Zidane Alia Na Morata Kuondoka Agoma
KOCHA wa Real Madrid, Zinedine Zidane amesema timu yake ina uhaba wa washambuliaji baada ya kumuuza Alvaro Morata kwenda Chelsea.
Kocha huyo amesema kuwa washambuliaji waliopo kwenye timu hiyo hawatoshi, huku akisisitiza kuwa mshambuliaji bora wa timu hiyo Cristiano Ronaldo, atabaki kwenye kikosi hicho..
Morata ambaye alikuwa akiwindwa kwa nguvu kubwa na Manchester United aliuzwa kwenye kikosi cha Chelsea kwa kitita cha pauni milioni 60, zaidi ya shilingi bilioni 171.
Hata hivyo, bado timu hiyo inamwinda staa wa Monaco, Kylian Mbappe, ambaye anaweza kumaliza tatizo hilo kwenye timu hiyo.
“Alvaro ameondoka na sasa tuna tatizo kubwa la washambuliaji kwenye timu yetu.
“Nafikiri kila mmoja aliona jinsi alivyocheza msimu uliopita, alionyesha kiwango cha hali ya juu sana na hakika tulitakiwa kuwa naye msimu huu.
“Tutajaribu kuona ni kitu gani tunaweza kufanya kabla usajili huu haujafungwa lakini naamini kuwa tutamaliza vizuri,” alisema kocha huyo raia wa Ufaransa.
Alipoulizwa kuwa taarifa kuwa anataka kumsajili, Mbappe kutoka Monaco, alisema: “Ni jambo ambalo limejadiliwa klabuni, lakini siwezi kuzungumza sana kwa kuwa tunajadili wachezaji ambao wapo nasi kwa sasa hawa ndiyo tupo nao kwenye timu hii.”
Zidane ni kati ya makocha waliofanikiwa kwa muda mfupi akiwa amefanikiwa kutwaa ubingwa wa Ligi ya Mabingwa Ulaya kwa misimu miwili mfululizo, lakini pia msimu uliopita alifanikiwa kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya Hispania, La Liga.
Post a Comment