ad

ad

Tusipoangalia; ujangili hauishi nchini mpaka tembo waishe



HAUWEZI kupita mwezi au miezi miwili bila kusikia kwamba kuna pembe za tembo zimekamatwa sehemu fulani. Hiki ni kiashiria kwamba vita ya ujangili haitaisha mpaka tembo wote katika nchi hii waishe. Lakini je, Watanzania tunakubaliana na hilo? Mimi nasema Watanzania wote tuungane na kusema hapana.
Lakini ukweli ni kwamba hiyo inatudhihirishia kuwa matukio ya ujangili nchini na hasa mauaji ya tembo au faru yanaendelea kwa kiasi kikubwa kwa sababu nyingi; kubwa naweza kusema ni siasa na uongozi.

Nasema ni tatizo la kisiasa kwa sababu vita dhidi ya ujangili inategemea uamuzi wa wanasiasa ambao wana masilahi mengi sana ya kisiasa; ni tatizo la kiuongozi kwa sababu kutokea kwake kumethibitisha kushindwa kwa uongozi kupanga, kutarajia, na kutekeleza mipango ya kuhami wanyama wetu lakini pia ni tatizo la kiusalama kwa sababu kutokea kwake kumeonesha ni jinsi gani vyombo vyetu vya ulinzi na usalama vimeachwa nyuma na wahalifu katika suala la ujangili. 

Naambiwa majangili siku hizi wana silaha kali kama askari wetu. Kama Rais Dk. John Magufuli alivyosema kuhusu majambazi kuwaambia polisi kwamba wanyang’anywe silaha, mimi nasema majangili nao wanyang’anywe silaha zao. Maliasili yetu na vyote vilivyomo ndani yake ni vitu ambavyo tumepewa na Mwenyezi Mungu kama zawadi ili iwe na manufaa kwa Watanzania wote wanaoishi sasa na vizazi vijavyo. Mali hizi za asili ni urithi ambao tuliachiwa na wazee wetu, na sisi tunatakiwa kuvitunza vizuri lakini wakati huo huo tukifikiria kuwaachia watoto wetu na watoto wa watoto wetu. 

Tembo, simba, faru, chui, twiga na wanyama wengine wengi – wakubwa na wadogo, wawindao na wale wawindwao wote hawa ni zawadi yetu lakini ni urithi kwa watoto wetu. Tunaposhindwa kwa sababu yoyote ile kusimamia uhai wa mali asili hizi, tunawaweka katika nafasi ngumu watoto na wajukuu wetu kwani wataendelea kuwa tegemezi na kuombaomba duniani hasa maliasili hizi yaani wanyama hao wakiendelea kuuawa.

Ni muhimu kuangalia kwanza siasa zetu. Tuliona jinsi kashfa ya Loliondo miaka zaidi ya ishirini iliyopita hadi leo hii ilivyozimwa, kuna kila dalili kuwa wanasiasa wetu wameshindwa kuja na sera zinazoeleweka za kulinda hifadhi zetu na mbuga zetu na kama vile wale walivyokuwa wamesalimishwa mbele ya wenye fedha, leo hii tunaanza kushuhudia tena watu wenye uwezo mkubwa wa kifedha wakiwazidi ujanja kwa fedha wanasiasa wetu kiasi cha kutishia urithi wetu na uhuru wetu.

Sera sahihi, bora na zinazotekelezeka zinatakiwa ziweke msingi wake kwenye kuelewa kuwa hizi mali asili ni mali zetu Watanzania wote; na yeyote anayetaka kuitumia anapaswa kuitumia kwa masharti yetu sisi na siyo yao; ni lazima tuweke kwenye sera zetu na watu wajue kuwa mali hii siyo ya kwetu tu bali ni ya watoto wetu na vizazi vijavyo. Hivyo, hatuwezi kuruhusu au kuachilia uwindaji au ugawaji wa vitalu vya uwindaji kama zawadi kwa watu wenye fedha nyingi ambao wanatumia utajiri wao kuhujumu nchi.
Hao wageni wakimaliza kuua wanyama wetu watakuja tena nchini mwetu kufanya nini? Mojawapo ya mambo ambayo tungepaswa kuyaweka na kueleweka ni kuhakikisha ni jinsi gani wawindaji haramu hawatishii uwepo wa wanyama wetu.
 

