ad

ad

DC ataka vijana wawe wazalendo


MKUU wa Wilaya ya Kilwa mkoani Lindi, Christopher Ngubiagai, amewataka vijana kuwa wazalendo kwa nchi na kuacha ubinafsi pamoja na tamaa ya kuwa na maisha bora ya haraka kwa njia zisizofaa.

Alitoa mwito huo mwishoni mwa wiki, alipozungumza na wanafunzi wa shule za sekondari za Jitegemee, Kigamboni, Wailes na Kibasila za Dar es Salaam, wakati wa uzinduzi wa kumbukumbu ya waathirika wa utumwa na biashara ya utumwa kwa ufadhili wa Umoja wa Mataifa (UN).

Ngubiagai alisema suala la uzalendo kwa vijana limeanza kutoweka na kwamba hali hiyo ilitokana na kuwepo kwa ubinafsi na tamaa ya kuwa na maendeleo binafsi kuliko ya taifa.

Alisema hali hiyo imesababisha kundi kubwa la vijana kuingizwa kwenye utumwa na ufisadi. Aliongeza kuwa hali hiyo inasababisha kutokuwa wazalendo kwa taifa lao na kushindwa kuleta maendeleo ya kiuchumi.

Alisema ni vyema vijana wakajitambua na kuwa na maadili mema na kuacha tamaa ya kuwa na maisha bora ya haraka kwa njia zisizofaa, ili kuijenga nchi kwa kufanya kazi kwa juhudi na maarifa.

Awali, Ofisa Habari wa UN, Stella Vuzo alisema lengo la ziara hiyo ni kuwaonesha wanafunzi maeneo ya historia ya biashara ya utumwa ili kuwaongezea uelewa kwa vitendo juu ya mchango wa watumwa katika nchi zao na kumbukumbu ya waathirika wa biashara ya utumwa.

Vuzo alisema kila Machi 25 ni siku ya kumbumbuku ya waathirika wa utumwa na biashara ya utumwa duniani, hivyo kwa Tanzania, wameamua kufanya ziara na uzinduzi wa siku hiyo wilayani Kilwa.

No comments

Powered by Blogger.