Msuva Aonyesha Ujuzi wa Morocco, Stars Ikiua
Mshambuliaji Simon Msuva amefanya kile kilichosubiliwa na mashabiki wa soka nchini kwa kufunga mabao mawili yaliyoipa Taifa Stars ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Botswana kwenye Uwanja wa Uhuru.
Akicheza mechi ya kwanza ya Stars tangu aliponunuliwa na klabu ya Difaa Al Jadida Morocco, Msuva alitumia kwa umakini nafasi mbili alizopata.
Bao la kwanza lilifungwa dakika ya 5 akimalizia pasi ya Mzamiru Yassin ambaye awali aligongeana naye pasi nzuri.
Licha ya Botswana kuamka na kufanya mashambulizi yaliyozaa kona dakika ya 13,14 na 17 lakini ilishindwa kuziitumia.
Dakika ya 24 Shiza Kichuya aliwahadaa walinzi wa Botswana na kuachia fataki lakini lilidakwa na kipa Mwampule Masule.
Bao la pili la Stars lilipatikana dakika ya 62 baada ya Msuva kupokea pasi kutoka kwa Shiza Kichuya na kuachia shuti kali lililomshinda kipa wa Botswana Mwampule Masule na kujaa wavuni.
Kocha mkuu wa Botswana David Bright alisema timu yake haikuwa makini katika kuzuia mashambulizi ya Stars.
"Goli la kwanza lilikuwa shambulizi la harakaharaka namsifu mfungaji, tulijitahidi kuudhibiti mchezo, lakini presha ya Tanzania ilikuwa juu zaidi yetu,"alisema kocha Bright.

Post a Comment