Chukulia kwa mfano, tembo ni mnyama mkubwa kabisa kwa wale watembeao ardhini; sasa inawezekana vipi watu kuweza kuua maelfu ya wanyama hao bila kuonekana au kukamatwa? Ni kwa namna gani mtu anaweza kufanya uhalifu huu kwa muda mrefu kiasi kwamba, hata kukamatwa inachukua muda na kesi hazijulikani mwisho wake, au ujangili utakwisha tembo wakiisha? 
Tusipokuwa wakali, wataisha kweli kwa sababu tumewahi kusikia kontena limekamatwa huko nchi za mbali likiwa na meno ya tembo. 

Fikiria ni tembo wangapi wameuawa hapo? Wanasiasa wangekuwa na fikra za ulinzi kweli basi wangeona kuwa sheria zenyewe nazo zingetakiwa kupitiwa ikiwemo kuharakisha kesi za ujangili, zisikae muda mrefu mahakamani na wahusika wahukumiwe ili liwe tishio kwa wenye tabia hiyo Kuchelewesha kesi hizi kwenye utoaji wa haki kwa muda mrefu kunasababisha watu waendelee kuua tembo na faru wetu na hii tunaweza kusema ni kuendeleza ufisadi kwani wenye nguvu wanaweza kutumia njia zozote kulainisha ukali wa kesi au ukali wa hukumu na matokeo yake watu wakabakia kulipishwa faini au kupata hukumu ndogo kulinganisha na uzito wa kosa au pengine kutotiwa hatiani kabisa. Wanasiasa wanabeba lawama kubwa zaidi ya tatizo la ujangili lakini pia wale waliopewa dhamana ya uongozi kwenye vyombo vya kutoa haki. Hivi ni kweli watu hawa yaani viongozi wa ngazi mbalimbali nchini- hawajajifunza yaliyotokea Lolindo na kwingine hadi leo hii? Hivi ni kweli tangu miaka ya tisini hadi leo hii bado tunahangaika na wawindaji kutoka nje ambao hupewa vitalu na kuwa wamenunua kipande cha nchi? 

Kwa nini, leo hii habari za kashfa za ujangili zinaonekana kana kwamba ni habari za mashindano na ugomvi kati ya matajiri wa Kimarekani na Waarabu wakati mwenye uamuzi wa mwisho ni Watanzania wenyewe? Kwa nini Rais Dk. Magufuli asitumie madaraka yake kusitisha uwindani na kufuta vibali vyote vya uwindani ili tuanze upya mchakato mzuri chini ya masharti mazuri? Najua tunalo Shirika la Hifadhi la Taifa (Tanapa) ambalo linajitahidi mno kusimamia maliasili zetu, lakini ni wazi majangili na wanaowatumia wanatuangusha. Tanapa peke yao hawawezi, ipo haja kwa Watanzania wote kuungana katika vita hii, tuwe pamoja kuhakikisha majangili wanashindwa.

 Najua kwamba majangili wengi tunaishi nao katika jamii yetu, hivyo ili tuendelee kuwaona tembo na faru nchini mwetu na ili watuingizie fedha za kigeni kama taifa, ni lazima wote tuwe walinzi kwa wanyama hao na wengine wanaowindwa na majangili. Nionavyo ni kwamba itakuwa aibu kubwa kama Tanzania ikiwa tutaishiwa tembo na faru na watoto au vizazi vyetu vijavyo wakawa wanawaona kwenye picha tu! Hakika tutakuwa tumemkufuru Mungu aliyetuwekea wanyama hao. Huu utakuwa ujinga wa hali ya juu kwani watalii wanaokuja kuwaona wanyama hao wakubwa, tutawapoteza. Mimi na wewe kuanzia sasa tuwe walinzi.

MAKALA: ELVAN SITAMBULI, UWAZI

No comments

Powered by Blogger.