Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) Yawajibu CHADEMA
Majibu hayo yametoka baada ya Chadema kuilalamikia tume na watendaji wake walioteuliwa kusimamia uchaguzi huo.
Katika
taarifa yake kwa vyombo vya habari jana, NEC ilidai haijapokea barua
yoyote kutoka Chadema licha ya chama hicho kikuu cha upinzani bungeni,
kuvieleza vyombo vya habari kwamba kimeiandikia barua tume kuhusu wakuu
wa wilaya kushiriki mikutano ya kampeni za kuwanadi wagombea wa Chama
Cha Mapinduzi (CCM) na tume haijachukua hatua zozote.
Taarifa
ya NEC ilibainisha kuwa hoja ya pili ya Chadema ni tume kuhamisha vituo
46 vya kupigia kura katika kata tatu za Kigogo, Mwananyamala na
Kijitonyama bila kuishirikisha Chadema.
Hoja
nyingine ni Msimamizi wa Uchaguzi kutoa uamuzi dhidi ya Chadema kwenye
Kamati ya Maadili kwa uonevu na Chadema kuadhibiwa na Kamati ya Maadili
kwa makosa yanayotuhumiwa kutendwa na mwanachama wa Chadema na kuwa
makosa hayo ni ya kijinai na yalipaswa kushughulikiwa kijinai na si
kukipa adhabu chama hicho.
Pia Chadema ilisema kikao hicho kiliendeshwa na mtu asiyepaswa kuwa Mwenyekiti wa Kamati.
Taarifa
ya NEC ilieleza kuwa hoja nyingine ni kitendo cha malalamiko ya Chadema
dhidi ya wakuu wa wilaya kushiriki kampeni za uchaguzi na Kamati za
Maadili kutotenda haki kwa kuwa wenyeviti wake ni makatibu tawala wa
wilaya.
Katika
taarifa hiyo iliyotolewa jana na Mkurugenzi wa Uchaguzi wa NEC, Kailima
Ramadhani, ilifafanua kuwa tume haijapokea barua au karatasi yoyote
kutoka Chadema inayoelezea malalamiko yao.
“Ukweli
ni kwamba, Chadema hawajawasilisha barua kwa tume. Hata kama
wangewasilisha barua za malalamiko yao, tume ingewaelekeza kusoma na
kuelewa Maadili ya Uchaguzi, kwa kuwa lalamiko namba mbili hadi sita
waliyoyataja kwenye vyombo vya habari yangeweza kushughulikiwa na Kamati
za Maadili ambazo Chadema kama chama chenye wagombea ni sehemu ya
wajumbe wa kamati husika,” alisema.
Kailima
katika taarifa hiyo, alisema uhamishaji wa vituo umezingatia matakwa ya
Kanuni ya 21 ya Kanuni za Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapigakura
za mwaka 2008 kama zilivyorekebishwa mwaka 2014.
“Kanuni
hiyo ikisomwa pamoja na kipengele cha 9.2(c) cha Kitabu cha Maelekezo
kwa Wasimamizi wa Uchaguzi ya mwaka 2015, vituo vya kupigia kura
havitakiwi kuwa kwenye maeneo ya Kambi za Jeshi, Polisi, maeneo ya
kuabudia kama vile misikiti na makanisa, nyumba za viongozi au mashabiki
wa vyama vya siasa,” alifafanua katika taarifa hiyo.
Kailima
pia alisema kuwa kwa kuzingatia matakwa ya kanuni na kipengele tajwa,
Januari 31, Msimamizi wa Uchaguzi wa Jimbo la Uchaguzi la Kinondoni,
aliitisha mkutano wa vyama vya siasa vyenye wagombea ubunge na ajenda
ilikuwa ni kuhamisha vituo vya kupigia kura.
“llifanyika
hivyo kwa sababu mbalimbali zikiwamo baadhi ya vituo kuwa kwenye maeneo
ya kuabudia, kuwa jirani mno na ofisi ya chama cha siasa, nyumba za
watu binafsi, kwenye maeneo finyu,” alisema.
Alidai kuwa kikao hicho kilishirikisha wawakilishi 16 kutoka vyama 11 vinavyoshiriki uchaguzi mdogo wa jimbo la Kinondoni.
“Chadema
kiliwakilishwa na Mwenyekiti wa Chadema Wilaya ya Kinondoni, Mustapha
Muro na Katibu wa Chadema wa Wilaya, Shabani Kirita,” Kailima alieleza
katika taarifa hiyo.
Kuhusu
malalamiko kwamba Msimamizi wa Uchaguzi alitoa uamuzi wa uonevu dhidi
ya Chadema kwenye Kamati ya Maadili, Kailima alisema uamuzi hufanywa na
Kamati ya Maadili na si Mwenyekiti wa Kamati.
“Tunaikumbusha
Chadema sheria, kanuni na maadili ya uchaguzi hayampi Mamlaka Msimamizi
wa Uchaguzi kutoa maamuzi kwenye Kamati ya Maadili. Msimamizi wa
Uchaguzi ni Mwenyekiti wa Kikao cha Maadili tu, na kwamba, maamuzi
hufanywa na Kamati ya Maadili na siyo Mwenyekiti wa Kamati,” alieleza
Kailima katika taarifa hiyo.
Kuhusu
Chadema kuadhibiwa kwenye Kamati ya Maadili kwa makosa ya kijinai,
Kailima alisema tume imekitaka chama hicho kama hakikuridhika na maamuzi
kufuata taratibu zilizoainishwa kwenye Maadili ya Uchaguzi wa Rais,
Wabunge na Madiwani ya mwaka 2015.
Kuhusu
malalamiko dhidi ya wakuu wa wilaya kushiriki kampeni za uchaguzi,
Kailima alisema tume inaitaka Chadema kuwasilisha malalamiko yake kwenye
mamlaka husika kwa kuwa sheria na kanuni zimebainisha mamlaka
zinazoshughulikia masuala hayo.
Post a Comment