MAZOEZI YA VIUNGO: Dawa bora kwa wagonjwa
MIONGONI mwa huduma ambazo bado hazijafahamika kwa wengi ni
matibabu ya mazoezi ya viungo vya mwili pamoja na kuchua ‘massage’ kwa
kutumia mikono na mashine za kisasa.
Salvatha Mushi, ni mtaalamu wa matibabu hayo, mwenye kituo chake
maeneo ya Upanga jirani ya Ukumbi wa Diamond Jubilee, kona ya Barabara
ya Nyangoro na Maliki kijulikanacho kwa jina la Pain Management Centre.
Mtaalamu huyu anasema matibabu hayo yamewasaidia wagonjwa wengi
waliokuwa wamekata tamaa ya kuishi, huku akifafanua kuwa upungufu wa
elimu kwa wagonjwa bado ni kikwazo.

Kuhusu elimu kwa wagonjwa, Mushi anasema bado ni tatizo, kwani ni
wachache wanaoamini kuwa mgonjwa anaweza kupona bila kupewa dawa ya
kumeza au kunywa, bali kwa kufanya mazoezi ya viungo pekee pamoja na
kuchua.
“Inatakiwa kwanza mgonjwa kumpa elimu atambue kuwa mazoezi pia ni
dawa. Mgonjwa anatakiwa kufanya mazoezi kadiri unavyomwelekeza, hata
kama atafanyia nyumbani asipuuze maelekezo,” anasema.
Aidha, anashauri kuwa mgonjwa anapoamua kufanya mazoezi akipata nafuu asiache hadi atakapopona kabisa.
Anabainisha kwamba mgonjwa anatakiwa kufanya mazoezi kati ya siku 10
hadi 14 mfululizo na asipofikisha muda huo hata kama atapata nafuu
lakini hawezi kupona.
Kuhusu gharama za matibabu, anasema kituo chake ni miongoni mwa vituo
vinavyolipisha fedha chache sana, lakini wagonjwa wamekuwa wakipatiwa
matibabu ya uhakika.
Anasema dawa zinazotumika katika kituo chake ni za kuchua, mashine
mbalimbali za kutibu viungo na misuli, dawa za kupunguza maumivu, dawa
za kushtua mishipa ya fahamu, mashine za kusaidia mzunguko wa damu na
‘massage’ ya mikono ambayo anasema ni njia nzuri zaidi.
Aidha, mtaalamu huyo anasema kuwa wana mashine za kuvuta uti wa
mgongo kwa ambao ‘disc’ zimeachia, kumeguka au hazijakaa sawa. Vilevile
wanatoa tiba kwa waliovunjika miguu baada ya kufanyiwa upasuaji,
wagonjwa wanaowekewa vyuma na wale wanaoumwa migongo na ‘disc’
zinagusana.
Mushi anasema wanatoa matibabu pia kwa wagonjwa ambao wamepooza upande
mmoja wa mwili, uso kupooza upande mmoja, ganzi kwenye mikono na miguu,
kichwa kuuma, mgongo, uchovu, watoto wenye mtindio wa ubongo na watu
wazima baada ya kufanyiwa operesheni ya kichwa.
Aidha, Mushi analalamikia ukubwa wa kodi inayotozwa na serikali katika
kuendesha vituo vya aina hiyo na ukubwa wa gharama za vifaatiba kuwa
chanzo cha malipo kuwa makubwa kwa wagonjwa na kusababisha wengi
kutomudu.
“Naomba gharama za vifaa tiba na zile zinazotozwa kwa ajili ya
kuendesha vituo hivi zipunguzwe ili kuwasaidia wagonjwa wengi wenye hali
ya chini kumudu gharama za matibabu.
“Vilevile natoa wito kwa serikali kuhakikisha kuwapo kwa vitengo vya
matibabu ya mazoezi katika zahanati na hospitali za umma ili kuwasaidia
wagonjwa wasioweza kugharamia matibabu hayo katika vituo vya watu
binafsi,” anasema na kuongeza kuwa jambo la kusikitisha ni kwamba hata
pale ambapo vitengo hivyo vipo hakuna vifaa vya kuhudumia wagonjwa.
Mushi anaitaka serikali isaidie katika kuhamasisha na kutoa elimu kwa
watu mbalimbali kutambua kwamba kuna huduma ya aina hiyo ya mgonjwa
kupona bila kupewa dawa isipokuwa kwa kufanya mazoezi ya viungo, hasa
vijijini ambako uelewa bado ni mdogo.
Anasema kituo chake kina ubora wa hali ya juu kutokana na mwitikio wa wagonjwa wengi wanaofika hapo kupata huduma.
Mtaalamu huyo wa tiba anawataka wote wenye matatizo aliyoyabainisha
hapo juu wafike katika kituo chake bila kusita kwani gharama za matibabu
ni nafuu na hupungua kulingana na mgonjwa anavyojieleza.
Alikotoka Mushi
Akielezea historia fupi ya maisha yake hadi kufikia kuwa ‘Physiotherapist’ anasema alizaliwa mwaka 1972 Moshi, Kilimanjaro.
Alianza masomo ya shule ya msingi mwaka 1981 katika Shule ya Msingi
Otaruni. Mwaka 1988 alianza masomo ya kidato cha kwanza katika Shule ya
Sekondari Weruweru ambako alisoma na kuhitimu kidato cha sita mwaka
1993.
Septemba 1993 hadi Mei 1996, alikuwa akisomea stashahada katika Chuo
cha Physiotherapy KCMC mjini Moshi. Baada ya kuhitimu masomo alianza
kazi katika Hospitali ya TMJ Mikocheni, mjini Dar es Salaam ambako
alifanya kazi kwa miaka kumi, tangu Julai 1996 hadi Januari 2006.
Anasema alipoajiriwa katika Hospitali hiyo ya TMJ ndiye alikuwa
mwanzilishi wa idara ya mazoezi ya viungo na akiwa mkuu wake kwa kipindi
chote cha miaka 10 aliyofanya kazi katika hospitali hiyo.
“Mwaka 2006 baada ya kutoka katika Hospitali ya TMJ nilianzisha kituo
changu cha Pain Management Centre kwa ajili ya kutoa matibabu ya viungo
kwa njia ya mazoezi,” anasema.
Post a Comment