watanzania wengine,” alisema.

Mbali na Nyamlani na Malinzi, pia Mwenyekiti wa Chama cha Soka Kigoma, Omari Mussa Nkwarulo naye amechukua fomu ya urais wa TFF.
Mwingine aliyechukua fomu jana ni Mwenyekiti wa Chama cha Soka Mbeya (Mrefa), Elias Mwanjala anayewania Ujumbe wa Kamati ya Utendaji na kuwakilisha Kanda ya Iringa na Mbeya.

Orodha kamili ya wadau waliochukua fomu ni Athuman Jumanne Nyamlani, Jamal Emil Malinzi na Omari Mussa Nkwarulo (Urais), Michael Wambura, Ramadhan Nassib na Wallace Karia (Umakamu Rais).

Kamati ya Utendaji na kanda zao kwenye mabano ni Salum Chama (Kagera na Geita), Mugisha Galibona, Samuel Nyalla, Titus Osoro na Vedastus Lufano (Mara na Mwanza).
Epaphra Swai na Mbasha Matutu (Shinyanga na Simiyu), Charles Mugondo na Elly Mbise (Arusha na Manyara), Yusuph Kitumbo (Kigoma na Tabora), Ayubu Nyaulingo, Nazarius Kilungeja na Selemani Kameya (Katavi na Rukwa) na James Mhagama (Njombe na Ruvuma).

Athuman Kambi (Lindi na Mtwara), Hussein Mwamba na Stewart Masima (Dodoma na Singida), Farid Nahdi na Twahili Njoki (Morogoro na Pwani), Elias Mwanjala (Iringa na Mbeya), Khalid Mohamed (Kilimanjaro na Tanga) na Muhsin Balhabou, Shaffih Dauda na Zafarani Damoder (Dar es Salaam).

Kwa upande wa Bodi ya Ligi Kuu (TPL Board) waliochukua fomu kwenye ofisi za TFF mpaka sasa ni wawili tu. Mmoja amechukua fomu ya Uenyekiti na Said Mohamed Makamu Mwenyekiti.
Powered by Blogger.